Mobhare Matinyi, Washington DC
NI kweli kwamba rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, si mtu rahisi kumwelewa hasa kama hukuwepo wakati akitawala, au ulikuwepo lakini hukumfuatilia au kama una mengine rohoni mwako.
Inaweza kuwa vigumu kumwelewa pia iwapo unakumbana na watu wanaotaka kuiandika historia upya kama mwandishi wa makala iliyotangulia aliyedai kuwa Nyerere alikuwa kitendawili.
Lakini basi, kwa vyovyote itakavyokuwa, hatuna budi kumchambua kwa kutumia ukweli na si porojo za alinacha. Wapo wasomi waliowahi kuonya kwamba ingawa kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni yake, lakini hakuna mwenye uhuru wa kuwa na ukweli wake yeye tu. Ndiyo, Nyerere kutokana na mengi aliyoyafanya, si rahisi kumwelezea kinagaubaga katika nafasi ndogo kama hii.
Si kweli kwamba Watanzania eti wamekuwa wakishindwa kutafsiri yale yote aliyoyasimamia ingawa ni kweli kwamba yapo machache yaliyopindwa na viongozi waliokuja baadaye ama yaliyobadilishwa kama ilivyostahili. Mathalani kuuawa kwa Azimio la Arusha pamoja na maadili ya uongozi, kufutwa kwa mfumo wa chama kimoja huku yeye mwenye akiunga mkono, na kutetereka kwa Muungano kunachipukia kutoka kwenye makubwa aliyoyaasisi.
Lakini kinyume na anavyodai mwandishi wa makala ile, Watanzania hawajashindwa kuelewa, mathalani, umuhimu wa kuishi kama Taifa na si kama mkusanyiko wa makabila yanayochukiana. Kadhalika, bado Watanzania wanapendelea kuishi bila kubaguana kidini ingawa viongozi wetu dhaifu hawalipendi hilo.
Watanzania walizielewa falsafa zake na sera zake kwa kadri ilivyowezekana ingawa ipo moja iliyowauma, nayo ni Operesheni Vijiji vya Ujamaa. Wazo lilikuwa zuri ila utekelezaji ulikuwa mbaya. Lakini pia ni kukosa busara kudai kwamba tungeendelea kuishi vile vile kama nyumbu mbugani Serengeti.
Ni uongo kudai kwamba hakuna anayekosoa mambo ya Nyerere wakati wanasiasa kama Edwin Mtei hufanya hivyo kwa heshima na wengine kama Christopher Mtikila hufanya kwa dhihaka. Watanzania wameandika kumkosoa Nyerere na sera zake, itikadi, falsafa na mengineyo nikiwemo miye binafsi lakini si lazima wawe wengi.
Mtanzania Ludovick Mwijage anayeishi Udeni alipata kuandika kitabu chake mwaka 1994 huku Nyerere akiwa hai bado, “Dark Side of Nyerere’s Legacy”, yaani kwa kutumia lugha za wanajimu, “Upande Mweusi wa Urithi wa Nyerere”. Mwaka 2008 alichapisha kingine, “Julius K. Nyerere: Servant of God or Untarnished Tyrant” akihoji iwapo Nyerere alikuwa mtumishi wa Mungu kweli au dikteta ambaye hakuchafuliwa.
Lakini kuna ukweli mmoja kwenye kumwandika Nyerere; pale inapofikia kwenye kumlinganisha na viongozi wengine waliomfuatia au wengine barani Afrika. Hapo ndipo watu wanaposita kutokana na tofauti kubwa iliyopo kati yao. Profesa Anyang Nyong’o wa Kenya alisema mwaka 1999 kwamba Nyerere hakuwa na mwenzake miongoni mwa viongozi wa Afrika wakati Profesa Ali Mazrui alisema kwamba ingawa marehemu Rais Leopold Senghor wa Senegal alikuwa na akili, na Mzee Nelson Mandela wa Afrika Kusini alikuwa mwadilifu, lakini Nyerere alikusanya vyote viwili na hakuna aliyemfikia.
Mwenyewe mwaka 1996 wakati akitunukiwa Tuzo ya Amani ya Kimataifa ya Mahatma Gandhi mjini New Delhi, India, alisema kwamba hakustahili kuipata kwa kuwa aliunga mkono harakati za ukombozi wa Afrika kwa kutumia bunduki. Hakupenda kujikweza na pengine ndiyo maana hakuandika wasifu wake, na hata mwanae aliwahi kuliambia Daily News kwamba kama baba yake angeulizwa kuhusu wazo la kumtafutia utakatifu angekataa.
Kudai kwamba Nyerere aliwapumbaza Watanzania si sahihi ingawa ni kweli kwamba aliyashikilia mengi mwenyewe kutokana na hali yenyewe ilivyokuwa enzi hizo. Aidha, hapa Afrika hakuna aliyekuwa akiijua nadharia sahihi ya maendeleo viongozi walikuwa wakifanya majaribio ila wengi wao hakuwakufika mbali wakapinduliwa.
Ni uongo wa dhahiri kudai kwamba Nyerere alistaafu mwaka 1985 kwa msaada wa masharti magumu ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Vyombo hivyo viwili viliivamia Tanzania baada ya Nyerere kuondoka madarakani na siku zote alivipinga. Ukweli ni kwamba Nyerere alishasema kwamba atastaafu tangu mwaka 1980 lakini mtikisiko wa Vita ya Kagera ukamfanya asogeze mbele uamuzi wake.
Aidha, ushauri wa vyombo hivi vya kimataifa ulituingiza kwenye shida kubwa kuliko iliyokuwapo na takwimu zipo na ndicho Nyerere alichowauliza Benki ya Dunia siku moja mjini Washington na wakashindwa kumjibu. “Mlisema sisi tulishindwa, lakini ninyi mmefanya nini sasa?” Nyerere alisema watu wa Benki ya Dunia walibaki wameduwaa.
Nyerere alipozungumza na waandishi wa kimataifa mjini London mwaka 1985 alisema kwamba anajiuzulu kwa kuwa Tanzania kuna uchaguzi, angependa kuona mtu mwingine anatawala na kwamba kama ameshindwa kuifanyia jambo nchi yake katika miaka 23 bado hataweza akipewa miaka mingine 23. Tulitaka nini zaidi ya uamuzi wake huu?
Kwamba alikuwa mtoto wa chifu mmoja asiyejulikana kutoka madongo kuinama inasaidia nini kuhoji hivyo? Kwamba alikuwa mkristo aliyependa kuvaa baraghashia ya kiislamu, tatizo lake ni nini? Je, hiyo ni baraghashia ya kiislamu au kiarabu, au ndiyo yale yale ya kuchanganya Uarabu na Uislamu? Mbona Augustine Mrema naye huivaa?
Kuhoji iwapo alikuwa mkomunisti aliyekuwa anakwenda kanisani na papo kudai kuwa aliungana na Zanzibar ili kuizuia isiingie kwenye ukomunisti ni kuchezea akili za watu. Kwamba eti huenda alikuwa muunganishi aliyetuachia Muungano wenye nyufa, je, nani kazuiwa kuziziba?
Kwamba alikuwa mmajumui wa Afrika aliyekataa katakata kuanzishwa kwa serikali moja ya Afrika ni uzushi mwingine. Nyerere alisema kwamba kwa hali halisi ilivyokuwa haikuwa rahisi kuzilazimisha nchi zinazopata uhuru ziingie kwenye muungano wa Afrika kama alivyotaka Kwame Nkrumah wa Ghana. Alisema iwapo muungano utaanzia kwenye kanda itakuwa rahisi kuliko kuburuzana.
Ni heri kwamba mwandishi amekiri kuwa Nyerere aliishi maisha ya kawaida, hakupendelea ndugu zake lakini ameshindwa kueleza upande wa pili wa faida za maamuzi yake aliyoyalaumu kama kufuta uchifu, serikali za mitaa, ushirika, vyama vya wafanyakazi na hata vyama pinzani vya siasa. Amelaumu utaifishaji wa mali binafsi, shule, hospitali na hatimaye na uanzishwaji wa vijiji vya ujamaa kwa mvurugano, kupiga marufuku maandamano na migomo na kuwasweka ndani wapinzani wake.
Lakini hali ingekuwaje kama uchifu ungedumu na kelele za ukabila? Serikali za mitaa na ushirika vilirejea na kimsingi wafanyakazi walikuwa na chama chao ingawa kilikuwa chini ya chama tawala, lakini pia utaifishaji wa mali ulifanywa kwa minajiri gani kama siyo kumsaidia mnyonge?
Ikumbukwe kuwa Waingereza hawakuacha kitu! Je, utaifishaji wa shule haukuwasaidia watoto wa Waislamu ambao waligomea shule za wamisionari wa kikrsto? Je, Watanzania masikini wangeweza kulipia gharama za matibabu kwenye hospitali za misheni bila serikali kutia mkono?
Ndiyo, kulikuwa na sheria za kikandamizaji lakini ni vema kumlinganisha Nyerere na wenzake wengine kama Ahmed Sekou Toure aliyekuwa akiwaua wapinzani wake. Abdel Nasser aliyekuwa akiwaua waandamanaji. Nkrumah aliyekuwa kama mungu-mtu. Jaffery Nimeiry aliyegoma kuwasikiliza watu wake na kisha kuwaua. Jomo Kenyatta aliyeruhusu magazeti binafsi lakini akawatesa waandishi. Idi Amin aliyekuwa akiwaua watu eti baada ya kuota kwamba watampinga siku zijazo. Nyerere hakuwa mtakatifu lakini alikuwa na utu na hata pale alipotumia nguvu alifanya hivyo akiamini anailinda Tanzania.
Madai kwamba nyaraka za Marekani zilizofunuliwa baada ya miaka mingi zinathibitisha kwamba Muungano wa Tanzania ulitokana na shinikizo la mataifa ya Magharibi ni utani mwingine. Mwaka 1966 Shirika Kuu la Intelijensia la Marekani (CIA), lilikamilisha utafiti juu ya Zanzibar katika juhudi za kuielewa na kujua Muungano ulikujaje. Mmoja wa watafiti alikuwa Helen-Louise Hunter ambaye baadaye aliandika muhtasari wa utafiti huo akisema kwamba Zanzibar haikuwa muhimu kwao. Hawakujua hata iliunganaje na Tanganyika.
Mwandishi wa vitabu, Godfrey Mwakikagile, katika kitabu chake cha mwaka 2008, “The Union of Tanganyika and Zanzibar: Product of the Cold War” yaani “Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Zao la Vita Baridi?”, anaongeza kwamba Wamarekani hawakuwahi kujisifia kwamba waliuleta Muungano huu. Anamnukuu balozi mdogo wa Marekani aliyekuwa Zanzibar, Frank Carlucci, kufuatia mahojiano yake ya mwaka 1986, akisema kwamba hajui Nyerere alipata wapi wazo la Muungano.
Carlucci hakuwa mtu mdogo nchini Marekani kwani enzi za utawala wa Rais Jimmy Carter kwenye miaka ya 1970 mwishoni alikuwa Naibu Mkurugenzi wa CIA na wakati wa Rais Ronald Reagan kwenye miaka ya 1980 alikuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Mshauri wa Usalama wa Taifa. Kwa kweli kudai kwamba Muungano huu uliletwa na Wamarekani ni ujinga wa dhahiri.
Lakini ukweli kwamba Nyerere alikuwa akisaka muungano wa Afrika Mashariki unawekwa wapi katika suala hili? Profesa Haroub Othman ananukuliwa na Mwakikagile akisema kwamba Abeid Amani Karume alipendekeza Nyerere awe rais wa Muungano, na hili nalo hatulikubali? Ndiyo, huenda watu wa Magharibi waliufurahia bila kutia mkono, lakini je, ina maana Waafrika hawawezi kuungana wenyewe?
Pengine watu wanahitaji kufuatilia historia zaidi ikiwemo ile hotuba ya Nyerere ya mwaka mpya, Januari 1, 1965 aliposema kwamba hata kama Mapinduzi yasingetokea huko Zanzibar bado Muungano ungekuja tu. Madai kuwa alikuwa anawalipa fadhila Waingereza kwa kuwa walimwokoa na uasi wa jeshi mwaka 1963, ni mzaha mwingine. Mbona alivunja uhusiano wa kidiplomasia na Uingereza mwaka 1967 kutokana na suala la Rhodesia?
Ni kichekesho kudai kuwa eti mjamaa Nyerere aliyewapinga mabepari na mabeberu angekubali ushauri wao ili aidhibiti Zanzibar isiwe ya kikomunisti. Sasa mbona alikuwa swahiba wa wakomunisti wa Kisovieti, Kuba na Korea Kaskazini na kisha akawaweka karibu akina Mengistu Haile Mariamu wa Ethiopia na Samora Machel wa Msumbiji?
Ni kweli jaribio la kujenga Ujamaa liliudhoofisha uchumi wa Tanzania lakini kudai kuwa kampuni za posta na simu, reli, na ujenzi wa barabara vilikwama kufikia mwaka 1975 ni uongo. Kwanza vyote kasoro barabara vilikuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na vimeanza kukwama miaka chungu mzima baada ya Nyerere kuondoka Ikulu. Tunashukuru sasa barabara zinaanza kurejea upya lakini reli iko chali bado.
Nyerere hakuwahi kuwaambia Watanzania wajiibie sasa anabebaje lawama zao? Pamoja na ubadhirifu ule wa fedha za umma tukiri kwamba uchumi wa Tanzania ulipatwa na mengi zaidi ya sera za Ujamaa kama vile mfumo wa kibeberu wa uchumi duniani. Lakini anastahili sifa kwa kujenga mashirika ya umma 400 mengi yakiwa ni viwanda. Mtafiti wa uchumi, John Nellis, alisema mwaka 1986 kwamba hakuna nchi yoyote ya Afrika iliyofikia hata nusu ya mashirika 400 ya Tanzania.
Aidha, misaada yote aliyopokea Nyerere ilifanya kazi zilizokusudiwa na Watanzania ni mashahidi lakini pia aliipataje mingi hivyo? Ilikuwa ngekewa tu? Nyerere hakuiba pesa zile. Mwandishi alalamikia hata haya, je, alitaka iweje? Kulikuwa na kosa gani Nyerere kuufuta ujinga kwa asilimia 92 na kuhakikisha Watanzania wanatibiwa bure?
Mwandishi anadai kuwa Vita ya Kagera ilileta maafa makubwa kwa uchumi wa taifa lakini hamchambui Idi Amin aliyeivamia Tanzania. Bila soni anasema kwamba eti mgogoro ule ungewezwa kumalizwa kwa mazungumzo! Yapi hayo?
Nyerere aliwaambia viongozi wa Afrika waliotaka kusuluhisha kwamba, kwanza wamwambie Amin aondoe majeshi yake Tanzania, halafu alipe fidia ya uharibifu alioufanya, na tatu aape kwamba hataivamia tena Tanzania. Hakuna kilichofanyika, sasa Tanzania ingemchekea mwendawazimu aliyekuwa anawaua Watanzania?
Anadai kuwa sababu ya vita ile ni Milton Obote kutaka kurejea madarakani tena, sasa mbona katika kitabu kimojawapo cha Mwakikagile, “Life Under Nyerere” cha mwaka 2006, yaani “Maisha Chini ya Nyerere”, Obote anaeleza kwamba alizuiwa na Nyerere kwenda mjini Moshi walikokuwa wanapanga nani awe rais wa muda wa Uganda baada ya Amin kukimbia? Aliteuliwa Yusuf Lule na akafuata Godfrey Binaisa, halafu Abel Muwanga kusimamia uchaguzi, na kisha Obote.
Waganda kuwa na kambi za kijeshi Tanzania haikuwa hoja kwani karibu kila taifa lililokuwa chini ya ukandamizaji lilikuwa na wapiganaji wake Tanzania. Lakini ni ukweli wa dhahiri pia kuwa wapiganaji wa Obote walianzia Sudan kwanza na wanasiasa wake walijazana Kenya. Amin aliwahi kutaka kuipiga Kenya mwaka 1976 lakini Wamarekani wakamwambia athubutu aone kilichomtoa kanga manyoya.
Lakini kuna hoja ya kitoto nyingine kwamba eti leo hii Tanzania bado inajiponya kutokana na athari za kiuchumi za vita ile, bila hata kutoa kielelezo walau kimoja. Hebu tupekue kidogo. Mwaka 1994 mwanazuoni Joyce Francis wa Chuo Kikuu cha Amerika, jijini Washington DC alifanya utafiti wa tasnifu yake ya shahada ya uzamivu kuhusiana na suala la gharama za vita hii. Alibaini kuwa hadi Juni 1979 Tanzania ilitumia vitani dola za Marekani milioni 500 za wakati ule.
Kwa kutumia kiwango cha ubadilishanaji fedha za kigeni cha enzi hizo, dola moja kwa shilingi za Tanzania 8.22, hizo zilikuwa ni sawa na shilingi bilioni 4.11. Matumizi ya serikali ya wakati huo kwa mujibu wa vielelezo vya Benki Kuu ya Tanzania, yalikuwa ni asilimia 29.46 ya Pato la Jumla la Taifa (GDP). Kwa kuwa pato lilikuwa shilingi bilioni 36.28, basi matumizi yalikuwa shilingi bilioni 10.69, kwa hiyo ile bilioni 4.11 ilikuwa sawa na asilimia 38.45 ya matumizi ya serikali kwa mwaka 1979.
Mwaka huo 1979 Tanzania iliagiza bidhaa kutoka nje zenye thamani ya wakati ule ya shilingi bilioni 8.94, ikiwa na maana kuwa gharama ya vita ilikuwa ni asilimia 45.97 ya thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje na ikumbukwe kuwa uagizaji huu haukuwa kwa ajili ya vita tu. Uwezo wetu wa kuagiza kutoka nje ulizidi gharama za vita.
Lakini pia kwa mujibu wa Umoja wa Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo (OECD), mwaka 1979 Tanzania ilipokea misaada ya dola za Marekani milioni 588, sawa na shilingi za wakati ule bilioni 4.83. Zaidi ya hapo, tuliibandika Uganda deni la dola milioni 67 ambazo ilimaliza kuzilipa mwaka 2007. Misaada ilizidi gharama za vita.
Mwaka huo huo uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 3 ambayo ilikuwa bora zaidi kuliko asilimia 1.8 ya mwaka 1969 au 1.4 ya mwaka 1994. Ni kweli kwamba mwaka 1980 uchumi ulianguka kwa nusu asilimia huku mfumuko wa bei ukifikia asilimia 30.8 lakini kwa kupima na hali ilivyokuwa kabla ya vita na kulinganisha na nchi nyingine ambazo wala hazikupigana na Amin, kutoa madai kwamba Tanzania bado inaumia na vita ile miongo mitatu baadaye ni uvivu wa kufikiri.
Lakini hebu tuangalie gharama za vita ile kwa macho ya leo. Kwa kufuata thamani ya fedha inavyobadilika kutokana na taarifa za Ofisi ya Kazi na Takwimu ya Marekani, dola milioni 500 za mwaka 1979 ni sawa na dola bilioni 1.593 za mwaka 2012 au shilingi trilioni 2.525. Bajeti ya serikali ya Tanzania leo hii ni shilingi trilioni 13.375, hivyo gharama za vita ile kwa fedha za leo ni sawa na asilimia 18.88 ya bajeti ya serikali leo hii.
Lakini kumbuka kuwa asilimia 30 hadi 40 ya bajeti hutoka kwenye misaada na huenda mwaka huu wahisani wakanuna. Je, kama tungepigana vita ile leo hii kwa gharama hizi, tungetumia zaidi ya miongo mitatu kuzilipa? Sisemi kwamba tulitumia fedha kidogo au kuchukulia mambo kirahisi kwa kisingizio cha takwimu; ninachosema ni kwamba kuendelea kudai kuwa hadi leo bado Tanzania inaumia na vita ni upuuzi mtupu.
Sidhani kwamba kampeni ya kuwadaka wahujumu wa uchumi iliyoongozwa na Edward Sokoine ilikuwa ya kubezwa kupita kiasi. Kulikuwa na sababu gani ya kuwaendekeza wahujumu uchumi? Mifano anayotoa mwandishi ni kutia chumvi bila kutoa ushahidi wowote. Kuita kampeni ile kwamba ilikuwa maafa yaliyosababisha vifo ni siasa tu.
Kwamba alipostaafu zilifanywa harakati kubwa na propaganda kuwa eti alistaafu na si kwamba aliachia ngazi kwa kushindwa, ni porojo tu. Nani walifanya kazi hiyo? Wapi?
Mwandishi amegusia suala la Biafra kwa macho ya udini kwa kuwa tu kiongozi wa harakati za kujitenga za Biafra mwaka 1969 alikuwa mkristo, Chukwuemeka Ojukwu, lakini hakusema pia kwamba hata kiongozi wa Nigeria naye alikuwa mkristo, Jenerali Yakubu Gowon.
Lakini ukweli zaidi ni kwamba Biafra iliungwa mkono pia na viongozi waislamu kama Omar Bongo wa Gabon na Habib Bourguiba wa Tunisia. Aidha, ni muhimu kufahamu ni nini hasa kiliwasibu watu wa Biafra mpaka wakataka kujitenga na Nigeria. Nyerere aliwatetea kwa sababu zile zile alizotumia kuwatetea Wapalestina dhidi ya Waisraeli.
Aidha, kuhoji kwa kebehi kwamba Nyerere alikimudu vipi Kiswahili na Kiingereza wakati hazikuwa lugha zake ni dhihaka tu. Mbona Sekou Toure alikijua Kifaransa kwa ustadi mkubwa bila kufika chuo kikuu, sembuse Nyerere aliyesomea shahada ya uzamili Uskochi? Kiswahili si kilikuwa chake pia kama watu wengine?
Madai kwamba aliishi maisha yake huku akiwaza jinsi historia itakavyomkaanga hapo baadaye hayana mantiki. Kivipi? Kuna uthibitisho? Ndiyo, ameacha msururu wa viongozi dhaifu nyuma yake na hata mbumbumbu na mafisadi, lakini miaka karibu 30 tangu atoke Ikulu bado tulalamikia tu?
Kwamba alitumia urais wake kuwanufaisha wakristo na ukristo na kwamba eti kaacha tatizo, ni madai ambayo hayana uthibitisho wowote zaidi ya kulalamika tu. Kama Nyerere alikuwa haupendi uislamu basi asingeungana na Zanzibar iliyokuwa na waislamu asilimia 98 na kisha aunde serikali na waislamu huku baraza lake la mawaziri wakiwa wengi. Tafuta rekodi za mwaka 1964. Sasa kwa nini alizitaifisha shule za wakristo? Je, waislamu hawakufaidika? Tuweni wakweli.
Aidha, mchakato wa waumini wachache wa Kanisa Katoliki kumwombea ili awe mtakatifu usiwe nongwa kwani hawajawahi kutaja kitu chochote cha urais wake bali masuala ya uumini wake kama mtu binafsi. Kumsingizia Nyerere kwamba alijenga udini Tanzania ni mzaha, na pengine tunapaswa kuzipekua nchi zilizopata nuksi ya kuwa na viongozi wa namna hiyo, mathalani Sudan au Nigeria.
Mwandishi anamalizia kwa kusema kwamba Nyerere alikufa akiwa mpweke asiye na marafiki; sasa ule umati wa watu mamilioni waliomlilia ulitoka wapi? Dunia nzima walituma salamu za rambirambi na watu wakalia kutwa kuchwa, hao marafiki ni akina nani? Haya ni madai ya kitoto.
Ni kweli chama chake kimetupilia mbali misingi ya uongozi ya Azimio la Arusha lakini sasa wanalikumbuka. Ni kweli kwamba Tanzania imeingia katika vyama vingi lakini naye alishiriki vema kuubadili mfumo muda ulipowadia. Ni kweli kwamba Muungano una matatizo lakini ni muungano gani duniani usiokuwa na shida zake?
Kama suala ni kuheshimu ukweli, basi hakika Nyerere hakuwa kitendawili.
No comments:
Post a Comment