MMETUPORA KILA KILICHO CHETU, TUACHIENI NYERERE WETU
Na Mwl. Sabatho Nyamsenda
Na Mwl. Sabatho Nyamsenda
Wanyonge walia, waporaji washerehekea
Siku ya leo nchi yetu inaadhimisha
miaka 14 tangu kuondokewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.Hivyo, leo ni siku ya furaha na huzuni; ni siku ya harusi na
matanga. Kwa waporaji, wanyonyaji, wabaguzi wa rangi, wadini na
wakabila, leo ni siku ya kunywa mvinyo na kusherehekea. Ule mwiba
uliowachoma siku zote na kuwakosesha raha hatimaye uliondoka siku kama
ya leo, nao wakapata nafasi ya kutamba.
Kwa wanyonge – wakulima wadogo,
wafugaji wadogo, warina asali, waokota makopo, wafagia barabara, wabeba
zege, machinga, mama ntiliye, wafanyakazi wa ngazi za chini, na wote
wanaoishi katika dhiki na kukosa huduma bora za afya, maji, elimu na
malazi – leo ni siku ya huzuni. Lile jabali lililoongoza mapambano yao
hatimaye lilistaafu rasmi kazi ya kupambana siku
kama ya leo. Nyerere, msemaji wa wanyonge, akaacha kusema. Kambarage,
mshairi wa makabwela, akaacha rasmi utunzi wa mashairi. Julius, mfasiri
wa vitabu, akaweka kalamu chini huku akiwa amekamilisha kutafsiri kwa
Kiswahili kitabu cha mwanafalsafa wa Kiyunani, Plato, kiitwacho ''The
Republic''. Mwalimu wa wanyonge akakoma kufundisha. Akatulia tuli.
Akalala usingizi wa kudumu.(P.T)
Tufurahie maisha yake kuliko kuomboleza kifo chake
Je, ni sahihi kwa wanyonge kulia? Ni
haki kwa wanyonge kuomboleza? Kulia na kuomboleza ni haki ya kila
ampotezae mpendwa wake. Lakini kwa kuwa Nyerere alikuwa binadamu wa
kawaida na sio malaika aliyeshushwa toka angani hatukutegemea kwamba
ataishi milele. Binadamu huzaliwa, hukua, huzeeka, huugua, hufariki.
Ndicho kilichotokea kwa Mwalimu. Pengine siku ya leo yapaswa kuwa siku
ya kufurahia maisha ya Mwalimu kuliko kuhuzunikia kifo chake. Kwa maana
hiyo, siku kama ya leo twapaswa kuzitafakari kwa kina fikra zake na
jinsi tutakavyozitumia kuendeleza mapambano ya wanyonge.
Nyerere hajafa, sisi ndio Nyerere
Aina hii ya kumwenzi kiongozi wa mapambano kwa kuendeleza yale aliyoyapigania niliiona kwa Wavenezuela walipoondokewa na shujaa wao wa mapinduzi ya kidemokrasia, rais wa wanyonge, Hugo Chavez, alipofariki mwezi machi mwaka huu. Nilipowaona katika televisheni mamilioni ya wanyonge wa Venezuela wakitiririkwa na machozi, nilidhani huo ndio mwisho wa mapinduzi ya kijamaa ya kibolivari (The Bolivarian Socialist Revolution) waliyoyaasisi wanyonge wa nchi hiyo wakiongozwa Chavez.
Aina hii ya kumwenzi kiongozi wa mapambano kwa kuendeleza yale aliyoyapigania niliiona kwa Wavenezuela walipoondokewa na shujaa wao wa mapinduzi ya kidemokrasia, rais wa wanyonge, Hugo Chavez, alipofariki mwezi machi mwaka huu. Nilipowaona katika televisheni mamilioni ya wanyonge wa Venezuela wakitiririkwa na machozi, nilidhani huo ndio mwisho wa mapinduzi ya kijamaa ya kibolivari (The Bolivarian Socialist Revolution) waliyoyaasisi wanyonge wa nchi hiyo wakiongozwa Chavez.
Kilichonitisha zaidi ni jinsi viongozi
wa mataifa ya mabeberu, na hasa Barack Obama wa Marekani, walivyotoa
kauli za kusherehekea kifo cha gwiji hilo la mapambano. Na mabeberu
walikuwa na haki kushangilia kifo hicho kwani ni Chavez aliyehakikisha
kuwa utajiri wa mafuta ya nchi hiyo unaenda kuwafaidisha wanyonge kwa
kuwapatia hudumu bora za kijamii zisizo na malipo. Mawakala wa ubeberu
nchini Venezuela wakisaidiwa na majasusi wa Marekani walijaribu
kumpindua Chavez lakini mamilioni ya wanyonge waliandamana hadi
aliporejeshwa madarakani.
Lakini kauli za wanyonge wa Venezuela
zilinipa matumaini: pamoja na kutiririkwa machozi, walipohojiwa na
waandishi wa nchi za Magharibi juu ya kifo cha kiongozi wao, walijibu:
''Chavez hajafa. Sisi ndio Chavez''. Kwa kauli hiyo wanyonge walikula
yamini kuendeleza mapinduzi ya kijamaa na kuhakikisha kuwa utajiri wa
nchi yao unaendelea kuwafaidisha wanyonge badala ya kikundi kidogo cha
mawakala wa mabeberu na mabwana wao.
Tena wanyonge wa Venezuela wameonyesha
mshikamano wa kitabaka na wanyonge wa nchi nyingine kama Cuba, Ecuador,
Nicaragua na Bolivia ambazo zote zinaongozwa na serikali za kijamaa.
Mathalani, Cuba yenye madaktari wengi waliobobea huwapeleka Venezuela
ili kutoa huduma za afya kwa wanyonge mijini na vijijini, wakati
Venezuela ikiipatia Cuba mafuta kwa bei rahisi na kuisaidia kiuchumi ili
iondokane na hali ngumu inayosababishwa na vikwazo vya Marekani.
Kambarage mpinga unyanyasaji
Historia ya Kambarage inaonyesha kuwa
tangu akiwa mdogo alichukia kila aina ya uonevu, ubaguzi, unyanyasaji na
ukandamizaji. Akiwa mtoto mdogo, Kambarage alikuwa akimsindikiza mama
yake shambani ; mama akiwa analima, Kambarage alikuwa akimbembeleza
mdogo wake. Huruma ilikiwa ikimwingia Kambarage kumwona mama yake
akifanya kazi za suluba siku nzima bila kupumzika. Hivyo akabuni mbinu
ya kumpumzisha mama yake. Akawa anamfinya mdogo wake, na kitoto kile
kichanga kikawa kikitoa kilio kikali, kilio kilichomfanya mama adhani
kuwa kichanga yule ana njaa. Hivyo, mama akaacha kulima na kuja
kumnyonyesha mwanawe. Kamnyonyesha mtoto, lakini pia kapumzika.
Kambarage alitabasamu na kujiona mshindi, hata kama ushindi wenyewe
ulikuwa wa muda mfupi tu.
Miaka mingi sana baadaye kitoto hiki,
ki-Kambarage, sasa akiwa kijana wa umri wa miaka 22 na mwanafunzi wa
Makerere aliandika insha ya kiswahili iliyoitwa ''Uhuru wa Wanawake''.
Ndani ya insha hiyo kijana Julius aliichambua na kuilaani mifumo ya
jamii zetu za Kiafrika iliyokuwa ikiwakandamiza na kuwanyanyasa wanawake
kana kwamba wao si binadamu kamili. Na ni mfumo wa kikoloni ulichochea
moto na kuhalalisha mfumo dume.
Insha hiyo, ambayo ambayo ilishinda tuzo ya Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki kwa wakati huo, na sasa imechapwa katika kitabu, inaishia na kisa cha kifaranga cha tai kilichochanganywa na kuku, kikalishwa chakula cha kuku, hata chenyewe kudhani ni kuku. Lakini tai huyo alipopelekwa kilimani na mtaalamu wa wanyama, na kuambiwa: tai, wewe sio kuku, kwako ni angani, hivyo ruka uende angani. Tai akaruka na kupotelea mawinguni. Kwa kutumia mfano huo, Nyerere akawataka wanawake kutokubali madhila ya mfumo kandamizi unaowaaminisha kuwa wao ni kuku, warukia chini, ilhali wao ni tai, warukia juu. Hivyo walipaswa kuruka na kupaa.
Insha hiyo, ambayo ambayo ilishinda tuzo ya Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki kwa wakati huo, na sasa imechapwa katika kitabu, inaishia na kisa cha kifaranga cha tai kilichochanganywa na kuku, kikalishwa chakula cha kuku, hata chenyewe kudhani ni kuku. Lakini tai huyo alipopelekwa kilimani na mtaalamu wa wanyama, na kuambiwa: tai, wewe sio kuku, kwako ni angani, hivyo ruka uende angani. Tai akaruka na kupotelea mawinguni. Kwa kutumia mfano huo, Nyerere akawataka wanawake kutokubali madhila ya mfumo kandamizi unaowaaminisha kuwa wao ni kuku, warukia chini, ilhali wao ni tai, warukia juu. Hivyo walipaswa kuruka na kupaa.
Hata hivyo mtazamo wa Mwalimu haukuwa
finyu kwa kudhani kuwa ni wanawake pekee ndio waliokandamizwa na
kunyimwa fursa. Mfumo wa kibepari, ambao kwa wakati huo ulichukua sura
ya ukoloni, uliwakandamiza wanyonge wote, wake kwa waume, katika Afrika
na mabara mengine. Hivyo, wanyonge wote walipaswa kupambana na kuushinda
ukoloni. Ndio maana Nyerere alikuwa mbele kuongoza mapambano dhidi ya
ukoloni, ubaguzi wa rangi na ukandamizaji, katika Afrika na dunia nzima
kwa ujumla.
Julius asiyenunulika
Shuleni Tabora, Julius alipewa
ukiranja. Hii ilitokea baada ya yeye kuamua kuacha shule kutokana na
kunyamazishwa na mwalimu mkuu wakati wa mdahalo. Kambarage alikuwa
ametoa hoja za kupinga uonevu na unyonyaji wa serikali ya kikoloni hali
iliyomwudhi mwalimu mkuu wa kizungu na kumwamuru akae chini. Kwa nini
anyamazishwe? Mwanafunzi huyo aliamua kufunga virago vyake na kurudi
kwao lakini utawala wa shule kwa kushirikiana na serikali ya kikoloni
walimkatiza na kumrudisha shuleni kisha wakampatia uongozi.
Kama walimu wa kikoloni walidhani kwa
kumpa ukiranja walikuwa wamemnunua Julius basi walikuwa wakiota ndoto
mchana kweupe. Ukiranja wa shule ulimpa Kambarage haki ya kupata nusu
lita ya maziwa kila siku, ilhali wasio viranja walipata robo lita. Ni
Kambarage, si mwingine, aliyeongoza mgomo wa wanafunzi kupinga ubaguzi
huo na kudai wanafunzi wote wapate mgao sawa wa maziwa. Mgao huwa wa
kibaguzi ukakoma. Tayari Nyerere alishaanza kupigania usawa.
Miongo kadhaa baadae serikali ya
kikoloni ilimpatia ujumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika
(ubunge kwa wakati huo). Walidhani wamemnunua na kumnyamazisha. Lakini
alipoona hoja zake hazipewi nafasi Nyerere alijiuzulu ubunge huo na
kuyarejea maisha yake ya dhiki aliyokuwa akiishi baada ya kuacha kazi ya
ualimu. Alikataa kuwasaliti wanyonge.
Kipo kisa katika kitabu cha Mohamed
Said kiitwacho Uamuzi wa Busara wa Tabora kinachoonyesha maisha
aliyoishi Nyerere baada ya kuacha kazi ya ualimu iliyokuwa na mshahara
mnono kwa wakati huo ili kuongoza mapambano ya uhuru. Familia yake
ikakosa hata mlo wa kueleweka. Siku moja, akiwa hana hata senti moja
mfukoni, Mwalimu aliamua kutembea kwa mguu toka nyumbani kwake Magomeni
hadi Kariakoo, akitegemea huenda atabahatisha kupata chakula. Njiani
akakutana na mzee Msume Kiate, mwana TANU ambaye alikuwa akifanya
biashara ya kuuza samaki. Baada ya kusikiliza shida ya Mwalimu, mzee
Kiate akampatia shilingi mia mbili akanunue mahitaji yake. Na baada ya
hapo mzee Kiate na wana TANU wenzake walijitolea kuihudumia familia ya
Mwalimu kwa chakula na wakaendelea kufanya hivyo hata baada ya uhuru
kupatikana. Tunapomkumbuka Nyerere tunapaswa pia kuwakumbuka mashujaa
wengine, kama Mshume Kiate, ambao vitabu vingi vya historia havitaji
majina yao.
Mwalimu Nyerere, kiongozi wa makabwela
Kitabaka, Mwalimu hakuwa katika kundi
la makabwela. Kwa kuzaliwa katika familia ya kichifu tayari alikuwa na
fursa ambazo watoto wengine hawakuwa nazo. Moja ya fursa hizo ilikuwa
elimu. Lakini elimu ikamfungua na kuiona dunia. Kadiri ilivyomfungua
ndivyo ilivyomtenganisha na watu wake. Toka Butiama akaenda Musoma, toka
Musoma akapita Mwanza, Shinyanga hadi Tabora. Akavuka mipaka ya kijiji
na mikoa. Akavuka mipaka ya nchi, akaenda Uganda. Akavuka mipaka ya
bara, akaenda Uingereza. Elimu yake haikumvusha mipaka ya ramani tu bali
mipaka ya kitabaka. Kadiri alivyoongeza vidato na shahada ndivyo
alivyolihama tabaka la "walalahoi".
Lakini japokuwa kitabaka alikuwa
katika "walalahai" kabla ya uhuru, na kuhamia katika "walalaheri" baada
ya uhuru, Mwalimu mwenyewe aliamua kwa makusudi kabisa kuliasi tabaka
lake. Hivyo usomi wake haukuwa na bei (exchange value) bali ulikuwa na
thamani (use value). Katika fikra za Mwalimu, msomi anayejitapa kuwa
yeye hawezi kutumika kwa wanyonge mpaka alipwe kiasi fulani cha fedha
huyo si binadamu kamili bali ni mtumwa. Binadamu pekee mwenye bei na
anayeuzika sokoni ni mtumwa.
Ndio maana hata baada ya kutoka
Uingereza, akiwa Mtanganyika wa kwanza kupata shahada ya umahiri
(master's degree), Mwalimu hakuhangaika kutafuta fursa za kujitajirisha
na kuishi maisha ya anasa. Kwa kuwa maslahi hayo ya kitabaka alishayaaga
haikuwa vigumu kwake kuachia nyadhifa zenye malipo manono ili
akawapiganie wanyonge.
Hata baada ya kukaa Ikulu kwa zaidi ya
miaka 20, alifanikiwa kujenga kajumba kadogo na ka kawaida kabisa
kijijini Butiama, na nyumba yake ya Msasani aliijenga kwa mkopo ambao
hata hivyo alishindwa kuumalizia, na kuiomba serikali imalizie mkopo na
kuchukua nyumba hiyo. Serikali ya Mwinyi ikafanya hivyo lakini ikampatia
Mwalimu nyumba hiyo. Mwaka 1966 Mwalimu alikata mshahara wake kwa
asilimia 20. Wakati huo alikuwa akipokea shilingi 5,000/=, hivyo
akabakia na shilingi 4,000/= na hakuwahi kujiongezea mshahara mpaka
anaondoka madarakani. Hivyo, wapo watumishi wengi kabisa wa serikali,
wakiwemo maprofesa, waliopokea mshahara mkubwa kumzidi.
Azimio liliwajali wanyonge
Lakini kutopenda mali inaweza kuwa hulka ya mtu yeyote kabisa. Mkristo au mwislamu mzuri, anayeamini katika pepo ya baadae, hawezi kujikita katika anasa za kidunia. Ila Nyerere alifanya hivyo si kwa sababu ya ukristo wake, ila kwa sababu ya itikadi iliyomwongoza, itikadi ya kijamaa. Ndiyo maana, baada ya kuwaona viongozi wenzake wanatumia nyadhifa zao kujitajirisha, aliasisi Azimio la Arusha, ambalo pamoja na mambo mengine liliwazuia viongozi kumiliki nyumba za kupangisha, kupokea mishahara miwili au zaidi na kumiliki hisa au kuwa wakurugenzi katika kampuni za kibepari.
Lakini kutopenda mali inaweza kuwa hulka ya mtu yeyote kabisa. Mkristo au mwislamu mzuri, anayeamini katika pepo ya baadae, hawezi kujikita katika anasa za kidunia. Ila Nyerere alifanya hivyo si kwa sababu ya ukristo wake, ila kwa sababu ya itikadi iliyomwongoza, itikadi ya kijamaa. Ndiyo maana, baada ya kuwaona viongozi wenzake wanatumia nyadhifa zao kujitajirisha, aliasisi Azimio la Arusha, ambalo pamoja na mambo mengine liliwazuia viongozi kumiliki nyumba za kupangisha, kupokea mishahara miwili au zaidi na kumiliki hisa au kuwa wakurugenzi katika kampuni za kibepari.
Kupitia Azimio la Arusha, njia kuu za
uzalishaji-mali na rasilimali za taifa, kama viwanda, mabenki, misitu,
madini, ardhi, njia na vyombo vya usafiri wa anga, reli na maji,
viliwekwa mikononi mwa umma. Umma wa wanyonge ulichagua serikali kwa
njia ya kidemokrasia, serikali ambayo ilipewa jukumu la kusimamia
rasilimali hizo kwa niaba ya wanyonge. Faida inayozalishwa ilitakiwa
kwenda kuwahudumia wanyonge, na sio kikundi cha watawala. Azimio
lilisisitiza juu ya kuwajali wakulima vijijini, na kuonya juu ya misaada
kutoka ughaibuni.
Azimio likahujumiwa na kupinduliwa
Kama inavyofahamika, wanyonge, wake kwa waume, vijana kwa wazee, waliandamana nchi nzima kuunga mkono Azimio la Arusha. Lilikuwa ramani yao kuelekea nchi ya usawa na matumaini. Lakini hata hivyo, utekelezaji wa Azimio uliwekwa mikononi mwa watu walewale walioanza kujitajirisha. Japo katika miaka ya 1970 sera za kijamaa zilifanya vema na serikali ikaanza kuonyesha mafanikio katika kutoa hudumu bora kwa jamii bila malipo, hali ilibadilika katika kipindi cha miaka ya 1980.
Kama inavyofahamika, wanyonge, wake kwa waume, vijana kwa wazee, waliandamana nchi nzima kuunga mkono Azimio la Arusha. Lilikuwa ramani yao kuelekea nchi ya usawa na matumaini. Lakini hata hivyo, utekelezaji wa Azimio uliwekwa mikononi mwa watu walewale walioanza kujitajirisha. Japo katika miaka ya 1970 sera za kijamaa zilifanya vema na serikali ikaanza kuonyesha mafanikio katika kutoa hudumu bora kwa jamii bila malipo, hali ilibadilika katika kipindi cha miaka ya 1980.
Nchi za kibeberu, Marekani na
Uingereza, zilishikwa na waumini wa sera za uliberali mambo-leo na hivyo
kuzilazimisha nchi maskini kufuata sera hizo kwa kubinafsisha kila
kilichotaifishwa, kufuta ruzuku katika kilimo na vyakula, na kuacha mara
moja kutoa huduma zisizo na malipo. Ndani ya nchi, tena Mwalimu akiwa
bado madarakani, sera hizi zilipata mashabiki wengi. Wachache
walijionyesha waziwazi. Wengi walijificha na kuendelea kuhujumu chini
chini.
Nchi ikiwa imetoka vitani, bidhaa za
msingi zikawa hazipatikani. Zilikuwa zimehodhiwa na kikundi cha watu
wachache, baadhi wakiwa katika dola na baadhi nje ya dola. Hivyo, baada
ya vita vya Uganda, Mwalimu alikuwa na vita viwili vya kupigana: vita
dhidi ya wahujumu uchumi/ujamaa ndani ya nchi, na vita dhidi ya mabeberu
nje ya nchi. Makundi hayo yalikuwa yakishirikiana kwa ukaribu sana, na
hata yakafanikiwa kuupindua Ujamaa baada ya Mwalimu kung'atuka.
Sera za kiporaji
Uzoefu wa zaidi ya miaka 25 ya
utekelezaji wa sera za uliberali mambo-leo umetuonyesha kuwa mfumo huu
ni katili zaidi pengine kuliko hata biashara ya utumwa na ukoloni.
Rasilimali za wanyonge zinaporwa, na wanyonge wanapojaribu kupinga
hutumiwa majeshi na serikali zao au za mabeberu. Tumeyaona hayo nchini
mwetu. Pia tumeyaona barani kwetu na duniani kote mifano ikiwa ni
uvamizi wa Libya na Iraq uliopelekea kuchinjwa kwa viongozi wa nchi
hizo, na mamilioni ya wanyonge kuuawa.
Akihutubia mjini Mbeya katika sherehe
za Mei Mosi mwaka 1995, Mwalimu aliziita sera za ubinafsishaji na
uwekezaji kuwa ni za kinyang'anyi. Akasema kuwa zitazalisha mabilionea,
lakini watakuwa wachache. Lakini pia zitazalisha maskini, na hao
watakuwa wengi sana. Hayo ndiyo yatokeayo nchini mwetu na duniani kote.
Jengeni sanamu zake, sisi tutazienzi fikra zake
Mwaka mmoja kabla ya kufariki Mwalimu alikuwa ametabiri kuwa ipo siku Tanzania itarejea katika misingi ya Azimio la Arusha. Katika Kongamano la kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha, Profesa Issa Shivji naye pia alisisitiza juu ya uwepo wa dalili zinazoonyesha kuwa Watanzania walio wengi wameanza kupigania kurudi katika misingi ya Azimio la Arusha lakini akaonya kuwa dalili hizo zinaweza kuzimwa na kakundi ka watu wachache kanakofaidika na mfumo uliopo.
Mwaka mmoja kabla ya kufariki Mwalimu alikuwa ametabiri kuwa ipo siku Tanzania itarejea katika misingi ya Azimio la Arusha. Katika Kongamano la kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha, Profesa Issa Shivji naye pia alisisitiza juu ya uwepo wa dalili zinazoonyesha kuwa Watanzania walio wengi wameanza kupigania kurudi katika misingi ya Azimio la Arusha lakini akaonya kuwa dalili hizo zinaweza kuzimwa na kakundi ka watu wachache kanakofaidika na mfumo uliopo.
Nafikiri kuwa miongoni mwa mbinu za
kuzima dalili hizo ni kuhodhi jina la Mwalimu huku wakijidai wanamuenzi.
Eti wanamuenzi kwa kuongeza idadi ya sanamu zake, na taasisi na viwanja
vyenye jina lake ilhali Mwalimu mwenyewe alishakataa hayo tangu akiwa
hai. Wakijidai kugusia fikra zake basi wanamhubiri kama mpenda amani na
umoja. Lakini ni Mwalimu mwenyewe aliyesema kuwa mahali pasipo na haki
(justice) wala usawa (equity) hapawezi kuwa na amani. Pia hauwezi kuwa
na umoja kati ya wanyonyaji/waporaji wachache na mafukara wengi.
Ili nisionekane nabandika maneno
katika mdomo wa Mwalimu, nitanukuu sehemu ya hotuba yake aliyoitoa mwezi
mei mwaka 1989 wakati akifungua semina ya wazalishaji wakubwa
iliyoandaliwa na Chama cha Mapinduzi:
"Si kwamba Azimio la Arusha limeondoa
umaskini hata kidogo, wala halikutoa ahadi hiyo. Azimio la Arusha
limetoa ahadi ya matumaini. Ya haki, ahadi ya matumaini kwa wengi, ndio
watu wengi wa Tanzania wanaendelea na kuwa na matumaini hayo. Madhali
yapo matumaini hayo, mtaendelea kuwa na amani... Kama wengi hawana
matumaini, tunajenga 'volcano'. Siku moja italipuka na lazima ilipuke.
Isipokuwa watu hao wajinga. Wengi wa nchi hiyo wajinga, wanakubali
kutawaliwa hivi hivi. Kuonewa hivi hivi na wingi wanao, wajinga hao. Kwa
hiyo, Watanzania hawa watakuwa wajinga, wapumbavu, kama wataendelea
kukubali kuonewa na watu wachache katika nchi yao. Kwa nini?''
Waporaji wa rasilimali za nchi,
wavunaji wa jasho la wanyonge, vibaraka wa mabeberu (wasemao 'tunapendwa
huko nje') hawana haki ya kutumia jina la Mwalimu. Wametupora kila
kilicho chetu (tangu viwanda, ardhi, madini hadi nyumba),
wamewanyang'anya wanyonge haki ya kupata huduma bora za afya, elimu,
malazi na chakula. Hawa hawana haki ya kutaja jina la Mwalimu. Njia
ambayo wanyonge wanaweza kumuenzi Mwalimu ni kwa kuzichambua kwa kina
fira zake, na hasa Azimio la Arusha, na kuzitumia kama silaha ya
mapambano!
Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa
Umma. Anapatikana kwa barua-pepe:
sany7th@yahoo.com
Source: http://www.wavuti.com/
No comments:
Post a Comment