Yadaiwa kuna njama kuitenganisha na urais
Wakati wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakitarajiwa kuanza kuwasili leo mjini hapa kwa ajili ya uchaguzi wa safu ya uongozi wa chama hicho kwa miaka mitano ijayo, taarifa za uvumi zimeaanza kusambaa kwamba baadhi yao wanataka kufanya mabadiliko ya nafasi ya uenyekiti.
Habari hizo ambazo zilianza kusambaa juzi na jana na kushika kasi zaidi zinasema kuwa wajumbe wa mkutano huo kutoka mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga wanadaiwa kuhongwa Sh. milioni 3 kila mmoja ili kulikataa jina la Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, ambalo linatarajiwa kupendekezwa na Kamati Kuu (CC) ili awe mgombea pekee wa nafasi hiyo.
Taarifa kutoka vyanzo vyetu vya kuaminika zinaweka bayana kuwa wajumbe hao walifanya kikao hicho pamoja na mgawo huo wa fedha nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa CCM mkoani Shinyanga, Jumanne wiki hii.
Habari hizo zinadai kuwa mpango huo pia unamhusisha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja.
“Wanashawishi wajumbe kulikataa jina la Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete ambalo linatarajiwa kupendekezwa katika Necna Kamati Kuu. Hoja wanazotaka kutumia ni kwamba eti mwenyekiti anazo shughuli nyingi na kwa hiyo lipendekezwe jina la mwenyekiti mwingine baada ya Kikwete kukataliwa,” kilisema chanzo hicho ambacho kilionyesha kuchukizwa na mpango huo na kuongeza:
“Tatizo lao wanashindwa kuelewa kuwa mtendaji wa chama katika shughuli za kila siku si mwenyekiti, bali ni Katibu Mkuu na Sekretariati ya Chama kwa ujumla. Kwa hiyo hoja yao haina mashiko. Tangu wakati wa Mwalimu Nyerere utaratibu ndio huo utendaji unafanywa na sekretariati kwa hiyo kama ni suala la hoja ya shughuli nyingi maana yake sekretariati ndiyo dhaifu.“
Tangu uongozi wa Mwalimu Nyerere, nafasi ya Rais imekuwa ikienda sambamba na ya uenyekiti wa chama lengo likiwa kuepusha mgongano.
KAULI YA MGEJA
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Mgeja, alisema kuwa huo ni mchezo mchafu unaofanywa na kundi linalotaka kuwachafua baadhi ya watu ili kumchonganisha na Rais Kikwete.
“Huu ni mchezo mchafu unaofanywa na makundi kutuchonganisha na bwana mkubwa (Rais Kikwete), kuna vyombo kama Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), wapo Usalama wa Taifa wafanye uchunguzi kuhusiana na jambo hili,”alisema Mgeja ambaye pia ni Mjumbe wa Nec na kuongeza kuwa:
“Watanzania wasiamini katika mambo haya. Huu ndio msimu wa udalali ambao kuna kuchafuana na kuchonganisha watu wengine kwa manufaa ya makundi yao…mimi sina shida ya hizo Shilingi milioni tatu.”
Alisema kuwa: “Hakuna hoja kama hiyo, Mwenyekiti anaweza kufanya kazi zake zote vizuri…niko tayari kujiuzulu nafasi zangu zote ikiwa uchunguzi wa Takukuru na Usalama wa Taifa utabaini kuwa nilikuwa mmoja wa watu waliokuwa katika mpango huo.”
Mgeja aliponea kwenye tundu la sindano katika kikao cha Nec kilichoteua majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.
Hatua hiyo ilitokana na Kamati ya Maadili na CC kulikata jina lake katika majina ya wagombea uenyekiti wa chama hicho mkoani Shinyanga.
NAPE: NA MIMI NIMESIKIA
Alipoulizwa kuhusiana na Mpango huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema: “Hata mimi nalisikia kwa baadhi ya watu kama unavyosikia wewe, lakini kama lipo jambo hilo si zuri…lakini huo ni uvumi tu wa mitaani.”
Tangu kuanza kwa uchaguzi wa ndani wa CCM, tuhuma za rushwa zimekuwa zikisikika na hatua zinazochukuliwa zimekuwa si za kuridhisha licha ya Takukuru kupewa idhini na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete kufanya kazi yao bila hofu.
Rais Kikwete alitoa idhini hiyo kwa Takukuru alipokuwa akifungua kikao kilichopita cha NEC kilichofanyika mjini hapa.
Chaguzi ambazo hadi sasa zimelalamikiwa na baadhi ya wanaCCM kuwa zimegubikwa na rushwa ni pamoja na uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM), Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM na Jumuiya ya Wazazi.
Katika chaguzi hizo, Sadifa Juma alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Sophia Simba Mwenyekiti wa UWT na Abdallah Bulembo Mwenyekiti wa Wazazi.
CCM inatarajiwa kufanya mkutano wake mkuu kuanzia Jumapili wiki hii na kukamilika Jumanne, wiki ijayo.
Katika mkutano huo, safu mpya ya viongozi wa CCM inatarajiwa kutangazwa.
Watakaochaguliwa ni wajumbe wa Nec 10 kutoka Tanzania Bara na 10 kutoka Visiwani. Wengine ni Mwenyekiti na Makamu mwenyekiti wawili mmoja kutoka Bara na mwingine Visiwani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment