Maoni ya Katuni
Bunge la Jamhuri ya Tanzania ni bunge la Watanzania
wote bila kujali tofauti za itikadi za vyama wanavyoviwakilisha,
ijapokuwa zipo hoja za msingi zinazohusu vyama vyenyewe.
Lakini pia zipo hoja nzito ambazo zinagusa maslahi ya taifa ambapo
wabunge wanatakiwa wazijadili kwa maridhiano na kuachana na masuala ya
vyama.
Mwishoni mwa wiki hii, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwataka wabunge
kujenga umoja wa kushirikiana bila kuingiza itikadi zao za vyama
wanapojadili masuala mazito na ya msingi kitaifa, ili kuweza kutengeneza
na kuibua masuala yenye maslahi kwa Watanzania.
Kutokana na malumbano yaliyojitokeza wakati wa kujadili Muswada wa
Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013, ambao Waziri Mkuu Pinda
alisisitiza kuwa haujakiuka Katiba kama ilivyokuwa ikidaiwa, alisema
muswada huo ulitungwa kwa kauli moja na mamlaka iliyopewa Bunge.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda ilitolewa wakati akifunga mjadala
wa muswada wa sheria ya kura ya maoni, akisisitiza kuwa Bunge hilo ni
la Watanzania, akasema ni vyema yanapokuwapo masuala mazito, yajadiliwe
na wabunge wote kwa kuangalia zaidi maslahi ya nchi kuliko umuhimu wa
vyama ambavyo wabunge wanavyoviwakilisha.
Wabunge wengi wamekuwa na mwelekeo wa kujenga na kutetea hoja
zinazolinda sera na maslahi ya vyama vyao, wanasahau kwamba baadhi ya
hoja kama hii ya sheria ya kura ya maoni ya Katiba Mpya ni suala nyeti
la kitaifa, ambalo kimsingi linatakiwa kujadiliwa kwa mtazamo wa
maridhiano thabiti.
Pinda aliwakumbusha wabunge kuwa wapo bungeni kwa ajili ya maslahi ya Watanzania, na si kwa ajili ya kuwakilisha vyama vyao.
Aidha, maneno ya kupeana vijembe ndani ya bunge ni katika kunogesha
mazungumzo, ila visivuke mipaka na kuharibu misingi yenyewe
iliyowaweka.
Kwa ajili ya kuweka msimamo wa maamuzi ya pamoja ndani ya Bunge,
Waziri Mkuu alisema anatamani kwa siku zijazo za Bunge, liwe mfano wa
kutengeneza kikundi kimoja kitakachokuwa na uwakilishi wa vyama vyote
vilivyopo Bungeni, na kuzungumzia maudhui ya mijadala na miswada
inayowasilishwa bungeni na kutoka na mtazamo mmoja wenye manufaa kwa
wananchi.
Tunakubaliana kwa dhati na ushauri alioutoa Waziri Mkuu Pinda,
tunaamini bunge letu lipo kwa ajili ya kutengeneza taratibu na sheria
zitakazokuwa na tija kwa Watanzania wote.
Tunaelewa pia wajibu wa wabunge katika kuikosoa na kuielekeza
serikali kwa namna ya kupeleka huduma bora za maendeleo kwa wananchi.
Wabunge wakijenga umoja wa kukubaliana katika masuala ya msingi,
migongano ya kimaslahi na malumbano yasiyokuwa na maslahi kwa wananchi
yataisha.
Matukio ya misuguano ya hivi karibuni miongoni mwa wabunge yameweka sura mbaya kwa wananchi.
Ni wakati muafaka sasa kurejesha imani ya Bunge hili kwa wananchi kwa kufanya mijadala na maamuzi yenye tija kwa taifa.
Kama ambavyo alisema Waziri Mkuu Pinda huko bungeni kuwa kwa kauli
moja walikubaliana kuwa, kwa mamlaka ya Bunge waliweza kutunga Sheria
yoyote kwa maslahi ya taifa, na kwamba wote wanafahamu kuwa suala la
muswada wa sheria ya kura ya maoni ni jema na limezingatia taratibu zote
za nchi.
Kinachotakiwa ni kuhakikisha mambo yanasonga mbele. Haipendezi
kuona miswada muhimu ikiendelea kukwamishwa kutokana na malumbano
yanayozingatia itikadi za vyama jambo ambalo litaturejesha nyuma na
kuchelewesha maendeleo ya wananchi.
Kinachotakiwa ni wabunge kushikamana na kufanya maamuzi ya pamoja kwa maelewano thabiti ili nchi isonge mbele.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment