WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, December 16, 2013

Mama Maria Nyerere,Kikwete wafunika mazishi ya Mandela

  Ndege zaranda angani akizikwa

 
Rais Jakaya Kikwete, akizungumza katika mazishi ya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, hayati Neson Mandela, yaliyofanyika katika kijiji cha Qunu nchini humo jana.
Rais Jakaya Kikwete na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, jana walifunika kwenye ibada maalumu ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, iliyofanyika kijijini kwake Qunu, Mashariki mwa Cape.
Tukio hilo lilitokea baada ya Rais Kikwete kupewa fursa ya kuzungumza kwenye ibada hiyo ambayo ilianza mapema asubuhi.

Rais Kikwete alishangiliwa wakati akizungumzia uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini ulioasisiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mandela wakati akiwaelezea maelfu ya watu kati ya 4,500 waliohudhuria, akiwamo mjane huyo wa Nyerere.

Vile vile, walimshangilia baada ya kuwaeleza kuwa mwingine aliyehudhuria ibada hiyo ni Vicky Swai, ambaye Mandela alisahau mabuti yake nyumbani kwake alipozuru Tanzania baada ya kutolewa gerezani alikotumikia kifungo cha miaka 29 jela.

Alisema wakati Mandela akizuru Tanzania, wananchi hawakusita kujitokeza kumpokea barabarani licha ya mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha wakati huo kutokana na jinsi walivyompenda kutokana na mchango wake katika harakati za ukombozi nchini humo na Afrika kwa jumla.

RAIS KIKWETE AHUTUBIA
Katika hotuba yake, Rais Kikwete kwa sehemu kubwa alizungumzia uhusiano mkubwa uliopo kati ya nchi hizo mbili tangu enzi za Marais, Julius Nyerere na Mandela na jinsi Tanzania ilivyokisaidia Chama cha African National Congress (ANC).

Alisema mwaka 1962, katika harakati za kupigania uhuru wa nchi yake, Mandela alikuja nchini kwa siri akipitia mkoani Mbeya na kuwasili Dar es Salaam, ambako alikutana na Nyerere kwa siri kuomba msaada zaidi juu ya harakati za ukombozi nchini humo.

Rais Kikwete alisema akiwa nchini, Mandela aliacha viatu vyake aina ya buti kwenye nyumba ya Mama Swai, alikokuwa amelala kabla ya kwenda Algeria, akitumaini kwamba baada ya kurudi angekuja kuvichukua, lakini alikamatwa na kufungwa nchini mwake kwenye Kisiwa cha Roben, kwa miaka 27 hadi alipokuja kufunguliwa mwaka 1992.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, baada ya Mandela kuwa kiongozi wa Jamhuri ya Afrika Kusini mwaka 1995, yeye pamoja na Mama Swai, walimpelekea viatu vyake, na baada ya kuvipokea alisema alikuwa anavikumbuka.

Huku akipigiwa makofi kutoka kwa umati huo, Rais Kikwete alisema Tanzania ilitoa ushirikiano mkubwa kwa Afrika Kusini ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa nchi hiyo katika maeneo ya Mazimbu mkoani Morogoro.

Mbali na taifa hilo, pia Tanzania ilitoa msaada wa kijeshi kwa vyama vya siasa vya MPLA, ANC, Zapu na Frelimo. Rais Kikwete aliuambia umati huo kuwa, yupo pamoja na mama Maria Nyerere, ambaye mumewe hayati Nyerere, alishirikiana kwa karibu na Mandela katika harakati za ukombozi wa taifa hilo, na hivyo kuwafanya kupiga makofi kwa utambulisho huo.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, Tanzania ilitumia Shirika lake la Utangazaji, kutangaza vipindi ambavyo vililenga kutoa elimu zaidi ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na kuleta uhuru wa taifa hilo na kuongeza kuwa Mandela alikuwa rafiki mkubwa wa taifa la Tanzania.

Alisema ANC waliiona Tanzania kama nyumbani kwao huku akipongeza umoja uliopo kati ya nchi hizo mbili.

ZUMA: MANDELA ATABAKI MWANGA WA KUJENGA S A

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amesema aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, hayati Mandela, atabaki kuwa nuru ya kuwaangazia katika safari ndefu waliyonayo ya kulijenga taifa hilo, ambalo lilikuwa ndiyo ndoto zake.

Katika hotuba yake ya mwisho kabla ya mwili wa Mandela kuagwa katika vilima vya Kijiji cha Qunu, huku akipigiwa makofi na umati wa watu 4,500, Rais Zuma, alisema: “Hatutasema kwa heri kwa sababu hujaenda.

Utakuwa ukiishi milele kwenye mioyo na akili zetu.”  Huku akipigiwa makofi, Rais Zuma aliwapongeza madaktari, ambao wamekuwa karibu na Mandela tangu Agosti, mwaka huu, alipoanza kusumbuliwa na matatizo kwenye mapafu yake na kukimbizwa katika hospitali mojawapo, iliyopo Pretoria, nchini humo.

Alisema madaktari hao walikuwa wakimhudumia Mandela wakiwa wameizunguka saa katika kukamilisha sura (hatima) yake  ya mwisho ya maisha hapa duniani.

“Mawazo yetu yapo pamoja na watu wa kijiji cha Qunu na mazingira, ambayo yamempoteza mtoto wao maarufu. Tunatuma salamu za rambirambi kwa Waafrika Kusini wote. Mioyo yetu inakwenda pia kwa marafiki zako, ambao pia walipoteza maisha yao pamoja na wewe katika jitihada zako za ukombozi,” alisema Rais Zuma. 

Alisema Mandela pamoja na mkewe, Graca Machel, walikuwa na upendo kwa watoto wao na kwamba, Afrika Kusini itaendelea kuinuka kwa sababu hawatathubutu kumwangusha.

Huku akipigiwa makofi na umati huo, Zuma pia alimpongeza mtalaka wa Mandela, Winnie, kwa mchango wake alioutoa kwa kushirikiana na mumewe enzi hizo kwa ajili ya kupigania kupatikana kwa uhuru wa taifa hilo kama kiongozi na mwanaharakati.

Rais Zuma aliongeza: “Tunakushukuru kwa kuwa kila kitu, ambacho tulikihitaji kama kiongozi.”

“Tunaahidi leo kwamba, tutaendelea kuupinga ubaguzi wa rangi, ukabila na kuhamasisha umoja, uvumilivu kwa ajili ya kuijenga Afrika Kusini, ambayo ni yetu sisi sote.”

Katika hotuba yake hiyo, Rais Zuma aliwaahidi wananchi wa Afrika Kusini kuwa serikali yake itaendelea kuwaboreshea maisha yao, ikiwa ni pamoja na kuwatimizia mahitaji yao ya kijamii, kama vile kuwapa elimu bora, kupiga vita umaskini na  kujenga hospitali.

Alisema Mandela siyo tu amewaachia uhuru wa siasa, bali pia uhuru mbali na machafuko na umaskini na kwamba alikuwa ni kiongozi mchapa kazi na mwaminifu.

KAUNDA: MANDELA AMETUONYESHA NJIA
RAIS wa zamani wa Zambia, Keneth Kaunda, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wakuu na  watu maalumu takribani 4,500 walioruhusiwa kuhudhuria utoaji wa salamu  za mwisho kwa hayati  Mandela katika kijiji cha Qunu alisema, kiongozi huyo alionyesha njia si kwa Bara la Afrika pekee, bali  kwa dunia nzima.

Alisema Mandela alikuwa ni kiongozi mwenye kutii amri za Mungu ikiwa ni pamoja na kumpenda jirani yake na adui yake kama kujipenda  mwenyewe kwa kuwa alipochaguliwa kuwa kiongozi wa Afrika Kusini mwaka 1994, hakulipiza kisasi kwa mabaya waliokuwa kinyume chake wakati wa harakati za kupatikana kwa uhuru wa nchi hiyo.

Alisema Mandela alikuwa mwana wa Mungu, ambaye amewaonyesha watu wote njia huku akihubiri kwamba kila mtu amtendee mwenzake kama anavyotaka atendewe na wengine.

Kaunda pia alisema mbali na Mandela kutokuwapo katika maisha haya ya kawaida, ataendelea kukumbukwa kwa kazi yake kubwa aliyoifanya, huku akiuacha ujumbe wa upendo kwa wote.

Akitoa hotuba yake hiyo, Kaunda pia alimkumbuka mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, ambaye anye alikuwa mmoja ya waliopata heshima miongoni mwa watu 450 kwa jinsi ambavyo hayati Nyerere alivyokuwa rafiki mkubwa wa Mandela na jinsi walivyoshirikiana bega kwa bega katika kupeana mbinu za kuikomboa Jamhuri ya Afrika Kusini.

Kaunda alimwomba Mama Maria Nyerere, kuendelea kumsaidia Rais wa sasa wa nchi hiyo, Jakob Zuma, katika kumpa ushauri juu ya uongozi wake, kama alikuwa anafanya Nyerere mumewe kwa marehemu Mandela.

Alisema Mandela alikuwa mwana mkuu wa ulimwengu na siyo tu wa Afrika Kusini pekee, aliwaonyesha njia, kwani hakujali rangi iwe mzungu, mwafrika, mwenye rangi ya njano au brauni,bali wote aliwaona kuwa ni watoto wa Mungu.

“Tuje pamoja, tufanye kazi pamoja na Mungu atatuonyesha njia,” alisema Kaunda, ambaye alipewa nafasi ya kutoa hotuba katika hafla hiyo maalumu ya kuuaga mwili huo baada ya kuvunjwa kwa itifaki kwa kuwa hakuwamo kwenye orodha ya wazungumzaji.

Wengine walioshangiliwa ni Rais wa Malawi, Joyce Banda, na aliyekuwa Rais wa Zambia, Keneth Kaunda, wakati wakimuelezea Mandela alivyokuwa na mchango wake katika bara la Afrika.

MWILI WA MANDELA WAZIKWA KWA SIRI
Safari ya mwisho ya mwanamapinduzi na mpinga ubaguzi huyo (Mandela) wa rangi siyo tu kwa Jamhuri ya Afrika Kusini pekee, bali pia duniani kote, ilifikia mwisho baada ya kuwekwa kwenye nyumba yake ya milele (kaburi) kwenye vilima vya Kijiji cha Qunu, Jimbo la Eastern Cape, nchini humo.

Mwili wa Mandela ulizikwa kwa heshima zote za kidini katika eneo maalumu alilokuwa ameandaliwa katika kijiji hicho alichozaliwa na kukulia, huku hakuna aliyeona jeneza lililokuwa limeubeba mwili huo wakati likishushwa kaburini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Utangazaji la nchini humo (SABC), ambalo kwa ushirikiano wa mashirika mengine ya habari kama vile la taifa (TBC), tukio zima la mazishi ya Mandela lilirushwa moja kwa moja, lakini familia yake, iliuomba uongozi wa nchi hiyo, kuuzika mwili huo kwa  siri.

AZIKWA NA WATU 450 TU
Shughuli za mazishi zilianza na ibada maalumu ya mwisho ya kuuaga mwili huo iliyohudhuriwa na watu takriban 4,500, wakiwamo wanafamilia wa kiongozi huyo pamoja na baadhi ya viongozi wakuu wa ndani na nje ya taifa hilo.

Idadi hiyo ilipungua, kwani ni watu 450 tu ndiyo walioruhusiwa kuelekea eneo hilo la mazishi kwa madai kwamba, lilikuwa dogo na hivyo kutoweza kutosheleza idadi kubwa ya watu. Baadhi ya watu walioruhusiwa kwenda mazikoni kati ya idadi hiyo, ni pamoja na maafisa wa kijeshi, wanafamilia, wake za marais, akiwamo mjane wa Mandela, Graca Machel, viongozi wa kimila takribani 15, viongozi wa dini mbalimbali, Spika wa Bunge la nchi hiyo, wabunge 18 na Jaji Mkuu. 

VIONGOZI WALIORUHUSIWA KUHUDHURIA IBADA
Viongozi waliopewa heshima ya kuhudhuria ibada hiyo ya watu 4,500, kutoa heshima za mwisho baada ya mwili huo kutolewa kwenye Hospitali ya Jeshi la nchi hiyo  juzi, ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete aliyeongozana na mama Maria Nyerere na Mama Swai, ambaye pamoja na mume wake, walivihifadhi viatu vya Mandela aina ya buti enzi za uhai wake mara baada ya kuwasili nchini na kukutana na aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Julius Nyerere mwaka 1964, ikiwa ni katika harakati za kutafuta msaada wa kupatikana kwa uhuru wa taifa lake na kulala nyumbani kwao (Mama Swai na mumewe), kabla ya kuelekea Algeria.

Wengine ni Rais wa zamani wa Zambia, Keneth Kaunda, mtoto wa Malkia wa II wa Uingereza, Prince Charles, Rais wa Malawi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc), Joyce Banda, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegin, Makamu wa Rais wa ANC, Baleka Mbete, Rais Jacob Zuma, wanafamilia, maafisa wa jeshi, Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Desmond Tutu, na baadhi ya viongozi wengine wa kidini.

Baada ya kumalizika kwa ibada hiyo iliyoanza saa 3:00 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki, maofisa wa jeshi la nchi hiyo, takriban 10, waliubeba mwili huo wa Mandela ukiwa kwenye jeneza, wanne wakiwa upande mmoja na wanne upande mwingine, huku mmoja akiwa mbele na mmoja nyuma, na kuupeleka kwenye gari  la jeshi, tayari kuelekea kwenye eneo hilo maalumu la maziko.

Wakati gari hilo lililobeba mwili huo wa Mandela, likipita, mbele walitangulia viongozi wa madhehebu tofauti, yakiwamo ya  Kikristo ambao baadhi walikuwa wamevaa makanzu na misalaba vifuani mwao, huku gwaride maalumu la kijeshi la mwendo wa taratibu likipita na pembeni mwa barabara wakiwa wamejipanga askari wa jeshi.

Baada ya kuwasili katika eneo hilo la maziko kwa dakika chache kutoka eneo palipofanyika ibada hiyo ya mwisho majira ya saa 6:30 mchana, Askofu Siwa, ambaye aliongoza ibada hiyo ya kuuzika mwili huo kwa taratibu za kidini alisema: “Tunaamini kwamba, baada ya maaumivu kuna uponyaji. Baada ya mapambano kuna amani. Baada ya ukimya, Mungu hunena:"

Askofu Siwa aliongeza kuwa: "Ulikuwa wa kweli katika mbio za kupatikana kwa uhuru  lakini sasa umepata kilele cha uhuru kamili  mbele ya Muumba wako, Mungu  Mwenyezi.”

Hata hivyo, baada ya kumaliza mahubiri hayo ya ibada maalumu,  jeneza hilo halikuonekana wazi kama lilikuwa limeshushwa kwenye kaburi hilo kabla ya Rais Zuma na baadhi ya viongozi wakuu wa taifa hilo waliokuwa wamekaa pembeni mwa maziko hiyo, kusimama kuonyesha shughuli imeisha na ndege sita za jeshi la anga la nchi hiyo ambazo zilifungwa bendera ya nchi hiyo, zikiruka juu ya eneo hilo  kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho na kutoweka.

Mbali na jeneza lililokuwa limebeba mwili huo wa Mandela kufunikwa na bendera ya taifa hilo, halikuzikwa pamoja nayo, kwani iliondolewa na afisa mmoja wa kijeshi mara tu baada ya kuwekwa juu ya lilipokuwa kaburi.

Jeneza lililokuwa limebeba mwili wa rais huyo wa kwanza mwafrika na kuchaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini, liliwekwa kwenye gari maalumu la kijeshi huku maofisa wa kijeshi takriban tisa ndiyo waliokuwa wamepewa heshima ya kulihudumia kwa kulipandisha na kulishusha kwenye gari hilo na kutembea nalo kwa taratibu kuelekea lilipokuwa kaburi lake.

Kabla ya kuzikwa mwili huo jana kwa taratibu za kidini,  kulikuwa na tetesi za kuzikwa kwa taratibu za kimila za kabila la Xhosa, la mzee Madiba, ikiwa ni pamoja na kuzikwa na ng’ombe na shughuli nzima kusimamiwa na machifu wa makabila ya nchi hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment