• ASEMA IMEPOTEZA MATUMAINI KWA WATANZANIA(na Danson Kaijage, Dodoma Tanzania Daima)
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameonyesha wasiwasi wa chama hicho
kushindwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2014 na uchaguzi mkuu wa
mwaka 2015 iwapo watendaji wake wataendelea na vitendo vya rushwa.
Alisema kuwa kwa sasa chama hicho
kikongwe kimepoteza matumaini kwa Watanzania kutokana na vitendo ambavyo
siyo vya kiungwana vinavyofanywa na watendaji.
Kwa kusisitiza, Kikwete alisema hata
kama CCM itashinda uchaguzi wa 2015, kama tabia walizonazo watumishi na
viongozi ndani ya chama hazitabadilika, ni wazi kuwa hakitapita kwenye
uchaguzi wa 2020.
Rais Kikwete alitoa onyo hilo mjini
hapa juzi usiku, alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa
makatibu na wenyeviti wa wilaya na mikoa wa chama hicho nchini nzima.
"Kama hatutabadilika katika suala la
rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana, na kama mwaka huo
tutafanikiwa kuishika serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena
madarakani.
"Najua rushwa ipo na mnaendelea
kupokea sh laki mbili za 'airtime' (muda wa mawasiliano), ndugu zangu
hatutafika, ama wengine watavuka na wengine kukwama," alisema.
Alisema tatizo la rushwa kwa viongozi
wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku hali ambayo inawapotezea
imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.(P.T)
"Viongozi wa chama ndio mmekuwa
mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu, nawaombeni tubadilike, kama
tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali
nawaambieni," alisema Kikwete ambaye alitumia muda wa saa mbili kufunga
mafunzo hayo.
Alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa
wapo baadhi ya watu ambao wameanza kujipitisha kwa viongozi wa chama na
kuwapatia hela kwa ajili ya kuwapigia debe ili wawachague katika nafasi
mbalimbali za urais ama ubunge.
Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo
watu ambao wameishaanza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali
za kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo linaendelea
kukishushia hadhi chama hicho.
Akizungumzia chuki ndani ya chama,
alisema Watanzania kwa sasa wameishakuwa na akili zao, na hivyo hawataki
kudanganywa kwani viongozi wengi ndani ya chama hawajui hata ilani ya
chama chao.
"Wapo baadhi ya viongozi ndani ya
chama hawajui hata ilani ya chama chao, wakipanda kwenye majukwaa
wanaanza kuzungumzia ujenzi wa daraja la Mkapa ama lile la Malagarasi,
watu hawataki kusikia hayo, mtu wa Ngara anataka kujua daraja lake
limeishaje siyo la Mkapa," alisema.
Hata hivyo, alisema kwa sasa vyama vya
upinzani vinafanya kazi kubwa zaidi ya kuwatembelea wananchi na
kusikiliza kero zao tofauti na ilivyo kwa CCM ambayo viongozi wake wapo
mbali na wananchi.
"Wapo watu ambao wanadai kuwa chama
kitafia mikononi mwangu, nataka niseme kuwa hakifii mikononi mwangu,
kitafia mikononi mwenu," alisisitiza.
Kikwete alisema kuwa siku hizi watu
wana mbadala wa vyama vingine na siyo CCM peke yao, na hivyo kuwataka
viongozi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa waondolewe mara moja
katika nafasi zao.
"Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo
mbalimbali ambao wanaweza kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu,
hivyo hatuna budi kuachana na hawa wala rushwa ambao watatupotezea sifa
yetu kwa wananchi. Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza
kufa."alisema.
Katika hatua nyingine, Kikwete
aliwaonya viongozi ambao wanajihusisha na uuzaji wa mali za chama kama
vile viwanja na baadhi yao kuingia mikataba yenye utata.
Hata hivyo, aliwataka makatibu hao na
wenyeviti wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanawatembelea wanachama wao na
kutafuta wengine wapya kwa ajili ya kujiimarisha kwa chaguzi mbalimbali
zijazo.
source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment