Muda uliotolewa kwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kumaliza kazi yake ya kutayarisha Rasimu ya Pili ya Katiba
Mpya na kuikabidhi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa
unakaribia ukingoni.
Baada ya Rais Kikwete kuiongezea Tume
hiyo muda wa mwisho wa wiki mbili hivi karibuni, sheria inaitaka Tume
hiyo iwe imewasilisha Rasimu hiyo kwa mamlaka husika katika kipindi cha
siku 60, ambazo zinamalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Itakumbukwa kwamba mara ya kwanza Tume
hiyo iliongezewa muda wa siku 45 mwezi Oktoba, mwaka huu. Kwa kuwa sasa
imeongezewa wiki mbili, maana yake ni kwamba itakuwa imeongezewa jumla
ya siku 59. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 iliyounda Tume
hiyo inasema Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza kuiongezea Tume hiyo
muda usiozidi siku 60.
Hivyo, kisheria siku ya mwisho ya
kukabidhi Rasimu hiyo ni Desemba 30 na Rais hana tena mamlaka kisheria
ya kuiongezea muda Tume hiyo nje ya siku hizo 60.Kwa maana hiyo, Tume
lazima ifanye kazi usiku na mchana kuhakikisha inamaliza kazi zake
katika muda huo.
Kwa kuwa Bunge Maalumu la Katiba
linakutana mwanzoni kabisa mwa mwaka ujao kuijadili Rasimu hiyo na
kufanya marekebisho yatakayowezesha kupatikana kwa Rasimu ya Tatu ya
Katiba kabla haijapigiwa Kura ya Maoni, hakuna tena uwezekano wa
kuiongezea Tume muda zaidi, hata kama Bunge lingekuwa tayari kukutana
kwa dharura kuifanyia marekebisho Sheria hiyo ya Mabadiliko ya Katiba ya
mwaka 2013.(P.T)
Hiyo ndiyo changamoto kubwa
inayoikabili Tume hiyo hivi sasa. Sote tunajua kuwa, mara ya kwanza
iliomba kuongezewa muda na kupewa siku 45 baada ya kutingwa na kazi ya
kuratibu na kuchambua maoni ya wananchi waliojitokeza kwa wingi kutoa
maoni kuliko ilivyotarajiwa.
Mara hii imeomba muda zaidi na kupewa
wiki mbili, baada ya mjumbe wa Tume hiyo, Dk Sengondo Mvungi kuvamiwa na
kujeruhiwa vibaya na majambazi na baadaye kufariki dunia.
Kifo cha ghafla cha Dk Mvungi
kilisababisha kusitisha kazi za Tume, kwani kwa zaidi ya wiki mbili
ndiyo iliyokuwa ikiratibu shughuli zote za matibabu yake ndani na nje ya
nchi na baadaye maziko.
Alikuwa kitovu na mmoja wa mihimili
mikubwa ya Tume, kiasi kwamba yeye kama mwanasheria wa kipekee na nguli
katika masuala ya katiba ndiye aliyekuwa akitegemewa na Tume katika
utayarishaji wa Rasimu zote mbili za Katiba Mpya. Tume siyo tu
ilitikiswa na kifo hicho, bali pia ilighadhabishwa na upotevu wa
kompyuta yake iliyoporwa na majambazi ikiwa na kumbukumbu muhimu kuhusu
mchakato huo wa Katiba Mpya.
Hiyo ndiyo hali ya kusikitisha
inayoikumba Tume hiyo. Hapana shaka kwamba kuiongezea muda Tume hiyo
hakukutokana na uzembe kwa upande wake, bali mazingira yaliyojitokeza
bila kutazamiwa na kuathiri kazi zake kwa namna moja ama nyingine.
Kwa vile bado ni mapema mno tangu kifo
cha Dk Mvungi, hatutarajii wajumbe wake kuwa na hali ya utulivu
kisaikolojia kutokana na kumpoteza mwenzi wao huyo.
Hata hivyo tunawasihi wapige moyo
konde na kurudi kazini ili waweze kuwasilisha serikalini Rasimu ya Pili
ya Katiba Mpya muda uliopangwa. Matumaini yetu ni kwamba wananchi wote
watawaunga mkono.
source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment