WIKI hii iliyopita
imekuwa na mijadala mingi kuhusu mtu aliyeiaga dunia miaka 14 iliyopita lakini,
pamoja na kuwa ni marehemu, amebakia kuonekana kama kiongozi wa kweli wa watu
wake.
Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere amekuwa na mvuto usiokuwa wa kawaida miongoni mwa Watanzania
wa rika zote, na hata miongoni mwa watu wa nje ya nchi hii waliomjua binafsi na
waliomsoma na kum-google.
Katika
kuadhimisha maisha yake, watu wengi wamejaribu kufanya tathmini ya kile ambacho
hasa kinamfanya mzee huyu aliyelala kijijini kwake Butiama aendelee kuwa na
ushawishi mkubwa kiasi hicho, na kila aliyetoa maoni yake amekuwa na lake la
kusema.
Nimesoma mahali
kadhaa, na pia nimesikia kwenye mijadala ya redio, watu wakistaajabu kutokana
na uwezo wa mtu aliyefariki muda wote huu kuwa anaendelea kuiongoza nchi kutoka
kaburini.
Hatuna sababu
ya kustaajabu kuhusu hili. Ingawaje haiwatokei binadamu wengi, lakini si ajabu
kwa mtu aliyeishi maisha ya aina fulani kuendelea kuwa na ushawishi mkubwa hata
baada ya kifo chake. Hii imetokea mara nyingi pale wanapoondoka watu waliofanya
mambo makubwa wakati wa maisha yao, na hususan wale waliotenda mema.
Kwa hakika,
hivyo ndivyo wanavyokuwa watu walioanzisha imani za kiroho zilizovuta hisia za
wafuasi wengi, na imani hizo zikazidi kukua, kusambaa na kutangaa hadi zikafika
sehemu ambazo waanzilishi wake hawakujua kwamba zipo sehemu za aina hiyo.
Ndivyo ilivyo kwa imani za dini zilizotoka Mashariki ya Kati na hivi sasa
zimetandaa ulimwenguni kote.
Viongozi wa
kisiasa pia wanaweza kuwa na ushawishi kama huo wakiwa wamelala kaburini, na
wakati mwingine wafuasi wao waliowarithi hujaribu kuwatumia ili wapate
kukubalika mbele ya halaiki. Nahisi hiki ndicho chanzo cha kuwajengea makaburi
ya aina ya makumbusho (mausoleum) na kuifanya miili yao ionekane kama wamelala
tu, hawakufa.
Nyerere amezikwa
Butiama, kama ilivyo ada ya imani yake ya kidini, lakini jina lake limeanza
kuwa na ladha ya kinabii, kama vile alianzisha imani ya kidini ambayo wafuasi
wake wanataka kuinedeleza na kuieneza kote wawezako kufika.
Nimesema hapo
juu kwamba hata nje ya nchi wako wafuasi wa Nyerere wanaochukua sura ya waumini
wake. Jaji Mkuu wa Kenya, Dk. Willy Mutunga amenukuliwa akisema kwamba yeye ni
“mwathirika wa virusi vya Azimio la Arusha” na kwamba ni muumini wa sera za
Nyerere. Si tofauti sana na imani za kidini, na wako wengi wa aina hii.
Inawezekana
kwamba hali hii inasababishwa na ukame wa viongozi tulionao, si hapa nchini
kwetu tu, bali katika bara la Afrika na duniani kote. Inawezekana ni kutokana
na ‘nostalgia’, kw amaana ya kukumbuka kwa kujutia siku za nyuma na kuziona
kama zilikuwa bora kuliko hizi tulizo nazo. Lakini inawezekana kuna jambo
jingine.
Nimewahi
kuandika mara kadhaa kwamba Nyerere hakuwa malaika, na kwamba alitenda makosa
mengi katika kuiongoza na kuitawala nchi hii. Yumkin, hilo ndilo
linatuthibitishia kwamba kwa hakika alikuwa binadamu, la sivyo tungemwita
muungu.
Tofauti kati
yake na wengine ni kwamba alitenda makosa aliyoyatenda katika jitihada za
kuiendeleza nchi yake na kuwainua wananchi wake kutoka katika masikini na
unyonge. Hakutenda makosa yaliyotokana na utashi wa kujitajirisha yeye na
familia yake wala kwa nia ya kusimamia maslahi ya mitaji mikubwa ya
“wawekezaji” na waporaji kutoka nje.
Aliishi maisha
ya mtu wa kawaida; alipenda kuvaa kama mtu wa kawaida; alichukia anasa na tabia
za kujipamba mithili ya tausi; magari yake yalikuwa si yake bali ya dola, na
yalikuwa magari ya kawaida kabisa; alichukia mbwembwe zisizo na maudhui.
Alipenda kufanya kazi, wakati mwingine kazi za ngwamba ambazo watu wengi
huzikimbia.
Misimamo yake
ilikuwa imara na isiyoyumba, na ndiyo maana wawakilishi wake nje ya nchi
waliweza kutoa matamko yalaiyofanana bila kuwasiliana juu ya wanachokisema, kwani
bosi wao alikuwa anaeleweka. Na tusisahau kwamba hii ilikuwa ni katikati ya
malumbano makali kuhusu mapambano ya ukombozi wa Afrika, na diplomasia yetu
ilibidi ipambane na diplomasia ya kinafiki ya nchi za Mgharibi maswahiba wa
makaburu.
Nakumbuka nilipokuwa
naanza kazi kama mwanahabari jijini, nikiwa na mijadala isiyoisha na
mwanahabari mwandamizi, tulikua tukijiuliza iwapo baada ya Mwalimu tungeweza
kumpata mtu wa kumrithi. Tuliona kwamba ingekuwa vigumu kumpata mtu ambaye
angekubali majukumu mazito kama hayo.
Muonekano wa
kazi ya kuongoza nchi wakati ule ulikuwa muonekano wa majukumu matupu, si raha.
Nani angekubali kuishi vijijini na Wagogo na Waha kwa mwezi mzima, na kuamka
kila siku saa 11 alfajiri kwenda kushinda analima kwa jembe la mkono?
Nani angekubali
kila siku kuwa katika kampeni vijijini na mijini kuhimiza kisomo cha watu
wazima, uzazi wa mpango, kilimo cha kisasa na kila aina ya kampmeni za
‘kipedagogia’ kwa watu wake?
Diplomasia
ulikuwa ni uwanja mwingine ambako Nyerere alitoa mchango mkubwa kuisogeza
Afrika mbele, hasa katika masuala ya ukombozi na kutofungamana na upande wo
wote. Aidha alikuwa msitari wa mbele katika kudai mabadiliko ya
mifumo ya kiuchumi wa kimataifa (NIEO), na juhudi zake zinakumbukwa
duniani kote.
Alikwenda mara
chache sana kuhutubia Baraza Kuu la Umoja waMataifa (UNGA), lakini kila
alipofanya hivyo hotuba yake ilibakia kuwa ni mpango wa kufanyiwa kazi na Umoja
wa Mataifa kwa mwaka uliofuata. Alikuwa kiongozi miongoni mwa viongozi wa
dunia.
Wiki ijayo
nitasimulia kisa kimoja cha kushangaza, lakini kilichonipa fundisho maridhwa
juu ya diplomasia ya Mwalimu, kisa ambacho kingeweza kuwafunda pia watawala
wetu wa leo na wa
kesho.
No comments:
Post a Comment