WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, November 1, 2012

Dk Nagu azidi kupingwa, UVCCM hali bado tete


Waandishi Wetu
ALIYEKUWA mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Agustine Matefu amewasilisha vielelezo kwa viongozi wakuu wa chama hicho, akishinikiza kutenguliwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Wakati vielelezo hivyo vikiwasilishwa, wanachama wa CCM, wilayani Hanang’ wamemwandikia Katibu mkuu wa chama hicho, wakipinga matokeo ya uchaguzi wa kiti cha mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa katika wilaya hiyo yaliyompa ushindi, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu.
Matukio hayo mawili yamekuja huku kukiwa na malalamiko mengi kwamba uchaguzi wa CCM na jumuiya zake, ulitawaliwa na vitendo vya rushwa, kitendo kinachowafanya walioshindwa washinikize kutenguliwa kwa matokeo yote.

Vielelezo vya kuthibitisha namna uchaguzi wa UVCCM ulivyovurugwa, vimesainiwa na saini za wajumbe 379 wanaopinga matokeo.

Vielelezo hivyo ni pamoja na CD mbili za video zenye sauti zinazoonyesha ukiukwaji wa sheria za uchaguzi baada ya kutawaliwa na rushwa.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akifungua rasmi mkutano mkuu wa UVCCM, mwishoni mwa wiki iliyopita, aliwaambia wajumbe kwamba “watajuta” ikiwa watachagua viongozi kwa misingi ya rushwa.

“Nawaambieni, mkifanya mchezo ipo siku mtakuja kujuta maana mkishamchagua kiongozi asiyefaa, mtalazimika kuwa naye huyohuyo hadi mwaka 2017 na kama waswahili wanavyosema majuto ni mjukuu,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Matefu alisema amewasilisha vielelezo hivyo kwa Rais Kikwete, Katibu Mkuu, Wilson Mkama, UVCCM na Kamati ya Maadili ya CCM.
Matefu ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka katika Mkoa wa Morogoro alisema mwenyekiti wa chama, anapaswa kutengua matokeo hayo kwa kuwa uchaguzi ulikithiri kwa vitendo vya rushwa.

Alisema katika uchaguzi huo wajumbe waliopiga kura walizidi nusu ya wajumbe wote 700 walioshiriki uchaguzi huo.

Alisema jina lake liliondolewa katika mazingira ya kutatanisha na kwamba kitendo hicho kilifanywa na baadhi ya makada wa UVCCM.

“Endapo hakutakuwa na hatua itakayochukuliwa na mwenyekiti, basi sisi tutakwenda katika Mkutano Mkuu wa Chama Taifa (NEC) utakaofanyika Novemba 6 mwaka huu kupinga usifanyike hadi pale hatua itakapochukuliwa,” alisema Matefu.

Matefu alikiri kuwaandaa vijana waliojitokeza wakiwa na mabango ya kupinga ushindi wa mwenyekiti mpya wa UVCCM, wakati utambulisho wa ugeni huo katika ofisi za makao makuu ya UVCCM.

Sherehe za kuwakaribisha viongozi wapya ziligeuka uwanja wa vita baada ya makundi yanayopingana, kuchapana makonde hadharani na kuwaacha umati wa watu wakiwashangaa.

Wiki iliyopita, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa UVCCM mjini Dodoma, kundi la vijana kutoka mikoa mbalimbali walipinga vitendo vya rushwa huku wakiwatuhumu viongozi wa UVCCM na baadhi ya makada wa chama hicho kwa kuhusika.

Waliotajwa ni pamoja na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo, Beno Malisa, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, Hussein Bashe na Fredy Lowassa.

Matefu alisema CD hizo zinawabainisha Bashe, Malisa na Shigela kuwa wahusika wakuu wa vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo.

“Malisa na Shigela waligawa Sh1 milioni kwa wajumbe ambao walikuwa wapigakura kitendo ambacho kinakiuka kanuni na sheria za uchaguzi,” alisema Matefu.

Hivi karibuni, Bashe alinukuliwa na gazeti hili akikanusha tuhuma hizo akisema si za kweli.

“Mimi sijatumwa na Lowassa, wala sifanyi kazi na Lowassa. Nafanya kazi ya CCM, lakini nampenda sana Lowassa kwa sababu ni mmoja wa viongozi na makada wa chama, ambao wameonyesha mapenzi ya dhati kwa CCM na uvumilivu wa hali ya juu,” alisema kada huyo.

Katika uchaguzi huo Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamisi aliibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM, baada ya kupata kura 483 dhidi ya Rashid Simai Msaraka aliyepata kura 263.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Mboni Muhita alishinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 489 na kumtimulia vumbi mshindani wake, Paul Makonda aliyepata kura 241.

Wakati huohuo wanachama wa CCM wilayani Hanang’ wamemwandikia Katibu mkuu wa chama hicho wakipinga matokeo ya uchaguzi wa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa wilaya hiyo yaliyompa ushindi, Dk Nagu.


Katika barua yao wanachama hao 11 wamesema uchaguzi huo ulitawaliwa na mazingira ya rushwa, kuvunja taratibu za uchaguzi na kwamba matokeo yanapaswa kutenguliwa na uchaguzi kurudiwa.
“Kwa niaba ya wajumbe wenzetu, tunawasilisha kwako pingamizi juu ya uchaguzi uliofanyika Desemba 28 mwaka huu hapa Hanang’ kwa nafasi ya ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC)” ilisema sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Mkama na kuzitaja sababu za kupinga kwao kuwa ni pamoja na kushamiri kwa vitendo vya rushwa vilivyodhihirika tangu hatua ya mwanzo wa uchukuaji fomu mpaka siku ya uchaguzi.
Wanachama hao wamedai kuwa Dk Nagu alikusanya wajumbe pamoja na wanachama wengine na kufanya nao mkutano kwenye eneo la Katesh ambako pia aliwakabidhi matrekta baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya.
Sababu nyingine zilizoorodheshwa na wanachama hao ni pamoja na mshindi huyo kuzunguka katika maeneo na kuwatisha wananchi kuwa kama hatachaguliwa kwenye nafasi hiyo basi wilaya hiyo isitegemee misaada yoyote toka kwake.
.
Kadhalika mgombea alitumia nyadhifa zake kama mbunge na waziri kuwaita wajumbe nyumbani kwake na kufanya nao mikutano ya mara kwa mara.”
.
Katika uchaguzi huo, Nagu alikuwa akichuana na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ambaye baada ya kushindwa naye alilalamikia vitendo vya rushwa vilivyotawala katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Imeandikwa na Raymond Kaminyoge na Ibrahim Yamola wa Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment