Ndugu zangu,
Yanayotokea katika nchi yetu kwa sasa
yanatutaka tufikiri kwa bidii. Kama nchi kuna safari tumeifunga. Na
tulivyo Waafrika, tu mahodari wa kufunga safari, lakini si mahodari wa
kupanga safari. Kufunga na kupanga safari ni vitu viwili tofauti.
Ndugu zangu,
Ni vigumu leo kwa Wana wa Israel
kuamua kurudi tena Misri, hata kama, pamoja na chawa na kunguni
walioaacha Misri, bado, kuna wanaokumbuka samaki na masufuria ya pilau
waliyoayaacha Misri. Lakini, kijamii, na kwa kuingalia jamii yetu hii
ilikotoka, ilipo sasa na inakoelekea, na tuone sasa, kuwa hakuna ugumu
wa kurudi tena Misri. Na hapa nitazungumzia umuhimu wa sisi WaTanzania
kujitambua.
Nahofia, kuwa moja ya kiini ya haya
yanayotukuta sasa ni dhambi ya Ubaguzi iliyoanza kututafuna pole pole.
Taratibu tunapoteza uwezo wetu wa kujitambua. Ni ukweli sasa, kuwa
Watanzania hatujitambui, na kibaya zaidi, baadhi ya viongozi wetu wa
kisiasa na kidini wanapoonyesha wazi wazi kuwa hawajitambui.
Maana, tumeanza sasa kuzungumza lugha
za ' Wao Wakristo' na ' Sisi Waislamu'. Tunasahau, kuwa sisi ni ndugu wa
damu. Kuwa SISI ni Watanzania Kwanza. Na lililo la kwanza kwetu ni '
Nchi Yetu' na maslahi yake.
Hii ni Nchi Yetu Sote. Kila Mtanzania
kwa nafasi yake ana lazima ya kupigania Usalama wa Taifa letu. Usalama
wa Nchi Yetu tuliyozaliwa. Hatuwezi kuilinda na kuijenga Nchi Yetu
kwenye mazingira ya kubaguana. Kwenye mazingira ya kugawanyika kwa
misingi ya udini, ukabila na rangi. Na hapa nitamrejea tena Baba wa
Taifa, Mwalimu Nyerere na dhana ya Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa.
Ni Mwalimu Nyerere aliyeuanzisha na
kuusimamia mradi mkubwa wa Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa, hata hivyo,
tunaona sasa unavyoporomoka na kuliacha taifa letu mashakani. Ndio,
Mwalimu alijenga misingi imara ya Ujenzi wa Umoja Wa Kitaifa ( Nation
Building).
Kuijenga jamii ya Watanzania yenye
kuamini kwenye ukweli kuwa sisi sote ni ndugu. Kwamba Nchi yetu haina
dini. Yenye kupiga vita ubaguzi wa aina zote, iwe wa rangi, kabila au
dini. Ilimchukua Mwalimu na taifa letu miaka mingi sana kuijenga misingi
hiyo iliyowawezesha pia Watanzania kuwa na mioyo ya uzalendo kwa Taifa
lao.
Tunaona sasa, kazi hiyo iliyochukua
miaka mingi, kutokana na ubinafsi na uroho wa madaraka ya baadhi ya
wanasiasa wetu, wanapelekea kubomoka kwa misingi hiyo na kuliacha taifa
letu kwenye hatari ya kuangamia.
Ndio, msingi wake ni ubaguzi wa
kisiasa unaotokana na ubinafsi na tamaa ya mali kwa baadhi ya tuliowapa
dhamana za kufanya maamuzi makubwa kwa niaba yetu. Ni hali ya baadhi ya
tuliowapa dhamana za uongozi kuishiwa chembe chembe za uzalendo; mapenzi
kwa nchi yao.Ni watu wenye kulinda maslahi yao na ya wanaowazunguka.
Wako tayari hata kutumia mbinu za Umafia kutimiza malengo yao. Kuna
Watanzania wengi sasa wanaopoteza mioyo ya uzalendo kwa nchi yao.
Kuna hata wenye kufikia kutamka; 'Nchi
hii ina wenyewe'. Kuna anayetamka hilo kwa lengo la kumtishia mwenzake
au kulazimisha kitu fulani kifanyike. Lakini, kuna wenye kutamka hivyo
kuashiria kukata tamaa. Kuwa hata wafanye nini, hakuna anayewasikiliza
ama kuwajali. Hizi si dalili njema kwa taifa. Kuna wanaoiba mali ya umma
mchana wa jua kali. Hakuna anayewagusa.
Ukiuliza utajibiwa; "Ah! Nchi ina
wenyewe!". Kwamba kuna baadhi yetu hawajisikii kuguswa na nchi hii,
hawajisikii kuwa na nguvu ya kupiga vita maovu yanayotusumbua. Baadhi
yetu wameanza kupungukiwa na mapenzi na nchi yao.
Juni 16, 2004 nilipata kuandika hili
kwenye gazeti la Majira; kuwa Tanzania ina vyote, kasoro Watanzania.
Niliandika; kuwa Tanzania ni nchi nzuri sana. Ni nchi ya kujivunia.
Kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana kwa eneo. Ni nchi yenye rasilimali
nyingi; ardhi yenye rutuba, mito, maziwa, milima, mabonde, bahari na
vivutio vingi vya asili.
Hata hivyo, Tanzania ni moja ya nchi
masikini sana duniani. Kwa nini? Ndio, kikubwa kinachokosekana Tanzania
ni Watanzania. Tanzania tunayoijenga sasa ni mkusanyiko tu wa watu wa
makundi mbali mbali wenye kwenda kwa staili ya 'kila mtu na lwake'.
Idadi ya Watanzania wenye uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi
kupungua. Ubinafsi umekithiri, na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye
kufanywa na viongozi.
Ndugu zangu, Hakuna ugumu wa kurudi Misri. Tuna lazima ya kupanga safari ya kurudi tena Misri. Inawezekana.
Ni Neno la Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252
0754 678 252
No comments:
Post a Comment