- Profesa Baregu, Kabudi, Butiku wawasha moto
TUME ya Mabadiliko ya Katiba
inayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba, sasa inasuburi
uamuzi wa mwisho wa serikali kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa hivi karibuni bungeni, ili hatimaye kwa
pamoja wajumbe wa tume hiyo waamue kujiuzulu ama waendelee na majukumu yao,
Raia Mwema limeelezwa.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu mbalimbali
vya habari ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, katika kikao chake cha
mwanzoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, sehemu kubwa ya wajumbe
walikuja juu wakionyesha kukerwa na namna mabaraza ya katiba yalivyoingiliwa na
Chama cha Mapinduzi.
Mbali na kukerwa huko, vyanzo vyetu vya
habari vinaeleza kwamba wajumbe hao pia hawakubaliani na baadhi ya vifungu vya
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambao uliungwa
mkono na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Mbunge wa Vunjo (TLP)
Augustine Mrema na kwa upande mwingine, muswada huo ukipingwa na wabunge
wengine wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ambao walifikia hatua ya kupambana na
askari wa Bunge ndani ya ukumbi wa vikao vya Bunge.
Tayari Profesa Mwesiga Baregu
amemweleza mwandishi wetu kwamba wajumbe wa tume hiyo wanayo matumaini kwamba
serikali itaruhusu marekebisho ya baadhi ya vifungu vya muswada huo, ili
hatimaye Tume ya Mabadiliko ya Katiba iendelee na shughuli zake hadi katika
hatua ya mwisho ya awamu ya pili ya kura ya maoni, kama itakuwapo.
Kwa mujibu wa sheria ya awali ya
mabadiliko ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapaswa kuendelea ‘kuishi’
hata baada ya Bunge la Katiba ambalo linaweza kuhitaji ufafanuzi kuhusu
kilichomo ndani ya rasimu ya Katiba itakayowasilishwa katika tume hiyo.
Katika muswada wa sasa, inaelezwa
kwamba uongozi wa Bunge la Katiba unaweza kumwita Mwenyekiti wa Tume ya Katiba
au mjumbe yeyote kutoa ufafanuzi huku Tume hiyo ikiwa tayari imevunjwa, mara
baada ya rasimu ya Katiba itakayowasilishwa bungeni kukamilika.
Lakini kinyume cha mapendekezo ya sasa,
inashauriwa kama ilivyokuwa katika sheria ya awali, Tume iendelee kuwapo wakati
wote wa Bunge la Katiba na wakati wa upigaji kura ya maoni wa awamu ya kwanza
na hata awamu ya pili kama utakuwapo na wakati huo huo, Tume iendelee kuwa na
jukumu la kutoa elimu kuhusu rasimu ya Katiba husika.
Mvutano ndani ya Tume
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya
habari, katika kikao cha mwanzoni mwa wiki iliyopita kilichoongozwa na Jaji
Warioba, Kamishna wa Tume hiyo, Mzee Joseph Butiku aliendeleza msimamo wake wa
kujuta akisema kama angejua kutakuwa na uchakachuaji katika mchakato wa Katiba
Mpya asiyengekubali uteuzi wa kuwa kamishna.
Butiku anaelezwa kwenda mbali zaidi
akisema amekubali uteuzi wa kuwa kamishna wa Tume hiyo si kwa sababu ya shida
ya kupata pesa kwani amekwishazoea kuishi maisha ya bila kuwa na pesa,
isipokuwa amekubali kuwamo kwenye Tume hiyo ili kujenga, kutetea na kulinda mustakabali
bora wa nchi na vizazi vijavyo.
“Ndugu Mwenyekiti, sisi wengine
tumeingia humo katika hii Tume si kwa sababu ya kupata pesa kama baadhi ya watu
wanavyodhani.
Kwanza tumekwishazoea kwa miaka mingi
kuishi bila pesa,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kikimnukuu Butiku, ambaye
naye anatajwa kuwa tayari kuachia ngazi endapo kusudio la ‘kuchakachua’
mchakato wa Katiba Mpya litaendelezwa kupitia jaribio la muswada wa sasa kuhusu
Katiba Mpya.
Lakini pia chanzo chetu hicho
kinamnukuu Profesa Mwesiga Baregu naye akitishia kujiuzulu akiamini kwamba kazi
nzuri iliyokwishafanywa na Tume inalenga kuchakachuliwa, kwa kuivunja kwanza
Tume kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba na kazi ya Tume iwasilishwe na
kusimamiwa kwa kutumia chombo kingine ambacho pengine kinaweza kuwa na utiifu
wenye lengo la kuvuruga kazi ya kiungwana iliyofanywa na Tume ya Jaji Warioba.
“Mimi niko tayari kujiuzulu endapo hali
hii itakuwapo,” Profesa Baregu anatajwa kutamka maneno hayo kwa Jaji Warioba
huku Profesa Palamagamba Kabudi akitajwa kupingana wazi wazi na uamuzi wa
serikali kupitisha muswada ambao anaamini umejaa udhaifu mkubwa unaoruhusu
mchakato wa Katiba Mpya kuingiliwa na kisha kuharibiwa.
Jaji Warioba ahangaika kusaka
suluhu
Vyanzo vyetu vya habari serikalini,
katika vyama vya siasa na hata Ikulu ya Dar es Salaam vinapasha kwamba Jaji
Warioba, amelazimika kuingia katika ‘kibarua’ cha ziada kwa kutafuta suluhu
kuhusu suala hilo, na hasa baada ya kuona kile kinachoitwa ‘moto’ wa makamishna
katika tume yake. Lengo la jitihada hizo za Warioba zinatajwa kusaka suluhu ili
hatimaye mchakato wa Katiba Mpya uendelee kutekelezwa kwa kutanguliza
maridhiano na si ubabe.
Taarifa zaidi zinabainisha kwamba kwa
kiasi cha kuridhisha, Jaji Warioba, anaweza kufanikisha kuwapo kwa suluhu hiyo,
huku Rais Jakaya Kikwete akitajwa kumuunga mkono ‘kimya kimya’ katika juhudi
zake hizo za chini kwa chini.
Profesa Baregu avunja ukimya
Katika mazungumzo yake na mwandishi
wetu Jumanne wiki hii, Profesa Baregu alisema wajumbe wa Tume ya Katiba wako
tayari kujiuzulu mapema zaidi ili kujiondoa katika lawama ambazo zinaweza
kujitokeza mbele ya safari, kwamba Tume hiyo haikufanya kazi zake vizuri na kwa
weledi.
“Kimsingi, wajumbe wanaamini kasoro
hizi zitafanyiwa kazi kwa busara na weledi zaidi ili hatimaye mambo yaweze
kwenda vizuri kwa maslahi ya nchi yetu, sote tunaamini Tanzania ni muhimu
kuliko mambo mengine. Hata hivyo, kama matarajio hayo ya wajumbe hayatakwenda
kama wanavyoamini, basi ni kama tumekwisha kubaliana wote tujiondoe
(kujiuzulu),” anasema Profesa Baregu.
Alitaja baadhi ya kasoro zilizomo
katika muswada wa sasa wa mchakato wa Katiba kuwa ni pamoja na kuivunja Tume ya
Mabadiliko ya Katiba katika wakati mgumu wa kuwapo kwa Bunge la Katiba na pia
kuelekea kuwa na kura ya maoni.
Kwa mujibu wa Profesa Baregu, huo ni
wakati mgumu ambao Tume inapaswa kuwapo ‘hai’ ili kuweza kufafanua kazi
waliyoifanya katika kipindi chote cha kuanza na kuendelea kwa mchakato wa
Katiba Mpya.
“Inatia shaka kuweka vifungu vya kutaka
Tume ya Katiba ivunje, ‘isiwe hai’ wakati wa Bunge la Katiba halafu unasema tu
eti mwenyekiti au mmoja wa wajumbe wa Tume (iliyokwishavunjwa) anaweza kuitwa
bungeni kutoa ufafanuzi wa kazi iliyofanywa na Tume nzima,”!
Lakini pia wakati huo huo, unaitaka
Tume kutoa elimu ya uraia huku ukiwa na mchakato wa kura ya maoni ambayo
inaweza kuwa katika awamu mbili kwa mujibu wa sheria.
Kama awamu ya kwanza ya kura ya maoni
itashindwa kuzaa uamuzi, awamu ya pili ya kura ya maoni itaitishwa, wakati huo
huo unasema Tume iwe imekwishavunjwa, na kama awamu ya pili itashindikana basi
tutarejea katika Katiba ya zamani,”
Vyama vya upinzani vyaongoza upinzani
Wakati hayo yakiendelea ndani ya Tume
ya Mabadiliko ya Katiba ambako inaelezwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri
wa Katiba na Sheria wamekuwa na vikao na Jaji Joseph Warioba, vyama vikuu vya
upinzani, CHADEMA chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, NCCR-Mageuzi
chini ya Mwenyekiti wake James Mbatia na CUF-chini ya Mwenyekiti wake Profesa
Ibrahim Lipumba, wameanza mikutano ya kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete kutosaini
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
uliopitishwa na Bunge mjini Dodoma hivi karibuni.
Viongozi hao wamepanga kuendelea na
mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwa ni pamoja na
kuhamasisha makundi mengine ya kijamii kuungana kuupinga muswada huo.
Hata hivyo, viongozi hao wamekuwa
wakitilia mkazo zaidi kipengele cha muswada huo kinachompa nguvu Rais kuteua
majina ya watu wanaoweza kuwa wabunge wa Bunge la Katiba, mbali na wabunge
wanaotokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la
Wawakilishi Zanzibar.
Katika shinikizo lao, viongozi hao
wakuu wa upinzani wanataka Rais asipewe uhuru wa kuchagua majina kutoka kwenye
orodha ya majina yanayowasilishwa na taasisi mbalimbali kwake na zaidi ya hapo,
aondolewe uhuru wa kupuuza majina hayo na kuamua kuchagua majina nje ya orodha
hiyo.
Wanataka Rais apelekewe majina
yanayojitosheleza kwa mujibu wa idadi inayopaswa na kazi yake iwe ni kutangaza
tu majina husika.
Kauli za Mawaziri
Tayari Waziri wa Katiba na Sheria,
Mathias Chikawe amekaririwa akisema atamshangaa Rais Jakaya Kikwete asipotia
saini muswada huo na endapo hatatia saini, basi anaweza kuingia katika mgogoro
na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbali na Waziri Chikawe, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais – Uhusiano na Uratibu Steven Wassira, naye ametetea muswada
wa sasa na akitoa maneno ya kejeli kwamba safari hii Rais Kikwete hana muda wa
kuwaita Ikulu kwa ajili ya mazungumzo ya faragha kama alivyofanya awali, mara
baada ya kupitishwa kwa Muswada na hatimaye kuwapo kwa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba.
Chanzo:
raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment