WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, December 11, 2013

Machozi ya Marais kwa Tata Mandela

Rais wa Marekani, Barack Obama akitoa hotuba jana MjiniAfrika Kusini wakati akitoa heshima za za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hayati Nelson Mandela.
Viongozi wakuu wa dini na siasa kutoka pande nne za Dunia, jana waliungana na maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hayati Nelson Mandela, licha kuwapo kwa hali mbaya ya hewa uwanjani hapo.
Mbali ya viongozi mashuhuri na wenye chuki na vinyongo miongoni mwao, mazishi hayo pia yalipambwa na vikundi vya ngoma, upulizwaji wa  mavuvuzela na nyimbo zilizotumika kipindi cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini humo.

Viongozi kutoka nchi mbalimbali akiwamo Rais wa Marekani, Barack Obama na Rais wa Cuba, Raul Castro, ni miongoni mwa mahasimu waliokutana jana.

Katika shughuli hiyo, viongozi mbalimbali wa kisiasa duniani wakiwamo wasiopatana (maadui), walikutana katika uwanja wa FNB kwa ajili ya kumuaga shujaa huyo wa Afrika.

Katika jambo la kushangaza ambalo halikutarajiwa na watu wengi, ndege ya Rais Obama ilipotua katika Uwanja wa Waterkloof ilikuwa na Rais wa zamani wa Marekani, George Bush, pamoja na mke wa Obama, Michelle na Laura.

Obama na Castro, ambao nchi zao zilitofautiana kwa uadui miaka 50 iliyopita, ni miongoni mwa viongozi waliokutana katika Uwanja wa Soccer City.

Rais Obama alisalimiana na viongozi kadhaa akiwamo Rais wa Cuba, Raul Castro, alipokuwa akienda kutoa salamu zake.

Uhusiano kati ya Cuba na Marekani ulitetereka mwaka 1959 na Serikali ya Marekani imeiwekea vikwazo Cuba kwa zaidi ya nusu karne sasa.

Kambukumbu zinaonyesha kuwa, mara ya mwisho kwa viongozi wa nchi hizo kushikana mkono ni mwaka 2000 wakati aliyekuwa Rais wa Cuba, Fidel Castro na aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton, walipokutana katika mkutano wa Umoja wa Mataifa, mjini New York.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa zaidi wa viongozi 100 walihudhuria shughuli hiyo ya kuuaga mwili wa Mandela, hata wale waliokuwa wanatofautiana kimtizamo na chuki, walikutana katika uwanja huo.

Baadhi ya mahasimu hao ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe na Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza, Tony Blair pamoja na aliyekuwa Rais wa Marekani, George Bush, ni miongoni mwa wageni waliofika katika ibada hiyo maalum.

Blair, aliwahi kumwita Mugabe ni diktekta, ambaye alitakiwa kung'olewa madarakani, huku Mugabe akimwita Blair bepari, hata muda mwingine alimwambia `kafie jehanamu.’

Mbali na kuwapo kwa viongozi hao, Israel haikumtuma mwakilishi yoyote katika shughuli hiyo siyo rais wala waziri mkuu, kadhalika Papa Francis I hakuhudhuria shughuli hiyo, badala yake alimtuma Kardinali kutoka Afrika kumwakilisha.

OBAMA ARUSHA KIJEMBE
Katika hotuba yake, Rais wa Marekani, Barack Obama amemwagia sifa Nelson Mandela na kumuelezea kama 'gwiji wa haki na jabali la historia' jana huku akirusha kijembe kwa kusema wapo viongozi wengi sana duniani waliojifanya kuwa pamoja naye katika mapambano yake ya kupigania uhuru "lakini wakishindwa kuvumilia fikra mbadala hata zinazotoka kwa watu wao wenyewe."

Obama akizungumza katika hafla maalum ya kumkumbuka Mandela jijini Johannesburg jana, alitoa kauli hiyo mbele ya hadhara ya wakuu wa nchi mbalimbali duniani wakiwamo Makamu wa Rais wa China, Li Yuanchao, Rais wa Cuba, Castro na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

“Mapambano yake ni yako, ushindi wake ni wako, ushujaa wake na matumaini analiyaleta katika maisha yake, na uhuru wako, demokrasia yako umeletwa nay eye,” alisema Obama

Obama alisema Rais Mandela amelipelea taifa la Afrika Kusini katika haki pamoja na mamia ya watu duniani.

Akimwelezea Mandela, Rais Obama alisema Rais Mandela alizaliwa kipindi cha vita vya kwanza vya dunia katika utawala wenye nguvu.

Alisema alikua katika jamii ya wafugaji kwa kuchunga mifugo kwa kufundishwa na viongozi wa kabila la Thembu, na kusema kuwa Madiba alianza kukua kama mpigania uhuru katika karne ya 20.

''Asanteni sana kwa kuturuhusu kumuenzi Nelson Mandela, alikuwa mkombozi aliyetetea demokrasia na anaweza tu kufananishwa na marehemu Mahatma Ghandi,ni vyema kumkumbuka Mandela kama mtu aliyejitolea sana na hakuogopa kushauriana nasi kuhusu maoni yake na hisia zake na kwa sababu Mandela aliweza kukubali kuwa mtu wa kawaida mtu ambaye aliweza kufanya makosa kama mwanadamu mwengine yeyote ule,'' alisema Obama

Obama alisema Mandela alifungwa gerezani kipindi cha John Kennedy na Khrushchev hadi kipindi cha vita baridi, alisema alitoka gerezani bila la mapigano, alikuwa ma Abraham Lincon aliyeunganisha nchi pamoja ilipotaka kumeguka.

Kadhalika, Rais Obama aliwata watu wamkumbuke Rais Mandela kama taswira katika maisha ya sasa kwa kuwa alikuwa ni mtu wa kufurahi na mpenda amani.

Obama alisema Rais Mandela alionyesha nguvu ya hatua ya kuchukua dhidi ya maadui.

Aliongeza kuwa katika kizazi cha sasa hajawahi kutokea kiongozi kama Mandela, na kuwataka vijana kote Afrika na duniani kuhakikisha wanafuata nyayo zake.

Alifafanua kuwa kumbukumbu za Mandela zinamvutia kuiga mfano wake na kutaka kuwa mtu mwema

“Kumbukumbu za Mandela hunifanya kila siku kutaka kuwa mtu mwema na nataka kuwashauri vijana kuhakikisha kuwa wanafuata nyayo za Mandela,” alisema Obama.

Obama aliyekuwa akihutubia huku mvua ikinyesha katika kiwanja hicho, alisema: "Swali tunalokutana sasa ni jinsi gani tutaendeleza usawa na haki kuenzi uhuru na haki za binadamu, kumaliza mapigano na vita."

Alisema: "Tusiwe na majibu mepesi, hakuna majibu mepesi mbele ya motto wa Qunu."
Obama alisema Mandela aliikumbusha jamii kuwa kitu chochote hakiwezekani hadi pale kitakapofanikiwa, na hilo limeonyeshwa katika nchi ya Afrika Kusini.

Alisema Afrika Kusini imeonyesha dunia kuwa watu wanatakiwa kubadilika kuwa wananatakiwa kuishi kwa pamoja pasipo tofauti miongoni mwao.

Alisisitiza kuwa kwa tumaini lililo moja, dunia inaweza kuchagua kuishi bila mapigano, ila kwa amani na haki na usawa, na kueleza kuwa dunia haitamuona tena mtu kama Mandela.

Obama alisema miaka 30 iliyopita akiwa mwanafunzi, alijifunza namna ya kupigania uhuru kutoka kwa Mandela.

Kadhalika, Obama amemtaja Mandela kama kielelezo cha jinsi gani watu wanaweza kufikia mabadiliko kwa kupigania maadili yao na kujenga hoja na sababu kufikia kujitoa kwao.

Alisema kuwa ni vigumu kumsifia mtu yeyote, lakini ni vigumu zaidi kufanya hivyo hasa kwa mkongwe wa historia ambaye amelifikisha taifa katika haki na mtu aliyemfanya yeye ashawishike kuingia katika siasa.

Aidha, Rais Obama alisema kuwa kifo cha Mandela kikumbukwe kwa kipindi cha maombolezo lakini pia kikumbukwe kwa kipindi cha kuhamasisha wakati watu wakitazama jinsi gani wanaweza kubadilisha maisha yao.

Leo mwili huo utahifadhiwa katika majengo ya Muungano kwa siku tatu mjini Pretoria, sehemu ambayo Mandela enzi za uhai wake aliapishwa kuwa Rais mwaka 1994.

Baada ya tukio hilo, mwili wake unatarajiwa kuzikwa Desemba 15, mwaka huu siku ya Jumapili kijijini kwake, Qunu kilomita 700 kutoka Kusini mwa Johannesburg.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment