WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, November 5, 2012

Prof. Lipumba ajitosa Kutatua mzozo wa dini


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameingilia kati mvutano kati ya Waislamu na serikali na kusema ataendelea na jitihada za kutafuta fursa ya kuzungumza na Rais Jakaya Kikwete, viongozi wa asasi za Kiislamu na Kikristo ili kutafuta suluhu.

Profesa Lipumba alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, ikiwa ni siku mbili tangu jitihada zake za awali za kuwashawishi Waislamu kutoshiriki katika maandamano baada ya swala ya Ijumaa wiki iliyopita, kufanikiwa. 

Mandamano hayo yalilenga kupinga kukamatwa kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (Baraza Kuu), Sheikh Ramadhan Sanze, pamoja na waumini wengine kadhaa wa dini ya Kiislamu.

“Katika kutafuta suluhu ya mtafaruku huu nitaendelea na jitihada za kutafuta fursa niweze kubadilishana mawazo na Rais Kikwete. Nitazungumza na viongozi wa asasi za Kiislamu. Nitazungumza na viongozi wa makanisa ya Kikristo,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema madhumuni ya mazungumzo yake na Rais Kikwete na viongozi hao wa dini, ni kuwafahamisha mantiki ya juhudi alizofanya na kushauriana misingi muhimu ya waumini wote kuheshimiana na kuvumiliana ili kujenga Tanzania yenye haki sawa kwa wote.

Profesa Lipumba alisema jana alipata fursa ya kuzungumza na Rais Kikwete na kumueleza juhudi alizozichukua kupunguza jazba na kuwaomba Waislamu kutoshiriki kwenye maandamano baada ya swala ya Ijumaa.

“Ni wazi hali hii ya mtafaruku ndani ya jamii inamsononesha sana Mheshimiwa Rais na ninaamini atajitahidi kwa uwezo wake wote kutafuta suluhisho,” alisema Lipumba.

Alisema anasikitika sana katika kipindi hiki tete, viongozi wa serikali wameshindwa kuchukua juhudia za makusudi kuzungumza na maimamu wa misikiti na viongozi wa asasi za Kiislamu kupunguza jazba.

Aliitaka serikali kutumia busara na kuwasiliana na maimamu wa misikiti na viongozi wa asasi za Kiislamu kuelewa hoja na malalamiko yao.

Alisema kushamiri kwa demokrasia ya kweli, msingi wake mkubwa ni amani na utulivu na kwamba, amani ya kweli haipatikani bila kuwapo haki.

Lipumba alisema baadhi ya watu wamemkosoa na kushauri kuwa ilifaa asubiri mpaka baada ya maandamano kufanyika na kama pangetokea majeruhi na vifo ndipo angetoa tamko la kulaani vitendo vya polisi na serikali.

Alisema katika mitandao ya kijamii, baadhi ya watu wamekejeli juhudi zake hizo, huku wengine wakihoji kuna agenda gani kati ya CUF na Uislamu?

“Mtaani leo wanasema kauli ya Lipumba ya jana (Ijumaa wiki iliyopita) kusitisha maandamano wameitii, na ukiangalia mikutano yake pale Jangwani utafikiri kuna mawaidha ni balaghashia na baibui,” alinukuu Profesa Lipumba.

Alisema jibu la hoja ni wazi, kwani CUF inasimamia haki sawa kwa wananchi wote na kwamba, kuna Watanzania wengi, ambao ni Waislamu na wao pia wanastahiki kutendewa haki katika nchi yao.

Mbali na kuwashawishi Waislamu kutoshiriki maandamano hayo, Profesa Lipumba pia alifanikiwa kulishawishi Jeshi la Polisi kumwachia huru Sheikh Sanze, aliyekuwa akishikiliwa na jeshi hilo, Alhamisi wiki iliyopita, hali iliyozua jazba miongoni mwa waumini wa Kiislamu na kutishia kuandamana kupinga hatua hiyo.

Profesa Lipumba alisema alizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, na ushawishi wake (Profesa Lipumba) ulizaa matunda na Sheikh Sanza na wenzake wakaachiwa.

“Ninakiri kuwa katika mazungumzo ya simu, IGP Mwema alikuwa msikivu na mkarimu sana katika kauli yake. Alinishukuru kwa kauli niliyoitoa katika vituo vya televisheni na kuwa atafuatilia suala nililomueleza. Hatimaye Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake waliachiwa,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Naamini kama Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wangeachiwa ingesaidia sana kupunguza jazba. Hata hivyo, Waislamu wengi na wananchi wengine kwa jumla walipokea vizuri wito wangu na hawakushiriki katika maandamano.”

 lisema awali, aliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, na kubaini kuwa suala la kukamatwa kwa Sheikh Sanze halikuwa chini ya uamuzi wake na lingekamilishwa siku zijazo.

Profesa Lipumba alisema usiku wa kuamkia Ijumaa wiki iliyopita, alijaribu kuwasiliana na Rais Kikwete kupitia wasaidizi wake ili kumfahamisha mantiki na sababu ya hatua alizozichukua na atumie uwezo alionao ili Sheikh Sanze na wenzake waachiwe.

“Kwa bahati msaidizi mmoja alipata ujumbe wangu wa simu na akanipigia simu saa 6.50 usiku na kunifahamisha atajitahidi kuufikisha ujumbe wangu kwa Mheshimiwa Rais ili nipate kuongea naye kuhusu jamaa wanaoshikiliwa na polisi waachiwe ili kupunguza jazba na kuepusha shari,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Niliyezungumza naye alikuwa Dodoma na Rais alikuwa Arusha na ratiba yake ilikuwa imebana sana na kwa hiyo hakuweza kupata fursa ya kunipigia simu siku hiyo ya Ijumaa…Nami katika kuhangaika ili waliokamatwa waachiliwe nilipata fursa ya kuzungumza na IGP na kumfahamisha sababu ya juhudi nilizochukua na mategemeo yangu kuwa Sheikh Sanze na wenzake wangeachiwa.”


 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment