Wafuasi wa dini ya Kiislamu jana
waliadhimisha Idd El-Haj katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania huku
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akitaka Watanzania wasahau suala
la maendeleo bila ya amani na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata)
likimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukutana na wapinzani.
Akihutubia Baraza la Idd El-Haj jana
katika Chuo Kikuu cha Taifa (Suza) kilichoko Mkoa wa Kusini Unguja,Dk
Shein alisema mipango ya maendeleo ya nchi haiwezi kufikiwa bila ya
kuwapo kwa mazingira ya amani na utulivu.
Alisema vitendo vya hujuma dhidi ya
raia vinavyofanyika kwa kutumia tindikali lazima vipigwe vita na
wananchi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
"Inafaa tuelewe kuwa, bila ya amani hatutoyafikia malengo tuliyojiwekea
ya kuendeleza ustawi wa nchi yetu na watu wake,"alisema Dk Shein.(P.T)
Dk Shein alisema kwamba vitendo vya
hujuma dhidi ya raia wasiokuwa na hatia vimekuwa vikisababisha hofu kwa
wananchi na wageni na vinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu
na mafundisho ya Mwenyezi Mungu dhidi ya waja wake.
Aidha alisema watalii wanaotembelea
Zanzibar wanavutiwa na ukarimu wa wananchi wake pamoja na hali ya amani
na historia ya visiwa vya Zanzibar.
"Tusichezee wala tusidharau amani
tuliyonayo badala yake,tuitunze na tuiendeleze kwani inapotoweka
inachukua muda mrefu kuirejesha sawa na kujenga nyumba ni kazi kuliko
kubomoa,"alisema Dk Shein.
Hata hivyo, aliwataka wananchi
kuunganisha nguvu zao kupitia vikundi vya Polisi jamii kwa kushirikiana
na vyombo vya dola kuwafichua watu wanaotaka kuchafua sifa ya Zanzibar.
Alisema kazi ya kulinda amani ya nchi
ni jukumu la kila mwananchi kuahidi Serikali itaendelea kuwasaka
wahusika wa vitendo hivyo na kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya
sheria.
Dk Shein alisema kuwa,Serikali
itaendelea kutekeleze dira ya Maendeleo ya 2020 pamoja na Mpango wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini kwa wananchi wake (MKUZA) na tayari
ufanisi wa mipango hiyo umeanza kuonekana licha ya kuwapo changamoto.
"Uchumi wetu umekuwa kwa asilimia 7.0
kutoka 6.7 kwa mwaka 2011 tofauti na ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.3
katika Bara la Afrika,"alisema Dk Shein.
Bakwata wamempongeza Rais Kikwete siku
moja baada ya Rais Kikwete kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi
wa vyama vya siasa vya CCM, Chadema,Cuf,NCCR-Mageuzi,TLP na UDP,Baraza
Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limepongeza hatua hiyo na kuita
yenye manufaa kwa taifa.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu
jijini Dar es Salaam juzi,Rais na vyama hivyo walikubaliana kwamba vyama
vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba,
viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na
maridhiano kwa lengo la kusukuma mbele mchakato huo kwa maslahi mapana
ya nchi yao na mustakabali wa taifa.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh
Suleiman Lolila akitoa salamu za Baraza la Idd jana katika Msikiti wa Al
Farouk uliopo Makao Makuu ya Baraza hilo, Kinondoni Dar es
Salaam,alisema uamuzi wa Rais Kikwete una lengo la kuhakikisha mchakato
wa Katiba unaoendelea unamalizika kwa amani.
Naye Mgeni rasmi kwenye baraza hilo,
Waziri wa Maji,Profesa Jumanne Maghembe, aliwataka Watanzania kuilinda
amani iliyopo nchini na kuepuka ushabiki wenye lengo la kuhatarisha
mustakabali wa amani nchini.
Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Ibrahim Yamola na Pamela Chilongola
No comments:
Post a Comment