Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza furaha na shangwe yake kufuatia ushindi wa jana, Jumanne, Novemba 6, 2012 wa Rais Barack Obama wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.
Katika salamu zake za pongezi kwa kiongozi huyo wa Marekani ambaye amechaguliwa tena na wananchi wa nchi hiyo kwa kipindi cha pili, Rais Kikwete amesema mapema leo, Jumatano, Novemba 7, 2012:
Rais Barack Obama akisheherekea ushindi wake dhidi ya mpinzani wake, Bw. Mitt Romney, na kuwa Rais wa Marekani kwa kipindi cha pili.
“Nimepokea kwa furaha na shangwe habari za kuchaguliwa tena kwako kuwa Rais wa Marekani kwa kipindi cha pili. Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa hakika, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukutumia wewe na kupitia kwako Chama cha Democratic pongezi nyingi kwa ushindi wako wa maana sana.”
Ameongeza Rais kikwete katika salamu zake hizo: “Kuchaguliwa kwako tena kuendelea kuongoza nchi yako muhimu na wananchi wake, ni ishara ya wazi ya uaminifu na imani ambayo wananchi wa Marekani wanayo katika uongozi wako wa mfano.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Wakati unajiandaa kuchukua tena uongozi wa nchi hiyo katika kipindi chako kipya, napenda kukuhakikishia msimamo wangu binafsi na ule wa Serikali yangu kuwa tutaendelea kufanya kazi kwa karibu kabisa na wewe na Serikali yako ya kutukuka, ili kuendeleza uhusiano bora ulioko kati ya nchi zetu mbili ndugu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu .
Dar es Salaam .
Ikulu .
Dar es Salaam .
7 Novemba, 2012
No comments:
Post a Comment