Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar. Waziri Kiongozi
mstaafu Shamsi Vuai Nahodha amesema mfumo wa Muungano wa Serikali tatu
unaweza kutetemesha misingi yake na kusababisha kuvunjika, kwa vile
Zanzibar haina uwezo wa kirasilimali kuchangia uendeshaji wake.
Nahodha ameyasema hayo kwenye mkutano wake wa
hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Alabama, Mwembeshauri, ambao ni
wa kwanza tokea uteuzi wake wa wadhifa wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa utenguliwe.
Nahodha alisema kwamba kutokana na vyanzo vya
mihimili ya uchumi wa Zanzibar kuwa vichache haitaweza kuchangia gharama
za uendeshaji na kutoa mfano wa bajeti ya wizara moja ya Ulinzi
inayotumia Sh1.2 trilioni, wakati Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
ikitumia Sh800 bilioni kwa mwaka kunakopita bajeti nzima ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar ambayo hutumia Sh600 bilioni kwa mwaka.
Nahodha alisema kama Zanzibar ingekuwa na uwezo wa
kumudu gharama hizo ingeweza kuboresha mishahara ya askari wake wa
Vikosi vya SMZ na kuwapa mikopo ya elimu ya juu wanayoomba kila mwaka
kutaka kuendelea na masomo.
“Vyanzo vya Zanzibar kimapato ni hafifu
tusijidanganye, ziko wapi fedha za kumudu gharama za uendeshaji kama
zipo ni kipi kinachozuia tusilipe mishahara minono kwa vikosi vyetu na
kuwapatia maisha bora, mfumo wa Serikali tatu una viashiria vya kutaka
kuvunja muungano,” alisema Nahodha akishangiliwa na wananchi waliokuwepo
mkutanoni.
Alisema wakati huu wa mjadala wa uundwaji wa
Katiba Mpya ni wakati mwafaka wa kushughulikiwa kwa maeneo yenye kasoro
za kimsingi na siyo kufikiria kubadilisha mfumo wa Muungano kama
inavyohitajiwa na baadhi ya wanasiasa kwa utashi na matakwa binafsi.
“Ndugu zangu, kama leo hii tukivunja Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, Wazanzibari tujue tutajuta na kusaga meno,
nasema wenye wazo hilo ni wapuuzi ila msiwapuuze,” alisema.
Alisema Muungano umeleta faida kubwa kwa pande
mbili na kutoa mfano wa Wazanzibari kuweza kulitumia soko la kiuchumi la
Bara lenye watu zaidi ya milioni 44, kupata huduma za matibabu katika
hospitali za Tanzania Bara, ulinzi na usalama na mambo mengine ambayo
Zanzibar hakuna.
source: mwananchi
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment