Na Salma Said
Siku ya Oktoba 6 mwaka huu kulifanyika Kongamano la wazi la kujadili mustakabali wa Zanzibar wakati wa mchakato wa utoaji maoni kuhusu katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kongamano lile walipokuwepo wanasiasa vijana wa Zanzibar, wenye kuvuta hisia za wengi, hao si wengine ni Mansoor Yussuf Himid na Ismail Jussa Ladhu. Lakini aliyefunika kongamano hasa ni Askofu wa Kanisa la Anglikan la Mkunazini Zanzibar Emmanuel Masoud.
Masoud alisema upepo wa mabadiliko hauwezi kurudhishwa nyuma na ikiwa wazanzibari wanahitaji kupewa fursa ya kuwa huru kwa nini wanazuiliwa wakati katika dunia ya sasa hakuna kulazimishana katika masuala ya utawala.
Askofu huo aliwakosha sana washiriki wa kongamano hilo ingawa awali kama kawaida ya wazanzibari ambao silimia kubwa ni waislamu wamekuwa na shaka juu ya wenziwao wakristo wakiamini kila mkiristo ni mtetezi wa Muungano lakini hali isivyotegemewa alipopanda jukwaani na kukamata kiriri Askofu Masoud alishangiriwa baada ya kuungana na wazanzibari wenzake na kudai Zanzibar huru kitaifa na kimataifa.
“Ni Jambo la ajabu sana kuona wazanzibari wakitaka kuwa na nchi yao halafu wasipewe ….wazanzibari wana madai yao ya msingi na hivyo lazima wasikilizwe na wasiposikilizwa tunaweza kuingia katika matatizo kwani wakati umefika Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili” alisema Askofu Masoud na kushangiriwa na ummati mkubwa uliofurika katika ukumbi huo.
Ingawa kila mchangiaji alipewa dakika kumi lakini dakika chache hizo watoaji mada walizitumia vyema ili kukidhi haja ya ukumbi ambapo baada ya kujitambulisha Askofu alijiita yeye ni Mpemba na anatambulika hivyo pale kanisani Mkunazini kwani yeye alizaliwa Pemba na hivyo kuzidi kuvuta hisia za wazanzibari wengi waliopo pale katika kongamano.
Watu wengine waliongara katika kongamano hilo wakawa ni wanasiasa hawa ni wanachama wa vyama tofauti, Mansoor CCM na Jussa CUF, lakini wanaunganishwa na uzalendo wa kizanzibari juu ya nchi ya uzao wao. Na licha ya hoja zao wanazotoa lakini wameweza kuwavuta wazanzibari wengi katika medani za siasa wakiwemo watu wa rika tofauti.
Aliyeanza kufungua dimba ni Mansoor ambaye aliwataka wazanzibari kutokuwa wepesi kuwanyooshea vidole wao kwa wao kwa sababu ya tofauti ya mawazo juu mfumo wa muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mansoor aliwataka wazanzibari na hasa vijana kuzungumza kwa uwazi na tena bila ya woga hasa katika mustakbali wa nchi yao katika Muungano.
Alishangazwa na baadhi ya wanasiasa tena wengine ni viongozi wakubwa wanaosimama na kusema hadharani kuwa “mkiutaka msiutake Muungano ndio huu huu” kuwa wanakosea kwani hakuna mwenye haki ya kumlazimisha mtu juu ya anachokitaka mwenyewe.
“Iweje leo baadhi ya viongozi wawatishe wananchi juu ya mustakbali wa nchi yao” Alihoji huku akishangiliwa na umati uliosheheni ukumbi wa salama pale Bwawani Hotel.
Pengine hoja ya mwanasiasa huyu ni kuwa Wazanzibari wanahitaji umoja zaidi kuliko kitu chengine chochote hususan katika wakati huu wa mchakato wa maoni ya Tume ya Jaji Wariona juu ya katiba mpya.
Je, Mpaka lini Wazanzibari tutakubali kugawiwa. Kwa nini viongozi wetu wa kisiasa badala ya kuweka maslahi ya Zanzibar mbele, wao wanaweka mbele maslahi yao au maslahi ya vyama vyao? Hayo ndio yalikuwa maneno ya Mansoor bila ya kuyatafuta na akaongeza kwamba.
“Msiogope kusema wala kuondoshwa katika nafasi zenu ikiwa umakamu wa raia utaupata tu ….” alisema bila ya kutafuna maneno.
Mansoor ambaye wakati huo alikuwa ni waziri ambapo sasa ameondoshwa katika wadhifa wake huku sababu kubwa ikidaiwa ni kauli yake aliyoitoa katika kongamano hilo lililofanyika Bwawani Hoteli na kurushwa moja kwa moja na baadhi ya vyombo vya habari nchini.
Alisema inafaa Wazanzibari tukaelewa kuwa huu si wakati mwafaka wa kupingana wenyewe kwa wenyewe. Huu si wakati wa kutazama maslahi ya mtu binafsi wala chama! Ni wakati wa kutazama maslahi ya Zanzibar kwanza na mustakabali wa Wanzanizbari.
Tuacheni tabia ya kushughulikia mambo madogo madogo ambayo hayana manufaa kwetu wala kwa kizazi chetu, twendeni pamoja katika yale mambo ya msingi kama hili la kutaka mabadiliko ya mfumo wa muundo wa Muungano.
Rais wa awamu ya pili Zanzibar, Al-Hajj Aboud Jumbe Mwinyi alilazimishwa ajiuzulu uongozi kwa kudai serikali tatu. Na baadhi ya Wazanzibari walisherehekea kufukuzwa kweke. Lakini Rais wa Zanzibar, aliyechaguliwa na Wazanzibari kwa kura anakuja kuondoshwa madarakani na kikao cha CCM cha NEC chenye wajumbe kiasi cha 200 tu! Niajabu! Wazanzibari hawalioni hilo.
Umefika wakati Wazanzibar tuache jazba, tuache ubinafsi, vyama vyetu tuviweke kando na tuungane katika kupigania maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano. Hakuna anayepinga muungano, lakini tunapinga kuburuzwa na mfumo dhaifu wa muundo uliopo ambao unaifanya Zanzibar kuwa kama mgeni mwalikwa katika Muungano.
Ndipo akina Mansoor walipoeleza kwa kina ulazima wa kuvumiliana katika tofauti ya mawazo, tofauti ya itikadi ya kisiasa, lakini pia katika madai ya haki za Zanzibar na mustakabali wake suala hilo halina dini, halina siasa wala kiongozi, kila mmoja anawajibu na haki.
“Si kila lililozungumzwa hapa mkakubaliana nalo, wapo wanaotofautiana nami, lakini nanyi mnapaswa kuwavumiliana wengine ambao hawatakubaliana na mawazo yetu, kwa hivyo tuheshimu haki ya kila mmoja,tuheshimu sheria na tutumie busara zaidi kuliko kutawaliwa na hisia za kijazba” alisema Mansoor.
Anazungumziaje kuhusu mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete katika kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar?
“Kwa hakika mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, anastahiki kila aina ya pongezi na sifa kwa ushupavu wake kushughulikia mpasuko wa kisiasa Zanzibar”
Mansoor anamtaja Rais Jakaya Kikwete kuwa ni kiongozi mkweli, makini, jasiri na mwenye upeo mkubwa akiwa ndio muasisi wa maridhiano ya kisiasa Zanzibar hadi kufanikiwa kwake na leo Wazanzibari wanaishi kwa amani na kuheshimiana.
“Kati ya Marais wote waliopita ni yeye aliyethubutu kusema hadharani tena kwa kichwa kipana kwamba anasononeshwa na mpasuko wa kisiasa Zanzibar na kuahidi kuutafutia dawa, kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa yaliyohitimishwa kwa kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni juhudi zake Rais Kikwete,Waziri Mansoor aliwakumbusha washiriki wa Kongamano la wiki iliyopita.
Hakuwa Waziri Mansoor bali washiriki wa kongamano nao hawakufanya khiyana kumwagia sifa Rais Kikwete kwani amekuwa mkweli wa ahadi yake ya kuheshimu haki za binadamu na amekuwa na dhamira ya dhati kuimarisha uhuru wa Watanzania.
Wanakongamano wamesema kitendo cha Rais Kikwete kukubali mchakato wa katiba mpya,viongozi wa kisiasa hususan wale wa CCM wanapaswa kumheshimu Mwenyekiti wao na kuwaachia wananchi kutoa maoni yao bila vitisho na masharti kwani hatuwezi kupata katiba na mfumo wa muundo Muungano iliyoridhiwa na Wazanzibari wote.
Wanasema kinyume chake tutaendelea kuwa na mfumo wa Muungano usiotakiwa. Wazanzibari wale kike kwa kiume wakasisitiza kwamba uhuru mpana wa kutoa maoni utaleta hali halisi hiyo itawapa fursaviongozi wa kisiasa kufanya maamuzi sahihi kwa niaba ya wananchi hali ambayo itaimarisha Muungano wetu.
Waziri Mansoor akasema ipo haja ya kuwa na Muungano wa mkataba ili kuondokana na malalamiko mengi ambayo yanalalamikiwa katika mfumo wa muundo wa sasa wa Muungano na kusisitiza bado ataendelea kuwa muumini wa mfumo wa Serikali mbili chini ya muundo wa Muungano wa mkataba mfumo ambao utaipa fursa zaidi Zanzibar kujijenga na kujitegemea kiuchumi.
Mzee Hassan Nassor Moyo hakuwa nyuma katika kongamano hilo kwani ni yeye aliyeanza kufungua dimba kwa kueleza kwanini leo anataka mabadiliko ya mfumo wa muundo wa Muungano, anasema mfumo wa sasa hauwezi kukidhi haja ya kizazi za leo na cha baade hivyo kuna haja ya kukubali mabadiliko ya mfumo kwa kuwa na Muungano wa mkataba baina ya Tanganyika na Zanzibar.
Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Salim Rashid akasema kwa uelewa wake ni kwamba mazingira ya wakati ule ya kuundwa kwa Muungano yalikusudiwa kuidhibiti Zanzibar kwani Mataifa ya nje hasa ya Magharibi yalikhofia Zanzibar kugeuka Cuba ya Afrika.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa yeye ameungana na wasemaji wengine waliomtangulia, lakini alitoa angalizo la Tume ya Jaji Warioba inayokusanya maoni ya wananchi kutofanya kinyume na matakwa ya Wazanzibari watakavyotoa maoni yao.
Jussa alisema maoni ya Wazanzibari hayana budi kubaki kama yatakavyotolewa katika mikutano ya Tume na kwamba ikiwa kutakuwa na uchakachuaji basi wajumbe wa Tume waelewe kuwa watabeba dhima mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kimsingi wengi wanakubali kwamba kongamano lile limetoa picha ya hali halisi ya hisia za Wananchi kutaka mabadiliko ya mfumo wa muundo wa Muungano wakitaka uwepo ule wa mkataba badala ya huu wa kikatiba ambao hautoi fursa sawia kwa Zanzibar kujiamulia mambo yake wenyewe kama kuingia mikataba ya kimataifa na mambo mengine.
Hata hivyo, wapo baadhi ya watu ambao hawaungi mkono vuguvugu la mabadiliko ya mfumo wa muundo wa Muungano, hawa wanasimamia nguzo za vyama vyao si utashi wao wala hisia zao,bali wanaongozwa na sera za vyama vyao vya siasa hata kwa mfano vyama vyao vikiwaelekeza sipo wao watafuata ilimradi ni Chama kinachotaka.
Siku za mwanzoni mwa harakati za madai ya wanamageuzi hawa ndio waliokuwa wakitamba kwamba wao ndio wanahaki zaidi na wana uchungu zaidi na nchi hii kuliko Wazanzibari wengine. Kwa tafsiri nyengine ni kwamba hawa hawachelewi kuyaelekeza mambo kule wanapopataka wao hata kama ni kinyume na hali halisi.
Nimeandika sana huko nyuma kwamba suala la mfumo wa muundo wa Muungano sio la Vyama vya siasa maana zilizoungana ni nchi mbili huru,iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ndizo zilizoingia mkataba wa kuunganisha Mataifa yao iweje leo hoja ya mabadiliko ya muundo wa Muungano iwe ya vyama vya siasa?
Waumini wa demokrasia wanaamini vitendo vya viongozi wa kijamii katika nafasi yoyote ile kinatakiwa kudhihirisha matakwa ya wananchi na sio yale matakwa wanayoyataka wao?
Nguzo muhimu ya demokrasia ya kweli ni pamoja na kuvumiliana katika maoni tofauti ya kisiasa na kwamba maoni ya kisiasa ya wananchi ni lazima yasikilizwe na haki zao za msingi kuheshimiwa?
Baadhi ya watu wanadhani kwamba wao wakisema chochote, hicho ndio huwa ‘sadakta’, lakini akisema mwingine asiye ‘mwenzao’, huyo hupewa majina ya kumkosanisha na jamii, watampakazia kuwa yeye “msaliti, Hizbu-ZNP, mchochezi” hakitakii mema Chama, “anataka kuvunja Muungano, msaliti wa Mapinduzi, anachanganya dini na siasa” na mengineyo.
No comments:
Post a Comment