Na Mwinyi Sadallah,
Zanzibar. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha ameelezea kushangazwa kwake na hatua za kutochukuliwa watu waliohusika na ufisadi wa Sh60 bilioni wakati wa utawala wa Rais Amani Abeid Karume.
Akihutumia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Polisi Ziwani mjini Unguja, Nahodha alisema ufisadi huo ulibainika baada ya uchunguzi wa Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi.
Nahodha alisema ripoti hiyo ilitaja hadi waliohusika na ufisadi huo lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
Nahodha ametoa tuhuma hizo licha ya ukweli kuwa kipindi cha utawala wa Karume, alikuwa Waziri Kiongozi kwa miaka 10.
Alisema fedha hizo zingeweza kusaidia kuimarisha huduma za jamii kama afya, elimu na upatikanaji wa maji safi na salama, lakini kinyume chake wanaharakati na wanasiasa wanashindwa kukemea ufisadi unaochangia kuikwamisha Zanzibar isipige hatua za kimaendeleo.
Waziri huyo wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alisema dhana ya kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 ilikuwa ni kuimarisha huduma za jamii kama utoaji wa elimu bure, umiliki wa ardhi kwa wananchi wanyonge na kupinga vitendo vya ubaguzi na matabaka.
Alisema suala hilo ni changamoto kwa CCM na viongozi wake ili kujiuliza na kutoa majawabu kwa kuwa chama hicho ndicho chenye dhamana ya utawala.
“Bila ya kutoa majibu sahihi kwa wananchi siku moja tutajikuta tukipotea uhalali,” alisema.
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment