Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Ernie Brandts sasa atavuna Sh170 milioni kutoka kwa uongozi wa timu hiyo baada ya kusitisha mkataba wake jana.
Kutokana na hali hiyo, Yanga italazimika kumlipa
mshahara wake wa miezi 10 iliyobakia ambayo ni zaidi ya Sh170 milioni
kwa kuwa kocha huyo alikuwa akilipwa mshahara wa Dola 10,000 kwa mwezi.
Uamuzi wa kumtimua kocha Brandts umefikiwa kwenye
kikao cha kamati ya utendaji ya Yanga iliyoketi juzi Jumamosi muda
mchache baada ya timu hiyo kunyukwa kwa mabao 3-1 na watani zao Simba
katika mchezo wa Nani Mtani Jembe.
Akizungumza Makao Makuu ya klabu hiyo iliyopo mtaa
wa Twiga na Jangwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Abdallah Bin
kleb alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea maoni ya wachezaji
mbalimbali wa zamani kuhusu kiwango cha timu.
“Tumempa notisi ya siku 30 ili tuendelee kutafuta
kocha mwingine na tupo kwenye mchakato wa kumlipa stahiki zake, tuachane
kwa amani.
“Mwanzoni alipandisha kiwango cha timu, kilipanda
sana, lakini baadaye kiwango kikaanza kushuka, tukasema tumpe muda
kidogo, lakini tunaona mambo yanazidi kuharibika, hivyo tumeamua
kuachana naye kwa sababu hana jipya, sisi tunalenga michuano ya
kimataifa zaidi sasa kwa kiwango hiki hatutafika mbali ni lazima
tuchukue hatua za haraka zaidi,” alisema.
Kuhusu wajumbe wengine wa benchi la Ufundi, Bin
Kleb alisema kwamba taratibu nyingine zinafuata na ndani ya wiki hii
kuna matukio mengi makubwa ambayo klabu yake itayafanya.
Hata hivyo tayari Brandts alikabidhiwa barua yake
ya kusitishiwa mkataba rasmi juzi na jana baada ya mazoezi Makamu
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga alikutana na wachezaji na
kuzungumza nao kwa zaidi ya nusu saa.
Naye Brandts alipozungumza na gazeti hili
kuhusiana na kuvunjiwa mkataba alisema kwa kifupi “Nasubiri notisi ya
siku 30 imalizike, kuna kitu nitaongea, lakini sasa hivi msikilizeni
Abdallah (Binkleb) anachosema ukifika muda na mimi nitazungumza.”
Yanga imevunja mkataba na kocha huyo ukiwa umepita mwezi mmoja tangu wamwongezee mkataba wa mwaka mmoja wa kuinoa timu hiyo.
Licha ya kufungashiwa virago, kocha, Brandts ameonyesha kukasirishwa na nidhamu mbovu ya mastaa wake.
Kwenye mazoezi yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa
Bora Kijitonyama, nyota wengi wa klabu hiyo hawakufika mazoezi bila ya
kutokuwa na taarifa zao zaidi ya Athuman Idd ‘Chuji’ ambaye amefiwa na
bibi yake.
Baadhi ya wachezaji ambao walikacha mazoezi ya kocha huyo ni
Ally Mustapha, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Emmanuel Okwi na Hamis
Kiiza.
“Sielewi, walitakiwa leo wawepo mazoezini, lakini sijawaona, sina taarifa zao labda ni kwa vile maprofesheno, sielewi.
“Profesheno nidhamu ni kitu cha kwanza, lakini
hapa profesheno ni tofauti anaamua vile anataka, najua Chuji amefiwa na
bibi yake, lakini Okwi na wenzake sielewi chochote labda viongozi
wanajua walipo mimi sijui.”
Yanga itaondoka Januari 2 kwenda visiwani Zanzibar
kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi na Januari 14 itakwea pipa
kwenda Hispania kwa kambi ya siku 10.
source: Mwananchi
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment