Lakini wataka waliompotosha Rais wawajibishwe
Washauri Rais akutane nao kabla ya Oktoba 10
Rais Jakaya Kikwete
Vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ,
vimekubali ushauri wa Rais Jakaya Kikwete wa kutaka hoja ya Zanzibar
kutoshirikishwa kutoa maoni irudishwe Bungeni.
Hata hivyo, vimetoa angalizo la kumtaka
atumie kama sababu mojawapo ya kutosaini muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Aidha, vimemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa Katiba na Sheria,
Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na
Bunge), William Lukuvi, wawajibishwe kwa kumpotosha Rais kuwa Zanzibar
ilishirikishwa kutoa maoni.
Viongozi wa Kamati ya Ufundi ya
Ushirikiano wa vyama hivyo, walisema hayo wakati wakizungumza na
waandishi wa habari jana makao makuu ya CUF jijini Dar es Salaam wakati
wakitoa maoni yao kuhusu hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa juzi.
Mkurugenzi wa Habari wa Chadema, John
Mnyika, alisema Rais atumie madaraka yake ya kwenye katiba ibara ya 97
(2) kuacha kusaini muswada huo na kutoa sababu za Zanzibar
kutoshirikishwa.
“Suala la ushirikishwa wa Zanzibar ni la
muhimu, kwa kuwa hii ni katiba ya Muungano, Rais amepewa maelezo yasiyo
ya kweli kuhusu umuhimu wa Kamati ya Bunge Katiba, Sheria na Utawala
kwenda Zanzibar kukusanya maoni ya wadau,” alisema Mnyika.
Kuhusu maandamano, Mnyika alisema kwa kuwa
Rais amekubali kukutana na viongozi wakuu wa vyama hivyo, awaandikie
barua ya kukutana nao kabla ya Oktoba 10, mwaka huu siku iliyopangwa
kufanyika maandamano nchi nzima.
Alisema vyama hivyo vitaendelea na
maandalizi kwa ajili ya maandamano yatakayofanyika nchi nzima na kwamba
kama Rais atakuwa hajakutana na viongozi wakuu wa vyama, maandamano yao
yatakuwapo kama walivyopanga.
Naye Mkuu wa Idara ya Taasisi za Dola na
Vyombo vya Uwakikishi NCCR- Mageuzi, Faustine Sungura, alisema Rais
awajibishe mawaziri hao, kutokana na kutoa kauli zinazokinzana katika
suala la katiba.
Sungura alisema hotuba ya Rais
ukiisikiliza na kuisoma kwa makini ina mitego kwa sababu hajaweka wazi
kama atasaini muswada huo au la.
Mkurugenzi wa Habari CUF, Abdul Kambaya,
alisema kama Rais atakutana na viongozi wakuu wa vyama hivyo, mapema,
Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Freeman
Mbowe (Chadema), watasitisha maandamano yao.
Kimbaya alisema katika kipindi hiki ambacho wanasubiri wito wa Rais, wataendelea na maandalizi ya kuratibu maandamano hayo.
Vyama hivyo vimeungana kupinga muswada huo
usisainiwe na Rais kutokana na baadhi ya vifungu kuingizwa kinyemela,
Zanzibar kutoshirikishwa kutoa maoni na pia umehodhiwa na CCM.
Juzi Rais Kikwete, katika hotuba yake ya
kila mwisho wa mwezi alisema hoja ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa
Zanzibar, irudishwe Bungeni ili wabunge walizungumze na kulifanyia
uamuzi muafaka.
WASOMI, WANASIASA WASIFU HOTUBA YA RAIS JK
Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa
juzi na kugusia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, kuhusu suala la Zanzibar kurudishwa bungeni imesifiwa na baadhi
ya wasomi na wanasiasa.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema Kikwete
ameonyesha usawa na kuwapa Watanzania fursa baada ya baadhi ya watu
kutaka kuwapotosha.
“Rais ameonyesha uwezo mkubwa na utashi
wake kuhusiana na mchakato wa katiba mpya…wanasiasa walijichukulia suala
hili kama lao pekee yao wakati katiba ni ya Watanzania wote hata mabao
si wanasiasa,” alisema Dk. Bana.
Dk. Bana alisema, lazima wanasiasa
wapinzani wapime kabla ya kuamua kama maandamano waliyopanga yafanyike
ama la kwa maslahi ya Watanzania.
Alisema, kilichozungumzwa na Kikwete
kuhusiana na kurejeshwa bungeni ili wabunge wazungumzie maoni ya wadau
wa Zanzibar, ni suala la msingi na kutakiwa kumpongeza.
Naye Profesa Palamagamba Kabudi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kinachotakiwa ni pande zote mbili kukaa
katika meza moja kwani suala la katiba ni la wananchi wote.
“Suala la katiba haliamuliwi kwa wingi wa
namba ama idadi ya watu, bali linatakiwa kukaa pamoja na kufikia muafaka
wa wengi na wachache,” alisema Profesa Kabudi.
Aliongeza kuwa mchakato wa katiba ya sasa
ni tofauti na ule wa miaka ya 1965, 1977, 1984 na 1992 ambao ulikuwa
unaamuliwa na Rais pekee, lakini Kikwete ameonyesha njia kwa kuupeleka
kwa wananchi na kumalizwa na wananchi wenyewe.
“Ni mara ya kwanza kwa wananchi
kushirikishwa kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa, hivyo
lazima suala hilo limalizwe na wananchi wenyewe,” alisema.
Akizungumzia maamuzi ya Rais kutaka suala
la Zanzibar lirudishwe Bungeni, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai
Ali Vuai, alisema anakubaliana na maamuzi ya ‘bosi’ wake kwa kurejesha
suala hilo bungeni.
Vuai alisema wapinzani walikimbia suala
hilo bungeni, lakini Kikwete ameamua kuwarejesha tena huko huko kwani
ndiko muafaka unakopatikana.
“Suala la bungeni litamalizwa bungeni na
wala si kwa maandamano, Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa taifa CCM
amefanya maamuzi ya busara sana,” alisema Vuai.
Akizungumzia suala hilo la Zanzibar,
Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema kwa sababu
Rais amekubali Zanzibar haijashirikishwa, basi anatakiwa kutumia
madaraka ya Rais kwenye Katiba Ibara ya 97 (2) kuacha kusaini muswada
huo.
“Kuhusu maamuzi kufanywa kwa awamu ya tatu
kwenye Bunge la Katiba kwa kutumia wingi mdogo badala ya kutumia
theluthi mbili na suala la kuchakachuliwa kwa kurasa, lazima Rais
aangalie suala hilo,” alisema Mnyika.
Nao viongozi wa Chama cha Kijamii (CCK) na
National Reconstruction Alliance (NRA), wameibuka kuushambulia muungano
wa vyama vitatu vilivyopanga kufanya maandamano nchi nzima Oktoba 10,
kushinikiza Rais asisaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba.
Mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda
akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema vya Chadema, CUF na
NCCR Mageuzi, havijaweka maslahi ya taifa mbele na badala yake vinataka
kujiweka pabaya zaidi.
“Tumefanya utafiti na kubaini vyama hivi
vinataka kusababisha katiba mpya isipatikane mwakani…tatizo lililopo
hapa ni kuhodhi mchakato mzima,” alisema Akitanda.
Naye mwenyekiti wa NRA, Rashid Mtuta
alisema wanasiasa wanatakiwa kutumia busara na hekima ili kupata wabunge
wengi zaidi uchaguzi ujao kuliko kukimbilia kuandamana na kulalamikia
mabadiliko ya muswada huo.
“Hawa wenzetu wanatumia mambo ya ajabu sana, inawezekana wenzetu wana mambo mengine nje ya amani ya Tanzania,” alisema Mtuta.
*Imeandaliwa na Thobias Mwanakatwe na Daniel Mkate
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment