Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wabunge wa Chadema, Chiku Abwao na
Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) mjini Iringa, jana wakati wa sherehe za
kuhitimisha mbio za Mwenge. Picha ya ikulu
Dar/Iringa. Rais Jakaya Kikwete amesema maadui
wote ambao walitaka kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kwa lengo
la kuvuruga amani ya nchi wamedhibitiwa .
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake itaendelea
kulinda amani ya nchi na maadui wote wanaohusika na kutaka kuvuruga
nchi watachukuliwa hatua kali za kisheria. “Kulikuwapo na upepo mbaya,
lakini kwa sasa Tanzania ni shwari na tumemshinda adui,” alisema Rais
Kikwete jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yaliyoandamana na sherehe za kuzima
Mwenge wa Uhuru, mkoani Iringa.
Alisema katika siku za hivi karibuni, maadui
wasioitakia mema Tanzania walikuwa na mkakati wa kuvuruga amani ya nchi,
lakini Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola vimewadhibiti na
nchi iko salama.
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali haiwezi
kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani kwa sababu inajua wazi kwamba
nchi ikiingia kwenye mgawanyiko, mshikamano utavurugika na shughuli za
maendeleo zitasimama.
Katiba Mpya
Rais Kikwete alisema mwaka 2014 ni mwaka wa kipekee kwa nchi kwa kuwa utakuwa na mambo makubwa matatu yatakayofanywa.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba Katiba Mpya ni lazima ikamilike mwakani kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa.
Vilevile, alisema mwakani Tanzania itasherehekea
miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na kuwarudishia
Wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake.
“Pia tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wetu.
Nawaomba Watanzania wajiandae kuyafanikisha vizuri mambo hayo ili
historia mpya ifunguliwe nchini.
“Wazanzibari waanze miaka mingine baada ya miaka
hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada ya miaka
hamsini na Katiba Mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,” alisema
Kikwete.
Rais Kikwete alionya kuwa asingependa mchakato wa
kupata Katiba Mpya uligawe taifa na kuleta mfarakano utakaovunja umoja
wa kitaifa badala ya kuuimarisha.
“Tunataka tuwe na Katiba itakayojenga, siyo kubomoa, kutugawa kwa misingi ya kiitikadi,” alionya Rais Kikwete.
Alisema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Baba wa
Taifa kwa mwaka huu ni kusisitiza mshikamano wa kitaifa unaopinga mbinu
zozote za kuligawa taifa. “Kaulimbiu ya mwaka huu; Tanzania ni wamoja,
tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zetu za dini, itikadi, rangi au
rasilimali,” alisema Rais Kikwete.
Alisisitiza kuwa amekusudia mabadiliko ya Katiba
ambayo mchakato wake unaendelea yawe ya kulipeleka mbele taifa
kimaendeleo kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema
atapendelea kuona Katiba Mpya inazinduliwa Aprili 13, mwakani, siku
ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa Baba wa Taifa.
Alisema kitendo hicho kitaienzi zaidi siku hiyo na
kuandamana na mpango wa kubadilisha maadhimisho ya kitaifa ya
kumkumbuka Mwalimu Nyerere kutoka Oktoba 14 siku aliyofariki na kuwa
Aprili 13, siku aliyozaliwa.
..ataka kuvuruga Mwenge
Maadhimisho ya Mwenge nusura yaingie dosari baada
ya mwanamume kujichomeka katika kundi la wanahabari akiwa na lengo la
kumdhuru kiongozi wa Mbio za Mwenge.
Kitendo hicho kilifanyika wakati Rais Kikwete
akiwa tayari ameshuka chini katika jukwaa dogo akisubiri kukabidhiwa
mwenge huo, mtu huyo alichomoka kutoka katika kundi la waandishi wa
habari na kujaribu kumvamia kiongozi wa Mbio za Mwenge, Juma Ali Sima
aliyekuwa ameshikilia Mwenge huo.
Hata hivyo, jitihada za mtu huyo za kutaka
kumvamia kiongozi wa Mwenge zilikwama baada ya kudhibitiwa vikali na
askari waliokuwa wakilinda amani uwanjani hapo.
Katika kipindi hicho, Rais Kikwete pamoja na
wasaidizi wake wengine walikuwa mita kama tisa kutoka katika eneo la
tukio akisubiri kukabidhiwa Mwenge huo.
Rais Kikwete alisema kilele cha maadhimisho ya
Mbio za Mwenge kimefanywa kuwa pia siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere tangu afariki miaka 14 iliyopita.
Alisema Watanzania wote bila kujali vyama vyao
wana wajibu wa kuyakumbuka mema yote ya Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni
pamoja na mafundisho yake.
Rais pia alisema ili kumkumbuka zaidi Mwalimu
Nyerere alipendekeza siku yake ya kuzaliwa ndiyo iitwe Nyerere Day na
ianze kusherehekewa kwa mbwembwe, iwe na mijadala ya kazi zake na
itumiwe kufanya shughuli mbalimbali za kujenga taifa kwa lengo la
kumuenzi.
Kuhusu dawa za kulevya
Katika maadhimisho hayo, Rais Kikwete alizungumzia
mkakati wa Serikali yake wa kupambana na dawa za kulevya kwamba
kitaanzishwa chombo maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema kazi ya kupambana na dawa za kulevya ni
ngumu na hatari kutokana na wanaofanya kazi hiyo kuwa na fedha nyingi,
lakini Serikali itawalinda wote.
Source: mwananchi
Source: mwananchi
No comments:
Post a Comment