Dar es Salaam. Mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiwemo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, walijitokeza kwa wingi kushiriki ibada ya kuaga mwili wa mtangazaji mkongwe nchini, Julius Nyaisanga ‘Uncle J’, kabla ya kusafirishwa kwenda Buhemba Wilaya ya Tarime, Mara kwa mazishi.
Ibada hiyo ambayo iliongozwa na Padri Stephano Kaombwe wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu Dar es Salam na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Dk Gharib Bilal, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, waandishi na watangazaji kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo, Dk Bilal alisema tasnia ya habari imekumbwa na msiba mkubwa wa kuondokewa na mtangazaji mahiri aliyetoa mchango mkubwa kwa Serikali na sekta binafsi nchini na licha ya uchache wa vyombo na waandishi waliokuwepo siku za awali, lakini Nyaisanga aliweza kudhihirisha umahiri wake.
Alisema Nyaisanga anakumbwa kwa mengi, lakini kubwa ni sauti yake ambayo itaendelea kubaki katika fikra za wengi.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat), Dk Reginald Mengi alisema marehemu Nyaisanga ameacha pengo kubwa na anamfahamu kama mtu mwenye weledi wa kazi na asiyependa kujikweza.
“Ingawa alikuwa na umaarufu kutokana na kazi yake, lakini alikuwa siyo mtu mwenye majivuno,” alisema Mengi na kuongeza kuwa msiba huo unasikitisha na unaumiza zaidi wazee.
Awali akizungumza katika ibada hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absolom Kibanda alisema Nyaisanga alikuwa mwalimu wa wengi na kuna watangazaji wengi wapya ambao wamekuwa wanamchukulia kama mfano katika kazi zao na tasnia imepoteza mtu mahiri.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwataka waandishi kuangalia uwezekano wa kuandika vitabu vya historia zao na za viongozi ili kizazi kijacho na kilichopo kiweze kutambua kazi na michango ya baadhi ya watu katika jamii.
Nestory Mapunda akisoma wasifu wa marehemu katika ibada hiyo alisema, marehemu ambaye ameacha mke na watoto watatu, alizaliwa mwaka 1960 katika Kijiji cha Buhemba na kupata elimu ya Msingi nchini Kenya kabla ya kurudi nchini na kujiunga na Shule ya Sekondari Buhemba.
Baadaye alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma Nyegezi (sasa Saut) na mwaka 1979 aliajiriwa na Shirika la Utangazaji la Voice of Kenya (VOK) wakati huo (sasa KBC)na alifanya kazi kwa muda kabla ya kujiunga na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) miaka ya themanini. Mwaka 1994 alijiunga na Radio One kabla hajaachana nayo na kuajiriwa Aboud Televisheni.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment