Mrisho Ngassa akipenya mabeki wa timu ya Ruvu
Shooting wakati timu hizo zilipomenyana jana katika uwanja wa Taifa Dar
es Salaam jana Yanga ilishinda 1-0.
Mrisho Ngasa alitoka katika kifungo cha mechi sita
jana na kuichochea Yanga kupata ushindi wake wa kwanza katika mechi nne
za ligi kuu ya Bara, ilipoifunga Ruvu Shooting 1-0 kwenye Uwanja wa
Taifa.
Kwa matokeo hayo Yanga ambayo ilikuwa
imeshinda tu mechi yake ya kwanza dhidi ya Ashanti imefikisha pointi
tisa kutokana na michezo sita, sawa na Ruvu ambayo imepoteza mechi ya
tatu katika sita pia.
Ngasa alifungiwa na shirikisho la soka,
TFF, kucheza mechi sita za kwanza za Yanga msimu huu, ukiwemo mchezo wa
Ngao ya Jamii wa Agosti 17, baada ya kuonekana na hatia ya kuchukua sh.
milioni 30 kwa Simba lakini akasajili Yanga.
Ilimchukua Ngasa dakika 40, hata hivyo,
kuanza hatari katika lango la Ruvu alipopiga shuti kali kutoka nje ya
eneo la hatari lakini likapanguliwa na mlinda mlango Abdul Seif wa timu
ya wageni.
Bao la Yanga lilifungwa na Hamisi Kiiza
kwa tiktaka baada ya saa moja ya mchezo, alipounganisha wavuni krosi ya
Ngasa ambaye alimtoka beki wa Ruvu na mchezaji wa zamani wa Yanga
Stephano Mwasika kwenye wingi ya kulia.
Kocha Ernie Brandt alisema timu yake ya
Yanga ilicheza vibaya licha ya ushindi iliyopata, lakini Ngasa alicheza
vizuri na kutoa mchango mkubwa katika kupata matokeo hayo.
Charles Mkwasa alisema Yanga ilitumia makosa ya timu yake ya Ruvu kupata ushindi huo.
Yanga ingeweza kwenda mapumziko ikiongoza
kwa angalau goli moja kama Mganda Kiiza asingempa mpira mikononi Seif,
kutokana na pasi ya akili ya Frank Domayo, katika dakika ya 39.
Tofauti na kukosa maarifa ya kufunga
magoli kulikopelekea mabingwa watetezi hao kutoka sare dhidi ya Coastal
Union, Mbeya City, Prisons na kufungwa na Azam kulikojitokeza katika
kipindi cha kwanza, Yanga ilibadilika katika ngwe ya pili.
Kutolewa kwa Domayo anayependelea pasi
fupifupi na kuingizwa kwa Athumani Iddi, kulimfanya kiungo huyo wa Taifa
Stars amechezeshe zaidi Ngasa kutokana na pasi zake toka nyuma
kuendeana na kasi ya winga huyo wa zamani wa Simba na Azam.
Katika mechi nyingine, Kagera Sugar
iliifunga Rhino Rangers 1-0 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Mgambo
Shooting na JKT Oljoro zilitoka suluhu kwenye Uwaja wa Mkwakwani na
mwanzo mzuri wa msimu wa Mbeya City uliendelea kwa sare ya 1-1 na
Coastal Union kwenye Uwanja wa Sokoine.
Timu zilikuwa:
YANGA: Ally Mustafa,
Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Frank Damayo
(Athumani Iddi dk.50), Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu,
Hamisi Kiiza, Mrisho Ngasa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment