Kigoma. Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe amewaomba wakazi wa Mkoa wa Kigoma kumuunga mkono
katika mapambano yake ndani ya chama hicho.
Akizungumza Mjini Kasulu katika mkutano wa hadhara, Zitto alisema atahakikisha anapigania haki yake ndani ya Chadema kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama hicho ili aweze kurudishiwa nyadhifa zake, hususan nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Bara aliyovuliwa na Kamati Kuu Novemba 21, 2013.
“Najua nakabiliwa na vita kubwa ndani ya Chadema, lakini kwangu mimi (Zitto) hii ni changamoto, naamini nitashinda tu. Lakini lolote litakalotokea ndani ya Chadema hata kama ni kunifukuza, nitarudi kwenu ndugu ili tuamue kwa pamoja nini tufanye, wapi twende kwa pamoja kama tulivyo kwani nguvu ya mamba ipo kwenye maji,” alisema Zitto.
Amesema kwa kipindi kirefu anaonekana kama msaliti ndani ya chama na anatuhumiwa kutoa siri za Chadema kwa CCM na Serikali. “Tuhuma hizi hazina ukweli, nalaumiwa na kubambikiwa mambo kutokana na msimamo wangu ndani na nje ya chama
“Watu wa Kigoma ambao ndiyo tulipokea mageuzi kabla ya wengine, tunaitwa wasaliti ndani ya Chadema, lakini waliokuja baadaye kutoka mikoa mingine hawa ndiyo wanajiona wasafi. Wapo Watu waliingia Chadema baada ya kukosa fursa za kugombea huko walipokuwa awali na sasa wanajifanya ndiyo Chadema damu-damu. Sitoki Chadema ng’o, labda wanifukuze,” alifafanua Zitto. “Mnakumbuka misukosuko iliyomkuta Dr Kabourou (Aman) alipokuwa Kiongozi wa Chadema, pia walimwondoa Kafulila (David) na sasa mimi (Zitto) natafutwa ili niondolewe. Lazima tuungane pamoja kutetea masilahi yetu watu wa Kigoma,” aliongeza Zitto.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment