WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, December 28, 2013

SMZ haina uwezo kifedha-Nahodha

“Kama Muungano unavunjika leo, Wazanzibari laki tatu waliokuwepo katika mikoa ya Tanzania Bara watakwenda kuishi wapi,” Nahodha 
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi

Zanzibar. Waziri Kiongozi mstaafu Shamsi Vuai Nahodha amesema mfumo wa Muungano wa Serikali tatu unaweza kutetemesha misingi yake na kusababisha kuvunjika, kwa vile Zanzibar haina uwezo wa kirasilimali kuchangia uendeshaji wake.
Nahodha ameyasema hayo kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Alabama, Mwembeshauri, ambao ni wa kwanza tokea uteuzi wake wa wadhifa wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa utenguliwe.
Nahodha alisema kwamba kutokana na vyanzo vya mihimili ya uchumi wa Zanzibar kuwa vichache haitaweza kuchangia gharama za uendeshaji na kutoa mfano wa bajeti ya wizara moja ya Ulinzi inayotumia Sh1.2 trilioni, wakati Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikitumia Sh800 bilioni kwa mwaka kunakopita bajeti nzima ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo hutumia Sh600 bilioni kwa mwaka.
Nahodha alisema kama Zanzibar ingekuwa na uwezo wa kumudu gharama hizo ingeweza kuboresha mishahara ya askari wake wa Vikosi vya SMZ na kuwapa mikopo ya elimu ya juu wanayoomba kila mwaka kutaka kuendelea na masomo.
“Vyanzo vya Zanzibar kimapato ni hafifu tusijidanganye, ziko wapi fedha za kumudu gharama za uendeshaji kama zipo ni kipi kinachozuia tusilipe mishahara minono kwa vikosi vyetu na kuwapatia maisha bora, mfumo wa Serikali tatu una viashiria vya kutaka kuvunja muungano,” alisema Nahodha akishangiliwa na wananchi waliokuwepo mkutanoni.
Alisema wakati huu wa mjadala wa uundwaji wa Katiba Mpya ni wakati mwafaka wa kushughulikiwa kwa maeneo yenye kasoro za kimsingi na siyo kufikiria kubadilisha mfumo wa Muungano kama inavyohitajiwa na baadhi ya wanasiasa kwa utashi na matakwa binafsi.
“Ndugu zangu, kama leo hii tukivunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Wazanzibari tujue tutajuta na kusaga meno, nasema wenye wazo hilo ni wapuuzi ila msiwapuuze,” alisema.
Alisema Muungano umeleta faida kubwa kwa pande mbili na kutoa mfano wa Wazanzibari kuweza kulitumia soko la kiuchumi la Bara lenye watu zaidi ya milioni 44, kupata huduma za matibabu katika hospitali za Tanzania Bara, ulinzi na usalama na mambo mengine ambayo Zanzibar hakuna.
source: mwananchi

Jairo, Nyoni wasafishwa kimyakimya


Jairo

Serikali imewasafisha aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo huku ikimpandisha cheo aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali Deo Mtasiwa.
Nyoni alisimamishwa kazi pamoja na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa  na wote kwa pamoja walikuwa na tuhuma za kutumia vibaya madaraka yao wakiwa watumishi wa umma.
Jairo kwa upande wake alisimamishwa kazi kutokana na kuchangisha fedha kinyume cha sheria kwa lengo la kusaidia mchakato wa kupitisha bajeti ya wizara yake, katika mwaka wa fedha 2011/2012 na sasa ameondolewa kwenye utumishi wa umma, huku Bunge likiwa bado halijapata taarifa ya utekelezaji wa maazimio yanayomuhusu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Nyoni kwa sasa amerejea kwa mwajiri wake wa awali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akishikilia nafasi ya mmoja wa wakuu wa idara, huku Dk Mtasiwa akiwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Katibu Mkuu Kiongozi
 Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amelithibitishia gazeti hili kuhusu watumishi hao na kwamba taratibu zimefuatwa.
“Mimi ninachojua ni kwamba Blandina alikuwa mwajiriwa wa TRA na mkataba wake ulikuwa haujaisha… Siyo kwamba alikuwa na mikataba miwili, kwenye utumishi wa umma huwa kuna utaratibu wa kuazima watumishi wa umma.
Ndiyo maana unaweza kukuta mwanajeshi anatolewa jeshini na kupelekwa uraiani au mtumishi kutoka idara moja kwenda nyingine. Kwa upande wetu sisi tulishamwondoa kwenye ukatibu mkuu na kule TRA hakuwa na tatizo,” alisema Balozi Sefue.
Kuhusu Dk Mtasiwa alisema: Uteuzi wa Dk Mtasiwa ulikuwa wazi na hata alipoapishwa mambo yote yalitangazwa hadharani.” Aliendelea kufafanua kuhusu Jairo akisema: “Jairo alishaondolewa kwenye ukatibu mkuu, siyo mtumishi tena wa umma.” Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alimtetea Nyoni akisema kuwa amerudi kwenye ajira yake ya awali.
“Siyo kwamba ameajiriwa TRA, amerudi tu kwenye ajira yake ya zamani, alikuwa akifanya kazi hapa akaazimwa na sasa amerudi,” alisema Kayombo na kuongeza: “Kwani amefanya kosa gani? Kuna mashtaka yoyote aliyofanya unaweza kuyathibitisha?”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Bernard Mchomvu ambaye alisema Nyoni alishasafishwa na Serikali ndiyo maana wamempokea. “Yule aliazimwa tu na Serikali…Sasa kama Serikali imesham-clear sisi tutamkataaje?” alihoji na kuongeza:
“Kwa sababu sikumwomba huyo mtu, nimeambiwa kwamba huyo yuko safi mimi nifanyeje? Unajua watu wanafurahia wengine wakipata matatizo, hata kama mtu ameua, basi walete ushahidi. Hata unaposema nchi imejaa rushwa, ulete ushahidi… kama Serikali imeshamsafisha, ningemkataa ningekuwa mtu wa ajabu.”
Jitihada za kumpata Nyoni kupitia simu yake ya mkononi hazikuzaa matunda, baada ya simu yake kupokelewa na sauti ya kiume iliyosema kuwa namba imekosewa.
Hata alipotafutwa kwa namba nyingine, simu ilipokelewa na mwanamke aliyejitambulisha kama mfanyakazi wa Wizara ya Afya na kwamba namba hiyo kwa sasa haitumii tena. Alipotafutwa kwa njia ya simu, Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashilillah, alisema suala hilo aulizwe msemaji wa Serikali juu ya Bunge.
“Ongea na msemaji wa Serikali juu ya mambo ya Bunge,” alijibu kwa njia ya ujumbe wa simu.
Lukuvi
Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi alisema kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hayuko ofisini.
“Niko ‘airport’ nasafiri kwenda South Africa, msinipigie simu, siko ofisini hadi mwezi ujao (Januari),” alisema Lukuvi na kukata simu yake.
Awali alipoulizwa kwa njia ya simu baada ya mwandishi kuelezea suala hilo alisema ana kazi nyingi na kwamba apigiwe baadaye.
Makani azungumza
Mwenye wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza tuhuma hizo, Ramo Makani, ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini, akizungumza na gazeti hili kuwa: “Ni kweli mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza suala hilo, kwa utaratibu kamati kama hiyo huundwa kwa kanuni za Bunge kwa kupewa majukumu maalumu… Kama mbunge tu ningefurahi kusikia taarifa ya Serikali bungeni baada ya kupata taarifa ya Bunge,” alisema Makani na kuongeza:
“Serikali iliahidi kuleta taarifa bungeni ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge. Mimi sikumbuki kama taarifa hiyo imeshasomwa bungeni, labda wewe mwenzangu umebahatika kuisikia. Kwa hiyo bado tunasubiri… Kama Serikali imechukua hatua, mimi sijui.”
Tuhuma za Nyoni
Nyoni alituhumiwa kutenda makosa saba ambayo yaliainishwa wakati wa mgomo wa madaktari ulioanza Januari mwaka jana, hali iliyomlazimisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kutangaza kumsimamisha kazi ili uchunguzi uweze kufanyika.
Baadhi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili ni pamoja na kujilipa mshahara wa ziada kupitia Mradi wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP) nje ya mshahara aliokuwa akilipwa na Serikali, kutengua utaratibu rasmi wa kila Idara ya Wizara ya Afya kuwa na ofisa ununuzi wake kwa kujiweka yeye mwenyewe.
Tuhuma nyingine zilikuwa kulazimisha Wizara ya Afya kununua sare za madereva, suti za sikukuu (Sabasaba na Nanenane) na maua kutoka Mariedo bila kushindanisha na muuzaji mwingine kinyume na kanuni za ununuzi.
Katika mikutano yote inayofanyika wizarani, alikuwa akilazimisha Kampuni ya Kaliula Catering Services kupewa zabuni ya kutoa huduma ya chakula kwa washiriki tangu alipotua wizarani kama Katibu Mkuu.
Sakata la Jairo
Hatua ya kumwondoa Jairo katika utumishi wa umma nayo imefanyika kimyakimya kwani Serikali hadi sasa haijawasilisha bungeni majibu ya maazimio ya Bunge kuhusu sakata hilo ambalo pia liliwagusa watumishi wengine wa Wizara ya Nishati na Madini. Maazimio hayo ni yale yaliyotokana na matokeo ya uchunguzi  wa Kamati Teule ya Bunge   iliyoongozwa na Makani na kubainisha kuwapo kwa makosa ya kiutumishi na kijinai ambayo yangewafikisha baadhi ya watumishi hao katika vyombo vya sheria.
Mbali na Jairo, kamati hiyo ilipendekeza kuwajibishwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.
Hata hivyo, ni Jairo pekee kati ya hao aliyewajibishwa kwa kusimamishwa kazi na baadaye kuondolewa katika wadhifa wake. Luhanjo alistaafu utumishi wa umma bila kuchukuliwa hatua zozote wakati Utouh anaendelea na wadhifa wake.
Pia katika taarifa yake, Kamati Teule ilisema utaratibu wa uchangishaji wa fedha Sh418.081 milioni uliofanyika katika Wizara ya Nishati na Madini haukuwa na uhalali kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.
Pamoja na mambo mengine, Bunge liliazimia kwamba ufanyike ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) kwa matumizi ya Sh214 milioni, ambazo kati ya hizo Sh126 milioni Kamati Teule ilikataa maelezo ya matumizi yake na Sh88 milioni ni zile zinaotajwa kwamba zilitumika katika kugharimia semina kwa wabunge.
Azimio jingine ni lile lililoitaka Serikali iviagize vyombo vya dola kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za kughushi na ubadhirifu zilizoelezwa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kama ilivyoelekezwa.
Baada ya kufikiwa kwa maazimio hayo, Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe iliahidi kuyafanyia kazi na kuwasilisha majibu bungeni.
“Kwa sababu ya ukubwa na uzito wa taarifa hii, ni vigumu kuitolea majibu yote hapa hapa, ninachoweza kufanya ni kuipokea pia tutakapokuja katika Mkutano wa Sita, tunatarajia kuleta majibu ya hoja zilizomo kwenye taarifa hii,” alisema Chakawe ambaye sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria
source: mwananchi

Friday, December 27, 2013

Nahodha: Sitavunjika moyo kwa yaliyonikuta





Zanzibar. Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha amesema licha ya kuvuliwa uwaziri ataendelea kuwa kiongozi wa kisiasa na kukitumikia chama chake na wananchi bila ya kuvunjika moyo.

Nahodha, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa ametoa kauli hiyo siku chache baada ya kuondolewa

kwenye Baraza la Mawaziri na Rais Jakaya Kikwete kutokana na matatizo yaliyotokea katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Akihutubia wanachama wa CCM waliomlaki na kumsikiliza kwenye Ofisi ya chama hicho Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja jana, Nahodha alisema yaliyomtokea ni mambo ya kawaida katika medani za utumishi wa umma.
“Pamoja na hayo yaliyotokea, nitaendelea kulitumikia taifa, chama changu na wananchi kwa uaminifu, juhudi na uwezo wangu wote,” alisema Nahodha, ambaye pia ni Mwakilishi wa Mwanakerekwe.
Alisema amewajibika serikalini kutokana na matakwa ya wajibu katika utendaji wa pamoja na kusema kitendo hicho ni mfano wa ajali inayoweza kumkuta mtu yeyote katika safari ya maisha.

“Sina kinyongo wala muhali, yaliyotokea ni mambo ya kawaida katika medani za uongozi, wajibu na dhati yangu ni kuwa mtii kwa Serikali zote. Pia kuitumikia CCM na kushirikiana na wananchi wenzangu. Binadamu hawezi kujiepusha na mitihani, ”alisema Nahodha.

Alisema alikabidhiwa dhamana na viongozi wake ili kulitumikia taifa na kutimiza wajibu ipasavyo katika nyadhifa mbalimbali na yaliyomtokea ameyapokea kwa mikono miwili na hana kinyongo.
Mawaziri walioenguliwa pamoja na Nahodha ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Dk Mathayo David (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).
Mapinduzi ya Zanzibar

Akizungumzia Mapinduzi ya Zanzibar, Nahodha alisema ni ufunguo uliofungua milango ya fursa kwa wananchi wanyonge waliokandamizwa na ukoloni huku akisifu uongozi kwa miaka minane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Mzee Abeid Amani Karume.

Alisema kiongozi huyo licha ya kuongoza Mapinduzi ya Januari 12, 1964, aliifanyia mema Zanzibar na watu wake katika kuwaletea maendeleo na kwamba atakumbukwa na vizazi vyote hadi mwisho wa dunia.
“Kufanya Mapinduzi haikuwa kazi nyepesi. Waliofanya walikuwa ni majasiri na wazalendo. Juhudi zao ni matunda haya leo baada ya miaka 50 kupita nchi ikiwa katika utulivu na amani,” alisema Nahodha, ambaye alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar kuanzia mwaka 2000 hadi 2010.

“Uongozi wa Mzee Karume ni mfano wa aina yake, mwaka 1964 hadi 1972 aliiletea mabadiliko makubwa Zanzibar. Alijenga viwanda, makazi bora, elimu bila malipo, barabara na kuimarisha huduma za jamii,” alisema Nahodha.

“Nasikia kuna watu hawataki kulisikia neno Mapinduzi, hao ni wapuuzi na wapuuzeni. Mapinduzi na Muungano ni uti wetu wa mgongo, Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Karume waliona mbali, tusibeze mitazamo yao kwa tamaa za madaraka,” alisema.

Kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Nahodha alisema angependa ubaki katika mfumo na Serikali mbili na kusema pamoja na uzuri wake, zipo changamoto na kasoro zinazohitaji kurekebishwa na kuwa na muungano wenye nguvu za kiuchumi.

Alisema kazi ya kurekebisha makosa ni nyepesi lakini wazo la kuvunja Muungano lina gharama kubwa kuliko inavyofikiriwa na baadhi ya watu wanaotaka uvunjike.
“Sina uwezo wa kuwachagulia watu kitu wanachokipenda na kukitamani. Imani yangu ni kwamba nje ya Muungano hatutabaki salama kama ilivyo sasa. Muungano wetu umekuwa kinga na nguzo kwa nchi zetu mbili na usalama na wake,” alisema Nahodha.

Aliitolea mfano Sudan Kusini ambayo ilitaka ipewe mamlaka yake kamili akisema hivi sasa imejikuta ikiwa katika machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na kuibuka kwa mgawanyiko wa kijamii unaotishia mustakabali wa Taifa hilo.

“Itazameni Sudan Kusini, tusipokuwa waangalifu na makini yanaweza kutukuta. Angalia vita ya Somalia inaitesa Kenya na kutukosesha amani, tusikubali kugawanywa na viongozi ambao wanawaza madaraka.”

source: mwnanchi

Thursday, December 26, 2013

Rais Kikwete awasili leo na siri nzito

 


Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete anatua nchini leo akiwa na lake moyoni kuhusu hatima ya baraza lake la mawaziri, baada ya kutengua uteuzi wa mawaziri wake wanne, wiki mbili zilizopita.

Rais Kikwete alikwenda Marekani, Desemba 18, mwaka huu kufanyiwa uchunguzi wa afya yake na akiwa huko, upepo wa kisiasa ulibadilika na kumlazimisha kuchukua hatua hiyo ambayo inampa wajibu wa kupanga upya safu yake ya uongozi.

Mawaziri ambao uongozi wao ulitenguliwa ni wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo David Mathayo.

Kung’oka kwao kunatokana na ripoti ya kamati ndogo ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu athari zilizotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo ilizua mjadala mkali kiasi cha wabunge kumshinikiza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwamba naye aachie ngazi.

Hivyo kitendawili kingine kikubwa kinachomkabili Rais Kikwete ni iwapo ataamua kuendelea kufanya kazi na Pinda ambaye alishambuliwa na wabunge kwamba naye ang’oke kwa madai kwamba ameshindwa kusimamia utendaji serikalini.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Ibara ya 52(1) Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka juu ya kudhibiti usimamiaji na utekelezaji wa siku wa kazi na shughuli za Serikali.

Katiba inasema: “Katika utekelezaji wa madaraka yake, Waziri Mkuu atatekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe. Ibara ya 53 (1) inaeleza: “Bila kuathiri masharti ya Katiba hii, Waziri Mkuu atawajibika kwa Rais kuhusu utekelezaji wa madaraka yake.”

Hata hivyo, ni kama Rais Kikwete alishaamua kumwokoa Pinda pale alipompa maagizo kwamba alitangazie Bunge uamuzi wake wa kutengua uteuzi wa mawaziri wanne.

Ripoti hiyo iliyosomwa na Mwenyekiti wake, James Lembeli ilifichua kuwapo kwa vifo na mateso ya wananchi vilivyofanywa wakati wa operesheni hiyo iliyoendeshwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), maofisa wa Usalama wa Taifa na Polisi.

Mbali ya pengo lililoachwa na mawaziri hao wanne, Rais Kikwete pia ndiye mwenye majawabu kuhusu hatima ya wale waliotajwa kuwa ni mawaziri mizigo kwa kushindwa katika utendaji wao, hasa ikizingatiwa kuwa shinikizo la kuwajibishwa kwao linatoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye ni mwenyekiti wake.

Kitendawili cha Pinda
Zipo hoja kadhaa, iwapo Rais Kikwete atamwondoa Pinda kama ambavyo wabunge walisisitiza wakati wakichangia ripoti hiyo, huku wakirejea yaliyowahi kutokea serikalini lakini Waziri Mkuu huyo akakwepa kuwajibika.

Hata hivyo, ikumbukwe kwamba isingekuwa rahisi kwa Pinda kuachia ngazi wakati Rais akiwa nje ya nchi kutokana na ukweli kuwa ingekuwa na maana kuwa Baraza la Mawaziri lingetakiwa kuondoka.

Akizungumza juzi, Jaji Mstaafu, Thomas Mihayo alisema kitendo cha Waziri Mkuu kujiuzulu kitamweka Rais katika wakati mgumu kwa sababu Serikali itavunjwa na kuundwa upya.

“Kuunda upya Baraza la Mawaziri ni gharama, tena ikizingatiwa kuwa tunaelekea katika Bunge la Katiba, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 2015, mabadiliko yakifanyika nadhani nchi itayumba,” alisema Jaji Mihayo.

Jaji huyo alisema haoni sababu za Pinda kung’olewa wakati imebaki miaka miwili tu ufanyike uchaguzi mkuu mwingine, na kufafanua kuwa hata kama akija Waziri Mkuu mpya hataweza kufanya mapya kutokana na muda uliobaki.

“Sidhani kama ni busara kushinikiza ang’oke ni wazi kuwa madhara yatakuwa makubwa kuliko mema, lakini ngoja tusubiri tuone uamuzi utakuwaje,” alisema Jaji Mihayo.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema hatua hiyo haitatatua tatizo la mfumo mbovu uliopo zaidi ya kuongeza gharama za kuwatunza mawaziri wakuu wastaafu.

“Ukichunguza kwa makini, Waziri Mkuu Pinda hana tatizo, bali ni mfumo mbovu ambao kimsingi unatakiwa urekebishwe na Rais Kikwete,” alisema na kuongeza:

“Ukimtoa Pinda leo, sanasana unaongeza tu gharama za kutunza mawaziri wakuu wastaafu. Tangu Rais Kikwete anaingia madarakani alishaujua mfumo alioukuta, kwa nini asingeurekebisha ili haya yasitokee?

“Rais anapaswa kupunguza safari za nje na ajikite kushughulikia matatizo kama haya kwa kurekebisha mfumo wa nchi ili usiingize nchi kwenye matatizo.”
Kwa upande mwingine kumekuwa na harakati za kukusanya saini za wabunge ili kuendesha mchakato wa kumng’oa Pinda iwapo Rais hatachukua hatua.

Mawaziri mizigo
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye ndiyo walikuwa watu wa mwanzo kutoa orodha ya mawaziri mizigo wakati walipokuwa katika ziara kwenye mikoa ya kusini.

Waliwataja Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Dk Mathayo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima.
Viongozi hao walitaka mawaziri hao wajieleze mbele ya Kamati Kuu (CC), ya chama hicho juu ya kushindwa kwao kwenye utendaji wao.

Hata hivyo, orodha hiyo iliongezeka baada ya Bunge kumtaja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Hawa Ghasia pamoja na Manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kupima na kutafakari kama wanatosha kusimamia wizara hiyo kutokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kufichua ufisadi katika wizara hiyo.

Kamati Kuu ya CCM iliyokutana Desemba 14, mwaka huu chini ya Rais Kikwete na iliwahoji Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Ghasia na Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum na baadaye taarifa ya chama hicho ilisema imeliacha suala hilo mikononi mwa Rais kwa hatua zaidi.
 source: Mwananchi

Wednesday, December 25, 2013

Zitto ‘awalipua’ Dk Slaa, Mbowe



Mbunge wa Kigoma kaskazini, Zitto

Kigoma.Mbunge wa Kigoma Kaskazini,Zitto Kabwe, amejibu mashambulizi kwa viongozi wa Chadema, kutokana na kile alichosema wanazunguka na kusema maneno yasiyo ya ukweli.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliokusanyika katika Uwanja wa Mwanga Centre, Kigoma mjini, alisema alichukua kadi ya uanachama wa Chadema mwaka 1993 wakati huo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa akiwa bado yuko CCM.

“Wakati hao wenye midomo mikubwa wanaoongea sasa, walipokuwa wamekumbatia watawala, nyinyi mlikuwa mnapigwa mabomu kutaka mageuzi, eti leo wao wapinzani zaidi kuliko sisi na ndiyo maana hatuwezi kuwaachia.
Hatuwezi kukubali, hatutoki, demokrasia ni mchakato na mwenzenu nimekuwa kwenye mchakato huu. Kadi yangu ya Chadema nimeichukulia kwenye uwanja huu, tarehe moja mwezi wa nne mwaka 1993, nikiwa na miaka 16, wakati nachukua kadi yangu, Katibu Mkuu wa chama changu alikuwa yuko CCM.

Akizungumza kile alichosema ni uongo unaosambazwa na viongozi wa juu wa chama hicho, Katibu Mkuu Dk Slaa na Mwenyekiti wake Mbowe waligawana maeneo Mbowe akaenda Kanda ya Ziwa na Dk Slaa Kanda ya Magharibi.

Alisema kwenye mikutano hiyo, Mbowe anasema kuwa endapo mbunge huyo atarudi yeye Mbowe atajiuzulu, suala alilosema linaonyesha kuwa tayari ameshafukuzwa bila hata utetezi wake kusikilizwa.

Alisema baada ya viongozi hao kuzungumza na kusema mambo hayo na yeye aliamua kurudi nyumbani Kigoma na baada ya kuona hilo Dk Slaa akahoji mbunge huyo anafanya vikao hivyo kama nani.

“Mimi nimekata rufaa, wajumbe wa baraza kuu wa Mtwara, Ruvuma wanaandika barua wanataka mkutano mkuu, Katibu Mkuu akiwa Igunga anasema hiyo ni haramu na hao wafuasi wa Zitto watafanya Zitto afukuzwe, si __wamwamesha nifukuza? takachokuja kunijadili, hivyo si wameshanifukuza ?

source: mwananchi

Tuesday, December 24, 2013

Lissu azungumzia maamuzi kuhusu Zitto

Mwanasheria Mkuu wa Chadema,Tundu Lissu
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, amesema chama hicho kitaendelea kusimamia misingi yake ya katiba na taratibu zake kwa ama kuwafukuza, kuwaonya au kuwasamehe viongozi na wanachama wanaopatikana na makosa ndani ya chama.
Aidha, amesema uamuzi wa kumvua nyadhifa zake Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na wenzake wawili haujachukuliwa eti kwa sababu baadhi ya viongozi wandamizi wanachuki naye.

Lissu alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Sherui Jimbo la Iramba Magharibi mkoa wa Singida katika mkutano wa hadhara.

“Tulilazimika kufanya maamuzi magumu ya kuwavua nyadhifa akina Zitto ili kukijenga chama na tutaendelea kufanya maamuzi zaidi na ikibidi kufukuza, kukemea na kusamehe bila kumuonea mtu wala kumpendelea,” alisema.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema chama chochote cha siasa ni lazima kifuate desturi na katiba yake kwani bila kufanya hivyo wananchi watakosa imani nacho.

Alisema nafasi ya Naibu Katibu Mkuu aliyokuwa nayo Zitto kabla ya uamuzi wa Kamati Kuu ni ya nne, lakini inashangaza inafikia kiongozi anamwita Mwenyekiti wa Taifa wa chama ana akili ndogo tena kwa maandishi na kuyaweka kwenye mitandao ya kijamii.

Lissu alijoji je, Zitto kama angekuwa CCM akamwita Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho kwamba ana akili ndogo je, angepona?”

Alisema chama chochote cha siasa kiwe ni CCM, CUF au Chadema kina sheria na katiba zake na kwamba mtu anayefikilia kuwa Zitto alichukuliwa hatua hizo kutokana na labda Dk. Slaa, Lissu na Mbowe  wanachuki naye ni hoja dhaifa na ya uongo.

Alisema mwaka 2007 Zitto alipofukuzwa Bungeni baada ya kuzungumzia suala la mgodi wa Buzwagi  yeye (Lissu) na Dk. Slaa ndiyo waliomtetea na kwenda jimboni kwake kijiji cha Mwandiga na kuwaeleza kuwa alichokisema ni sahihi hivyo alionewa.

Alisema maamuzi yaliyochukuliwa na yanapaswa kupongezwa kwa sababu hata chama tawala kinaogopa kuyafanya.
 
CHANZO: NIPASHE

Zitto afunguka




Kigoma. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewaomba wakazi wa Mkoa wa Kigoma kumuunga mkono katika mapambano yake ndani ya chama hicho.

Akizungumza Mjini Kasulu katika mkutano wa hadhara, Zitto alisema atahakikisha anapigania haki yake ndani ya Chadema kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama hicho ili aweze kurudishiwa nyadhifa zake, hususan nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Bara aliyovuliwa na Kamati Kuu Novemba 21, 2013.

“Najua nakabiliwa na vita kubwa ndani ya Chadema, lakini kwangu mimi (Zitto) hii ni changamoto, naamini nitashinda tu. Lakini lolote litakalotokea ndani ya Chadema hata kama ni kunifukuza, nitarudi kwenu ndugu ili tuamue kwa pamoja nini tufanye, wapi twende kwa pamoja kama tulivyo kwani nguvu ya mamba ipo kwenye maji,” alisema Zitto.

Amesema kwa kipindi kirefu anaonekana kama msaliti ndani ya chama na anatuhumiwa kutoa siri za Chadema kwa CCM na Serikali. “Tuhuma hizi hazina ukweli, nalaumiwa na kubambikiwa mambo kutokana na msimamo wangu ndani na nje ya chama

“Watu wa Kigoma ambao ndiyo tulipokea mageuzi kabla ya wengine, tunaitwa wasaliti ndani ya Chadema, lakini waliokuja baadaye kutoka mikoa mingine hawa ndiyo wanajiona wasafi. Wapo Watu waliingia Chadema baada ya kukosa fursa za kugombea huko walipokuwa awali na sasa wanajifanya ndiyo Chadema damu-damu. Sitoki Chadema ng’o, labda wanifukuze,” alifafanua Zitto. “Mnakumbuka misukosuko iliyomkuta Dr Kabourou (Aman) alipokuwa Kiongozi wa Chadema, pia walimwondoa Kafulila (David) na sasa mimi (Zitto) natafutwa ili niondolewe. Lazima tuungane pamoja kutetea masilahi yetu watu wa Kigoma,” aliongeza Zitto.

source: mwananchi

Brandts kuvuna Sh170 mil


Kocha wa Yanga, Ernie Brandts 



Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Ernie Brandts sasa atavuna Sh170 milioni kutoka kwa uongozi wa timu hiyo baada ya kusitisha mkataba wake jana.
Kutokana na hali hiyo, Yanga italazimika kumlipa mshahara wake wa miezi 10 iliyobakia ambayo ni zaidi ya Sh170 milioni kwa kuwa kocha huyo alikuwa akilipwa mshahara wa Dola 10,000 kwa mwezi.
Uamuzi wa kumtimua kocha Brandts umefikiwa kwenye kikao cha kamati ya utendaji ya Yanga iliyoketi juzi Jumamosi muda mchache baada ya timu hiyo kunyukwa kwa mabao 3-1 na watani zao Simba katika mchezo wa Nani Mtani Jembe.
Akizungumza Makao Makuu ya klabu hiyo iliyopo mtaa wa Twiga na Jangwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Abdallah Bin kleb alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea maoni ya wachezaji mbalimbali wa zamani kuhusu kiwango cha timu.
“Tumempa notisi ya siku 30 ili tuendelee kutafuta kocha mwingine na tupo kwenye mchakato wa kumlipa stahiki zake, tuachane kwa amani.
“Mwanzoni alipandisha kiwango cha timu, kilipanda sana, lakini baadaye kiwango kikaanza kushuka, tukasema tumpe muda kidogo, lakini tunaona mambo yanazidi kuharibika, hivyo tumeamua kuachana naye kwa sababu hana jipya, sisi tunalenga michuano ya kimataifa zaidi sasa kwa kiwango hiki hatutafika mbali ni lazima tuchukue hatua za haraka zaidi,” alisema.
Kuhusu wajumbe wengine wa benchi la Ufundi, Bin Kleb alisema kwamba taratibu nyingine zinafuata na ndani ya wiki hii kuna matukio mengi makubwa ambayo klabu yake itayafanya.
Hata hivyo tayari Brandts alikabidhiwa barua yake ya kusitishiwa mkataba rasmi juzi na jana baada ya mazoezi Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga alikutana na wachezaji na kuzungumza nao kwa zaidi ya nusu saa.
Naye Brandts alipozungumza na gazeti hili kuhusiana na kuvunjiwa mkataba alisema kwa kifupi “Nasubiri notisi ya siku 30 imalizike, kuna kitu nitaongea, lakini sasa hivi msikilizeni Abdallah (Binkleb) anachosema ukifika muda na mimi nitazungumza.”
Yanga imevunja mkataba na kocha huyo ukiwa umepita mwezi mmoja tangu wamwongezee mkataba wa mwaka mmoja wa kuinoa timu hiyo.
Licha ya kufungashiwa virago, kocha, Brandts ameonyesha kukasirishwa na nidhamu mbovu ya mastaa wake.
Kwenye mazoezi yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama, nyota wengi wa klabu hiyo hawakufika mazoezi bila ya kutokuwa na taarifa zao zaidi ya Athuman Idd ‘Chuji’ ambaye amefiwa na bibi yake.
Baadhi ya wachezaji ambao walikacha mazoezi ya kocha huyo ni Ally Mustapha, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza.
“Sielewi, walitakiwa leo wawepo mazoezini, lakini sijawaona, sina taarifa zao labda ni kwa vile maprofesheno, sielewi.
“Profesheno nidhamu ni kitu cha kwanza, lakini hapa profesheno ni tofauti anaamua vile anataka, najua Chuji amefiwa na bibi yake, lakini Okwi na wenzake sielewi chochote labda viongozi wanajua walipo mimi sijui.”
Yanga itaondoka Januari 2 kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi na Januari 14 itakwea pipa kwenda Hispania kwa kambi ya siku 10.

source: Mwananchi

Monday, December 23, 2013

Slaa:Ushabiki kumfukuzisha Zitto

 
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe

Katibu  Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Willibrod Slaa, amesema Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amevuliwa nyadhifa zake ndani ya chama hicho kwa misingi ya maadili na kutahadharisha kwamba ushabiki ukianza kujiingiza katika suala hilo unaweza kusababisha chama kichukue uamuzi wa kumfukuza kabisa.
Alitoa tahadhari hiyo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa mjini Nzega katika Jimbo la Nzega wilayani hapa ikiwa ni mfululizo wa ziara zake ya siku 20 katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Singida.

Dk. Slaa ambaye hata hivyo, hakufafanua ushabiki unaofanywa katika suala  hilo, alisema Zitto alivuliwa nyadhifa za Naibu Katibu Mkuu na Naibu Mkuu wa Kambi ya upinzani Bungeni kwa misingi ya maadili kama katiba ya Chadema inavyoelekeza.

Alisema kuweka ushabiki kwa masuala ya maadili haitamsaidia Zitto bali ni kumharibia zaidi kwa kuwa chama kinaweza kuchukua hatua zaidi dhidi yake kwa kumfukuza kabisa.

Alisema msimamo wa Chadema unajulikana kutoka mwaka 2010 kwamba kabla ya kuiingia Ikulu hatua ya kwanza ni kusafisha ubovu wa maadili katika nchi hii.

“Ubovu wa maadili tusipousafisha ndani ya Chadema hatutausafisha hata tukiingia Ikulu, kama tutashindwa kusimamia maadili ndani ya Chadema basi na Ikulu tusiende sababu hatutastahili kwenda Ikulu,” alisema.

Dk. Slaa alimtaka Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kigoma, Shaban Mambo, kusaidia kumshauri Zitto ili kumsaidia vinginevyo ushabiki ukiingia itakuwa ni kummaliza.
Alisema Kamati Kuu ya Chadema ilimpa siku 14 Zitto na wenzake kujieleza kutokana na tuhuma zinazowakabili ambazo zimekwisha na ameshajibu.
“Naomba nitoe tahadhari msipoangalia mtamfanya afukuzwe kweli, kama mnaomshauri hamuwezi kumshauri vizuri ikifika mahali mimi kama Katibu Mkuu ninapoona mambo yanaendelea ni lazima nitoe ufafanuzi,” alisema.

Alisema amepata taarifa kuwa baadhi ya wenyeviti wa mikoa na wilaya wameanza kupelekewa barua na fomu wazisaini ambazo wanadai zimetoka ofisi ya Katibu Mkuu wakati siyo kweli na kutaka watu wasisaini vitu wasivyovijua.

“Hizo fomu zikishasambazwa wanasema zimetoka makao makuu kwa Katibu Mkuu, msidanyanywe sijatoa fomu, sijaagiza chochote, chochote mnacholetewa kama hicho kataeni kwa sababu katiba ya chama na kanuni inaelekeza taratibu za vikao.
Tukifika mahali baadaye na haya yakiendelee mimi nisilaumiwe, nitalazimika kuyajibu,” alisema.
Kauli hiyo ya Dk. Slaa imekuja siku mbili baada ya Zitto kupokelewa kwa maandamano na wananchi wa jimbo lake juzi akitokea Bungeni mjini Dodoma.

Zitto katika maandamano hayo aliwaeleza wanachama na wakazi wa Kijiji cha Mwandiga kuwa wawe wavumilivu ili aweze kupambana hadi haki ipatikane.
“Wananchi msisikitike kwamba mtoto wenu anaonewa kwa sababu mtoto wenu ni mpambanaji.

Mimi nimevumilia sana mishale ninayorushiwa mimi kama mwanasiasa mdogo kabisa ni mingi mno, kinachoniuma mimi wananchi wangu ni kwamba mishale hii narushiwa na wenzangu wa ndani ya chama, hicho ndicho kinachoniuma, lakini kinachonitia moyo ni nyinyi wanananchi wangu,” alisema.

Alisema kila akifikiria kukata tamaa anawaza watu wa Kigoma. “Nasema watu wa Kigoma watasikitika sana acha nipambane na nitapambana, muhimu ni sharti haki kutendeka na nitahakikisha haki inatendeka.”

Aidha alisema wao walishiriki kujenga chama na wameumia kwa ajili ya chama na watakuwa wa mwisho kutoka.

Zitto alisema ni lazima waende kwa utaratibu ule ule kwa sababu wao wameweka misingi ya hicho chama na kwamba wakikimbia watakuwa wanawachia watu ambao wamekuja badaye kuja kula matunda ya kazi ambayo wameifanya.

Alisema kuvuliwa nyadhifa zake za chama siyo sahihi wala usaliti ni kwa sababu ya kutaka kugombea uenyekiti wa chama hicho Taifa na kutaka matumizi bora ya chama.

Alisema wanachama wa vyama vya siasa wanapojenga uoga kwa viongozi wao ni udikiteta, lakini viongozi wanapojenga uoga kwa wanachama hiyo ndiyo demokrasia.

Novemba 22, mwaka huu Kamati Kuu ya Chadema iliwavua uongozi Zitto, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kwa madai ya kukisaliti chama kwa kuanaa waraka ambao pamoja na mambo mengine ulikuwa unawakashfu viongozi wakuu wa chama hicho.
 
CHANZO: NIPASHE

Ivo amtetea Juma Kaseja, amshangaa

 
Kipa wa Simba ambaye ni mkali wa kupangua mikwaju ya penalti, Ivo Mapunda.
Kipa  wa Simba ambaye ni mkali wa kupangua mikwaju ya penalti, Ivo Mapunda amemtetea kipa wa Yanga, Juma Kaseja kwa kufungwa mabao mawili 'laini' katika mchezo wa 'Nani Mtani Jembe' uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi, lakini akamshangaa kwa kumsusia kumpa mkono.
Kabla ya kuanza kwa mchezo huo uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, Kaseja aligoma kumpa mkono Ivo wakati wachezaji wa timu zote mbili wakisalimiana mbele ya Mgeni Rasmi wa mchezo huo, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe ambaye alikuwa amefuatana na Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamali Malinzi na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe.  

Akizungumza na NIPASHE mara tu baada ya mchezo huo kumalizika huku 'Wanajangwani' wakijawa na nyuso za huzuni, Ivo alisema hakutarajia kufanyiwa hivyo na Kaseja kwa vile hawajawahi kuwa na ugomvi wowote.

"Soka ni sehemu nzuri ya kukutanisha watu, nimekutana na Kaseja uwanjani na nilitegemea atanipokea vizuri kama Mtanzania na mchezaji mwenzake, lakini amenishangaza sana kwa kuninyima mkono," alisema Ivo.

"Sijawahi kutukanana wala kuwa na mgogoro wowote na Kaseja.

Alichokifanya ni picha mbaya kwa wapenzi wa soka, hasa watoto ambao wanatuangalia sisi (wachezaji) kama kioo chao," aliongeza Ivo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa nchini Kenya kwa kudaka mikwaju ya penalti akiwa na mabingwa wa soka wa nchi hiyo, Klabu ya Gor Mahia huku taulo zake mbili ambazo hupenda kuziweka juu ya nyavu baadhi wakizihusisha na imani za kishirikina.

Mapema katika kipindi cha pili cha mchezo wa juzi, refa wa kati aliyechezesha mchezo huo, Ramadhan Ibada kutoka Zanzibar alilazimika kuzishusha nyavu taulo hizo na kuziweka chini kwa kutokana na Ivo kuzianika juu ya nyavu la lango la Kusini la Uwanja wa Taifa.

Simu ya Kaseja, ilikuwa ikiita bila kupokewa alipotafutwa na NIPASHE jana kuzungumzia kitendo chake cha kumnyima mkono Ivo.

Hata hivyo, ikumbukwe kuwa kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Mdenmark Kim Poulsen alilazimika kumtema Kaseja katika kikosi chake kilichoshiriki mashindano ya Kombe la Chalenji nchini Kenya mwaka huu huku akimtumia Ivo kama kipa chaguo la kwanza.

Mara tu baada ya mchezo huo kumalizika na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali alikaririwa na vyombo vya habari akimlalamikia Kaseja kufungwa mabao rahisi huku akiweka wazi kwamba uongozi wa 'Wanajangwani' ulifanya makosa makubwa kumsajili tena kipa huyo.

Lakini Ivo alisema ni jambo la kawaida kipa mzuri kufungwa mabao kama hayo, kikubwa ni kujipanga kusahihisha makosa.

"Sijashangazwa na hali iliyomkuta Kaseja leo (juzi) uwanjani, najua ameumia sana hasa ukizingatia mabao mawili, la kwanza na la tatu yalikuwa mepesi.
Lakini ni jambo la kawaida kipa mzuri kama yeye kufungwa mabao hayo kwa sababu katika uzoefu wangu makipa wazuri kina Buffon na Heart (Joe) wamewahi kufungwa mabao mepesi kama hayo," alisema Ivo.
"Ninachoshauri wapenzi wa soka nchini, hasa mashabiki wa Yanga walichukulie kama jambo la kawaida tu, wasitafute mchawi.
Makipa wazuri wakati mwingine hufungwa mabao rahisi sana," aliongeza Ivo ambaye ametua Simba katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo kilichofungwa Desemba 15, mwaka huu.
Kaseja alionekana akitiririkwa na machozi baada ya kipyenga cha mwisho cha refa Ramadhan Ibada kutoka Zanzibar kupulizwa huku mchezaji 'kiraka' wa Yanga, Mbuyu Twite akimfuata na kumtuliza.

Tayari uongozi wa Yanga umeshamtetea kipa huyo na kusema haukumsajili mlinda mlango huyo wa zamani wa Simba ili  kuwakomoa Simba kwa kuwafunga, bali kuisaidia Yanga katika mashindano ya kimataifa.
 
CHANZO: NIPASHE

HOTUBA YA MH ZITTO Z. KABWE - KIGOMA – 21 DESEMBA 2013







Leo nina furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye changamoto nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si salamu za kawaida bali nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji. Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma! Na popote niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na zao la Ujiji.

Tuna mengi ya kujivunia kama taifa lakini Ujiji na watu wake mna nafasi ya pekee katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru wa nchi yetu mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji mlikuwa wa kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995. Kabla ya hapo mlitoa madiwani wengi mwaka 1994. Wakati Watanzania wengine wakiwa wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa, watu wa Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza maisha yao, wengine kazi zao na wengine hata ndoa zao katika kupata
mbegu ya mabadiliko katika nchi yetu. Nawataka msichoke. Wekeni nguvu mpya katika kusimika mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.

Na nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana. Na haya si maneno tu ambayo ninayazungumza kama mwanasiasa. Hii ni hali halisi na maisha niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule ya Msingi Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari Kigoma. Malezi yangu yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma. Nimekuwa nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na kwenye siasa kwamba nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la tatu. Viatu hivyo viliitwa 'asante Salim' vilivyokuwa vinatengenezwa na Kampuni ya Bora Shoes. Vililinunuliwa na mama Coretha Furugunya ambaye tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa Kisangani Mwanga. Mama Coretha hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa ana uwezo mkubwa, la hasha! Alifurahishwa na matokeo yangu ya mitihani ya darasa la pili kwenda la tatu. Ninaamini kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa uungwana, upendo na hata uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania. Uwajibikaji kwani alichukua jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu, lakini aliona kuwa kama mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto wote. Jamii hii ya watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana kwa bidii kwenye masomo na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili katika maisha yangu na ni somo hili ndilo limenifanya nijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia kwa uadilifu na mafanikio ya hali ya juu sana.

Nikiwa nimejaa matumaini haya kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka niwakumbushe kwa nini kama jamii tulichagua kufuata njia ya demokrasia. Demokrasia ina maana pale ambapo inatumika kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya wananchi. Maisha yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha mwananchi kupata huduma zake stahili kama Elimu, Afya, Maji na miundombinu. Demokrasia haina maana pale wananchi wanakufa njaa kwa kukosa ajira na kukuza umasikini. Demokrasia inahusu maendeleo. Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa mkoa wa Kigoma kutoka mikoa isiyo na miundombinu kabisa ya maendeleo mpaka kuwa mkoa unaotumika kama mfano kwa miradi mingi ya Maendeleo ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa ndege wa Gombe-Mahale, barabara za lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa bandari ndogo mpya na ujenzi wa kituo cha Usafirishaji Mwandiga. Asije mtu akasema yeye ndio kafanya haya. Haya ni matunda ya nyinyi watu wa Kigoma kupokea demokrasia na bila woga kuchagua viongozi wenu bila kujali vyama bali kwa kuangalia uwezo. Haya ni matunda ya viongozi wenu kupaza sauti yenu kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya ni matunda ya uvumilivu wenu na uamuzi wenu wa kutaka maendeleo. Juhudi hizi lazima ziendelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa Kigoma katika uchumi wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa makuu.

Lakini tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni Uwajibikaji. Katika kipindi cha utumishi wangu kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka kwenu,nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa Wananchi. Nakumbuka wakati napambana kuhusu sheria mbovu ya madini kuna watu hapa nyumbani walisema 'sasa huyu kawa mbunge wa Taifa' lakini watu wengi zaidi wakasema tumemtuma Dodoma kusemea Watanzania wote na sio Kigoma tu. Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye sera ya Madini na sheria ya madini ambapo baadhi ya mambo ambayo yalikuwa hayafikiriki sasa yametungiwa sheria ikiwemo Serikali kuwa na hisa kwenye migodi, Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini ya asilimia 50 na kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya thamani. Uwajibikaji ulipelekea kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri kwa kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana. Hii ilitokana sio tu na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia ushiriki mkubwa wa wananchi kupitia simu na mitandao ya kijamii ambapo wabunge walishinikizwa kuweka saini kwenye karatasi za kumtoa Waziri Mkuu. Toka wakati huo kumekuwa na utaratibu sasa ambapo wabunge hawaoni taabu kutaka uwajibikaji waziwazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za Umma. Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na kufukuzwa kazi kutokana na kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na ripoti ya kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika kuimarisha demokrasia yetu.

Pamoja na matunda haya mengi mazuri lakini bado kuna changamoto katika juhudi zetu.

Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.

Kutoaminiana. Ni dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa kwa kiasi kikubwa. Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania kumi, wanane hawaaminiani. Ni changamoto kubwa sana. Wananchi wameacha kutuamini wanasiasa na wanasiasa wameacha kuaminiana wenyewe kwa wenyewe. Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa ukweli na ukweli umekuwa ni uongo. Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa maarufu inabidi ujue kudanganya na ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema kweli. Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa ni kansa katika siasa zetu. Itachukua muda mrefu sana kujenga demokrasia imara katika nchi yetu kama hatutapata jibu la changamoto hii ya kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa ukweli umekuwa unatengenezwa badala ya kutafutwa. Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na kamati maalum iliyoundwa na Bunge kufuatilia mabilioni ya uswisi na kwamba chini ya kiapo nilisema sina majina ya watu wenye akaunti huko Uswisi. Huu ulikuwa ni uongo. Ni uongo kwa sababu niliitika wito wa kamati hata nilipokuwa katika mafunzo ya mgambo huko Tanga na nilikutana nao mara nne. Ni uongo kwa sababu niliwapa wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na taarifa nyingi sana kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na umiliki wa mali nje ya nchi kinyumecha sheria. Ni uongo kwa sababu mimi kutotaja majina haya haina maana sina majina, bali ni kwamba ninaheshimu utaratibu na nimeachia vyombo husika vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi kama mtu binafsi nikianza kuchukua majukumu ya taasisi ninaweza kutia dosari harakati hizi muhimu na hata kupelekea mchakato mzima kuvurugika. Sitaingia mtego huu! Lakini hatua hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa mfano uongo kama huu ulifanywa kwa malengo gani? Na ninajikuta hata mimi ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya KUTOAMINIANA. 

Lakini mtambue pia kuwa kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa kuwa na mawazo tofauti katika vyama vya siasa au hata asasi za kijamii ni uhaini. Lakini bila kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi kujenga vyama imara wala Taifa imara. Demokrasia imara ni zao la tofauti za mawazo na uhuru wa mawazo. Kama hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa mawazo na tofauti za mawazo, tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa na waliojaa woga. Wanachama wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini uongozi unapoogopa wanachama ni demokrasia. Bila demokrasia ya uwazi na kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta. Lazima vyama vya siasa, viongozwe kwa namna ile ile ambayo Taifa litaongozwa.

Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli.
Juzi nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa yanayoendelea ndani ya chama chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu. Wabunge wengine walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni vicheko na mazungumzo. Hii ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule. Mmenifunza kutojenga chuki na watu na badala yake kuchukua kila tukio kama changamoto ya maisha. Siasa ni kupambanisha mawazo tofauti na hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na siasa ina misingi yake ambayo sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi. Msingi wa siasa ni kuwa inapaswa kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio malumbano tu ya kurushiana maneno na kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa kisiasa. Siasa si kuwekeana chuki na kuonyeshana ubabe.

Na hapo ni muhimu muelewa wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi ninatafuta umaarufu, ni uongo! Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu, ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote hivi ni ninyi. Ninasukuwa kila ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu;kila ninapoona akina mama wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila ninapoona vijana ambao hawana uhakika wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa kazi; ninapoona wazee wa Kigoma kukosa hata shilingi mia moja kununua chai asubuhi. Ninawaona si wanaKigoma bali mamilioni ya watanzania wakiishi katika hali hii. Alafu nalinganisha na taarifa tunazozipata kuhusu ufujaji na utoroshwaji wa pesa zetu. Hebu sasa linganisheni na ukweli kuwa ripoti ya kimataifa iliyotolewa hivi karibuni imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee, jumla ya dola za kimarekani milioni 1315 (bilioni 1.3), yaani shilingi trilioni  2,113,930,000,000 (sh trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania. Mwaka 2011 kiasi cha dola za kimarekani milioni 817 yani shilingi za kitanzania zipatazo trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni 1.3) zilitoroshwa. Ripoti hiyo inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania zilizotoroshwa nje ya nchi katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za kimarekani milioni 4526 (bilioni 4.5) sawa na shilingi za kitanzania trilioni 7,286,860,000,000 (trilioni 7.3).  Nimewatajia hapa namba chungu nzima na matrilioni na mabilioni hayaleti maana. Lakini hii ina maana kwamba kiasi cha pesa zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa - robo yake tuingeweza kujenga barabara ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka Kigoma mpaka Dar-es-salaam! Pesa hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi wengine ili kuhakikisha tunapata huduma bora na kutengeneza ajira bora kwa vijana wetu. Pesa hizi zingeweza kununua madawa muhimu na kuokoa maisha ya maelfu ya akina mama tunaowapoteza kila mwaka wakati wa uzazi. Pesa hizi zingeweza kuwanunulia watanzania wote si watoto tu angalau pea 10 ya viatu. Sasa nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi mnono na kufumbia macho utoroshwaji wa fedha au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa njia ya sisi wabunge kujilipia posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu kukaa kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi au msaliti!

Lakini naomba niwasihi kuwa katika nyakati kama hizi za changamoto za kisiasa jambo la msingi kuliko yote ni kutulia maana hakuna linalotokea bila sababu. Licha ya kwamba kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika mambo haya lakini pia kuna wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana mawazo yao, ndani na nje ya chama chetu;ndani na nje ya Serikali na ndani nanje ya nchi yetu. Ndio maana lazima kuibadili nchi yetu ili kuweza kuhakikisha kila raia anakuwa na fursa ya kutoa mawazo na fikra zake zinakuwa huru.

Maisha ni mabadiliko; mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki kwa sababu bila mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna maendeleo. Mabadiliko ni kiu kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko huleta matumaini. Na kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi hiki kipya. Siasa za kizazi kipya cha viongozi ni siasa za majawabu ya kero za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa za kujenga na kuimarisha; ni siasa za kuaminiana na kuheshimiana hata pale mnapopingana kimawazo. Ninataka tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za mabadiliko; siasa zinazojenga matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.