Na DANIEL MBEGA
Salaam Mwalimu Nyerere,
Sina shaka kwamba huko uliko
umepumzika kwa amani, kwa uwezo wa Mungu. Yawezekana umekuwa mwenyeji
huko na kazi yako njema uliyoifanya katika kuhakikisha Tanganyika
inajitawala, na hatimaye inaungana na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuzaa
Tanzania, bado ni kitambulisho tosha ndiyo maana leo hii, miaka 14 baada
ya kifo chako, bado Watanzania tunakukumbuka huku duniani.
Lakini nina uhakika hujui yanayotokea
huku Tanzania. Kwa kifupi, mambo yameharibika. Natamani waraka wangu
ungekufikia mwenyewe mkononi ili nikukumbushe ama nikupashe
yanayoendelea huku.(P.T)
Wale wote uliowanadi mwaka 1995 ili
waienzi Ikulu yetu, walikugeuka miezi michache tu baada ya wewe kulala
na babu zako. Wakaigeuza Ikulu kuwa sehemu ya biashara – ingawa wapo
wengine uliwauliza "...Mnakimbilia Ikulu kufanya biashara gani!" Viwanda
vyote ulivyopigania kuanzishwa waauziana wenyewe. Ikulu ikawa sehemu ya
kusaini mikataba mibovu ambayo immeshuhudia madini yetu yalikuvunwa na
kupelekwa nje huku sisi tukibaki na mashimo tu.
Kwa kifupi, uliona wanafaa
walikusailiti. Maadili ya uongozi uliyoyasisitiza yakatoweka. Vita ya
rushwa imeshindikana kwani wenye dhamana ya kupambana nayo ndio vinara
wa kutoa na kupokea rushwa. Natamani hata Chifu Fundikira angekuwepo
naye aone wenzake wanavyofaidi – pengine angesikitika kwa nini yeye
aliondolewa kwenye Baraza lako la Mawaziri miaka michache tu baada ya
uhuru.
Ufisadi umetamalaki kila kona, chaguzi
zimegubikwa na rushwa mbaya. Chama chako cha Mapinduzi kimekuwa 'Chama
cha Matajiri'. Bora hili ni neon zuri, lakini wengine wanakiita 'Chama
cha Mafisadi', au 'Chama cha Majangili' na wengine wanathubutu kusema ni
'Chama cha Majambazi', ilimradi kila mmoja anatamka neno analoona
linafaa. Maskini hawana nafasi, wachache tu ndio wana sauti kwa sababu
ya fedha zao.
Wale uliowapinga ndani ya Chama wakati
ule, uliowahoji kuhusu walikopata utajiri wao, leo hii ndio
wanaoabudiwa. Mbaya zaidi wanapita mpaka misikitini na makanisani kutoa
misaada, halafu wanapigiwa makofi na kuimbiwa mapambio. Ungewaona, nina
imani ungemwaga machozi. Naamini mama yetu Maria anaugulia moyoni kwa
yanayotokea.
Mwalimu, sikuwepo wakati huo, lakini
nakumbuka ilikuwa Jumapili, Aprili 26, 1964, saa 4.00 asubuhi wakati
wewe – ukiwa Mwenyekiti wa TANU – ulipokutana na Mwenyekiti wa
Afro-Shiraz Party (ASP) Sheikh Abeid Amani Karume mjini Dar es Salaam na
kusaini hati ya makubaliano ya kuziunganisha nchi zenu. Muungano huu
ulifikiriwa kwa takribani miezi mitatu na siku 24 tu tangu yalipofanyika
mapinduzi ya kuung'oa utawala dhalimu wa Kisultani visiwani Zanzibar
Januari 12, 1964. Kabla ya kutiwa saini, nyote wawili mlikuwa mmefanya
mazungumzo mara kadhaa mjini Dar es Salaam na Unguja na ndipo mkafikia
mwafaka wa kuziunganisha nchi hizo.
Wapo walioupinga wakati huo (na
wanaendelea kuupinga) kwamba haukufuata misingi inayotakiwa katika
muungano halisi, lakini pia wapo walioufurahia na wanaendelea kuufurahia
kwa kuwa umeleta udugu na kujenga umoja na mshikamano.
Mwalimu, imebaki miezi michache tu ili
Muungano huu utimize miaka 50, lakini nina mashaka kama hautakufa kabla
ya miaka hiyo kutimia. Umoja, amani, upendo na mshikamano uliojengwa na
muungano huo umetoweka kabisa.
Ndiyo, si unaelewa kwamba hivi sasa
Watanzania wako kwenye mchakato wa Katiba Mpya? Ile ambayo wewe
uliikataa kipindi kile na kushauri kasoro ndogo ndogo ziwe
zinarekebishwa (yaani itiwe viraka), sasa inaelekea kupatikana, maana
mabilioni ya fedha za walipa kodi yamekwishatumika.
Halafu nikwambie kitu kimoja, ile
serikali iliyowaponza John Malecela na Horace Kolimba mpaka ukawatungia
kitabu – serikali ya Tanganyika – sasa inazaliwa rasmi. Ndiyo, na
Wanzibari uliokuwa ukiwatetea kwa kuulinda Muungano, safari hii ndio
vinara wa kuupinga Muungano. Tena basi kuna vikundi tayari huko Visiwani
vinavyohamasisha kuupinga na kutaka Serikali ya Tanganyika iwemo ndani
ya Katiba.
Mwalimu, nafahamu kwamba unatambua
jinsi Muungano ulivyopitia katika vipindi vigumu mno na kuna nyakati
ambapo umetiwa msukosuko kiasi cha kutishia hatma yake. Hilo, kwa kiasi
kikubwa, limetokana na baadhi ya watu kutoa mapendekezo anuai
yanayoashiria muungano huo ama unaweza kuendelea kudumu au kuvunjika
kabisa.
Wananchi wa Tanzania wanazijua faida
na hasara za muungano huo kwa kipindi chote hicho na ni wazi kwamba
ndiyo maana wengi wao wamejitokeza kuchangia mawazo yao katika Rasimu ya
Katiba wakitaka Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Wazanzibari wanasema wanataka kuona
nchi ambayo waliungana nayo ikitajwa kwenye Katiba, lakini Wabara nao
wanasema wanataka Tanganyika ili wawe na sauti. Ni changamoto kweli
Mwalimu. Wakati Wazanzibari wanasema Muungano umeumeza utaifa wao,
baadhi ya Watanganyika nao wamekuwa wakisema rasilimali nyingi za
Tanzania Bara zimekuwa zikitoweka kuwanufaisha Wazanzibari katika kile
kinachoonekana kama kujipendekeza kwa serikali ya CCM kulinda kwa nguvu
zote ili usivunjike.
Wazanzibari, kwa upande wao
wanaendelea kusema kwamba kwa kipindi chote hicho wameshindwa kufanya
jambo lolote kwa maendeleo yao kutokana na kivuli cha muungano na kwamba
kila wanalotaka kulifanya lazima serikali ya Muungano ihoji.
SUALA LA UTAIFA...
Mwalimu, nadhani unatambua kuwa yapo mambo mengi ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekuwa ikitaka kufanya bila kupitia kwenye Muungano na mojawapo ni uamuzi wake wa kutaka kujiunga na Shirikisho la Nchi za Kiislamu Duniani (Organisation of Islamic Conference - OIC) mwaka 1992. Hapo ndipo hasa 'chunusi' wa Muungano alipoingia.
Mwalimu, nadhani unatambua kuwa yapo mambo mengi ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekuwa ikitaka kufanya bila kupitia kwenye Muungano na mojawapo ni uamuzi wake wa kutaka kujiunga na Shirikisho la Nchi za Kiislamu Duniani (Organisation of Islamic Conference - OIC) mwaka 1992. Hapo ndipo hasa 'chunusi' wa Muungano alipoingia.
Lengo kubwa la SMZ kwa wakati ule,
chini ya Dk. Salmin Amour Juma, lilikuwa kuifanya Zanzibar kuwa nchi au
taifa la Kiislamu, wakati inafahamu fika suala kama hilo lilipaswa
kujadiliwa kabla ya kuchukua maamuzi mazito kama aliyokuwa amechukua Dk.
Salmin.
Utakumbuka vyema jinsi uamuzi huo
ulivyozua mjadala mrefu ndani ya CCM (wakati huo serikali ilikuwa bado
ya chama kimoja) na hata bungeni, ambako wabunge na wana-CCM wa Bara
waliona wamesalitiwa na kiongozi huyo wa Zanzibar ambaye pia kikatiba,
ndiye Makamu Mwenyekiti wa CCM upande wa Zanzibar na pia wakati huo
alikuwa ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano!
Lakini Mwalimu, Zanzibar haikujiondoa
OIC kama tulivyoelezwa na viongozi wetu, bali kilichotokea ni kwamba,
OIC ilichunguza na kukuta Zanzibar siyo Taifa linalojitegemea, yaani
Sovereignty State, na kwa mujibu wa masharti yao, haikustahili kuwa
mwanachama, hivyo wakaiondoa, siyo kwamba yenyewe ilijitoa baada ya
shinikizo.
Pamoja na kuondolewa huko, Zanzibar
iliendelea kulalamika kwa kuingiliwa katika mambo yake ya ndani kwa
kisingizio cha muungano, ambao kwa kizazi cha sasa wanaiona hali hiyo
kana kwamba imewadumaza.
Kujiunga kwa Zanzibar katika OIC kuliwazindua wabunge wa Tanzania Bara, ambao waliona kuwepo kwa serikali mbili ndani ya Muungano kulikuwa ni kama kuwapa kiburi Wazanzibari, kiasi cha kufanya lolote wanalotaka bila kusubiri baraka za upande mwingine.
Kujiunga kwa Zanzibar katika OIC kuliwazindua wabunge wa Tanzania Bara, ambao waliona kuwepo kwa serikali mbili ndani ya Muungano kulikuwa ni kama kuwapa kiburi Wazanzibari, kiasi cha kufanya lolote wanalotaka bila kusubiri baraka za upande mwingine.
Ndipo katika kikao cha Bunge la Bajeti
cha mwaka 1993, aliyekuwa Mbunge wa Chunya, Mheshimiwa Njelu Edward
Mulugale Kasaka akawasilisha hoja binafsi bungeni na kudai Serikali ya
Tanganyika ndani ya Muungano ili kutoa uwiano sawa. Hoja hiyo ilipata
baraka za Waziri Mkuu wa wakati huo, John Samwel Malecela 'Cigwiyemisi'
na kupitishwa na Spika wa Bunge wa wakati huo, marehemu Chifu Adam Sapi
Mkwawa ili ijadiliwe ingawa alizuia mjadala usiwe mrefu sana. Hata
katika Bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba iliyokuwa chini ya Spika wa
sasa Samuel Sitta, waliainisha kwamba kulikuwa na 'Waraka wa Kutaka
Maoni ya Wananchi kuhusu Hoja ya Tanganyika (White Paper)'.
Mwalimu, ni katika mjadala huo ambapo
kulionekana kuna mchanganyiko; wengine wakiunga mkono na wengine
wakipinga mabadiliko ya Katiba ya Muungano kufanya ziwepo serikali tatu.
Wabunge 55 waliofahamika kama G55,
wakiongozwa na mtoa hoja, Njelu Kasaka, waliiunga mkono hoja hiyo.
Baadaye wakaongezeka wengine kumi na kuifanya idadi yao kuwa 65 hadi
kufikia Julai 22, 1994. Wabunge waliounga mkono na majimbo yao ya wakati
huo yakiwa kwenye mabano ni; Mateo Tluway Qaresi (Babati), Jenerali
Twaha Khalfani Ulimwengu (Taifa/Jumuiya ya Vijana), Mbwete Polile Hombee
(Mbeya Vijijini), John Byeitima (Karagwe), Chediel Yohane Mgonja
(same), Japhet Sichona (Mbozi), Benedict Losurutia (Kiteto), Dk. Mganga
Kipuyo (Arumeru Magharibi), Stanley Kinuno (Nyang'hwale), Dk. Aaron
Chiduo (Gairo), Edward Oyombe Ayila (Rorya) na Shashu Lugeye (Solwa).
Wengine walikuwa John Mwanga (Moshi
Mjini), Dk. Deogratius Mwita (Serengeti), Abel Mwanga (Musoma Mjini),
Juma Jamaldin Akukweti (Tunduru), Patrick Silvanus Qorro (Karatu),
Steven Mwaduma (Iringa Mashariki), Dk. Ndembwela Ngunangwa (Njombe
Kusini), Richard Koillah (Ngorongoro), Ahmed A. Mpakani (Iringa
Magharibi), Paschal K. Mabiti (Mwanza), Luteni Lepilal Ole Moloimet
(Monduli), Lumuli Alipipi Kasyupa (Kyela), Profesa Aaron Masawe (Hai) na
Arcado Ntagazwa (Kibondo).
Mwalimu, inakumbukwa pia walikuwemo
Phineas Nnko (Arumeru Mashariki), Paschal Degera (Kondoa Kusini), Mussa
Nkhangaa (Singida Mjini), Halimenshi Kahema Mayonga (Kigoma Kaskazini),
Said Abdallah Nakuwa (Lindi Mjini), na Mosi Tambwe (Taifa/Wanawake).
Wengine ni Luteni Kanali John Mhina
(Muheza), Charles Kagonji (Mlalo), Kisyeri Werema Chambiri (Tarime),
Tobi Tajiri Mweri (Pangani), William H. Mpiluka (Mufindi), Aidan Livigha
(Ruangwa), Philip Sanka Marmo (Mbulu), Erasto K. Lossioki (Simanjiro),
Shamim Khan (Morogoro Mjini), Raphael Shempemba (Lushoto), Phares Kabuye
(Biharamulo), Evarist Mwanansao (Nkasi), Mussa Masomo (Handeni), Jared
Ghachocha (Ngara), na Mariam Kamm (Taifa/Wanawake).
MAMBO WALIYOYATAKA...
Mwalimu, wote hawa walitaka Muungano wa Tanzania, uliozaliwa bila kupata baraka za wananchi wengine na hivyo kuwa na mapungufu, utazamwe upya. Walifikiria kwamba kwa wakati huo ulizaliwa kwa makubaliano tu kati ya TANU na Afro-Shiraz Party (ASP), lakini bila ridhaa ya wananchi.
Mwalimu, wote hawa walitaka Muungano wa Tanzania, uliozaliwa bila kupata baraka za wananchi wengine na hivyo kuwa na mapungufu, utazamwe upya. Walifikiria kwamba kwa wakati huo ulizaliwa kwa makubaliano tu kati ya TANU na Afro-Shiraz Party (ASP), lakini bila ridhaa ya wananchi.
Wakaeleza kwamba kwa wakati huo
ilikuwa lazima Muungano huo ufanywe haraka ili kulinda mapinduzi ya
kumwaga damu ya ndugu zatu wa Zanzibar; Unguja na Pemba, ambavyo ni
visiwa vidogo sana, kwa hiyo Sultan Jamshid angeweza kurejea tena kwa
msaada kutoka kokote kule duniani na inasemekana tayari alikuwa ameandaa
majeshi ili arudi kuivamia Zanzibar.
Lakini baada ya kusikia Zanzibar na
Tanganyika zimeungana hata yeye kule alikokimbilia na wafadhili wake
walikata tamaa kurejesha tena utawala wa kibwanyenye (Usultani) visiwani
humo.
Kwa maana nyingine, tunaweza kusema
nchi hizo ziliungana kwa sababu za ki-ulinzi au kiudugu zaidi na kwa
uzalendo wa Kiafrika, Muungano ambao haukupata baraka za wananchi kama
walivyokuwa wakipigania uhuru wao. Lakini sasa baada ya miaka 49 hakuna
tena tishio kama hilo (dhidi ya ndugu zetu wa Visiwani).
Kwanza, hata wale ambao wangefanya
hivyo, sasa nao wamekata tamaa kabisa. Pili, kikubwa zaidi ni kwamba
hata serikali yenyewe ya Mapinduzi Zanzibar sasa ina uhusiano mzuri tu
hata na watawala wake wa zamani.
Ni suala la u-taifa tu kwa sababu
chini ya mwavuli wa Muungano, Mtanganyika amepoteza kabisa utaifa wake
(National Identity). Hakuna popote katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano
panapotaja kitu kinachoitwa 'Tanganyika' au u-Tanganyika. Badala yake
sehemu kama hiyo imemezwa na neno Tanzania. Lakini Zanzibar ina serikali
yake yenyewe, SMZ.
Ndiyo maana hata serikali ya CCM
ilipoagiza hoja hiyo iondolewe Bungeni mwaka 1994 na kuamua kuendelea na
mfumo wa serikali mbili ndani ya Muungano huku ikifanya mikakati kuunda
serikali moja, Wazanzibari waligoma kabisa kuafiki muundo huo wa
serikali moja.
Mwalimu, unakumbuka jinsi Wazanzibari,
wakiongozwa na Rais wao wa wakati ule Dk. Salmin Amour Juma,
walivyosema katu SMZ haiwezi kufa na kwamba hawaafiki serikali moja.
Wengine wakaendelea kusema kwamba Muungano haujainufaisha Zanzibar kwa
lolote, hivyo kumaanisha kwamba hawana haja nao.
CCM iliamua kuendesha kura za maoni
kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla ili kuona walikuwa na mtazamo
gani kuhusu suala la Muungano. Waliokuwa wakitetea Muungano ilionekana
waliutetea kwa lugha kali ya hasira, ghadhabu na hata vitisho vya
kuwafukuza wenzao kwenye Chama. Waliodai Utanganyika nao walidai kwa
lugha hiyo hiyo ya ukali, wakijibu mapigo.
Kitu kilichopaswa ama kinachopaswa
kutazamwa hapa ni mambo machache kama yafuatayo; Kwanza kabisa, kudai
Utanganyika siyo kosa la uhaini wala la jinai. Pili, Chama cha Mapinduzi
siyo wananchi kwa sababu wananchi wako milioni 35, lakini wanachama wa
CCM hadi kufikia mwaka 1994 walikuwa 3,506,355 tu. Pengine kutokana na
kuwepo kwa vyama vingi vya siasa idadi hiyo imepungua kwa sasa.
Tatu, walioulizwa maoni hayo kuhusu
Muungano mwaka 1994 ni wanachama wa CCM peke yao, tena wapatao
1,349,501. Hesabu hiyo ilikuwa sawa na asilimia 33.49 tu ya wanachama
wote nchi nzima. Asilimia 61.75 ya asilimia 33.49 walipendekea serikali
mbili, asilimia 29.21 walipendekeza serikali moja, na asilimia 8.27
walitaka serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Kura za maoni
zilizoharibika zilikuwa asilimia 0.67.
Mwalimu, Wtanzania wanajiuliza, kura
hizo zilihesabiwa na nani? Waliopiga kura ni wana-CCM na waliozihesabu
ni hao hao wanachama wa CCM pamoja na viongozi wao, ambao walikuwa
wakipinga hoja hiyo. Unategemea wangetoa majibu gani? Walichosahau ni
kwamba, suala hilo ni nyeti na linawagusa wote, wananchi wa Tanzania kwa
ujumla wao, bila kujali itikadi zao za siasa.
Nakumbuka Mkuu wa Mkoa wa Mara wa
wakati huo, Bwana Joseph Butiku, alitoa kauli kali kwamba msimamo
uliokuwa umefikiwa na CCM ni kuwa na serikali mbili katika Muungano
kuelekea serikali moja na kwamba kama Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour
Juma, alikuwa anapinga shauri yake. Butiku aliyasema hayo Jumanne,
Agosti 23, 1994 kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam wakati
akishiriki mjadala wa hoja ya serikali ya kufuta Azimio la Bunge la
mwaka 1993 la kuanzishwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Nanukuu maneno yake: "Wananiuliza, umemsikia Rais wa Zanzibar? Aah mimi
nasema Rais wa Zanzibar ni kiongozi wetu... tunamheshimu ... lakini
kakosea ... Huu ndio msimamo wa Chama; serikali mbili kuelekea serikali
moja na kama Waziri Mkuu hataki, shauri yake, kama Rais wa Zanzibar
hataki, shauri yake, maana Chama cha Mapinduzi kina utaratibu wa
kuliongoza taifa hili..." mwisho wa kunukuu.
Mwalimu, nakumbuka hapa ndipo
ulipoamua kuingilia kati hoja ya Tanganyika na kusema kwamba, kuundwa
kwa serikali hiyo kungemaanisha kifo cha Muungano. Hivyo, ukasema
usingekuwa tayari kuona Muungano unakufa hali wewe ukiwa hai!
Pengine kwa vile tayari
umekwishatangulia mbele ya haki ndiyo maana waliobaki wameamua kuua
Muungano – mwanao pekee aliyesalia – kama walivyoua Ujamaa na
Kujitegemea, tena kule kule Zanzibar.
SERIKALI ILIKUWEPO...
Wazanzibari wanaendelea kupinga muundo wa muungano wa serikali moja, na sasa hawazitaki hata hizo mbili. Sababu kubwa inayowafanya wakatae muundo huo ni kwamba wanadai Zanzibar ilikuwa na serikali yake kamili wakati Muungano ulipofanyika Aprili 26, 1964!
Wazanzibari wanaendelea kupinga muundo wa muungano wa serikali moja, na sasa hawazitaki hata hizo mbili. Sababu kubwa inayowafanya wakatae muundo huo ni kwamba wanadai Zanzibar ilikuwa na serikali yake kamili wakati Muungano ulipofanyika Aprili 26, 1964!
Mwalimu, hapa Wazanzibari
hawajadanganya. Ni kweli kabisa, tangu Januari hadi Aprili 1964 Zanzibar
ilikuwa nchi huru (Sovereign State) ikiitwa Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar. Mnamo Aprili 6, 1964 Zanzibar ilikuwa imefungua Balozi tatu;
London, Uingereza alikuwepo Othman Shariff; Cairo, Misri alikuwepo Salim
Ahmed Salim, na New York, Marekani alikuwepo Hasnu Makame. Waziri wa
Mambo ya Nje alikuwa Profesa Abdulrahman Mohammed Babu.
Pia nchi 17 zilikwishaitambua Zanzibar
hadi kufikia Aprili 26, 1964. Nchi hizo ni Ghana (28/1/1964), Cameroon
(30/1/1964), German Democratic Republic - GDR (30/1/1964), Poland
(30/1/1964), Israel (1/2/1964), Misri (4/2/1964), Urusi (4/2/1964),
China (6/2/1964), Czechoslovakia (18/2/1964), Algeria (18/2/1964), India
(22/2/1964), Uingereza (24/2/1964), Marekani (24/2/1964), Mali
(26/2/1964), Congo-Brazzaville (26/2/1964), Ceylon (26/2/1964) na
Liberia (29/2/1964).
Aidha, nchi tisa zilikwishafungua
Balozi zao huko Zanzibar kabla ya Muungano. Nchi hizo ni Ghana, GDR,
Israel, Urusi, China, Uingereza, Vietnam, Marekani na Ufaransa.
Zanzibar pia tayari ilikuwa mjumbe katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN), mnamo Aprili 6, 1964, na ilikuwa inashirikishwa UNESCO, ADB na mashirika mengine ya kimataifa.
Zanzibar pia tayari ilikuwa mjumbe katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN), mnamo Aprili 6, 1964, na ilikuwa inashirikishwa UNESCO, ADB na mashirika mengine ya kimataifa.
Mwalimu, lakini kilicho wazi ni
kwamba, Wazanzibari wamesahau kuwa hata Tanganyika ilikuwa na serikali
yake kamili kabla ya Muungano. Pengine kwa kutambua hilo ndiyo maana
safari hii wenyewe wamesimama kidete kuitaka Serikali ya Tanganyika.
Na kwa vile Katiba siyo Msahafu, hata
Watanganyika nao wameamua kuwa na serikali yao. Hata hivyo, ninavyoona –
ukiacha wananchi wa kawaida – wale wote wanaoipigia kelele ambao wako
kwenye nyadhifa mbalimbali, wanakililia siyo serikali, bali madaraka.
Yaani Mwalimu, ukiwaona
wanavyozungumza huku mishipa ya shingo imewatoka na mate yanawadondoka
ungecheka badala ya kusikitika. Wanataka kwenda Ikulu ya Tanganyika na
wengine wanataka kwenda Magogoni. Lakini sijui hiyo Ikulu ya Tanganyika
itakuwa wapi? Sijui wataidai na Ikulu yao halafu Serikali ya Muungano
itafute Ikulu nyingine?
Samahani Mwalimu, usingizi umenibana, wacha nisinzie kidogo. Keso asubuhi nitakutumia salamu nyingine. Alamsiki. <MWISHO>.
source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment