JUMAPILI 15 DISEMBA 2013
Mheshimiwa Jacob Zuma wa Jamhuri ya Afrika Kusini;
Mama Graca Machel,
Mama Winnie Mandela,
Wanafamilia waliondokewa na mpendwa wao,
Mtukufu Mwanamfalme Charles,
Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali,
Waheshimiwa Mawaziri,
Wajumbe wa Mashirika ya Kidiplomasia na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa,
Waombolezaji wenzangu,
Mabibi na Mabwana;
Ninawaleteeni salamu za undugu na
mshikamano kutoka kwa kaka zenu na dada zenu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Wameniomba niwafikishieni salamu za dhati za rambirambi kwako
Rais, Mama Graca Machel, Mama Winnie Mandela, familia nzima ya Madiba na
watu wote wa Afrika Kusini kutokana na kifo cha Mheshimiwa Nelson
Rolihlahla Mandela, Rais wa zamani wa Afrika Kusini na African National
Congress.
Wanapenda mfahamu kuwa hampo peke
yenu. Wapo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu na chenye majonzi.
Wanasema huzuni yenu ni huzuni yetu, kuondokewa kwenu ni kuondokewa
kwetu. Nelson Mandela alikuwa kiongozi wetu, shujaa wetu na baba yetu
kama alivyokuwa kwenu. Watu wa Tanzania wamempoteza rafiki mkubwa na
komredi mkubwa katika mapambano.
Rais Mandela amekuwa na uhusiano
thabiti wa muda mrefu na Tanzania. Umeanza zamani wakati wa uhuru na
mapambano ya ukombozi hapa Afrika Kusini na Tanzania. Vyama vyetu,
African National Congress (ANC) na Tanganyika African National Union
(TANU) vilikuwa na uhusiano maalum. Haikutokea tu, kuwa, baada ya ANC
kuamua kuanzisha kitengo cha jeshi, Umkotho we Sizwe, baada ya njia za
amani kushindikana, Dar es Salaam ikawa kituo cha kwanza cha Madiba
baada ya kuondoka Afrika Kusini mwaka 1962 akiwa njiani kutafuta msaada
kwa ajili ya mapambano ya kijeshi na mahali pa mafunzo kwa ajili ya
wapiganaji wa MK.
Makomredi na marafiki;
Kimsingi, ziara yake ilihanikiza
mafanikio. Ni ziara hiyo iliyochangia kubadili mwelekeo wa historia ya
hili taifa kubwa iliyofanikiwa kuuangusha ubaguzi wa rangi na kuzaliwa
kwa Afrika Kusini mpya mwaka 1994. Ingawa Rais wetu wa kwanza na Baba wa
Taifa Mheshimiwa Julius Nyerere alisita mwanzoni, baadaye alilikubali
ombi la Madiba na kuwapa wapiganaji wa MK ruhusa ya kuishi na kuendesha
mafunzo ndani ya Tanzania.
Nina hakika kwa wakongwe wa MK, majina
kama Kongwa, Mgagao, Mazimbu na Dakawa yamezoeleka kwao na pengine
kuamsha kumbukumbu nzito za maisha waliyoishi Tanzania. Rais Nyerere
alikwenda mbali zaidi ya kuwapa mahali pa kuishi na kuendesha mafunzo,
akajitolea msaada wa Tanzania na akawa nyenzo katika kuhamasisha msaada
wa kimataifa katika kutoa mafunzo na silaha kwa wapambanaji. Kimsingi,
msaada huu ulifanywa kwa vyama vyote vya ukombozi Kusini mwa Afrika
ambavyo ni MPLA, SWAPO, ZANU, ZAPU na FRELIMO.(P.T)
Makomredi na marafiki;
Ziara hii pia iliyabadili majaliwa ya
ANC baada ya kuwa kimepigwa marufuku na utawala wa ubaguzi wa rangi hapa
Afrika Kusini. ANC ikapata nyumbani kupya Tanzania ambako iliendesha,
kupanga na kuchochea mapambano. Kutoka Tanzania ANC ikaweza kuwafikia
makada na wanachama wake waliobaki na kuendesha mapambano kutoka ndani
ya Afrika Kusini kwa kupitia mawasiliano ya tahadhari kubwa.
Kutoka Tanzania ANC ilimudu kufikisha
ujumbe kwa hadhira kubwa ya watu wa Afrika Kusini kwa dhati kwa kupitia
matangazo ya redio. Kama haitoshi, Serikali ya Tanzania ikajenga kituo
cha redio kwa ajili ya mapambano ya ukombozi. ANC ikaweza kuifikisha
sauti iliyokuwa imezuiliwa na utawala wa ubaguzi wa rangi.
Makomredi na marafiki;
Kuna jambo la kufurahisha kuhusu ziara
ya kwanza ya Madiba Tanzania mwaka 1962. Ili kuifanya ziara ya kuwa na
usiri mkubwa, asingeweza kukaa mahotelini; aliishi nyumbani kwa Mhazini
wa TANU ambaye kwa wakati huo alikuwa Waziri wa Biashara na Viwanda
ndugu Nsilo Swai (sasa ni marehemu). Wakati akiondoka kuelekea Accra,
Lagos, Addis Ababa na Algiers, aliviacha viatu vyake nyumbani kwa ndugu
Swai akiwa na matumaini ya kuvipitia akiwa njiani kurejea. Kwa bahati
mbaya, hakupitia Dar es Salaam na muda mfupi tu alipowasili Afrika
Kusini, Mandela alikamatwa, kushitakiwa, na kufungwa jela kwa miaka 27.
Kwa bahati nzuri, familia ile ilivitunza viatu hivyo na kusubiri.
Madiba alipoachiwa kutoka jela na
mwaka 1994 kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini mpya, jozi ya
viatu vya kahawia ilikabidhiwa kwake mwaka 1995. Alikabidhiwa na Mama
Vicky Nsilo mjane wa marehemu Nsilo Swai aliyefariki mwaka 1994 ambao
Madiba alikuwa Rais. Nilichukua jukumu la kumleta Mama Vicky Nsilo
sambamba name aweze kumuaga mgeni wao maalumu na rafiki.
Yeye na marehemu mumewe ni binadamu wa
kipekee mno kuvitunza viatu vya mtu mgeni aliyeishi nao kwa siku tatu
tu na kutoweka kwa zaidi ya miaka 32. Nilipomwuliza nini kiliwafanya
kuvitunza viatu kwa muda mrefu huo, aliniambia kuwa mumewe aliamini kuwa
Mandela angetoka jela siku moja na kuvidai. Ili wakiulizwa wawe navyo
mkononi. Hata hivyo, hawakusubiri, badala yake akamtafuta Madiba na
kumkabidhi kilichokuwa chake. Ni marafiki waaminifu kiasi gani ambao
Mandela alikuwa nao.
Makomredi;
Baada ya kutoka kwake jela na baada ya
kuitembelea Zambia kwa ajili ya mkutano wa NEC ya ANC alikuja Dar es
Salaam. Alikutana na halaiki kubwa ya watu ambao jiji halijawahi
kuwashuhudia. Kumbukeni, mvua kubwa ilinyesha siku ile lakini watu
walisongamana uwanja wa ndege na kujipanga katika mitaa ya Dar es Salaam
wakiivumilia mvua ili kumwona kiongozi wao. Haiba kubwa ya Mandela
haikuwa na kifani. Pia alizuru Morogoro na kulala Mgagao kwenye kambi ya
mafunzo ya MK.
Makomredi na marafiki;
Nimesimulia hadithi hizi zote na
michapo ya matukio ya kweli ili kuwafanya watu wafahamu ni muda mrefu
kiasi gani, uhusiano wa sasa uliotukuka baina ya nchi zetu umetoka. Si
jambo la kushangaza kuwa Afrika Kusini na Tanzania wanafurahia uhusiano
wao uliotukuka baina yao. Tunatazama kwa pamoja mambo mengi ya kikanda
na kimataifa. Tunaungana mkono kwenye kila baraza la kikanda na
kimataifa.
Sisi ni marafiki na washirika wa
karibu kwa sababu ya historia yetu inayofanana inyotuunganisha. Si
kingine zaidi ya waasisi wetu Rais Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki
mwaka 1999 na Rais Nelson Mandela tunayemwombeleza leo waliofanikisha
hili. Walijenga misingi imara mno. Ndiyo maana nilisema mwanzoni kuwa
Madiba ni kiongozi wetu, shujaa na baba mno kama alivyo kwenu. Hii ndiyo
sababu huzuni yenu na simanzi yenu ni yetu pia.
Makomredi na Marafiki;
Tunapoomboleza kifo cha huyu shujaa
Nelson Rolihlahal Mandela ni vemu tujikite katika kuyaimarisha mahusiano
baina ya Afrika Kusini na Tanzania. (Hii ni alama na urithi wa kipekee
aliotuachia ili tuukamilishe). Tufanye kazi kwa ushirikiano katika
mabaraza ya kikanda na kimataifa ili kukuza falsafa zake kwa SADC imara,
Umoja wa Afrika ulio hai na Umoja wa Mataifa wenye uwezo wa kupigania
haki na usawa kwa mataifa yote na watu wote. Na, tunapaswa kuzitimiza
ndoto zake kwa kuona nchi zinazoendelea zikishirikiana kwa umoja na
mshikamano katika kutafuta haki zao na kujikwamua kutoka katika
umasikini kuelekea kwenye ustawi.
Nanyi, kaka zangu na dada zangu wa
Afrika Kusini, Madiba ameishi maisha yake vema, mnatakiwa kuhakikisha
urithi wake unadumu. Ameliacha taifa lenye demokrasia bora ambapo
Waafrika Kusini Weusi na Weupe wanaishi kwa maelewano.
Taifa ambalo weusi pia wanaweza
kustawi tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma waliposhutumiwa na kuishi
katika kudhalilishwa, kupokwa utu wao kama raia wa daraja la pili ama la
tatu ndani ya nchi yao wenyewe. Tunafahamu kuwa siyo yote
aliyoyasimamia yamefikiwa. Ni kujipotosha kudhani kuwa maovu yote ya
mfumo uliopita wa ubaguzi wa rangi yamesahihishwa katika hii miaka 19.
Tafadhali simameni katika hilo na
daima mpanie kufanikiwa zaidi. Namna hii, mtamuenzi kiongozi huyu
mweledi kwa namna ambayo ingemridhisha kama angekuwa hai. Hii ndiyo
namna bora zaidi ya kuuishi urithi wake.
Udumu milele Nelson Mandela!
Mdumu milele watu wa Afrika Kusini!
Ninawashukuruni kwa ukarimu wenu.
Imetafsiriwa katika Kiswahili na Fadhy Mtanga.
source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment