.
Makazi ya Rais wa Kwanza mzalendo wa
Afrika Kusini yaliyopo katika Mtaa wa Laa namba 12, Houghton ambako
ndiko alikokuwa hadi alipokutwa na mauti, ni kama hapaingiliki kutokana
na wingi wa watu, magari na vyombo vya habari kutoka sehemu mbalimbali
duniani ambavyo vimeweka kambi katika eneo hilo, usiku na mchana
kufuatilia safari ya mwisho ya kiongozi huyo.(HD)
Anga la mtaa huo na sehemu za jirani,
limehanikizwa na sauti nyingi za nyimbo zikiongozwa na Wimbo wa Taifa wa
Afrika Kusini 'Nkosi Sikeleli Afrika' (Mungu Ibariki Afrika),
ukifuatiwa kwa zamu na nyimbo za kidini na zile za asili ambazo zinasifu
ushujaa wa Mandela.
Katika lango la kuingia kwenye makazi
hayo ya Mandela, kuna maombolezo ya aina yake kwani yameambatana na kitu
ambacho kwa macho kinaonekana kama shamrashamra kwa nyimbo za sifa na
kufurahia kile Waafrika Kusini wanachokiita kazi nzuri ya kutukuka ya
Mandela aliyoifanya katika umri wa miaka 95 ya uhai wake.
Mwandishi wetui alitembelea makazi
hayo ya Mandela jana na kushuhudia umati mkubwa wa watu wakifika nje ya
nyumba yake kwa ajili ya kuomboleza; wakiweka mashada ya maua, mishumaa
na kadi zenye ujumbe wa pole kwa familia yake.
Miongoni mwa waliokuwapo katika eneo hilo ni Mtanzania, Christer Mwageni na watoto wake; Sabina na Faraja.
Mwageni alisema: "Kwa jinsi hali
ilivyo, huwezi kukwepa kuwa mwombolezaji, mimi na wanangu tulikuja hapa
kutembea tu kwa siku tatu hivi lakini tumejikuta tukishiriki msiba na
hata kama tungekuwa hatutaki kushiriki, uhalisia unatulazimisha".
"Kweli tuna mengi ya kujifunza,
inaonekana msiba huu wa Mzee Mandela umewaunganisha zaidi Waafrika
Kusini, maana wote bila kujali rangi wala kingine chochote, wanaonekana
kuomboleza kwa dhati kutoka mioyoni kabisa."
Katika eneo hilo la Houghton, ulinzi
umeimarishwa na polisi wako kila kona na wamekuwa wakiwaelekeza
waombolezaji na watu wengine njia sahihi za kufuata hadi kuyafikia
makazi ya Mzee Mandela kutoka na barabara nyingi za kuingia katika eneo
kufungwa na nyingine kugeuzwa maegesho ya magari ya waombolezaji.
Kwa ujumla, pilikapilika ni nyingi,
lakini katika lango kuu la kuingia makazi ya Mandela, ulinzi ni mkubwa
na hakuna anayeruhusiwa kulikaribia isipokuwa wanafamilia, vingozi wa
Serikali na watu wengine wenye shughuli maalumu.Soweto, Mandela Square
Hali kama hiyo ipo katika makazi yake
ya zamani Mtaa wa Vilakazi Na: 8115, Orlando Magharibi, Soweto ambako
kuna pilikapilika nyingi zinazoyahusisha makundi ya watu kutoka ndani na
nje ya Afrika Kusini.Mandela aliishi katika Mtaa wa Vilakazi kabla ya
kukamatwa na kuwekwa kizuizini na alirejea katika nyumba hiyo miaka 27
baadaye alipoachiwa huru na kuishi humo kwa siku kumi na moja kabla ya
kuhamia katika nyumba ya aliyekuwa mkewe, Winnie Mandela katika eneo
hilohilo la Soweto.
Kama ilivyo Houngton, katika eneo hilo
pia ulinzi umeimarishwa na baadhi ya njia zimefungwa kutokana na wingi
wa watu na magari. Vyombo vya habari kutoka kila pembe ya dunia navyo
vipo vikiendelea kufuatilia maombolezo hayo.
Katika nyumba ya Soweto ambayo sasa ni
makumbusho ya Mzee Mandela, idadi kubwa ya watu wanafurika kujifunza
historia ya kiongozi huyo na nje vipo vikundi vinavyoimba nyimbo za
maombolezo na kumsifu Mandela kwa ushujaa wake.
Eneo la tatu ni Mandela Square
lililopo katika Jiji la Sandton, Johannesburg ambako kuna sanamu kubwa
ya kiongozi huyo yenye urefu wa mita sita kwenda juu,
likimwonyesha
katika hali ya kucheza muziki. Iliwekwa katika eneo hilo, Machi 31,
2004.
Katika eneo hilo, pia ulinzi
umeimarishwa na askari wanalazimika kusimamia jinsi watu wanaovyoingia
na kutoka. Watu wamekuwa wakisimama katika msitari mrefu kupata fursa ya
kupiga picha katika sanamu hiyo yenye uzito wa tani mbili na nusu (kilo
2,500).
Pembezoni mwa sanamu hiyo, kama ilivyo
Houghton na Malakazi, limetengwa eneo maalumu kwa ajili ya watu
wanaoomboleza kuweka maua, nembo, nyaraka na mishumaa.
Maombolezo ya kifo cha Mandela
yanaingia katika siku ya nne leo na yataendelea hadi Jumapili ijayo ya
Desemba 15 wakati kiongozi huyo atakapozikwa kijijini kwake Qunu,
Mthatha Mkoa wa Eastern Cape
source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment