Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema, Zitto Kabwe amejiweka katika mazingira magumu zaidi kisiasa
ndani ya chama hicho, kutokana na shaka kubwa iliyougubika mkutano wake
na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam juzi.
Zitto pamoja na viongozi wengine
wawili wa Chadema; Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba walivuliwa
nyadhifa zao na Kamati Kuu ya Chadema baada ya kubainika kupanga mbinu
za uasi, kupitia waraka ambao ulikuwa ukieleza mkakati wa kufanya
mabadiliko makubwa ya kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani.(P.T)
Leo, uongozi wa Chadema umeitisha
mkutano wa waandishi wa habari ambao pamoja na mambo mengine, utajibu
baadhi ya hoja za utetezi ambazo zilitolewa na Zitto pamoja na Dk
Kitila. Katika mkutano wa juzi, Zitto na Dk Kitila ambaye alikuwa Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema, walizungumzia kuvuliwa kwao madaraka, lakini
maandalizi na uendeshaji wa mkutano huo yanazua shaka kutokana
kuwahusisha watu wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa Jumuiya ya Vijana ya
Chama cha Mapinduzi (UVCCM).
Miongoni mwao, wamo waliowahi kuwa
wanachama wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Habib Mchange na
Mtela Mwampamba ambao walitimuliwa kwa makosa yanayofanana na yale
yalizosababisha Zitto na wenzake kuvuliwa nyadhifa zao.
Mchange na Mwampamba pamoja na
aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza, walivuliwa
uanachama wa Baraza hilo Januari 5, mwaka huu baada ya kupatikana na
hatia ya kutumia mitandao ya kijamii kukihujumu Chadema na kuwatukana
viongozi wake wakuu. Baadaye walihamia CCM wanakoendeleza harakati zao
za kisiasa.
Jana, Machange alipotafutwa, alisema:
"Mimi sikuwahi kuondoka Chadema, nilifukuzwa kihuni kama walivyowafanyia
Zitto na Kitila. Nimepeleka malalamiko yangu tangu Januari hadi leo
sijajibiwa, hivyo siwezi kusema nimeondoka.
Nataka nimuunge mkono mwathirika mwenzangu kama ilivyokuwa mimi lakini nitabakia kuwa mwanachama mwaminifu.
"Mimi ni mwanaChadema na sikuwahi
kujiunga na CCM au chama chochote, walioondoka ni Mwampamba na Shonza."
Mwampamba alisema: "Nilijitokeza pale kuonyesha mshikamano kwa sababu
mimi pia ni mwathirika. Kwa hiyo nilitaka ulimwengu ufahamu kuwa mimi ni
kati ya wanaopinga siasa za aina hii... Chadema ni chama kinachojiandaa
kuchukua dola, sasa kama kila mwenye mawazo tofauti anaonekana mhaini
itakuwaje siku wakichukua dola? Ubaguzi huu haujalishi uko chama gani,
hata kama niko CCM, hilo halinizuii kuungana na mtu aliyepatwa na tatizo
kama langu."
Kuwepo kwao katika mkutano wa Zitto
kunaweza kutumiwa na uongozi wa Chadema kuwa uthibitisho wa kiongozi
huyo kushiriki katika uasi na kunaweza kupuunguzia nguvu utetezi
unaotolewa na Dk Kitila kwamba hakuwa sehemu mpango wa kuuondoa uongozi
wa sasa madarakani. Zitto, Dk Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba wanasubiri kukabidhiwa barua za kuvuliwa
kwao madaraka na katika siku 14 wanapaswa wawe wamewasilisha utetezi
wao wakieleza kwa nini wasifukuzwe uanachama kutokana na tuhuma
zinazowakabili.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod
Slaa alisema jana kuwa ilikuwa lazima viongozi hao wavuliwe madaraka
hasa baada ya Dk Kitila kukiri kuhusika na waraka ambao anasema ulilenga
kushinda kupitia uchaguzi halali ndani ya chama hicho.
"Hata katika ya nchi ukihusika
kutengeneza mbinu za siri lazima ushughulikiwe.Hakuna Katiba
itakayokuruhusu kufanya mipango ya siri. Kwanza uchaguzi wa Chadema nani
katangaza mpaka mipango ianzwe kutengenezwa sasa hivi?" alihoji Dk
Slaa.Alikiri kwamba watuhumiwa hao hawajapewa barua za uamuzi wa Kamati
Kuu na alipoulizwa sababu, alisema Katiba ya chama hicho haitoi mwisho
wa mtu kupewa barua, huku akihoji: "Wao nani kawaambia waende kwa
waandishi wa habari?"
"Mimi ndiye Katibu Mkuu. Katiba
inasema ni lini barua iandikwe? Utatokaje kwenye kikao alfajiri na
wakati huohuo uandae barua za kuwapa?" alihoji Dk Slaa.
Mkutano leo
Mkutano wa waandishi wa habari
ulioitishwa leo unatarajiwa kujibu baadhi ya hoja za utetezi za viongozi
hao zilizotolewa juzi. Zitto alifichua kile alichokiita tuhuma
zilizotolewa dhidi yake mbele ya Kamati Kuu akimaanisha kwamba tuhuma
zilizotamkwa kwenye vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe hazikuwa kamilifu.
Habari zinasema uongozi wa Chadema
utaweka wazi kile kinachodaiwa kuwa ni "Zitto kujitungia tuhuma, kisha
kuzipatia majibu", badala ya kujibu hoja ambazo zilitolewa na Kamati
Kuu.
Jana, Dk Slaa akizungumzia suala hilo
alisema Kamati Kuu haiwezi kuchaguliwa tuhuma za kusema na za kuacha...
"Hiyo hoja walete kwenye vikao, nani anayeipangia Kamati Kuu ichukue
hatua gani pale inapotaka kufanya hivyo?"
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini
Makene akizungumza jana alisema: "Kamati Kuu ilijadili mambo mengi na
hayo ndiyo tunataka umma ufahamu msimamo wetu kama chama."
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili
zinasema katika mkutano huo, huenda uongozi wa Chadema ukaweka wazi
"makosa mengine" ambayo Zitto anadaiwa kuwa amewahi kuyafanya na kuonywa
katika vikao vya ndani ikiwa ni pamoja na kiongozi huyo kutofika makao
makuu ya chama hicho kwa zaidi ya miezi sita. "Kuna makosa mengi (Zitto)
ameyafanya yenye sura ya kukiumiza chama chetu na alionywa mara nyingi
tu, tena na vikao vya juu vya chama kuhusu mwenendo wake, lakini
aliendelea na uasi.Sasa Kamati Kuu imechoka," alisema mmoja wa maofisa
wa Chadema Makao Makuu.
Habari zaidi zinasema katika mkutano
wake wa leo, chama hicho kitatoa ufafanuzi kuhusu mikutano yote ya
kichama ambayo imekuwa ikifanywa na Zitto, huku kukiwa na hoja kwamba
alikuwa akifanya hivyo bila kuwashirikisha maofisa wa makao makuu wala
sekretarieti ambayo kimsingi ndiyo inapaswa kuiandaa.
Wasomi wanena
Akizungumzia mgogoro huo, mtaalamu wa
mambo ya siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard
Mbunda alisema hali inayoendelea ndani ya Chadema ni matokeo ya vyama
vya siasa kutofanya kazi kama taasisi.
"Misingi ya vyama haiweki wazi misingi
ya watu kuwa viongozi. Kwa mfano, kesho nikitaka kujiunga na Chadema
nitaweza kuwa Mwenyekiti? Misingi ya wazi hakuna," alisema
Mbunda.Alisema hali ilivyo ndani ya Chadema kwa sasa ni furaha ndani ya
CCM, kwani watu wanaona kuwa chama kilichoonekana kuwa mbadala hakiwezi
hata kushughulikia mambo yake ya ndani.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya
Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema vyama
vya siasa ni watu au kikundi cha watu wenye malengo na mitazamo tofauti.
"Ukisoma huo waraka utaona kuwa
unazungumzia uongozi, upungufu uliopo kwenye uongozi na namna ya
kubadili uongozi, mimi binafsi niseme ieleweke kwamba hata kwenye
jumuiya yoyote mambo haya yapo hasa kwa kuwa walikuwa wanaelekea kwenye
uchaguzi," alisema. Alisema haoni kwa nini Zitto na Dk Kitila waonekane
wahaini kwa kupanga mikakati yao ambayo walitaka kuitekeleza kupitia
uchaguzi.
"Mabadiliko ni jambo la kawaida, hali
hii ya kuwaondoa kwenye nyadhifa zao inawezekana ikawagharimu Chadema na
inaweza kuwagharimu zaidi wakiwafukuza uanachama," alisema Makulilo.
source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment