Serikali imewasafisha aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo huku ikimpandisha cheo aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali Deo Mtasiwa.
Nyoni alisimamishwa kazi pamoja na aliyekuwa
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa na wote kwa pamoja walikuwa na
tuhuma za kutumia vibaya madaraka yao wakiwa watumishi wa umma.
Jairo kwa upande wake alisimamishwa kazi kutokana
na kuchangisha fedha kinyume cha sheria kwa lengo la kusaidia mchakato
wa kupitisha bajeti ya wizara yake, katika mwaka wa fedha 2011/2012 na
sasa ameondolewa kwenye utumishi wa umma, huku Bunge likiwa bado
halijapata taarifa ya utekelezaji wa maazimio yanayomuhusu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Nyoni kwa
sasa amerejea kwa mwajiri wake wa awali, Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), akishikilia nafasi ya mmoja wa wakuu wa idara, huku Dk Mtasiwa
akiwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, katika Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Katibu Mkuu Kiongozi
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amelithibitishia gazeti hili kuhusu watumishi hao na kwamba taratibu zimefuatwa.
“Mimi ninachojua ni kwamba Blandina alikuwa
mwajiriwa wa TRA na mkataba wake ulikuwa haujaisha… Siyo kwamba alikuwa
na mikataba miwili, kwenye utumishi wa umma huwa kuna utaratibu wa
kuazima watumishi wa umma.
Ndiyo maana unaweza kukuta mwanajeshi anatolewa
jeshini na kupelekwa uraiani au mtumishi kutoka idara moja kwenda
nyingine. Kwa upande wetu sisi tulishamwondoa kwenye ukatibu mkuu na
kule TRA hakuwa na tatizo,” alisema Balozi Sefue.
Kuhusu Dk Mtasiwa alisema: Uteuzi wa Dk Mtasiwa
ulikuwa wazi na hata alipoapishwa mambo yote yalitangazwa hadharani.”
Aliendelea kufafanua kuhusu Jairo akisema: “Jairo alishaondolewa kwenye
ukatibu mkuu, siyo mtumishi tena wa umma.” Naye Mkurugenzi wa Huduma na
Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alimtetea Nyoni akisema
kuwa amerudi kwenye ajira yake ya awali.
“Siyo kwamba ameajiriwa TRA, amerudi tu kwenye
ajira yake ya zamani, alikuwa akifanya kazi hapa akaazimwa na sasa
amerudi,” alisema Kayombo na kuongeza: “Kwani amefanya kosa gani? Kuna
mashtaka yoyote aliyofanya unaweza kuyathibitisha?”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya
TRA, Bernard Mchomvu ambaye alisema Nyoni alishasafishwa na Serikali
ndiyo maana wamempokea. “Yule aliazimwa tu na Serikali…Sasa kama
Serikali imesham-clear sisi tutamkataaje?” alihoji na kuongeza:
“Kwa sababu sikumwomba huyo mtu, nimeambiwa kwamba
huyo yuko safi mimi nifanyeje? Unajua watu wanafurahia wengine wakipata
matatizo, hata kama mtu ameua, basi walete ushahidi. Hata unaposema
nchi imejaa rushwa, ulete ushahidi… kama Serikali imeshamsafisha,
ningemkataa ningekuwa mtu wa ajabu.”
Jitihada za kumpata Nyoni kupitia simu yake ya mkononi hazikuzaa
matunda, baada ya simu yake kupokelewa na sauti ya kiume iliyosema kuwa
namba imekosewa.
Hata alipotafutwa kwa namba nyingine, simu
ilipokelewa na mwanamke aliyejitambulisha kama mfanyakazi wa Wizara ya
Afya na kwamba namba hiyo kwa sasa haitumii tena. Alipotafutwa kwa njia
ya simu, Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashilillah, alisema suala hilo
aulizwe msemaji wa Serikali juu ya Bunge.
“Ongea na msemaji wa Serikali juu ya mambo ya Bunge,” alijibu kwa njia ya ujumbe wa simu.
Lukuvi
Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi alisema kuwa hawezi kuzungumzia
suala hilo kwa kuwa hayuko ofisini.
“Niko ‘airport’ nasafiri kwenda South Africa,
msinipigie simu, siko ofisini hadi mwezi ujao (Januari),” alisema Lukuvi
na kukata simu yake.
Awali alipoulizwa kwa njia ya simu baada ya mwandishi kuelezea suala hilo alisema ana kazi nyingi na kwamba apigiwe baadaye.
Makani azungumza
Mwenye wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza
tuhuma hizo, Ramo Makani, ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini,
akizungumza na gazeti hili kuwa: “Ni kweli mimi nilikuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge iliyochunguza suala hilo, kwa utaratibu kamati kama hiyo
huundwa kwa kanuni za Bunge kwa kupewa majukumu maalumu… Kama mbunge tu
ningefurahi kusikia taarifa ya Serikali bungeni baada ya kupata taarifa
ya Bunge,” alisema Makani na kuongeza:
“Serikali iliahidi kuleta taarifa bungeni ya
utekelezaji wa maagizo ya Bunge. Mimi sikumbuki kama taarifa hiyo
imeshasomwa bungeni, labda wewe mwenzangu umebahatika kuisikia. Kwa hiyo
bado tunasubiri… Kama Serikali imechukua hatua, mimi sijui.”
Tuhuma za Nyoni
Nyoni alituhumiwa kutenda makosa saba ambayo
yaliainishwa wakati wa mgomo wa madaktari ulioanza Januari mwaka jana,
hali iliyomlazimisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kutangaza kumsimamisha
kazi ili uchunguzi uweze kufanyika.
Baadhi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili ni pamoja na kujilipa
mshahara wa ziada kupitia Mradi wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP) nje
ya mshahara aliokuwa akilipwa na Serikali, kutengua utaratibu rasmi wa
kila Idara ya Wizara ya Afya kuwa na ofisa ununuzi wake kwa kujiweka
yeye mwenyewe.
Tuhuma nyingine zilikuwa kulazimisha Wizara ya
Afya kununua sare za madereva, suti za sikukuu (Sabasaba na Nanenane) na
maua kutoka Mariedo bila kushindanisha na muuzaji mwingine kinyume na
kanuni za ununuzi.
Katika mikutano yote inayofanyika wizarani,
alikuwa akilazimisha Kampuni ya Kaliula Catering Services kupewa zabuni
ya kutoa huduma ya chakula kwa washiriki tangu alipotua wizarani kama
Katibu Mkuu.
Sakata la Jairo
Hatua ya kumwondoa Jairo katika utumishi wa umma
nayo imefanyika kimyakimya kwani Serikali hadi sasa haijawasilisha
bungeni majibu ya maazimio ya Bunge kuhusu sakata hilo ambalo pia
liliwagusa watumishi wengine wa Wizara ya Nishati na Madini. Maazimio
hayo ni yale yaliyotokana na matokeo ya uchunguzi wa Kamati Teule ya
Bunge iliyoongozwa na Makani na kubainisha kuwapo kwa makosa ya
kiutumishi na kijinai ambayo yangewafikisha baadhi ya watumishi hao
katika vyombo vya sheria.
Mbali na Jairo, kamati hiyo ilipendekeza
kuwajibishwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja;
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh na
aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.
Hata hivyo, ni Jairo pekee kati ya hao
aliyewajibishwa kwa kusimamishwa kazi na baadaye kuondolewa katika
wadhifa wake. Luhanjo alistaafu utumishi wa umma bila kuchukuliwa hatua
zozote wakati Utouh anaendelea na wadhifa wake.
Pia katika taarifa yake, Kamati Teule ilisema
utaratibu wa uchangishaji wa fedha Sh418.081 milioni uliofanyika katika
Wizara ya Nishati na Madini haukuwa na uhalali kwa mujibu wa Katiba,
Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.
Pamoja na mambo mengine, Bunge liliazimia kwamba
ufanyike ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) kwa matumizi ya Sh214
milioni, ambazo kati ya hizo Sh126 milioni Kamati Teule ilikataa maelezo
ya matumizi yake na Sh88 milioni ni zile zinaotajwa kwamba zilitumika
katika kugharimia semina kwa wabunge.
Azimio jingine ni lile lililoitaka Serikali
iviagize vyombo vya dola kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za kughushi na
ubadhirifu zilizoelezwa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kama
ilivyoelekezwa.
Baada ya kufikiwa kwa maazimio hayo, Serikali
kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora),
Mathias Chikawe iliahidi kuyafanyia kazi na kuwasilisha majibu bungeni.
“Kwa sababu ya ukubwa na uzito wa taarifa hii, ni
vigumu kuitolea majibu yote hapa hapa, ninachoweza kufanya ni kuipokea
pia tutakapokuja katika Mkutano wa Sita, tunatarajia kuleta majibu ya
hoja zilizomo kwenye taarifa hii,” alisema Chakawe ambaye sasa ni Waziri
wa Katiba na Sheria
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment