WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, October 23, 2013

Siri ya sare Simba, Yanga

Mashabiki katika Mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa juzi uwanja wa Taifa na kutoka sare ya goli 3-3
Licha ya kugubikwa kwa siri kubwa ya matokeo ya mechi ya watani wa jadi iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3 Uwanja wa Taifa juzi, NIPASHE limebaini chanzo cha miamba hiyo kumaliza dakika 90 ikiwa nguvu sawa. 
Katika mechi hiyo ya raundi ya tisa ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo ambaye aliumudu vema mchezo huo, hadi timu hizo zinakwenda mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 3-0, hali iliyowafanya mashabiki wa timu hiyo kuamini kwamba wangeweza kulipa kipigo cha 5-0 walichokipata mwaka jana.

Yanga ambayo ilimiliki mpira kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Simba ilipata mabao yake kupitia kwa mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza na moja la kwanza kutoka kwa winga Mrisho Ngasa.

Hata hivyo, kipindi cha pili Simba iliwanyang'anya Yanga utawala wa mechi hiyo na kurejesha mabao yote matatu kupitia kwa Betram Mwombeki, Mganda Joseph Owino na Mrundi Gilbert Kaze, hiyo ikiwa rekodi mpya katika uwanja huo kwa mechi inayowakutanisha watani hao wa jadi mabao sita kufungwa goli moja.

Ubora wa Yanga dakika 45 za kwanza
Katika kipindi cha kwanza, Yanga haikufanya makosa kutokana na kucheza kandanda safi la kuonana huku wakitawala nafasi ya kiungo na kuwapoteza Haruna Chanongo na Abdulhalim Humud waliokabidhiwa jukumu zima la katikati.

Hali hiyo iliifanya Simba kupoteana katikati na kushindwa kusukuma mashambulizi mbele jambo lililotoa nafasi kwa  Yanga kuwashambulia, hivyo dakika ya 15, Didier Kavumbagu kupiga krosi iliyowahiwa na Ngasa ambaye bila kufanya makosa aliuzamisha mpira kimyani.

Bao hilo liwafanya Yanga kucheza kwa kujiamini zaidi huku Simba wakitawaliwa na hofu na katika dakika ya 35, makosa ya mabeki wa Simba kutokuwa makini yalisababisha Kiiza kuutendea haki mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite kwa kuuzamisha nyavuni.

Kosa la beki wa Simba, Nassor Masoud 'Chollo' la kumruhusu Kavumbagu kumchambua, hapa lilionekana, hivyo Mrundi huyo hakufanya makosa kabla ya kutoa pasi iliyomkuta Kiiza katika dakika ya 45 ambaye aliifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa  inaongoza kwa mabao 3-0.

Uzito wa Dhaira kufanya maamuzi na mawasiliano na mabeki

Kipa wa Simba, Abel Dhaira alikuwa mzito wa kufanya maamuzi, mara nyingi alikuwa mzito wa kutoka na pindi alipotaka kufanya hivyo alikuwa anasita, jambo liloifanya safu ya ushambuliaji ya Yanga kuutumia udhaifu huo.

Kwa ujumla safu nzima ya ulinzi ya Simba ilipoteana kuanzia kwa kipa hadi mabeki kwani hapakuwapo mawasiliano kati yake na Chollo, Haruna Shamte, Gilbert Kaze na Joseph Owino. 

Lawama za Kibadeni kwa Humud

Kocha wa Simba Abdallah Kibadeni alimshushia lawama Humud kutokana na kucheza chini ya kiwango katika mechi huku kukiwapo na neno 'hujuma'.
Hata hivyo, lawama hizo hazikuwa sahihi kwa Kibadeni kumtuhumu moja kwa moja baada tu ya kipindi cha kwanza kumalizika, kwani licha ya kumtoa, kimchezo haikuleta picha nzuri kwa wachezaji wenzake.
Ikumbukwe huo ni mchezo wa pili kwa Humud kucheza tangu msimu huu wa Ligi Kuu Bara kuanza, hivyo katika hali ya kawaida hakuandaliwa vya kutosha na isingekuwa rahisi kuhimili vishindo vya Athumani Iddi 'Chuji' ama Niyonzima ambaye kakosa mechi moja tu msimu huu.

Yanga ilimaliza dk. 90 kipindi cha kwanza Licha ya mashabiki na baadhi ya viongozi wa Yanga kuwashushia lawama kipa wao, Ali Mustafa 'Barthez', mabeki Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani na kiungo Chuji kwa kutokuwa makini huku wengine wakiwahusisha na neno 'hujuma' hilo kaliwezi kuwa sahihi.

Kwa ujumla wanapaswa kulaumiwa kwa makosa ya kiufundi na si hujuma, kwani kikosi kizima cha Yanga baada ya kwenda mapumziko kikiwa mbele kwa mabao 3-0, kiliamini huo ndiyo mwisho wa mchezo na kujiona tayari kimeshinda.

Wachezaji wa Yanga waliingia vyumba vya kubadilishia wakiwa wanashangilia ushindi, hatua iliyomfanya Kocha Mkuu, Ernie Brandts kufanya kazi kubwa ya kuwabadili kisaikolojia, lakini hilo halikiwezekana.

Hata hivyo, hiyo haikusaidia kitu kwani tayari kisaikojia walishaona wameshinda na kwamba kipindi cha pili walikuwa wanakwenda kukamilisha muda tu.

Kosa la Brandts
Hapa hakuna kushikana uchawi, licha ya juhudi kubwa za Brandts kuwaonya wachezaji kutoridhika na matokeo hayo, lakini alifanya makosa makubwa kiufundi, kwa kuendelea kuwaruhusu wachezaji kucheza mchezo wa kufurahisha badala ya kulinda 'kupaki basi' na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Simba ilianza kupata bao la kwanza katika dakika ya 53  kupitia kwa Betram Mombeki, bao hilo liliwachanganya Yanga, hivyo alichotakiwa kufanya Brandts ni kupunguza washambuliaji wawili na kuingiza mabeki huku akihimiza kupaki basi.

Hilo lingesaidia mashambulizi ya Simba kuishia katikati huku wakiwavuta wote kushuka kushambulia, wakati huo Yanga ikimbakiza winga mwenye mbio mbele, Ngasa kwa ajili ya mashambulizi ya kushtukiza jambo ambalo lingetoa nafasi kwao ya kupata bao la nne.

Brandts kumtoa KiizaHilo ni moja ya kosa kubwa lililofanywa na Mholanzi huyo, kwani Kiiza alikuwa katika kiwango cha juu sana na alishakuwa mwiba kwa mabeki wa Simba ambao walikuwa wakimkaba wawili wawili, hivyo kumsahau Kavumbagu, Ngasa na Niyonzima.
Kutoka kwa Kiiza na kuingia kwa Simon Msuva haikuwa 'sab' nzuri kwa kwa Yanga, kwani alichotakiwa kufanya ni kuingiza beki na tena si kumtoa mshambuliaji huyo.
Yanga haikuwa na kumbukumbu ya AC Milan vs Liverpool  2005
Kama Yanga ingekumbuka mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya AC Milan na Liverpool 2005, isingefanya makosa ya kutopaki basi.

Katika mechi hiyo, hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Milan ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-0. Mashabiki wa Liverpool hawakusita kuimba wimbo wao wa "You will never walk alone', kisaikolojia hilo liliwatia ari wachezaji wa Liverpool ambao walipigana na kusawazisha kipindi cha pili na kisha kuibuka na ushindi.

"Niliwashangaa mashabiki nini walichokuwa wanakiimba wakati tunaelekea kwenye vyumba vya kubadilishia na tulipokuwa tunaingia uwanjani kipindi cha pili tukiwa tumeshalala 3-0, kila tulipowatazama wachezaji tulijiona tuna deni kubwa na hakuna lisilowezekana," Steven Gerrard.
'Sab' na saikolojia kali ya Kibadeni 
Katika mechi za Simba na Yanga huwezi kukosa kusikia imani za kishirikina zikitawala, wapo wanaodai kuwa 'Yanga waliweka dawa katika lango lao ili kuzuia mabao kuingia' na kipindi cha pili wakasahau kuhama nayo, jambo lililofanya kibao kuwageukia.

Lakini kwa wachambuzi wa soka, hilo halipo, kwani hakuna asiyemjua Jamhuri Kihwelu 'Julio'  kuwa  ni kocha anayeaminika kwa uhamasishaji na mtaalam wa saikolojia kwa wachezaji, hivyo kwa kushirikiana na Kibadeni ni wazi kwenye chumba cha kubadilishia wachezaji waliambiwa 'hakuna lisilowezekana'.

"Tukiwapiga bao moja tu watachanganyikiwa na hapo tusifanye kosa", hicho ndicho kilichotokea baada ya Simba kufunga bao la kwanza, waliona hakuna cha kupoteza kama walivyoelezwa.

Hata walipofunga bao la kwanza, wachezaji waliiacha kazi ya kushangia kwa mashabiki na wao waliuwahi mpira na kuukimbiza kati, la pili hali ilikuwa hivyo na la tatu pia.
Mabadiliko aliyoyafanya Kibadeni kwa kuwatoa Humud na kumuingiza Said Hamisi (dk.49) huku Chanongo akimpisha William Lucien, ilikuwa ni sahihi kabisa na hilo liliifanya safu ya kiungo ya Simba kubadilika na kusukuma mipira mbele.
Mabao mawili ya haraka haraka yaliipoteza Yanga na kuanza kukanyagana huku wakipoteana katikati, hatua iliyotoa utawala kwa Simba kuweza kufunga la tatu dakika ya 84.

Tambwe alitoa fursa kwa wenzakeKwa muda wote wa mchezo, mabeki wa Yanga waliamini kumkaba Amisi Tambwe watamaliza safu ya ushambuliaji ya Simba, lakini hilo lilisababisha kusahaulika kwa  Mombeki aliyepata mpira akiwa mwenyewe na kuachia shuti lililojaa kimyani.

Hali kadhalika mambo yalikuwa hivyo kwa mabeki wa Yanga kuzembea na kumwacha huru Owino na baadaye Kaze waliofunga bila bughudha.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment