Dar es Salaam. Rais Jakaya
Kikwete anatua nchini leo akiwa na lake moyoni kuhusu hatima ya baraza
lake la mawaziri, baada ya kutengua uteuzi wa mawaziri wake wanne, wiki
mbili zilizopita.
Rais Kikwete alikwenda Marekani, Desemba 18, mwaka
huu kufanyiwa uchunguzi wa afya yake na akiwa huko, upepo wa kisiasa
ulibadilika na kumlazimisha kuchukua hatua hiyo ambayo inampa wajibu wa
kupanga upya safu yake ya uongozi.
Mawaziri ambao uongozi wao ulitenguliwa ni wa
Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,
Shamsi Vuai Nahodha, Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na
Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo David Mathayo.
Kung’oka kwao kunatokana na ripoti ya kamati ndogo
ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu athari
zilizotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo
ilizua mjadala mkali kiasi cha wabunge kumshinikiza Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda kwamba naye aachie ngazi.
Hivyo kitendawili kingine kikubwa kinachomkabili
Rais Kikwete ni iwapo ataamua kuendelea kufanya kazi na Pinda ambaye
alishambuliwa na wabunge kwamba naye ang’oke kwa madai kwamba ameshindwa
kusimamia utendaji serikalini.
Kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Ibara ya 52(1)
Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka juu ya kudhibiti usimamiaji na
utekelezaji wa siku wa kazi na shughuli za Serikali.
Katiba inasema: “Katika utekelezaji wa madaraka
yake, Waziri Mkuu atatekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote
au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe. Ibara ya 53
(1) inaeleza: “Bila kuathiri masharti ya Katiba hii, Waziri Mkuu
atawajibika kwa Rais kuhusu utekelezaji wa madaraka yake.”
Hata hivyo, ni kama Rais Kikwete alishaamua
kumwokoa Pinda pale alipompa maagizo kwamba alitangazie Bunge uamuzi
wake wa kutengua uteuzi wa mawaziri wanne.
Ripoti hiyo iliyosomwa na Mwenyekiti wake, James
Lembeli ilifichua kuwapo kwa vifo na mateso ya wananchi vilivyofanywa
wakati wa operesheni hiyo iliyoendeshwa na askari wa Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ), maofisa wa Usalama wa Taifa na Polisi.
Mbali ya pengo lililoachwa na mawaziri hao wanne,
Rais Kikwete pia ndiye mwenye majawabu kuhusu hatima ya wale waliotajwa
kuwa ni mawaziri mizigo kwa kushindwa katika utendaji wao, hasa
ikizingatiwa kuwa shinikizo la kuwajibishwa kwao linatoka ndani ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye ni mwenyekiti wake.
Kitendawili cha Pinda
Zipo hoja kadhaa, iwapo Rais Kikwete atamwondoa
Pinda kama ambavyo wabunge walisisitiza wakati wakichangia ripoti hiyo,
huku wakirejea yaliyowahi kutokea serikalini lakini Waziri Mkuu huyo
akakwepa kuwajibika.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba isingekuwa rahisi kwa Pinda kuachia
ngazi wakati Rais akiwa nje ya nchi kutokana na ukweli kuwa ingekuwa na
maana kuwa Baraza la Mawaziri lingetakiwa kuondoka.
Akizungumza juzi, Jaji Mstaafu, Thomas Mihayo
alisema kitendo cha Waziri Mkuu kujiuzulu kitamweka Rais katika wakati
mgumu kwa sababu Serikali itavunjwa na kuundwa upya.
“Kuunda upya Baraza la Mawaziri ni gharama, tena
ikizingatiwa kuwa tunaelekea katika Bunge la Katiba, Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 2015, mabadiliko
yakifanyika nadhani nchi itayumba,” alisema Jaji Mihayo.
Jaji huyo alisema haoni sababu za Pinda kung’olewa
wakati imebaki miaka miwili tu ufanyike uchaguzi mkuu mwingine, na
kufafanua kuwa hata kama akija Waziri Mkuu mpya hataweza kufanya mapya
kutokana na muda uliobaki.
“Sidhani kama ni busara kushinikiza ang’oke ni
wazi kuwa madhara yatakuwa makubwa kuliko mema, lakini ngoja tusubiri
tuone uamuzi utakuwaje,” alisema Jaji Mihayo.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria
cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema hatua hiyo haitatatua tatizo
la mfumo mbovu uliopo zaidi ya kuongeza gharama za kuwatunza mawaziri
wakuu wastaafu.
“Ukichunguza kwa makini, Waziri Mkuu Pinda hana
tatizo, bali ni mfumo mbovu ambao kimsingi unatakiwa urekebishwe na Rais
Kikwete,” alisema na kuongeza:
“Ukimtoa Pinda leo, sanasana unaongeza tu gharama
za kutunza mawaziri wakuu wastaafu. Tangu Rais Kikwete anaingia
madarakani alishaujua mfumo alioukuta, kwa nini asingeurekebisha ili
haya yasitokee?
“Rais anapaswa kupunguza safari za nje na ajikite
kushughulikia matatizo kama haya kwa kurekebisha mfumo wa nchi ili
usiingize nchi kwenye matatizo.”
Kwa upande mwingine kumekuwa na harakati za
kukusanya saini za wabunge ili kuendesha mchakato wa kumng’oa Pinda
iwapo Rais hatachukua hatua.
Mawaziri mizigo
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu
wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye ndiyo walikuwa watu wa mwanzo kutoa
orodha ya mawaziri mizigo wakati walipokuwa katika ziara kwenye mikoa ya
kusini.
Waliwataja Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Dk Mathayo,
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake,
Adam Malima.
Viongozi hao walitaka mawaziri hao wajieleze mbele ya Kamati Kuu (CC), ya chama hicho juu ya kushindwa kwao kwenye utendaji wao.
Hata hivyo, orodha hiyo iliongezeka baada ya Bunge
kumtaja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Hawa Ghasia pamoja na
Manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kupima na kutafakari
kama wanatosha kusimamia wizara hiyo kutokana na ripoti ya Mkaguzi na
Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kufichua ufisadi katika wizara
hiyo.
Kamati Kuu ya CCM iliyokutana Desemba 14, mwaka
huu chini ya Rais Kikwete na iliwahoji Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Ghasia na Naibu Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya Salum na baadaye taarifa ya chama hicho ilisema imeliacha suala
hilo mikononi mwa Rais kwa hatua zaidi.
source: Mwananchi