RAIS KIKWETE AOMBOLEZA KIFO CHA MZEE MANDELA, ATANGAZA SIKU 3 ZA MAOMBOLEZO KITAIFA, BENDERA KUPEPEA NUSU MLINGOTI
Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za
rambirambi Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na kupitia kwake, kwa
mkewe Bi. Graca Machel, wanafamilia wote na wananchi wote wa Afrika ya
Kusini kufuatia kifo cha Mzee Nelson Mandela kilichotokea tarehe 5
Desemba, 2013 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Rais ameuelezea msiba huu kuwa ni msiba mkubwa kwetu sote.
"Afrika
ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na shujaa
mkubwa wa Karne ya 20 na 21.Tunaelewa machungu waliyonayo wananchi wa
Afrika ya Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu, jasiri, mwana mapinduzi ,
mvumilivu na mstahimilivu". Ameongeza Rais Kikwete.
Rais amemuelezea Mzee Mandela kuwa ni
kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma
na upendo uliomuwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini kuwa
taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa
rangi.
"Mandela ni mfano bora kwa wanadamu wa
jinsi binadamu muungwana anavyopaswa kuwa . Ni wajibu wa wana Afrika
Kusini, Afrika na dunia kwa jumla kuiga mfano wake hasa moyo wake wa
uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake"
.Rais ameongeza kusema, "Tuzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze
roho ya Marehemu Mzee Mandela mahali pema peponi".
Kufuatia kifo hicho Rais ametangaza siku 3 za maombolezo kuanzia leo tarehe 6 hadi 8 Disemba, 2013.
Aidha, Mheshimiwa Rais ameagiza kuwa katika siku hizo 3 bendera zote zipepee nusu mlingoti.
Mwisho.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu,
DAR AS SALAAM.
06 Desemba,2013
No comments:
Post a Comment