Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad, amewataka viongozi wa Chadema kutafakari upya kwa
kuyaunganisha makundi yaliyopo ndani ya chama hicho ili waweze kuelekeza
nguvu ya mapambano kwenye vyama vingine.
Hamad ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho alisema hayo juzi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Tanganyika Parkers, Kawe
jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulilenga kuwaeleza wanachama
mambo mawili ambayo ni mchakato wa katiba mpya pamoja chaguzi
zinazotarajiwa kufanyika ndani ya CUF.
Akizungumzia migogoro ndani ya vyama vya upinzani, Hamad alisema
imekuwa ikiwakatisha tamaa Watanzania ambao wana kiu ya chama mbadala
hivi sasa.
Alitoa wito kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kuyaunganisha makundi yote waliyonayo ili washindane na vyama vingine.
Akielezea kuhusu mchakato wa chaguzi ndani ya CUF, Hamad alitaka
wanachana kuhakikisha hawawapi nafasi mapandikizi ambao wamekuwa
wakivuruga vyama.
Aliwaeleza wanachama kuwa, ili kuwapata viongozi bora lazima waachane na majungu, fitna wao kwa wao na makundi.
Kuhusu Katiba mpya, Hamad amemuunga mkono Rais Jakaya Kikwete kuwa,
kabla ya bunge la Katiba kuanza kuwe na mkutano utakaowashirikisha
wadau wote ambao utawezesha kuondoa tofauti zilizopo.
Alisema kwenda kwenye bunge la katiba huku kila mtu akiwa na msimamo wake, itasababisha kupatikana katiba isiyo ya Watanzania.
Alisema kuingia katika bunge bila kikao hicho kutafanya katiba itakayopatikana kuwa ya CCM kwa sababu wabunge wake ni wengi.
Katika hatua nyingine, Hamad ameitaka serikali kuhakikisha
Watanzania wote wenye sifa hasa vijana kushiriki katika uchaguzi mkuu
ujao.
Aliongeza kuwa Watanzania wengi hawana vitambulisho vya kupigia kura na wengine ndio wametimiza umri wa miaka 18.
Alisema serikali kwa namna yoyote inatakiwa kuangalia namna watakavyowawezesha kupata haki hilo.
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi ndani ya chama hicho, Abdul
Kambaya alisema kuwa tatizo la nchi sio usalama wa Taifa, polisi bali ni
utaratibu unaowaongoza.
Aliwaeleza wananchi kuwa wakitaka kuondoa matatizo hayo njia pekee ni kuing’oa CCM madarakani.
Naibu Katibu wa Jumuiya ya Vijana ya CUF (Juvicuf), Hamidu Bobali,
alisema wabunge waliochukua fedha za safari bila kwenda walikokutakiwa
wanatakiwa kufikishwa mahakamani.
“Tumeshtushwa na kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwa,
wabunge hao warejeshe fedha hizi, tunadhani adhabu ni kufikishwa
mahakamani kwa sababu hizi ni kodi za Watanzania wanyonge,” alisema.
Jana, Mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba katika
kikao cha baraza kuu la uongozi wa Taifa, alitoa ushauri kwa Chadema
kuwa sio muda muafaka wa kuendeleza migogoro badala yake washirikiane
katika kuandaa katiba ya Wananchi.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment