WATAALAMU wa hesabu wana usemi wao
wanaoupenda 'Namba haziongopi'. Ukirudisha usemi huo kwenye tathimini ya
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lugha nyepesi unayoweza
kusema ni kwamba 'hakuna kama Yanga'.
Sahau kwamba imemaliza ikiwa kileleni
na pointi zake 27. Takwimu za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL),
zimethibitisha kwamba Yanga imeongoza takwimu zote kuanzia mapato mpaka
idadi ya mashabiki walioingia uwanjani.
Takwimu zilitolewa na Ofisa Mtendaji
Mkuu wa TPL, Silas Mwakibinga, ni kuwa Yanga imekusanya kiasi cha
Sh334.2 milioni katika mechi 13 za mzunguko huo. Katika takwimu hizo,
Simba SC ni ya pili kwa kupata Sh304 milioni huku timu iliyopanda daraja
msimu huu, Mbeya City, ikiipiku Azam FC kwa kushika nafasi ya tatu kwa
kujikusanyia Sh83.8 milioni. Azam imekusanya Sh67.1 milioni.(P.T)
Nyingine na fedha zilizokusanya katika
mabano ni Coastal Union (Sh65. 7 milioni), Mtibwa Sugar (Sh49.9
milioni), Ruvu Shooting (Sh46.1 milioni), Tanzania Prisons
(Sh38.1milioni), JKT Ruvu (Sh36.1 milioni), Ashanti United (Sh35.7
milioni), Rhino Rangers (Sh31.1milioni), Mgambo JKT (Sh25.8 milioni),
Oljoro JKT (Sh20.8 milioni) na Kagera Sugar (Sh18.5 milioni).
"Huu ni mwanzo tu wa kusimamia ligi na
mpaka sasa hatujafikia lengo letu, tunataka kuona kila timu inakuwa na
uwiano sawa wa makusanyo na kama kuzidiana, basi iwe kiasi kidogo,
tumefurahishwa na mwenendo wa Mbeya City ambao wamefanya mambo makubwa
japo wapo katika msimu wa kwanza," alisema Mwakibinga.
Kwa upande wa mashabiki walioingia
viwanjani, Yanga pia imekuwa kinara kwa kuingiza mashabiki wengi katika
mechi. Jumla ya mashabiki 107,890 wa timu hiyo wameingia katika mechi na
kufuatiwa na Simba ambao wameingiza mashabiki 97,364 mpaka mwisho wa
mzunguko huo.
Timu ya Mbeya City imezidi
kung'ang'ania nafasi ya tatu na kuendelea kuitambia Azam FC kwa kuingiza
mashabiki 43,439 tofauti na Azam ambao mpaka sasa wameingiza mashabiki
30,236.
Nyingine ni Coastal Union (mashabiki
27,880), Mtibwa Sugar (20,794), Rhino Rangers (20,263), Prisons
(19,923), Ruvu Shooting (19,000), JKT Ruvu (16,095), Ashanti United
(16,093), Mgambo (11,726) na JKT Oljoro (10,430).
Kwa mujibu wa Mwakibinga, jumla ya Sh
2.4 bilioni zimekusanywa katika mzunguko huo wa kwanza. Kiasi hicho ni
ongezeko la Sh599. 5 milioni katika mzunguko wa kwanza wa msimu
uliopita.
"Hii ni historia na hasa ukizingatia
kuwa baadhi ya mechi zimekuwa zikionyeshwa 'laivu' katika televisheni na
baadhi ya mashabiki kuangalia kupitia luninga zao, lakini bado tumezidi
kupata makusanyo makubwa," aliongeza Mwakibinga.
"Haya ni matokeo mazuri ya kuzinadi
mechi za ligi na mfano mzuri mechi ya Yanga na Mbeya City ambayo iliweka
historia kwa kuingiza Sh100 milioni na huku tiketi zikiwa zimemalizika
kufikia saa 5:00 asubuhi ya siku ya mchezo."
Kwa upande wa viwanja, Uwanja wa Taifa
unaongoza kwa kukusanya fedha nyingi mpaka sasa ambapo kiasi cha Sh1.8
bilioni kimepatikana hapo, kiwango hicho ni sawa na asilimia 75 ya
mapato yote ya mzunguko wa kwanza.
Uwanja wa Sokoine wa Mbeya umeshika
nafasi ya pili kwa kukusanya Sh260.5 milioni na kufuatiwa na Mkwakwani
wa Tanga Sh105.264 milioni.
Viwanja vingine na mapato yake ni Ali
Hassan Mwinyi wa Tabora (Sh100.2 milioni), Sheikh Amri Abeid wa Arusha
(Sh57.4 milioni), Azam Complex wa Dar es Salaam (Sh32.1 milioni),
Kaitaba wa Bukoba (Sh26.1 milioni), Manungu wa Turiani, Morogoro (Sh9.4
milioni) na Mabatini wa Mlandizi, Pwani (Sh3.584 milioni).
Chanzo:Mwanasport mtandaoni
No comments:
Post a Comment