Qunu: Yametimia. Saa 6:45 kwa
saa za Afrika Kusini (sawa na saa 7:45 za Afrika Mashariki) ni muda
ambao pengine hautasahaulika katika historia ya nchi hiyo, kwani
wananchi wake walishuhudia ukomo wa maisha ya Rais wao wa kwanza
mzalendo, Mzee Nelson Mandela.
Ukimya ulitawala katika makaburi ya familia ya
Mandela, Qunu, katika Jimbo la Eastern Cape, wakati mwili wa Mandela
ukiwa umewekwa ndani ya jeneza lililotengenezwa kwa mbao na kwa ustadi
mkubwa lilipokabidhiwa kwa viongozi wa mila za Kabila la abaThembu kwa
ajili mazishi.
Mwili huo ulishushwa kaburini katika tukio la
mazishi ambalo halikuwa wazi kwa waombolezaji wengine, isipokuwa kwa
familia ya Mzee Mandela, Rais Jacob Zuma na viongozi wa kimila katika
jamii hiyo ya Waxosa ambako Mandela anatoka. Hata hivyo, mazishi hayo
yalionyeshwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni ya SABC.
Kwa mujibu wa mila na desturi za kabila hilo
alipaswa kuzikwa mchana wakati jua likiwa utosini, muda ambao kama
angekuwa hai, kivuli chake kingekuwa kifupi kuliko muda mwingine.
Mwili wa Mandela ulikabidhiwa kwa viongozi wa
kimila na Majenerali wa Jeshi la Afrika Kusini (SANDF) baada ya kumpa
kiongozi huyo heshima kubwa, sawa na ile ambayo hupewa kiongozi ambaye
hufariki akiwa madarakani.
Kabla ya kukabidhi mwili huo, waliondoa bendera ya
Taifa ya Afrika Kusini ambayo ilikuwa imefunika jeneza pamoja na vifaa
vingine, ili kutoa mwanya kwa jeneza hilo kufunikwa kwa ngozi ya chui
kama mila zinavyotaka.
Bendera na vifaa vilivyoondolewa vilikabidhiwa kwa familia ya Mandela.
Ni watu 450 tu kati ya zaidi ya 5,000 walioshiriki
katika ibada ya mazishi, ambao walipata kibali cha kwenda makaburini na
majina yao yalisomwa mmoja baada ya mwingine.
Mara baada ya mwili wa Mandela kukabidhiwa, Askofu
Don Dabula, alifanya sala ya mwisho na alipohitimisha anga la Qunu
lilishamiri sauti za helikopta tatu za kijeshi ambazo zilikuwa
zimening’iniza bendera za Afrika Kusini.
Helikopta hizo zilifuatiwa na ndege nyingine sita
ambazo zilikuwa zimerushwa zikitengeneza umbo la pembe tatu, matukio
ambayo yalifanywa kwa heshima ya kiongozi huyo.
Kulikuwa na ukimya na wakati ndege hizo
zikitokomea, baragumu lilipigwa wakati ambao mazishi rasmi ya Mandela
yalikuwa ya kianza kwa taratibu za kimila.
Mapema Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alisema
wiki iliyopita imekuwa ni wiki ya uchungu, kwani kwa siku tisa za
maombolezo watu wameomboleza kwa ukimya, vilio na nyimbo ikionyesha kuwa
walifurahishwa na kumpenda Mzee Mandela.
Rais Zuma, Mjane wa Mandela, Graca Machel, Mtalaka wake, Winnie
Medikizela pamoja na watoto, wajukuu, vitukuu na wanafamilia wengine,
walikuwa wameketi viti vya mbele wakati taratibu zote za mazishi
zilipokuwa zikiendelea.
Ibada ya mazishi
Ulikuwa ni wakati mgumu kwa familia ya Mandela
ikiongozwa na Graca, Medikizela, watoto wake; Makaziwe, Zenani na
Zindziswa, wajukuu; Mandla na Ndaba pamoja na ndugu jamaa na marafiki
ambao walijawa na huzuni wakati wa ibada hiyo.
Vilio na nyimbo za maombolezo vilisikika tangu
asubuhi wakati wa mchakato wa kuelekea kuanza kwa taratibu za mazishi na
hali ya huzuni ilizidi miongoni mwa waombolezaji na wageni waalikwa
kadiri muda wa mazishi ulivyokaribia.
Baadhi ya waandishi wa habari wa Afrika Kusini,
polisi na wanajeshi, waliweka majukumu yao kando na kuomboleza hasa
wakati mmoja wa marafiki wakubwa wa Mandela, Ahmed Kathrada alipokuwa
akisoma wasifu ambao ulihitimishwa kwa maneno ya uchungu.
“Wakati Walter (Sisulu) alipofariki dunia,
nilipoteza baba na sasa Mandela amefariki nimepoteza kaka, sijui ni nani
nitakayemwendea,” alisema Kathrada ambaye alifungwa gerezani pamoja na
Mandela kwa miaka 26.
Mishumaa 95 ambayo ni idadi sawa na miaka
aliyotimiza Mandela, iliwashwa wakati wa ibada ya mazishi nyumbani kwake
Qunu alikokulia, katika Jimbo la Estern Cape, umbali wa kilometa zaidi
ya 1,000 kutoka Johannesburg.
Mandela alizaliwa katika Kijiji cha Mvezo eneo la
Transkei, Julai 18, 1918 akiwa mtoto wa Nongaphi Nosekeni na Henry Gadla
Mandela, ambaye alikuwa mshauri muhimu katika utawala wa abaThembu na
alipewa nafasi ya kuwa Chifu wa Mvezo alipokuwa kijana.
Mazishi hayo yanahitimisha siku kumi
zilizotangazwa na Rais Zuma kwa ajili ya maombolezo baada ya kufariki
dunia Desemba 5, 2013 saa 02:50 usiku, nyumbani kwake Mtaa wa Laa Na:12,
Houghton, Johannesburg.
Miongoni mwa wageni mashuhuri alikuwamo, Rais
Jakaya Kikwete aliyeongoza ujumbe wa Tanzania ukimjumuisha Mjane wa Baba
wa Taifa, Mama Maria Nyerere.
Mama Maria alishangiliwa sana pale alipotambulishwa na Mmoja wa Waongozaji; Cyril Ramaphosa na baadaye Rais Kikwete.
source: mwananchi
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment