NAREJEA somo la lugha ya Kiswahili na
narejea neno langu ninalolirejea mara kwa mara nikitumai kwamba siku moja, au
katika maeneo fulani, litaeleweka. Neno lenyewe ni ‘hamnazo.’
Neno hili ni mojawapo ya maneno
yanayotumika holela, kila mmoja anayelitumia akilipa maana na tafisri
inayompendeza yeye. Hii ni dalili mojawapo ya upuuzi tunaoufanya katika maeneo
mengi hapa nchini.
Nimewahi kutumia hadithi mojawapo kati
ya hadithi za kusisimua katika maandishi matakatifu kueleza umuhimu wa
maelewano ya kilugha. Simulizi hiyo inatuhadithia kwamba huko zamani, zama za
mitume na manabii, watu walijaa kiburi na jeuri iliyotokana na uwezo mkubwa wa
kiuchumi na ujuzi mkubwa wa kutenda mambo waliokuwa wamejijengea.
Kutokana na ujuzi huo na uwezo mkubwa
waliokuwa nao wakaamua kufanya jambo moja kubwa kuliko yote waliyokuwa
wameyafanya hadi wakati huo: wakaamua kujenga mnara mrefu ambao ungepanda hadi
juu mbinguni ili wafike huko na wajionee wenyewe maajabu ya mbingu na uwezo wa
Mungu.
Wakaanza kujenga kile kilichokuja
kujulikana kama Mnara wa Babel (Biblia, Kitabu cha Mwanzo, 11) . Wasanifu
majengo walikuwa nao wa kutosha, wahandisi na waashi mahiri walikuwa tele. Na
watu wote waliongea lugha moja iliyowafanya waelewane.
Inaelekea Bwana Mkubwa hakupenda jeuri ya
watu hawa, na akaamua kuwasambaratisha. Ili kuwasambaratisha Bwana Mkubwa
hakuwashushia radi wala tetemeko la ardhi kubomoa mnara ule, jambo ambalo bila
shaka angeweza kufanya. La hasha, aliwashushia kutoelewana katika lugha,
wakaisahau lugha yao, wakawa wanasemasema sana lakini hakuna anayemwelea
mwenzake. Mradi mzima ukasambaratika na mnara ule ukaporomoka.
Hadithi hii inatufundisha kwamba iwapo
tutaendelea kupoteza lugha na kujisemeasemea hovyo tutakuja kufika mahali
tushindwe kuelewana kabisa, na huo uwe ndio ukomo wa juhudi zetu za kujenga
taifa au jamii.
Sasa nirudi katika neno langu
‘hamnazo’. Kujifanya hamnazo ni kujibaraguza, kujifanya huoni, hujui,
huelewi au hutambui jambo ambalo kila mmoja analitambua ila wewe.
Ukweli ni kwamba wewe mwenyewe unalitambua
vilivyo jambo hilo, lakini unaangalia kando kwa sababu ukionyesha kwamba
unalitambua utahitajika kufanya jambo ambalo kwa sababu uzijuazo mwenyewe
hutaki kulifanya.
Kwa mfano sote tunajua kwamba dawa za
kulevya zimechangia mno kuwaharibu vijana wetu. Tunajua kwamba katika mitaa
yetu dawa hizi zinauzwa kama njugu na vijana wetu wamekuwa “mateja,” hali
ambayo imesababisha madhara makubwa katika jamii. Haya yote tunayajua.
Hivi sasa nchi yetu imepata sifa ya
hovyo, ya kuwa njia kuu ya kusafirishia dawa hizi, na vijana wetu wamekuwa kila
kinachoitwa ‘punda’ na hili limetangaa duniani kote. Wakuu wa usalama katika
vituo vya mipakani wanamuona kila mwenye pasi ya kusafiria ya Tanzania kama
mshukiwa.
Wakuu wa serikali yetu wanalijua hili,
lakini wanajifanya hamnazo, wanajibaraguza. Tuliwahi kuambiwa kwamba vinara wa
dawa za kulevya wanajulikana, kwa majina na kwa anwani. Pamoja na kujulikana
huko hawakamatwi, hawachukuliwi hatua, wanaachiwa waendelee kukua na kujitanua.
Tunaangalia duniani na tunaziona nchi
zilizovurugwa kutokana na biashara hii. Miaka ishirini iliyopita tulikuwa
tukizungumzia Colombia na akina Pablo Escobar. Huyu ndiye aliyejijengea nguvu
za kiuchumi kiasi kwamba hata alipokamatwa na kufungwa jela aliachiwa asanifu
jengo la jela atakamofungwa. Ilibidi serikali ijadiliane naye hadi wakubaliane
namna atakavyofungwa.
Hivi sasa tunazungumzia nchi nyingine
ambayo imekwisha nayo kugeuka kuwa ‘narco-state’ au dola-mihadarati, Mexico,
ambayo miaka michache iliyopita haikujulikana hivyo. Katika Bara la Afrika
tunayo Guinea-Bissau, ambayo imekuwa na zahama zisizoisha kwa sababu serikali
inaendeshwa na dawa za kulevya, na sehemu kubwa ya wanasiasa, wanajeshi, polisi
na wanausalama na mawakala wa biashara hiyo.
Waswahili wanasema, asiyejua kifo aangalie
kaburi, nami naongeza: Kaburi lako hutaliona wewe, hivyo angalia makaburi ya
wenzio. Ni busara kujifunza kutoka kwa makosa yako mwenyewe, lakini ni bora
kujifunza kutokana na makosa ya wenzako.
Ni kweli kwamba wanaosukuma biashara ya
dawa za kulevya wamejenga nguvu kubwa, na dalili mojawapo ni haya matukio ya
punda wanaotokana na nchi yetu wakibeba mizigo ya kifo. Ni kweli pia kwamba
sehemu kubwa ya siasa na utawala wa nchi yetu vinaendeshwa kwa fedha kwa maana
ya ununuzi wa kura na rushwa katika mifumo yetu yote ya utawala.
Sasa, kama fedha nyingi kiasi cha
kutisha ndio mtaji mkuu wa kutafuta ‘uongozi’ wa kisiasa na ukuu serikalini, na
kama biashra ya mihadarati ndiyo inayoingiza fedha nyingi kuliko biashara
nyingine yoyote, kwa nini anayesaka kiti cha ubunge au urais asifanye biashara
hiyo, hasa kama anajua kwamba hata akijulikana hakuna hatua zo zote
zitakazochukuliwa dhidi yake?
Aidha, iwapo imetokea kwamba
wajasiriamali wa mihadarati wanafanikiwa kuingiza fedha zao chafu ndani ya
siasa na utawala na wakaweza kupata nafasi za kuitawala nchi, ni kwa nini
wasihakikishe kwamba biashara hiyo inalindwa, inakuzwa, inaendelezwa na
kudumishwa? Nashuku kwamba hali hii tunayo tayari.
Ukweli ni kwamba tumekwisha kupelekea
‘siasa’ yetu sokoni, na ukishapeleka ‘siasa’ yako sokoni, huna budi kujua
kwamba itapata mnunuzi, na mwenye mtaji mkubwa zaidi ya wengine ndiye
atakayemudu kuinunua. Tayari hili linafanyika nchini, na hakuna anayebisha.
Ikifikia hapo, kilichobaki ni kukubali
kwamba, kwa njia moja au nyingine, serikali inayotokana na uuzaji na ununuzi wa
kura katika mazingira ambamo fedha iliyotumika katika biashara hiyo ni matunda
ya mihadarati, itakuwa ni serikali ya mihadarati na itajenga dola-mihadarati.
Serikali inayojifanya hamnazo mbele ya biashra hii ni wazi inafaidkia nayo.
Anayebisha tukutane miaka michache
ijayo.
Source:
http://raiamwema.co.tz: Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment