WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, October 31, 2013

CAF yampongeza Malinzi TFF

Jamal Malinzi Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
Rais  wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou amempongeza Jamal Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, mwaka huu.
Katika salamu zake kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya CAF na familia ya mpira wa miguu Afrika, Hayatou amesema uchaguzi huo unampa Rais Malinzi fursa ya kuupeleka mbele mpira wa miguu nchini Tanzania.

Alisema CAF ina imani uwezo wake katika uongozi, uzoefu na ujuzi kwenye soka vitasaidia si tu mpira wa miguu Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla, na kuongeza kuwa ataendeleza ushirikiano uliopo ili kuwanufaisha zaidi vijana wa bara hili.

Hayatou amemtakia Malinzi kila la kheri katika kipindi chake cha uongozi na kumhakikishia kuwa CAF iko pamoja naye katika kusukuma mbele gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu.

TASWA YAMSIFU
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa), pia kimeupongeza uongozi mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliochaguliwa Jumapili iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Taswa, Amir Mhando, chama hicho kinaungana na wapenda michezo na Watanzania kwa ujumla kuitakia kila la heri Kamati ya Utendaji ya TFF na shirikisho hilo kwa ujumla chini ya Rais mpya, Jamal Malinzi na Makamu wake, Wallace Karia.

"Taswa inaamini Malinzi, Karia na wajumbe wao ni wazoefu na ni watu wenye kujua mambo mengi yanayohusu mpira wa miguu nchini, hivyo tunaamini watakuwa viongozi wazuri kwa nafasi zao katika kuhakikisha shirikisho hilo linasonga mbele," ilisema taarifa hiyo.

Iliongeza: "Tunawatakia kila la heri wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji, huku tukiamini hawatawaangusha Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF waliowaamini kushika nafasi hizo. Taswa na waandishi wa habari za michezo kwa ujumla hapa nchini tunaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha ili watekeleze majukumu yao ipasavyo."
 
CHANZO: NIPASHE

Marando ataka kina Babu Seya waachiwe huru

Mwanamuziki maarufu nchini, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya (kulia) na mwanawe Johnson Nguza maarufu kama Papii Kocha, wakisindikizwa na askari Magereza baada ya ombi lao la kutaka hukumu ya kifungo cha maisha waliyopewa na Mahakama ya Rufaa nchini ipitiwe upya.(PICHA:OMAR FUNGO)
Wakili  anayewatetea wanamuziki  Nguza Vicking maarufu kama 'Babu Seya'  na mwanawe Papii Nguza wanaotumikia kifungo cha maisha kwa makosa ya  kulawiti na kubaka, Mabere Marando ameiomba Mahakama ya Rufani Tanzania kuwaachia huru wateja wake kwa kile alichoeleza ushahidi uliotumika kuwatia hatiani kuwa na mapungufu ya kisheria.
Aidha, amedai kuwa ushahidi uliotolewa na baadhi ya mashahidi wa Jamhuri haukufuata masharti ya sheria ya kupokea ushahidi wa watoto wadogo.
Marando alitoa ombi hilo jana wakati akitoa hoja ya ombi la warufani Babu Seya na mwanawe Papii maarufu kama Papii Kocha mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti Jaji Nathalia Kimaro, akisaidiana na  Mbarouk Mbarouk na Salum Massati.
Alieleza kuwa lengo la kufikisha ombi hilo mahakamani ni kutaka kuonyesha jinsi mahakama iliyotoa hukumu ilivyokosea kutowaachia huru wateja wake na badala yake ilitumia ushahidi wa watoto ambao ulikuwa na mapungufu ya kisheria.

“Katika hukumu yenu ya Februari 11, mwaka 2010 mlikubali kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikosea katika kupokea ushahidi wa watoto wadogo ambao hakufuata masharti ya kupokea ushahidi huo japo uliungwa mkono na ushahidi mwingine katika kuwatia hatiani warufani…” alieleza Marando.

Alidai kuwa mbali na mapungufu hayo, pia upande wa Jamhuri haukuita mashahidi muhimu kwenye kesi hiyo ambao walitajwa na baadhi ya mashahidi akiwamo Mangi mwenye duka jirani na nyumba ya Babu Seya.

“Mangi angeitwa mahakamani angesema ukweli kinyume na ushahidi wa Jamhuri hivyo kwa kuwa waliona atawaharibia kesi yao wakaamua kumuacha kwa makusudi …
pia kuna kijana mwingine Zizeli aliyetajwa katika ushahidi kwamba alikuwa akikusanya watoto kwa ajili ya kuwapeleka kwa warufani, hajaitwa mahakamani kuthibitisha tuhuma hizo” alidai Marando wakati akitoa hoja za utetezi alizowasilisha kwa saa mbili.
Upande wa Jamhuri ulikuwa na jopo la mawakili watano, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Jackson Mdaki akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Angaza Mwipopo, Imakulata Banzi, Joseph Pande  na Wakili wa Serikali Abrimark Mabruki.
Akijibu hoja za utetezi, Mdaki alieleza kuwa ombi lililowasilishwa na upande wa utetezi halina mashiko ya kisheria kwa sababu kifungu kilichotumika ni cha mashauri ya madai na siyo ya jinai kama ilivyo kesi hiyo iliyopo mahakamani.
“Tunaomba mahakama iyatupilie mbali maombi haya kwani kukubali kuyasikiliza na kuyatolea maamuzi ni sawa na matumizi mabaya ya mahakama… maombi haya yamefunguliwa chini ya kifungu cha mashauri ya madai na siyo kesi za jinai tunaomba mahakama kuyatupilia mbali” alieleza Mdaki.

Jaji Kimario baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alisema mahakama inakwenda kuyapitia na itayatolea maamuzi tarehe itakayopangwa.
 
CHANZO: NIPASHE

RUFAA YA BABU SEYA, PAPII KOCHA KILICHOBAKI HUKUMU

babuseyarufaa3_93851.jpg
Nguza Viking 'Babu Seya' (kulia) na mwanaye Johnson Nguza 'Papii Kocha' wakitoka mahakamani kwa furaha.
babuseyarufaa1_c9aa8.jpg
Nguza Viking 'Babu Seya' (wa pili kulia) na mwanaye Johnson Nguza 'Papii Kocha' (wa pili kushoto) wakiwa mahakamani.
babuseyarufaa3_1_3a090.jpg
Babu Seya na Papii Kocha wakiwa na furaha nje ya mahakama.

Baada ya majaji wa Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam kupitia hoja za mawakili wa serikali na utetezi kwenye Rufaa ya hukumu ya kifungo cha maisha jela katika kesi iliyokuwa ikimkabili mwanamuziki Nguza Viking 'Babu Seya' na mwanaye Johnson Nguza 'Papii Kocha', wameamua kuhairisha rufaa hiyo mpaka tarehe husika ya kutoa hukumu ya kesi hiyo
itakapopangwa hapo baadaye.

(Picha na Richard Bukos / GPL) (P.T)

source: mjengwa blog

Monday, October 28, 2013

Balozi Isaac Sepetu afariki dunia

Mke wa marehemu Balozi Sepetu,Mariamu Sepetu
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Balozi Isaac Sepetu, amefariki dunia jana alfajiri jijini Dar es Salaam.
Alikutwa na mauti hayo katika hospitali ya TMJ alipokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza na NIPASHE jana nyumbani kwa marehemu Mwenge, jijini Dar es Salaam, mke wa marehemu Balozi Sepetu, Mariamu Sepetu, alisema mumewe alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na kiharusi.

Alisema Agosti 21, mwaka huu, marehemu alipatwa na ugonjwa wa kiharusi na kulazwa katika hospitali tiba Mbadala, Zanzibar.

“Baada ya kupokea taarifa kwamba amepata ‘stroke’ nilikwenda Zanzibar kumuangalia na nilivyoona hali yake hairidhishi, nikawasiliana na watoto, tukakodi ‘charter’ (ndege) na kumleta hapa kwa matibabu zaidi,” alisema.

Alisema baada ya kupatiwa matibabu na kufanyiwa ya mazoezi ya viungo, na hali yake ilionekana kuimarika.

Jaji Mkusa Sepetu akizungumza na NIPASHE kwa niaba ya watoto wa marehemu, alisema mipango ya mazishi inafanyika, huku wakiwasubiri watoto wengine wa marehemu waliopo nje ya nchi ili tukubaliane, lakini marehemu atazikwa Unguja Mbuzini, Zanzibar.

Naye Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally, alisema serikali inasubiri kupewa taarifa za taratibu za mipango ya mazishi kutoka kwa ndugu wa marehemu.

Balozi Sepetu aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje miaka ya 1970 katika serikali ya awamu ya kwanza.

Kadhalika aliwahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Urusi tangu mwaka 1982 na hadi anafariki alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Uwekezaji wa Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).

Marehemu ameacha wajane wawili Angelika Sepetu na Mariamu Sepetu pamoja na watoto tisa.
 
CHANZO: NIPASHE

RAIS KIKWETE NA MAMA SALMA KIKWETE WATOA POLE KWA MJANE NA FAMILIA YA BALOZI ISAAC SEPETU

w1_1ad78.jpg
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimpa pole mjane wa Balozi Isaac Sepetu, Mama Miriam Sepetu, alipokwenda na Mama Salma nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kwa mjane huyo na familia ya Marehemu Sepetu aliyefariki jana jijini Dar es salaam.
w2_993f8.jpg
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa pole kwa wanafamilia wa Balozi Isaac Sepetu alipokwenda na Mama Salma nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kufuatia msiba Marehemu Sepetu aliyefariki jana jijini Dar es salaam.
w3_f097a.jpg
Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji mjane wa Balozi Isaac Sepetu alipokwenda nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kufuatia msiba Marehemu Sepetu aliyefariki jana katika jijini Dar es salaam.(P.T)
w4_3b765.jpg
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini katika kitabu cha maombolezo ya msiba wa Balozi Isaac Sepetu alipokwenda nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole. Marehemu Sepetu aliyefariki jana katika jijini Dar es salaam.
w5_85aec.jpg
Mama Salma Kikwete akiweka saini katika kitabu cha maombolezo ya msiba wa Balozi Isaac Sepetu nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam. . Marehemu Sepetu aliyefariki jana katika jijini Dar es salaam.
w6_d87f7.jpg
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji mjane wa Balozi Isaac Sepetu, Mama Miriam Sepetu, alipokwenda na Mama Salma nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kwa mjane huyo na familia ya Marehemu Sepetu aliyefariki jana jijini Dar es salaam.
PICHA NA IKULU

source: mjengwa blog

AZAM FC YAICHARAZA SIMBA SC 2-1 NA KUPAA KILELENI LIGI KUU BARA

kipre_95ce6.jpg

AZAM FC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba SC ikitoka nyuma kwa bao 1-0.
 
Shujaa wa Azam leo alikuwa ni mshambuliaji kutoka Ivory Coast na mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Kipre Herman Tchetche aliyefunga mabao yote ya timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa.
 
Kwa matokeo hayo, Azam inatimiza pointi 23 na kujinafasi kileleni, ikiwazidi kwa pointi tatu Simba SC na Mbeya City katika nafasi ya pili.
Wachezaji wa Azam wakishangilia ushindi wao leo(P.T)

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Oden Mbaga aliyesaidiwa na Hamisi Chang'walu na John Kanyenye wote Dar es Salaam, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
Simba SC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 21 kupitia kwa Ramadhani Singano 'Messi' aliyemalizia mpira ulioingizwa kutoka pembeni na Zahor Pazi.
Bao hilo liliwaongeza kasi Simba SC na kushambulia zaidi langoni mwa Azam FC, lakini hawakufanikiwa kupata bao la pili.
Azam ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 44 kupitia kwa Kipre Tchetche aliyemalizia mpira wa Erasto Nyoni kutoka pembeni kulia.
 

Kipindi cha pili, timu zote zilishambuliana kwa zamu kabla ya Salum Abubakar 'Sure Boy' kumpa pasi nzuri Kipre Tchetche upande wa kushoto, akamfunga tela William Lucian 'Gallas' kisha kumchambua Abbel 

Dhaira kwa ustadi wa hali ya juu.
Mfungaji wa mabao mawili ya Azam leo, Kipre Tchetche akimtoka Issa Rashid 'Baba Ubaya' wa Simba SC


Katika kipindi hicho, Simba SC ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 60 kupitia kwa Sino Augustino aliyebaki yeye na kipa na kupaisha juu ya lango kufuatia pasi nzuri ya Ramadhani Singano 'Messi'.
Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa; Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Aggrey Morris, Said Mourad/David Mwantika dk47, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Salum Abubakar 'Sure Boy', John Bocco, Humphrey Mieno/Khamis Mcha dk 73 na Joseph Kimwaga/Farid Mussa dk47.
Simba SC; Abbel Dhaira, William Lucian 'Gallas', Issa Rashid 'Baba Ubaya', Joseph Owino, Hassan Hatibu, Jonas Mkude, Ramadhani Singano 'Messi', Said Ndemla, Betram Mombeki, Zahor Pazi/Sino Augustino dk55 na Amri Kiemba/Edward Christopher dk55.
Ligi hiyo itakamilisha raundi ya 11 kesho kwa mechi tatu huku Yanga ikiwa mwenyeji wa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons. Rhino Rangers na JKT Ruvu zitacheza katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Raundi ya 12 ya ligi hiyo itaanza Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Novemba Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Yanga na JKT Ruvu kwenye uwanja huo huo.
Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).
Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
 

Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.
 

Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
princezub@hotmail.com Mahmoud Zubeiry at 07:14 10/28/2013 06:26:00 PM Email ThisBlogThis!Share to TwitterShare to Facebook

source: mjengwa blog

Saturday, October 26, 2013

K AIKATIA TAMAA CCM

2_f799f_1391b.jpg

ASEMA IMEPOTEZA MATUMAINI KWA WATANZANIA(na Danson Kaijage, Dodoma Tanzania Daima)

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameonyesha wasiwasi wa chama hicho kushindwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 iwapo watendaji wake wataendelea na vitendo vya rushwa.

Alisema kuwa kwa sasa chama hicho kikongwe kimepoteza matumaini kwa Watanzania kutokana na vitendo ambavyo siyo vya kiungwana vinavyofanywa na watendaji.

Kwa kusisitiza, Kikwete alisema hata kama CCM itashinda uchaguzi wa 2015, kama tabia walizonazo watumishi na viongozi ndani ya chama hazitabadilika, ni wazi kuwa hakitapita kwenye uchaguzi wa 2020.
Rais Kikwete alitoa onyo hilo mjini hapa juzi usiku, alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu na wenyeviti wa wilaya na mikoa wa chama hicho nchini nzima.

"Kama hatutabadilika katika suala la rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana, na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani.

"Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea sh laki mbili za 'airtime' (muda wa mawasiliano), ndugu zangu hatutafika, ama wengine watavuka na wengine kukwama," alisema.

Alisema tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku hali ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.(P.T)

"Viongozi wa chama ndio mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu, nawaombeni tubadilike, kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali nawaambieni," alisema Kikwete ambaye alitumia muda wa saa mbili kufunga mafunzo hayo.

Alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza kujipitisha kwa viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili ya kuwapigia debe ili wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama ubunge.

Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo watu ambao wameishaanza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali za kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo linaendelea kukishushia hadhi chama hicho.

Akizungumzia chuki ndani ya chama, alisema Watanzania kwa sasa wameishakuwa na akili zao, na hivyo hawataki kudanganywa kwani viongozi wengi ndani ya chama hawajui hata ilani ya chama chao.

"Wapo baadhi ya viongozi ndani ya chama hawajui hata ilani ya chama chao, wakipanda kwenye majukwaa wanaanza kuzungumzia ujenzi wa daraja la Mkapa ama lile la Malagarasi, watu hawataki kusikia hayo, mtu wa Ngara anataka kujua daraja lake limeishaje siyo la Mkapa," alisema.

Hata hivyo, alisema kwa sasa vyama vya upinzani vinafanya kazi kubwa zaidi ya kuwatembelea wananchi na kusikiliza kero zao tofauti na ilivyo kwa CCM ambayo viongozi wake wapo mbali na wananchi.

"Wapo watu ambao wanadai kuwa chama kitafia mikononi mwangu, nataka niseme kuwa hakifii mikononi mwangu, kitafia mikononi mwenu," alisisitiza.

Kikwete alisema kuwa siku hizi watu wana mbadala wa vyama vingine na siyo CCM peke yao, na hivyo kuwataka viongozi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa waondolewe mara moja katika nafasi zao.

"Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo mbalimbali ambao wanaweza kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, hivyo hatuna budi kuachana na hawa wala rushwa ambao watatupotezea sifa yetu kwa wananchi. Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa."alisema.

Katika hatua nyingine, Kikwete aliwaonya viongozi ambao wanajihusisha na uuzaji wa mali za chama kama vile viwanja na baadhi yao kuingia mikataba yenye utata.

Hata hivyo, aliwataka makatibu hao na wenyeviti wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanawatembelea wanachama wao na kutafuta wengine wapya kwa ajili ya kujiimarisha kwa chaguzi mbalimbali zijazo.

source: mjengwa blog

Friday, October 25, 2013

Shujaa wa Tanzania,Mwl.Nyerere

184495_288229154613280_419551865_n_df9ee.png
Shujaa wa Tanzania, Afrika na Dunia,anatembea kwa miguu si kwa kukosa usafiri wa gari au hercopter anajua anataka kufanya anachojua hasubiri ripoti,hajavaa suti wala sare ya chama cha mapinduzi kwa kuwa si mtumwa wa chama au tangazo la chama ni mtumwa wa watanzania na tangazo la watanzania,kavaa gwanda anajua yuko katika mapambano,ameshika fimbo mkononi kwajili ya kuchunga,kuongoza kondoo wake ambao anajua wana kiu na njaa lakini pia kuchapa wenye viburi,warafi,wakorofi,wanyonyaji na wengine wenye tabia kama hizo.(P.T)

''Mwalimu Julias Kambarage Nyerere,Baba wa Taifa wa kwanza katika Taifa hili,ulijitolea kwa moyo wako wote kwajili yetu,ulipigania usawa,uhuru na haki,kuimalisha ujamaa na upendo miongoni mwetu,ulipigana na ujinga,maradhi na umaskini na ulimanisha kwa vitendo,leo haupo kimwili lakini bado unaishi katika vichwa na mioyo yetu,binafsi sijawahi kukusahau na kamwe abadani asilani sitakusahau''

HEADER

Guest
0Guest2013-10-25 10:29#1
Amen! huyu mzee nadhani alishushwa na mungu ili aje kutukomboa.laki ni sasa tumebakiwa na viongozi warafi,wanaopen da kujinufaisha nafsi zO.

Hakuna mwenye nia thabiti ya kutetea wanyonge. Tanzania inahitaji kiongozi anaeweza kuthubutu kumwambia mtu akufukuza kazi leo, lakini wapi kila mtu anaangalia vx yake ina mafuta baada ya kustaafu atakua na nini mwisho.inauma saaana

Mungu ibariki Tanzania
Mnukuu
Guest
0Guest2013-10-25 11:41#2
Mungu huwainua viongozi kama Nyerere kwa nadra. Yawezekana vikapita vizazi vingi sana hadi kumpata kiongozi mwingine kama Nyerere. Katika kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere 14/10/2013 TBC TV hawakuandaa 'documentary' nzuri kuhusu Mwalimu aliyeandaa ni kama hakujipa umakini wowote. Si TBC TV bali vituo vyote vya TV kama ITV, STAR TV, EAT TV n.k. havikujishughul isha kuandaa 'makala' zenye mashiko kuhusu Mwalimu. wangefanya BBC au DW hata kama ni kuwa 'biased' bado wangetoa makala nzito. Picha hiyo hapo juu inasema mengi kuliko makala ya TBC siku hiyo.
Mnukuu
Guest
0Guest2013-10-25 18:06#3
Tulioteseka na hayo mashamba ya ujamaa bila kunufaika na mazao yake hamtuuzii hizo story ng'o! Unamuona yule Jombi wa kushoto kabisa, shati lake lilivyojaa viraka? Unayajua makatambuga weye?
 
source: mjengwa blog

Uswisi sasa kurejesha mabilioni ya mafisadi

mabilion_d5634.jpg

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (katikati) akiwa na maafisa wa Serikali ya Uswiss pamoja na timu uchunguzi kufuatilia mabilioni ya fedha zilizowekwa katika benki za nchi hiyo. 

Sakata la vigogo kuficha mabilioni ya shilingi katika benki za Uswisi, limechukua sura mpya baada ya Serikali ya nchi hiyo kutunga sheria inayowabana walioweka fedha kwenye benki zake kuzithibitisha, la sivyo zitarejeshwa katika nchi husika.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alifanya mazungumzo na Serikali ya nchi hiyo ambayo imemweleza kuwa imebadili sheria zake ili kuwadhibiti wageni wanaoficha fedha nchini humo.

Akizungumza na gazeti hili, Zitto alisema amepata taarifa hizo juzi baada ya kukutana na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo ambaye alimwandalia mazungumzo na watalaamu wake.

Alibainisha kuwa tangu kuibuka kwa sakata hilo mwaka 2012 na Bunge kuiagiza Serikali kufuatilia, Serikali haijaomba taarifa yeyote kutoka Uswisi kuhusu Watanzania waliohifadhi fedha nchini humo.(P.T)

"Jana nilikutana na Waziri wa Fedha na akatuacha na mazungumzo na wataalamu wake. Wamesema hadi sasa, Tanzania haijasaini mkataba wa kubadilishana taarifa za kikodi (Multilateral convention on administrative assistance in tax matters)," alisema Zitto na kuongeza;

"Kwa kutosaini, Tanzania inajinyima haki ya kupata taarifa hizi na kutoza kodi kwa watu walioficha fedha huku (Uswisi), maana Sheria ya Kodi ya Tanzania inataka kila Mtanzania popote anapopata kipato halali lazima alipe kodi."

Zitto alieleza kuwa kitendo cha Serikali ya Uswisi kubadili sheria zake, kinaiwezesha nchi hiyo kutoa taarifa za benki za watu walioweka fedha nchini humo wakiwamo Watanzania, ambao sasa watatakiwa kuthibitisha kama fedha hizo ni safi au la.

"Kiufupi, Tanzania haijaomba taarifa yeyote kutoka Uswisi. Ila Uswisi wamebadili sheria yao na sasa mmiliki wa fedha ndiyo anapaswa kuthibitisha kwamba ni safi, na ikithibitika kuwa hazina mwenyewe wala maelezo, zitarudishwa nchi husika," alisema.
Zitto alisema mbali na kukutana na watendaji hao wa Serikali amezungumza na Umoja wa Mabenki wa nchi hiyo uliobainisha kuwa Uswisi ina Watanzania wachache wenye fedha.

"Wamesema Watanzania wengi wana fedha Uingereza, Jersey, Cayman Islands na Mauritius. Dubai pia imetajwa sana," alisema Zitto. Zitto alielezea kuwa umoja huo wa benki za Uswisi umeanzisha mkakati wa kusafisha fedha uitwao 'clean money strategy', na wamegundua watu wengi ambao ni wanasiasa, wamezuia akaunti zao na kupeleka majina kwenye Serikali zao.

"Tanzania haijafanya maombi rasmi hapa Uswisi na hivyo wao kama benki hawawezi tu kutoa taarifa bila kuombwa. Sheria yao imerekebishwa ambapo sasa ni wajibu wa mwenye akaunti kusema kama fedha zake ni halali au hapana," alisema Zitto na kuongeza.
Hivi sasa hawapokei pesa kutoka nchi za Afrika au wanapokea kwa tahadhari sana, maana kuna reputational risk (kupoteza heshima)," alisema.
Wito wa timu ya uchunguzi

Zitto alipendekeza timu iliyoundwa kuchunguza fedha hizo itoe taarifa yake kwenye Mkutano wa Bunge unaoanza Oktoba 29, mwaka huu, akieleza kuwa, "Kuendelea kukaa na taarifa, kutaongeza tetesi za kweli au za uwongo."

Alisema mpango huo wa kusaka fedha zilizofichwa nchini Uswisi, umelenga zile zilizofichwa na watu binafsi kutokana na rushwa au kuuza dawa za kulevya na kampuni kubwa za kimataifa.

Alibainisha kuwa wengi waliotambulika ni wanasiasa, vigogo wa jeshi na wakuu wa mashirika ya umma na watendaji wa Serikali.

"Katika mabenki ya Uswisi, kuna kiasi cha Dola za Marekani 197 milioni. Fedha nyingi zipo katika benki za Uingereza na visiwa vyake, Dubai na Mauritius," alisema na kuongeza;
"Wapo watu waliopata fedha kihalali, lakini wanaficha fedha hizo na mali zao nje ili kukwepa kodi. Wengi wa hao ni wafanyabiashara wakubwa nchini. Tanzania inapoteza Dola za Marekani 1.25 bilioni kati ya mwaka 2001 na 2012 kwa njia hizi."

Alibainisha kuwa Tanzania lazima itunge sheria ya kufilisi mali ambazo mtu anashindwa kuthibitisha amezipataje.

"Tayari ninafanyia kazi muswada binafsi wa sheria wa kubadilisha sheria ya makosa ya jinai ya mwaka 1991. Wasaidizi wangu wanafanyia kazi muswada huo ili usomwe kwa mara ya kwanza kwenye mkutano wa Bunge unaonza Oktoba 29 na kueleza kuwa sheria ya sasa ina upungufu," alisema.

Madai hayo ya Zitto yamekuja ikiwa umepita mwaka mmoja tangu Bunge kuipa Serikali muda wa kuchunguza sakata la vigogo walioficha mabilioni katika benki za Uswisi.

Zitto ndiye aliibua sakata hilo mwishoni mwa mwaka 2012. Kufuatia hoja hiyo, Serikali iliunda timu kutokana na Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka jana.
Werema ahoji Mwananchi ni Bunge?
Timu hiyo inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye jana baada ya kutafutwa na gazeti hili alisema, "Uchunguzi kuhusu walioficha fedha Uswisi bado haujakamilika."

Viongozi wengine wanaounda tume hiyo ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.

Alipoulizwa kama kuna uwezekano wa ripoti hiyo kuwekwa wazi katika Mkutano ujao wa Bunge, Werema alisema, "Kwa nini, kwani wewe ndiyo Bunge. Uchunguzi bado unaendelea"
Hata hivyo, kwa mujibu wa agizo la Bunge, tume hiyo inatakiwa kuwa imekamilisha uchunguzi wake mwezi huu na kuwasilisha ripoti yake katika mkutano huo wa Bunge.

Alipoulizwa kuhusu ripoti hiyo, Naibu Spika, Job Ndugai alisema, "Wiki ijayo katika kikao cha Kamati ya Uongozi, Serikali itatakiwa kutoa taarifa za uchunguzi huo na kama haujakamilika kikao hicho kitaamua jambo la kufanya na endapo uchunguzi utakuwa umekamilika zitapangwa taratibu za kuiwasilisha ripoti bungeni."

Waziri wa Fedha anena

Chanzo:Mwananchi

Naye Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema jana kuwa sheria za kimataifa zipo wazi kwamba fedha chafu zinazogundulika kufichwa nchi fulani, hurejeshwa katika Serikali ya nchi husika.

"Lengo la sheria hizi za kimataifa ni kuhakikisha kuwa fedha za wizi zinazoibwa nchi fulani, haziwezi kuhifadhiwa katika nchi nyingine," alisema.
Alipoulizwa kama wizara yake ina taarifa zozote kuhusu Watanzania walioficha fedha Uswisi alisema, "Kuna Tume iliundwa na Bunge kufuatilia suala hilo nadhani ndiyo itakuwa na majibu sahihi."

Uchunguzi wa walioficha mabilioni ya Uswisi uliibuka baada ya Benki ya Taifa ya Uswiss (SNB) kutoa taarifa mapema Juni 2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki nchini humo.

Orodha hiyo inadaiwa kuwa na majina ya baadhi ya Watanzania wenye akaunti zinazofikia Dola 196 za Marekani milioni ambazo ni sawa na Sh323.4 bilioni.

source: Mjengwa Blog

Wednesday, October 23, 2013

Siri ya sare Simba, Yanga

Mashabiki katika Mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa juzi uwanja wa Taifa na kutoka sare ya goli 3-3
Licha ya kugubikwa kwa siri kubwa ya matokeo ya mechi ya watani wa jadi iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3 Uwanja wa Taifa juzi, NIPASHE limebaini chanzo cha miamba hiyo kumaliza dakika 90 ikiwa nguvu sawa. 
Katika mechi hiyo ya raundi ya tisa ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo ambaye aliumudu vema mchezo huo, hadi timu hizo zinakwenda mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 3-0, hali iliyowafanya mashabiki wa timu hiyo kuamini kwamba wangeweza kulipa kipigo cha 5-0 walichokipata mwaka jana.

Yanga ambayo ilimiliki mpira kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Simba ilipata mabao yake kupitia kwa mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza na moja la kwanza kutoka kwa winga Mrisho Ngasa.

Hata hivyo, kipindi cha pili Simba iliwanyang'anya Yanga utawala wa mechi hiyo na kurejesha mabao yote matatu kupitia kwa Betram Mwombeki, Mganda Joseph Owino na Mrundi Gilbert Kaze, hiyo ikiwa rekodi mpya katika uwanja huo kwa mechi inayowakutanisha watani hao wa jadi mabao sita kufungwa goli moja.

Ubora wa Yanga dakika 45 za kwanza
Katika kipindi cha kwanza, Yanga haikufanya makosa kutokana na kucheza kandanda safi la kuonana huku wakitawala nafasi ya kiungo na kuwapoteza Haruna Chanongo na Abdulhalim Humud waliokabidhiwa jukumu zima la katikati.

Hali hiyo iliifanya Simba kupoteana katikati na kushindwa kusukuma mashambulizi mbele jambo lililotoa nafasi kwa  Yanga kuwashambulia, hivyo dakika ya 15, Didier Kavumbagu kupiga krosi iliyowahiwa na Ngasa ambaye bila kufanya makosa aliuzamisha mpira kimyani.

Bao hilo liwafanya Yanga kucheza kwa kujiamini zaidi huku Simba wakitawaliwa na hofu na katika dakika ya 35, makosa ya mabeki wa Simba kutokuwa makini yalisababisha Kiiza kuutendea haki mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite kwa kuuzamisha nyavuni.

Kosa la beki wa Simba, Nassor Masoud 'Chollo' la kumruhusu Kavumbagu kumchambua, hapa lilionekana, hivyo Mrundi huyo hakufanya makosa kabla ya kutoa pasi iliyomkuta Kiiza katika dakika ya 45 ambaye aliifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa  inaongoza kwa mabao 3-0.

Uzito wa Dhaira kufanya maamuzi na mawasiliano na mabeki

Kipa wa Simba, Abel Dhaira alikuwa mzito wa kufanya maamuzi, mara nyingi alikuwa mzito wa kutoka na pindi alipotaka kufanya hivyo alikuwa anasita, jambo liloifanya safu ya ushambuliaji ya Yanga kuutumia udhaifu huo.

Kwa ujumla safu nzima ya ulinzi ya Simba ilipoteana kuanzia kwa kipa hadi mabeki kwani hapakuwapo mawasiliano kati yake na Chollo, Haruna Shamte, Gilbert Kaze na Joseph Owino. 

Lawama za Kibadeni kwa Humud

Kocha wa Simba Abdallah Kibadeni alimshushia lawama Humud kutokana na kucheza chini ya kiwango katika mechi huku kukiwapo na neno 'hujuma'.
Hata hivyo, lawama hizo hazikuwa sahihi kwa Kibadeni kumtuhumu moja kwa moja baada tu ya kipindi cha kwanza kumalizika, kwani licha ya kumtoa, kimchezo haikuleta picha nzuri kwa wachezaji wenzake.
Ikumbukwe huo ni mchezo wa pili kwa Humud kucheza tangu msimu huu wa Ligi Kuu Bara kuanza, hivyo katika hali ya kawaida hakuandaliwa vya kutosha na isingekuwa rahisi kuhimili vishindo vya Athumani Iddi 'Chuji' ama Niyonzima ambaye kakosa mechi moja tu msimu huu.

Yanga ilimaliza dk. 90 kipindi cha kwanza Licha ya mashabiki na baadhi ya viongozi wa Yanga kuwashushia lawama kipa wao, Ali Mustafa 'Barthez', mabeki Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani na kiungo Chuji kwa kutokuwa makini huku wengine wakiwahusisha na neno 'hujuma' hilo kaliwezi kuwa sahihi.

Kwa ujumla wanapaswa kulaumiwa kwa makosa ya kiufundi na si hujuma, kwani kikosi kizima cha Yanga baada ya kwenda mapumziko kikiwa mbele kwa mabao 3-0, kiliamini huo ndiyo mwisho wa mchezo na kujiona tayari kimeshinda.

Wachezaji wa Yanga waliingia vyumba vya kubadilishia wakiwa wanashangilia ushindi, hatua iliyomfanya Kocha Mkuu, Ernie Brandts kufanya kazi kubwa ya kuwabadili kisaikolojia, lakini hilo halikiwezekana.

Hata hivyo, hiyo haikusaidia kitu kwani tayari kisaikojia walishaona wameshinda na kwamba kipindi cha pili walikuwa wanakwenda kukamilisha muda tu.

Kosa la Brandts
Hapa hakuna kushikana uchawi, licha ya juhudi kubwa za Brandts kuwaonya wachezaji kutoridhika na matokeo hayo, lakini alifanya makosa makubwa kiufundi, kwa kuendelea kuwaruhusu wachezaji kucheza mchezo wa kufurahisha badala ya kulinda 'kupaki basi' na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Simba ilianza kupata bao la kwanza katika dakika ya 53  kupitia kwa Betram Mombeki, bao hilo liliwachanganya Yanga, hivyo alichotakiwa kufanya Brandts ni kupunguza washambuliaji wawili na kuingiza mabeki huku akihimiza kupaki basi.

Hilo lingesaidia mashambulizi ya Simba kuishia katikati huku wakiwavuta wote kushuka kushambulia, wakati huo Yanga ikimbakiza winga mwenye mbio mbele, Ngasa kwa ajili ya mashambulizi ya kushtukiza jambo ambalo lingetoa nafasi kwao ya kupata bao la nne.

Brandts kumtoa KiizaHilo ni moja ya kosa kubwa lililofanywa na Mholanzi huyo, kwani Kiiza alikuwa katika kiwango cha juu sana na alishakuwa mwiba kwa mabeki wa Simba ambao walikuwa wakimkaba wawili wawili, hivyo kumsahau Kavumbagu, Ngasa na Niyonzima.
Kutoka kwa Kiiza na kuingia kwa Simon Msuva haikuwa 'sab' nzuri kwa kwa Yanga, kwani alichotakiwa kufanya ni kuingiza beki na tena si kumtoa mshambuliaji huyo.
Yanga haikuwa na kumbukumbu ya AC Milan vs Liverpool  2005
Kama Yanga ingekumbuka mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya AC Milan na Liverpool 2005, isingefanya makosa ya kutopaki basi.

Katika mechi hiyo, hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Milan ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-0. Mashabiki wa Liverpool hawakusita kuimba wimbo wao wa "You will never walk alone', kisaikolojia hilo liliwatia ari wachezaji wa Liverpool ambao walipigana na kusawazisha kipindi cha pili na kisha kuibuka na ushindi.

"Niliwashangaa mashabiki nini walichokuwa wanakiimba wakati tunaelekea kwenye vyumba vya kubadilishia na tulipokuwa tunaingia uwanjani kipindi cha pili tukiwa tumeshalala 3-0, kila tulipowatazama wachezaji tulijiona tuna deni kubwa na hakuna lisilowezekana," Steven Gerrard.
'Sab' na saikolojia kali ya Kibadeni 
Katika mechi za Simba na Yanga huwezi kukosa kusikia imani za kishirikina zikitawala, wapo wanaodai kuwa 'Yanga waliweka dawa katika lango lao ili kuzuia mabao kuingia' na kipindi cha pili wakasahau kuhama nayo, jambo lililofanya kibao kuwageukia.

Lakini kwa wachambuzi wa soka, hilo halipo, kwani hakuna asiyemjua Jamhuri Kihwelu 'Julio'  kuwa  ni kocha anayeaminika kwa uhamasishaji na mtaalam wa saikolojia kwa wachezaji, hivyo kwa kushirikiana na Kibadeni ni wazi kwenye chumba cha kubadilishia wachezaji waliambiwa 'hakuna lisilowezekana'.

"Tukiwapiga bao moja tu watachanganyikiwa na hapo tusifanye kosa", hicho ndicho kilichotokea baada ya Simba kufunga bao la kwanza, waliona hakuna cha kupoteza kama walivyoelezwa.

Hata walipofunga bao la kwanza, wachezaji waliiacha kazi ya kushangia kwa mashabiki na wao waliuwahi mpira na kuukimbiza kati, la pili hali ilikuwa hivyo na la tatu pia.
Mabadiliko aliyoyafanya Kibadeni kwa kuwatoa Humud na kumuingiza Said Hamisi (dk.49) huku Chanongo akimpisha William Lucien, ilikuwa ni sahihi kabisa na hilo liliifanya safu ya kiungo ya Simba kubadilika na kusukuma mipira mbele.
Mabao mawili ya haraka haraka yaliipoteza Yanga na kuanza kukanyagana huku wakipoteana katikati, hatua iliyotoa utawala kwa Simba kuweza kufunga la tatu dakika ya 84.

Tambwe alitoa fursa kwa wenzakeKwa muda wote wa mchezo, mabeki wa Yanga waliamini kumkaba Amisi Tambwe watamaliza safu ya ushambuliaji ya Simba, lakini hilo lilisababisha kusahaulika kwa  Mombeki aliyepata mpira akiwa mwenyewe na kuachia shuti lililojaa kimyani.

Hali kadhalika mambo yalikuwa hivyo kwa mabeki wa Yanga kuzembea na kumwacha huru Owino na baadaye Kaze waliofunga bila bughudha.
 
CHANZO: NIPASHE

POLISI WAREJESHA VITITA VYA FEDHA ZA WACHINA VILIZOIBWA KATIKA TUKIO LA UTEKAJI

kamanda_4f88e.jpg
"Jamani pesa yenu iliyoibiwa hii hapa," Ni kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Iringa ACP Athmani Mungi akiwaonyesha raia wa China maburungutu ya fedha zilizonusurika kutoka kwa majambazi waliowateka na kuwapora raia wa China.
fedha_9623f.jpg
Fedha shilingi Milioni 80 ambazo zimerejeshwa na jeshi la polisi kutoka mikononi wa majambazi wa tukio la utekaji wa raia wa Kichina, waliovamiwa katika mlima wa Nyang'olo mkoani Iringa.
silaha_e88e3.jpg
Kamanda Mungi akiwa ameshika Silaha aina ya ShortgunGreener ambayo imekatwa Mtutu (kitako) silaha iliyotupwa na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi baada ya kuzidiwa nguvu na askari polisi katika mapambano ya kuokoa fedha za raia wa China.
mamilioni_f716e.jpg
Mamilioni ya fedha yakiwa yameshikwa na kamanda wa jeshi la Polisi mkoni Iringa, mara baada ya kusalimika kutoka mikononi mwa majambazi, ambao walipora vitita vya fedha hizo kutoka kwa raia wa China.
raia_65da1.jpg
Raia wa China wakiwa na askari polisi katika ukumbi wa ofisi ya kamanda wa jeshi la polisi wakipewa taarifa za kupatikana kwa baadhi ya fedha zao na vifaa walivyoporwa na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi.(P.T)
raiaaa_21526.jpg
Raia wa China wakiwa katika ofisi ya kamanda wa jeshi la Polisi mko wa Iringa, wakifurahia kuziona fedha zao ambazo zilikuwa zimepolwa na majambazi katika mlima wa Nyang'olo Wilaya ya Iringa, wengine ni askari wa jeshi la Polisi.
WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wamewateka raia wanne wa China mkoani Iringa, na kisha kuwapora fedha, zaidi ya shilingi Milioni 130 za Kitanzania, fedha za Kichina, pamoja na vifaa mbalimbali zikiwemo simu tano katika mlima wa Nyang'oro uliopo mkoani Iringa.
Akizungumzia tukio hilo kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Iringa ACP Athmani Mungi amesema raia hao wa china wa kampuni ya SIETCO, inayojenga barabara ya Iringa- Dodoma, walikutwa na mkasa huo wakati wakirejea kutoka Iringa mjini, ambapo msako mkali wa jeshi hilo umefanikisha kupatikana kwa shilingi Milioni 80.
ACP Mungi amesema wachina hao walitekwa na kuporwa kiasi hicho cha fedha na vitu mbalimbali, mara baada ya kuchukua fedha hizo katika benki ya CRDB tawi la Iringa, na wakiwa katika gari lao aina ya Toyota yenye namba za usajili T. 335 CMX lilizuiliwa na gari kubwa aina ya Lori katika mlima wa Nyang'olo huku watu watano wenye siraha wakapora mfuko uliokuwa na fedha hizo.
Amesema majambazi hao walichukua pia simu za mkononi tano na funguo za gari la wachina na kutokomea nalo pamoja na kiasi hicho cha fedha cha shilingi Milioni 135, ambazo walikuwa wanarudi
nazo katika kambi yao ya Mtera.
"Wachina hao walikuwa wametoka kuchukua fedha hizo katika benki ya CRDB tawi la Iringa mjini bila kuwa na ulinzi wowote wa askari Polisi, na walikuwa wanazipeleka katika kambi yao iliyopo
Mtera," Alisema Mungi.
Amesema jeshi la polisi baada ya kupata taarifa hiyo walifanya oparesheni la kuwasaka majambazi hao mchana na usiku, kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vya tarafa ya Isimani, ambapo zoezi hilo liliendelea mpaka siku ya tarehe 23 alfajiri walipowaona majambazi hao.
"Oparesheni ya kuwasaka majambazi waliofanya tukio hilo iliendelea usiku na mchana, askari polisi kwa kushirikiana na wananchi, na alfajiri ya leo majira ya saa kumi askari yaliyaona majambazi hayo na ndipo mapambano makali yalianza, huku majambazi na askari wakirushiana risasi za moto," Alisema.
Pia amesema mapambano makali yaliwachanganya majambazi hayo na kupelekea kutupa Silaha aina ya Shortgun Greener iliyokuwa imekatwa Mtutu (Kitako) ikiwa na risasi moja chemba, huku majambazi hayo yakitupa begi moja lililokutwa na shilingi Milioni 80, na lingine likiwa na Biscuit na vitu vingine vya kichina.
Mungi amesema katika oparesheni hiyo pia wamefanikiwa kumkatata jambazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuhofia kuharibu upelelezi wa kuwasaka majambazi wengine wanne waliofanikiwa kutoroka.
Mungi amesema jambazi huyo amekamatwa katika kijiji cha Itono akiwa katika gari aina ya Hiace na kukutwa na Pochi ya wachina ambayo ilikuwa na vitu vilivyoibwa kwenye eneo la tukio hilo la
utekaji.
"Vitu alivyokutwa navyo mtu tuliyemkamata ni fedha za kichina zinazofahamika kama Yuan zikiwa 97, nyingine ni fedha hizo hizo za kichina zinaitwa Jiao hizo zilikuwa tatu, leseni ya udereva mali ya mchina Gang Cheng, Leseni ya udereva ya Hua -Li-wei, Simu moja ya kichina pamoja na Vitambulisho vilivyoandikwa kwa lugha ya Kichina," Alisema Mungi.
Aidha kamanda Mungi ametoa onyo kwa majambazi kuacha mara moja uharifu kwa madai kuwa mkoa wa Iringa si salama kwa majambazi na waharifu wa aina yoyote kwani hata wanaotoka nje ya mkoa huo wakiingia kufanya uharifu hawatatoka salama, huku akiwaasa wananchi kuacha mara moja kusafiri na fedha kiasi kikubwa pasipokuwa na ulinzi wowote.
Pia Kamanda Mungi amewashukuru wananchi walioshirikiana na jeshi la polisi katika kufanikisha zoezi la kupatikana kwa fedha hizo, pamoja na baadhi ya vitu vya wachina hao.
Hata hivyo siku za hivi karibuni, gari la kampuni ya E. Awadhi, kampuni inayojihusisha na usafirishaji wa mafuta nchini Zambia na Malawi lilitekwa katika eneo la Igumbilo mjini Iringa na kisha
watekaji kutoroka na gari ambalo lilikuwa limejaza mafuta katika mataki yake, huku jeshi hilo likifanikiwa kumnasa mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo.
MWISHO

Chanzo:Oliver Motto/ mjengwa blog

Katiba kicheko vyama vyote

Viongozi wa vyama vya Siasa,(kushoto)Isaack Cheyo(UDP) Nancy Mrikaria(TLP) Fahmi Nassoro Dovutwa (UPDP),James Mbatia NCCR-Mageuzi,Profesa Ibrahim Lipumba(CUF),Philip Mangula(CCM) na Dk Willibrod Slaa(Chadema)wakiwa wameshikana mikono baada ya kikao cha pamoja jijini Dar es Salaam jana.

Dar es Salaam. Serikali inatarajia kuandaa hati ya dharura ili kuwezesha kufanyika kwa maboresho ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba ambayo yatajadiliwa upya katika Mkutano wa Bunge unaoanza Oktoba 29 mjini Dodoma.

Tayari vyama vya upinzani na chama tawala vimekubaliana taratibu muhimu za kufuata ili maboresho hayo yaweze kupita ndani ya Bunge. Muswada huo haukuwa umepangwa kujadiliwa katika mkutano ujao wa Bunge ndio maana itabidi iombwe hati hiyo ya dharura. Hatua hiyo ni ushindi kwa vyama vitatu vya upinzani vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi, ambavyo vilipinga muswada huo wakati wa mkutano uliopita wa Bunge Septemba, mwaka huu.

Muswada wa sheria hiyo uliopitishwa Septemba na Bunge ulisusiwa na wabunge wa vyama hivyo wa upinzani kwa maelezo kuwa una kasoro kwenye baadhi ya vipengele.

Hata hivyo, wabunge wa CCM waliamua kuendelea na mjadala na kupitisha muswada huo kitendo ambacho kilisababisha mvutano mkubwa uliomfanya Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge kumaliza tofauti zao.
Mbatia asoma tamko la vyama

Akisoma tamko la vyama vya siasa mbele ya waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema hatua ya Serikali itakuja baada ya vyama vya siasa kufikia mwafaka wa vipengele vinavyotakiwa kufanyiwa marekebisho kwenye muswada huo. Mbatia alisema kuwa tayari kazi hiyo imefanyika na mapendekezo yao yameshapelekwa serikalini ingawa hakutaka kuingia kwa undani walichopendekeza katika marekebisho hayo.

Vyama vilivyokutana ni pamoja na CCM, Chadema, CUF, NCCR -Mageuzi, TLP. Pia vyama vya UDP na UPDP vilishiriki kwa niaba ya vyama visivyo na wabunge.

Mbatia alisema hatua inayofuata ni vyama kuunda kamati yao na Serikali kuunda yake ili kukubaliana kwa pamoja maeneo muhimu ya marekebisho.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kuufanya mchakato wa Katiba kuwa shirikishi baada ya kamati hizo kumaliza kazi yake.

“Baada ya hapo, Serikali itaandaa hati ya dharura ili marekebisho yapelekwe haraka katika Mkutano wa Bunge unaoanza Oktoba 29, “ aliongeza Mbatia.
Mbatia alisema wanataka kabla ya Bunge la Katiba halijaanza basi sheria husika ifanyiwe marekebisho. “Tunawaomba Watanzania hasa wabunge waunge mkono juhudi hizi za vyama na Serikali ili kuhakikisha mchakato wa Katiba Mpya unakuwa shirikishi. Wabunge waridhie marekebisho haya na kuyapitisha,” alisema mbunge huyo wa kuteuliwa na Rais.

JK awapa goli wapinzani
CCM, ambayo wabunge wake walipitisha muswada kwa kauli moja, iliweka kando tofauti zake za kiitikadi na kimtizamo na kuungana na Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na vyama vingine vya upinzani.

Kitendo hicho cha CCM kilikuja baada ya Rais Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge na vile visivyokuwa na wabunge, wiki iliyopita na kuvitaka vyama hivyo kukaa pamoja na kutoa mapendekezo ili yafanyiwe kazi na Serikali.
Kitendo hicho ni sawa na ushindi wa vyama vya upinzani kwani pamoja na kuwa wabunge wachache tofauti na CCM bado Rais Kikwete aliamua kusikiliza hoja zao.

CCM na Chadema damu damu
Katika hatua ya kuashiria kuwa vyama hivyo viko bega kwa bega, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa walishikana mikono pamoja na viongozi wengine watano wa vyama vya siasa na kutoa tamko la pamoja kuhusu kuboresha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Tukio hilo la aina yake lilifanyika jana na kuongozwa na Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania ambacho kilipewa jukumu na Rais kuratibu ukusanyaji wa maoni ya maboresho ya muswada huo.

Mangula alipoulizwa kama wabunge wa CCM watakuwa tayari kupitisha maboresho ya sheria hiyo itakaporejeshwa tena bungeni alisema kwa kifupi; “Siwezi kuwasemea wabunge wa CCM.”

Alipobanwa zaidi kuhusu ushiriki wa CCM kwenye umoja wa vyama hivyo. Alisema: “CCM haijawahi kuandaa rasimu yake ya Katiba, ila nachojua ni kwamba kila chama kilipewa nafasi na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa maoni yake na CCM ni miongoni mwa vyama hivyo. Katiba Mpya ni kitu kizuri kwa taifa letu.”

Serikali yakubali ombi la tume
Serikali imekubali ombi la Tume ya Mabadiliko ya Katiba la kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na wananchi na asasi mbalimbali.

Habari zilizopatikana kutoka vyanzo vya habari ndani ya Serikali na kuthibitishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe zilisema kuwa awali kabla ya kuomba muda huo, tume hiyo ilikutana na Rais Kikwete ili kuomba kuongezewa muda.

Maana yake ni kuwa Tume hiyo iliyoanza kazi Mei Mosi, mwaka jana ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba Mosi, mwaka huu hivyo sasa kazi yake itakamilika Desemba. Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Chikawe alisema, “ Kwa nini wakataliwe kama wanaona muda hauwatoshi.” Kwa mujibu wa Waziri Chikawe, muda waliomba unakubalika kisheria na kwamba wanaweza kuongezewa hadi miezi miwili.

Alipoulizwa kama haoni muda huo utasababisha kuchelewesha mchakato mzima wa Katiba, Waziri Chikawe alisema, haoni kama kuongezwa kwa muda huo kutaathiri chochote. “Nataka kuwahakikishia Watanzania hakuna haja ya kuwa na wasiwasi mchakato utaendelea kama kawaida kitakachoongezeka ni mwezi mmoja hivyo badala ya rasimu ya pili kukabidhiwa kwa Rais Novemba sasa itaenda mpaka Desemba,”alisema Waziri Chikawe.
Imeandikwa na Tausi Mbowe, Fidelis Butahe na Editha Majura.

source: mwananchi