Dar es Salaam. Mshambuliaji Amis Tambwe
ameitibua sherehe ya utambulisho wa Emmanuel Okwi baada ya kupachika
mabao mawili wakati Simba ilipoichakaza Yanga 3-1 katika mchezo wa ‘Nani
Mtani Jembe’ jana kwenye Uwanja Taifa, Dar es Salaam.
Mrundi Tambwe alifunga mabao mawili huku Awadh
Juma akifunga bao moja kwa Simba kabla ya Okwi kufunga bao la kufutia
machozi kwa Yanga.
Tambwe aliwainua mashabiki wa Simba dakika ya 13
baada ya kupokea pasi nzuri ya Said Ndemla akiwa peke yake na kupiga
shuti pembeni kwa kipa Juma Kaseja.
Baada ya Simba kupata bao mashabiki wa Yanga
walikaa kimya hali iliyomfanya mwenyekiti wao Yusuf Manji kusimama na
kuwataka washangilie huku akionyesha vidole vitano. Jambo lililowafanya
mashabiki wa Simba kuanza kuzomea kwa nguvu.
Tambwe alipatia Simba bao la pili kwa mkwaju wa
penalti dakika ya 43 baada ya Ramadhani Singano kuchezewa vibaya na
David Luhende, kabla ya kuhitimisha kwa bao la tatu dakika ya 60,
akitumia vizuri uzembe wa Kaseja kupachika bao la tatu.
Manji aliinuka kwenye kiti chake na kwenda
kumkumbatia Zaccaria Hanspope na kuondoka uwanjani hali iliyowafanya
mashabiki wa Simba kumzomea.
Okwi aliingia akitokea benchi na kuifungia Yanga
bao la kufutia machozi dakika ya 79, akimalizia vizuri krosi ya Haruna
Niyonzima.
Mashabiki wa Simba walikuwa wakiwakejeli wenzao wa
Yanga kwa kuwaambia waendelee kusajili wachezaji wa Simba faida yake
wameiona.
Baada ya kukabidhiwa kombe mashabiki wa Simba
walizunguka nalo, na wengine wakisukuma gari la Hanspope huku wakiimba
‘Okwi, Okwi, Okwi..’
Katika mchezo huo Yanga walionekana kuwa na presha na kucheza zaidi kibinafsi kuliko kitimu kulinganisha na wapinzani wao Simba.
Yanga waliondoka kabisa mchezoni baada ya bao la
Simba na kuwaacha viungo Mkude, Henry Joseph, Chombo wakifanya watakalo
katika kuanzisha mashambulizi ya vijana hao wa Msimbazi.
Beki wa Yanga, Luhende alikuwa na bahati ya pekee
kwa kukosa kupewa kadi nyekundu baada ya kumkwatua kwa nyuma winga
Simba, Singano na kusababisha penalti iliyofungwa na Tambwe.
Beki Kelvin Yondani alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Singano dakika ya 74 na mwamuzi Ramadhan Ibada.
Kocha wa Simba, Zdravko Lugarusic alikuwa kivutio
uwanjani hapo kutokana na mambo yake na kushindwa kutulia sehemu moja
katika muda wote wa mchezo.
Pamoja na kutompa kadi nyekundu mwamuzi wa mchezo
huo, Ibada kutoka Zanzibar alishindwa hata kumwonyesha kadi ya njano
Luhende kwa kitendo chake hicho.
Simba iliwapumzisha Joseph, Ndemla, Chanongo,
Tambwe na kuwaingiza Singano, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Uhuru Seleman
wakati Yanga katika kipindi cha pili iliwatoa Haroub, Kiiza, Kavumbagu
na kuwaingiza Simon Msuva, Okwi, Hassan Dilunga.
Mabadiliko hayo hayakuweza kuwasaidia Yanga
walioshindwa kabisa kuelewana huku wachezaji wake wakionekana wakicheza
bila ya malengo na kupoteza kasi yao ya kawaida.
Mashabiki wa Yanga baada ya kufungwa bao la tatu kutokana na uzembe wa Kaseja waliinuka kwenye viti na kuanza kuondoka.
Pia, Jerryson Tegete aliyekuwa amekaa benchi baada
ya bao hilo alimwinua kipa Deo Munishi kumtaka aende kudaka, lakini
kocha Brandts alikataa kufanya mabadiliko hayo. Mashabiki wanne wa Yanga
walizimia na kuondolewa na machela uwanjani, huku wengine wakizingira
basi la wachezaji wao na kuwashutumu kwa kucheza chini ya kiwango.
Yanga waliingia uwanjani saa na robo, huku
mshambuliaji wake Okwi akizunguka uwanja wa mzima kuwapungia mashabiki
waliofurika uwanjani hapo.
Mashabiki wa Yanga waliamka kwa shangwe kwa
kitendo hicho cha Okwi kuwapungia, wakati wale wa Simba wengi walikaa
kimya na wachache walimpigia makofi.
Vikosi
Yanga: Juma Kaseja, Mbuyu Twite, David Luhende,
Nadir Haroub, Athuman Idd, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier
Kavumbagu, Mrisho Ngassa, Hamis Kiiza.
Simba: Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid,
Joseph Owino, Donald Msoti, Johas Mkude, Henry Joseph, Haruna Chanongo,
Hamis Tambwe, Said Hamis, na Awadh Juma
source: mwananchi
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment