Rais Kikwete akiwa katika picha ya
pamoja na Viongozi wa Vyama vya upinzani na wasaidizi wao waandamizi
muda mfupi kabla ya kuanza mazungumzo kuhusu rasimu ya katika ikulu
jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto mbele Isaack Cheyo UDP, James
Mbatia NCCR Mageuzi, Professa Ibrahim Lipumba CUF, Freeman Mbowe
CHADEMA, Philip Mangula CCM, na Bibi Nancy Mrikaria aliyemwakilisha
Mwenyekiti wa TLP Mhe.Agustine Lyatonga Mrema.Waliosimama Nyuma kutoka
kushoto ni Naibu Katibu Mkuu CUF Bwana Julius Mtatiro,Mhe. Tundu Lissu
CHADEMA, Bwana Martin Mng'ong'o NCCR Mageuzi ,Waziri wa nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera,Uratibu na Bunge William Lukuvi, Mhe.Habib Mnyaa CUF,
Mbunge wa Ubungo Kwa tiketi ya CHADEMA Mhe.John Mnyika, Waziri wa nchi
Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu Mhe.Steven Wassira na Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe.Mathias Chikawe. (picha: Freddy Maro/IKULU).
TAARIFA KWA UMMA KUTOKA KURUGENZI YA MAWASILIANO IKULU
MKUTANO kati ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wa
vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni umemalizika Ikulu, Dar Es
Salaam, muda mfupi uliopita leo, Jumanne, Oktoba 15, 2013 kwa pande hizo
mbili kukubaliana kama ifuatavyo:
Moja , kwamba vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
viwasilishe mapendekezo yao haraka Serikalini ili ifatutwe namna ya
kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya Sheria hiyo.
Pili, kwamba vyama vya siasa nchini,
kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya
kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa
pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato huo kwa maslahi mapana ya nchi yao
na mustakabali wa taifa. Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa
jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa
vyama hivyo na wadau wengine nchini.
Viongozi wa vyama vyama vya siasa
waliokutana na Mheshimiwa Rais Kikwete ni Mheshimiwa Profesa Ibrahim
Lipumba, Mwenyekiti wa CUF; Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa
CHADEMA na Mheshimiwa James Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM
Mheshimiwa Philip Mangula, Mheshimiwa Isaack Cheyo ambaye amemwakilisha
Mwenyekiti wa Chama cha UDP Mheshimiwa John Cheyo na Mheshimiwa Nancy
Mrikaria ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa TLP Mheshimiwa Augustine
Mrema. Waheshimiwa John Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.
Wengine ambao wameambatana na
wenyeviti wao ni Mheshimiwa H. Mnyaa na Bwana Julius Mtatiro wa CUF,
Waheshimiwa Tundu Lissu na John Mnyika wa CHADEMA na Bwana Martin
Mng'ongo wa NCCR-Mageuzi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
15 Oktoba, 2013
No comments:
Post a Comment