Vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vimeahirisha maandamano ambayo yalitakiwa kufanyika keshokutwa (Alhamisi).
Vyama hivyo vilipanga kuandamana nchi
nzima ili kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete asisaini muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwa una kasoro
nyingi ikiwamo Zanzibar kutoshirikishwa katika mchakato.
Viongozi wa vyama hivyo wamesitisha
uamuzi huo baada ya Rais Kikwete kusema yuko tayari kufanya nao
mazungumzo kujadili suala hilo.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema hayo Jumanne mara baada ya kukutana na viongozi wenzake
katika Ofisi za NCCR-Mageuzi, Ilala Dar es Salaam.
Mbele ya Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Profesa
Lipumba alisema viongozi wa vyama hivyo wametafakari na kuona ni busara
kumsikiliza Rais Kikwete kwanza kabla ya kuamua kuendelea na uamuzi wao
au la.
"Lengo la kuandaa maandamano ni
kuhakikisha kwamba tunapata Katiba bora isiyo na kasoro, ndiyo maana
tunaona kwa kuwa Rais ameonyesha nia ya kuzungumza na sisi tumeona ni
bora tukakutana naye kwanza," alisema.
Profesa Lipumba alisema baada ya kuzungumza na Rais kuhusu muswada huo, ndipo watakapotoa uamuzi.
Alisema bado hawajapata taarifa rasmi
kutoka Ikulu kuhusu lini watakutana na Rais na kwamba taarifa hizo
wamezipata kupitia vyombo vya habari.
Jana, vyombo vya habari vilikariri
taarifa kutoka ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ikisema Rais
Kikweta anatarajia kukutana na viongozi wa vyama hivyo kati ya Oktoba 13
na 15 mwaka huu.
Rais Kikwete katika hotuba yake ya
kila mwezi Ijumaa iliyopita, alisema hoja na kauli za wanaopinga muswada
huo zinazungumzika ili kutafuta mwafaka badala ya kufanya maandamano.
Katika kikao cha Bunge kilichopita,
wabunge wa vyama hivyo walitoka nje ya ukumbi wakipinga Muswada
usijadiliwe kwa kuwa una kasoro nyingi.
Miongoni mwa kasoro hizo ni
kutoshirikishwa kwa Serikali ya Zanzibar, madaraka ya Rais ya kuteua
wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba na kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba baada ya kuwasilisha rasimu ya pili kwenye Bunge la Muungano
badala ya kuwepo hadi katika kura ya maoni.
Chanzo:Mwananchi mtandaoni
No comments:
Post a Comment