Tangu aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,
Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati kuu, Dk Kitila Mkumbo na aliyekuwa
Mwenyekiti wa mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kuvuliwa nyadhifa zao,
kumekuwa na mijadala mingi kwenye vyombo vya habari.
Ingetarajiwa kuwa Zitto na kambi yake wangetumia
muda huu kutekeleza masharti waliyopewa na Kamati kuu ya chama hicho
ndani ya siku 14.
Badala yake amekuwa akitumia vyombo vya habari
kujitetea. Leo yupo kwenye chombo hiki kesho kile, leo gazeti hili,
kesho televisheni au redio ile.
Hata kama ameonewa alitakiwa afuate taratibu ikiwa
ni pamoja na kuandika barua ya kupinga uamuzi huo wa kamati kuu. Kama
haridhiki zaidi, aende kwa Msajili wa Vyama vya Siasa akalalamike.
Hizo ndiyo ofisi zinazoweza kumsaidia kwa sasa, siyo kulalamika kwenye vyombo vya habari.
Ni sawa na ninaunga mkono jitihada zake ndani ya
chama chao, lakini haya siyo ya kutuambia sisi. Aende kuwaambia viongozi
wenzake ndani ya chama.
Huo ni udhaifu mkubwa wa Zitto kama kiongozi.
Hajui wapi aseme lipi na wapi asiseme. Ni mtu anayekurupuka, hana subira
wala utulivu.
Ukiangalia mifano michache tu, utaona Zitto yupo
Chadema kimwili lakini kiroho yuko kwingine. Tangu mwaka 2009 alipotaka
kugombea uenyekiti wa chama hicho na baadaye kushauriwa kujitoa, Zitto
alianza kujitenga taratibu. Mwaka uliofuata wakati wa uchaguzi, wakati
wenzake wanazindua kampeni za urais, yeye naye alikuwa akizindua kampeni
za ubunge jimboni kwake tena akatangaza kuwa mwaka 2015 kuwa atagombea
urais.
Kwa nini Zitto asingejumuika na wenzake kwenye
uzinduzi wa kumnadi Dk Willibrod Slaa aliyekuwa akigombea urais? Au
ndiyo uchu wa madaraka?
Kama hiyo haitoshi, baada ya kwenda bungeni, Zitto
akataka apewe nafasi ya Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani. Kulikuwa
na ulazima gani kwa Zitto kwenda kupambana na Mwenyekiti wake kwenye
nafasi hiyo?
Baada ya uchaguzi mkuu, siku Rais Jakaya Kikwete
alipokuja Dodoma kuzindua Bunge, wabunge wa Chadema wakiongozwa na Mbowe
walisusa wakatoka nje ikiwa ni ishara kupinga matokeo ya uchaguzi.
Lakini siku hiyo Zitto hakutokea. Maswali yakazidi, je Zitto amewagomea wenzake?
Mara nyingi haonekani kwenye mikutano na operesheni za chama
hicho na mawasiliano na viongozi wenzake utayakuta mitandao ya intaneti
kama vile Facebook au tweeter au Jamii forum.
Kwa nini hakuwa na mawasiliano mazuri na viongozi wenzake kwenye ofisi zao, hadi ayalete kwenye mitandao ya intaneti.
Hivi leo Zitto akiwa mwenyekiti wa chama si
atahamisha siri zote kwenye mitandao yote na vyombo habari? Kutakuwa na
chama tena hapo?source: mwananchi
No comments:
Post a Comment