Ramadhani Singano wa Simba akijaribu kumpita beki
wa timu ya Prisons Mwangama Lugano katika mechi ya ligi kuu ya Bara
kwenye Uwanja wa Taifa jijini jana. (Picha: na Omar Fungo)
Bao lililotokana na shuti kali kutoka mita 20
lililofungwa na kiungo Jonas Mkude, jana liliiwezesha Simba kuendelea
kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Bara, ilipoilaza Prisons
1-0 kwenye Uwanja wa Taifa.
Kwa ushindi huo Simba imefikisha pointi 18
lakini kocha Abdallah Kibadeni aliisifu Prisons kwa kucheza vizuri na
kusema timu yake, ambayo wiki ijayo itawakabili watani wa jadi Yanga
kwenye uwanja huo pia, haijawa vizuri.
Mwalimu wa Prisons Jumanne Chale alisema
makosa katika safu yake ya ulinzi ndiyo yaliyosababisha kupoteza mchezo
huo, lakini bao la Mkude lilistahili kuwa la ushindi katika ligi yoyote
duniani.
Mkude alifunga bao hilo baada ya kuuwahi
nje ya eneo la hatari mpira uliokuwa umeokolewa kwa kichwa na beki ya
Prisons kutokana na kona iliyopigwa na mshambuliaji Christopher Edward
wa Simba.
Licha ya kuwapo kwa msitu wa wachezaji wa
timu zote, shuti kali la kiungo huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars, pia
lilikwenda kutinga moja kwa moja kwenye nyavu za juu kupitia karibu
kabisa na kona ya kulia mwa lango la wapinzani hao.
Akiwa ametiwa hamasa na bao kali hilo,
Mkude alikaribia kuipa Simba bao la pili, na kwa staili ile ile, dakika
nne kabla ya filimbi ya mwisho lakini shuti lake kali la mbali liliguswa
kidogo na kipa wa Prisons Beno David na kuwa kona.
Prisons ambayo kwa kipigo hicho inabaki na
pointi saba baada ya mechi nane, ingeweza kulinganisha idadi ya michezo
na alama zake hata hivyo kama ama mshambuliaji Peter Michael angepiga
shuti la nguvu zaidi ama beki Joseph Owino asingekuwa mahala muafaka
wakati muafaka, mwishoni kabisa mwa mchezo.
Mpira wa juu uliodakwa na kipa Abel Dhaira
katika dakika ya 89 ulionekana kuwa usingekuwa na madhara yoyote
langoni mwa Simba lakini wakati akianguka ardhini, mpira uliponyoka
mikononi mwa Mganda huyo na kutua kwenye mguu wa kulia wa Michael.
Shuti lake dhaifu wakati akikabwa na
Gilbert Kaze liliokolewa na Owino wakati likielekea nyavuni Mganda huyo
akiwa alikuwa amesimama kwenye mstari wa goli wakati wa shambulizi hilo
la mwisho la mechi likifanyika.
Timu zilikuwa:
SIMBA: Abel Dhaira, Nasoro Iddi, Omar
Salum (Haruna Shamte dk.38), Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude,
Ramadhani Singano, Abulhalim Humud, Amis Tambwe, Edward Chritopher
(Zahoro Pazi dk.67), Harun Chanongo.
PRISONS: Beno David, Kimenya Mashaka,
Laurian Mpalile, Nurdin Issa, Mwangama Lugano, Nimkaza Jumanne, Kwanga
Julius, Jimmy Shoji, Peter Michael, Omega Seme, Jeremiah Mgunda.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment