Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (katikati) akiwa na maafisa wa Serikali ya
Uswiss pamoja na timu uchunguzi kufuatilia mabilioni ya fedha
zilizowekwa katika benki za nchi hiyo.
Sakata la vigogo kuficha mabilioni ya
shilingi katika benki za Uswisi, limechukua sura mpya baada ya Serikali
ya nchi hiyo kutunga sheria inayowabana walioweka fedha kwenye benki
zake kuzithibitisha, la sivyo zitarejeshwa katika nchi husika.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe alifanya mazungumzo na Serikali ya nchi hiyo ambayo imemweleza
kuwa imebadili sheria zake ili kuwadhibiti wageni wanaoficha fedha
nchini humo.
Akizungumza na gazeti hili, Zitto
alisema amepata taarifa hizo juzi baada ya kukutana na Waziri wa Fedha
wa nchi hiyo ambaye alimwandalia mazungumzo na watalaamu wake.
Alibainisha kuwa tangu kuibuka kwa
sakata hilo mwaka 2012 na Bunge kuiagiza Serikali kufuatilia, Serikali
haijaomba taarifa yeyote kutoka Uswisi kuhusu Watanzania waliohifadhi
fedha nchini humo.(P.T)
"Jana nilikutana na Waziri wa Fedha na
akatuacha na mazungumzo na wataalamu wake. Wamesema hadi sasa, Tanzania
haijasaini mkataba wa kubadilishana taarifa za kikodi (Multilateral
convention on administrative assistance in tax matters)," alisema Zitto
na kuongeza;
"Kwa kutosaini, Tanzania inajinyima
haki ya kupata taarifa hizi na kutoza kodi kwa watu walioficha fedha
huku (Uswisi), maana Sheria ya Kodi ya Tanzania inataka kila Mtanzania
popote anapopata kipato halali lazima alipe kodi."
Zitto alieleza kuwa kitendo cha
Serikali ya Uswisi kubadili sheria zake, kinaiwezesha nchi hiyo kutoa
taarifa za benki za watu walioweka fedha nchini humo wakiwamo
Watanzania, ambao sasa watatakiwa kuthibitisha kama fedha hizo ni safi
au la.
"Kiufupi, Tanzania haijaomba taarifa
yeyote kutoka Uswisi. Ila Uswisi wamebadili sheria yao na sasa mmiliki
wa fedha ndiyo anapaswa kuthibitisha kwamba ni safi, na ikithibitika
kuwa hazina mwenyewe wala maelezo, zitarudishwa nchi husika," alisema.
Zitto alisema mbali na kukutana na
watendaji hao wa Serikali amezungumza na Umoja wa Mabenki wa nchi hiyo
uliobainisha kuwa Uswisi ina Watanzania wachache wenye fedha.
"Wamesema Watanzania wengi wana fedha
Uingereza, Jersey, Cayman Islands na Mauritius. Dubai pia imetajwa
sana," alisema Zitto. Zitto alielezea kuwa umoja huo wa benki za Uswisi
umeanzisha mkakati wa kusafisha fedha uitwao 'clean money strategy', na
wamegundua watu wengi ambao ni wanasiasa, wamezuia akaunti zao na
kupeleka majina kwenye Serikali zao.
"Tanzania haijafanya maombi rasmi hapa
Uswisi na hivyo wao kama benki hawawezi tu kutoa taarifa bila kuombwa.
Sheria yao imerekebishwa ambapo sasa ni wajibu wa mwenye akaunti kusema
kama fedha zake ni halali au hapana," alisema Zitto na kuongeza.
Hivi sasa hawapokei pesa kutoka nchi
za Afrika au wanapokea kwa tahadhari sana, maana kuna reputational risk
(kupoteza heshima)," alisema.
Wito wa timu ya uchunguzi
Zitto alipendekeza timu iliyoundwa
kuchunguza fedha hizo itoe taarifa yake kwenye Mkutano wa Bunge unaoanza
Oktoba 29, mwaka huu, akieleza kuwa, "Kuendelea kukaa na taarifa,
kutaongeza tetesi za kweli au za uwongo."
Alisema mpango huo wa kusaka fedha
zilizofichwa nchini Uswisi, umelenga zile zilizofichwa na watu binafsi
kutokana na rushwa au kuuza dawa za kulevya na kampuni kubwa za
kimataifa.
Alibainisha kuwa wengi waliotambulika ni wanasiasa, vigogo wa jeshi na wakuu wa mashirika ya umma na watendaji wa Serikali.
"Katika mabenki ya Uswisi, kuna kiasi
cha Dola za Marekani 197 milioni. Fedha nyingi zipo katika benki za
Uingereza na visiwa vyake, Dubai na Mauritius," alisema na kuongeza;
"Wapo watu waliopata fedha kihalali,
lakini wanaficha fedha hizo na mali zao nje ili kukwepa kodi. Wengi wa
hao ni wafanyabiashara wakubwa nchini. Tanzania inapoteza Dola za
Marekani 1.25 bilioni kati ya mwaka 2001 na 2012 kwa njia hizi."
Alibainisha kuwa Tanzania lazima itunge sheria ya kufilisi mali ambazo mtu anashindwa kuthibitisha amezipataje.
"Tayari ninafanyia kazi muswada
binafsi wa sheria wa kubadilisha sheria ya makosa ya jinai ya mwaka
1991. Wasaidizi wangu wanafanyia kazi muswada huo ili usomwe kwa mara ya
kwanza kwenye mkutano wa Bunge unaonza Oktoba 29 na kueleza kuwa sheria
ya sasa ina upungufu," alisema.
Madai hayo ya Zitto yamekuja ikiwa
umepita mwaka mmoja tangu Bunge kuipa Serikali muda wa kuchunguza sakata
la vigogo walioficha mabilioni katika benki za Uswisi.
Zitto ndiye aliibua sakata hilo
mwishoni mwa mwaka 2012. Kufuatia hoja hiyo, Serikali iliunda timu
kutokana na Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka jana.
Werema ahoji Mwananchi ni Bunge?
Timu hiyo inaongozwa na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye jana baada ya kutafutwa
na gazeti hili alisema, "Uchunguzi kuhusu walioficha fedha Uswisi bado
haujakamilika."
Viongozi wengine wanaounda tume hiyo
ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk
Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid na Gavana
wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.
Alipoulizwa kama kuna uwezekano wa
ripoti hiyo kuwekwa wazi katika Mkutano ujao wa Bunge, Werema alisema,
"Kwa nini, kwani wewe ndiyo Bunge. Uchunguzi bado unaendelea"
Hata hivyo, kwa mujibu wa agizo la
Bunge, tume hiyo inatakiwa kuwa imekamilisha uchunguzi wake mwezi huu na
kuwasilisha ripoti yake katika mkutano huo wa Bunge.
Alipoulizwa kuhusu ripoti hiyo, Naibu
Spika, Job Ndugai alisema, "Wiki ijayo katika kikao cha Kamati ya
Uongozi, Serikali itatakiwa kutoa taarifa za uchunguzi huo na kama
haujakamilika kikao hicho kitaamua jambo la kufanya na endapo uchunguzi
utakuwa umekamilika zitapangwa taratibu za kuiwasilisha ripoti bungeni."
Waziri wa Fedha anena
Chanzo:Mwananchi
Naye Waziri wa Fedha, Dk William
Mgimwa alisema jana kuwa sheria za kimataifa zipo wazi kwamba fedha
chafu zinazogundulika kufichwa nchi fulani, hurejeshwa katika Serikali
ya nchi husika.
"Lengo la sheria hizi za kimataifa ni
kuhakikisha kuwa fedha za wizi zinazoibwa nchi fulani, haziwezi
kuhifadhiwa katika nchi nyingine," alisema.
Alipoulizwa kama wizara yake ina
taarifa zozote kuhusu Watanzania walioficha fedha Uswisi alisema, "Kuna
Tume iliundwa na Bunge kufuatilia suala hilo nadhani ndiyo itakuwa na
majibu sahihi."
Uchunguzi wa walioficha mabilioni ya
Uswisi uliibuka baada ya Benki ya Taifa ya Uswiss (SNB) kutoa taarifa
mapema Juni 2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki
nchini humo.
Orodha hiyo inadaiwa kuwa na majina ya
baadhi ya Watanzania wenye akaunti zinazofikia Dola 196 za Marekani
milioni ambazo ni sawa na Sh323.4 bilioni.
source: Mjengwa Blog
No comments:
Post a Comment