Je, hali yetu Tanzania itakuwaje- miaka kumi ijayo? Sharti tujifunze sana mambo yanayotokea Kongo leo. Toka alipouawa Waziri Mkuu mteule wa kwanza, Patrice Lumumba mwaka 1961, Kongo imegeuzwa makamasi na matope. Sasa hivi askari wanafanya dhambi tupu. Kuwalazimisha kina baba kulala na binti zao, wakikataa wakatolewa macho na kukatwa katwa masikio kisha wakauawa mbele ya familia zao? Askari wanaowabaka kina mama wazee na watoto wadogo wa miaka mitatu kisha wakachomeka mtutu wa bunduki ndani ya uke na kufyatua risasi!
Askari mmoja mstaafu aliyehojiwa runinga ya SKY,
Jumapili iliyopita, alieleza upo ubakaji aina mbili –wa “kunajisi kwa
ashki” iliyotokana na miezi mingi msituni (bila wanawake) na wa kufuata
amri ya maofisa viongozi ilikuharibu motisha wa wananchi wa kawaida.
Jamii ya Kongo inaendelea kuangamia kama ilivyo Mexico.
Kuna video imesambazwa mtandaoni karibuni
ikiwaonyesha wanawake wanne wa Kimeksikana: mmoja kigoli, mwingine
nyanya, wa tatu na wa nne wanawake wa makamo. Wamefungwa mikono,
wakavuliwa sidiria, wakapigishwa magoti na baada ya kusema majina na
shughuli zao kwa woga, wakatukanwa, wakasukumwa kifudifudi kisha
wakakatwakatwa, shingo, mikono kwa shoka na panga wangali hai.
Hii ni mifano ya jamii zilizovurugwavurugwa- kwa
utajiri wa madini, ukorofi wa viongozi wanaoshirikiana na makampuni ya
Magharibi (Kongo) na ushetani wa dawa za kulevya (Mexico) ambapo hata
polisi na wanausalama ‘wanaogopa’ kufanya kazi.
Zamani sana mawe, mikuki, visu na mashoka
vilitumika kuua. Huo utamaduni umeibuka tena dunia ya sasa. Ukatili
umefika saa sita mchana.
Tumemwona kiongozi wa Kitanzania akivamiwa kwake
na kukatwakatwa kwa mapanga. Hadi safu hii ikiandikwa, Dokta Sengondo
Mvungi - mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba Mpya na kiongozi wa
NCCR-Mageuzi alikuwa mahututi hospitali na juhudi za kumpeleka je ya
nchi kwa matibabu zaidi zilikuwa zikiendelea. Tumtakie kila la kheri
apone haraka...
Kabla ya kujitoma katika siasa, Sengondo Mvungi
alikuwa mwanahabari. Tulianza kazi pamoja magazeti ya chama enzi hizo
(TANU) -Uhuru na Mzalendo- mwaka 1976.
Mvungi alikua mchapa kazi.
Lakini takriban kila mtu pale alikua mchapakazi.
Sema Mvungi alikua na ngozi na mabaka tofauti. Tuchukue mfano wa namna
alivyoianza siku yake. Miye nilikua naishi Mwananyamala; yeye, Mwenge.
Ni mbali sana na Barabara ya Nyerere ambayo miaka hiyo iliitwa Pugu.
Ukingoni mwa barabara hii zilisimama ofisi za magazeti ya Chama na pia
Redio Tanzania (RTD).
Ilikubidi upande mabasi kadhaa (yaliyoitwa UDA)
hadi ofisini saa mbili na nusu asubuhi. Daladala hazikuwepo mwaka 1976,
na UDA ilishindwa hata na konokono kimwendo na kiufanisi.
Ingawa baada ya muda tulipewa mikopo ya
pikipiki(iliyokatwa mishaharani), wakati tunaanza kazi(tuliyoichangamkia
kwa hamasa za ujana) ilibidi kuwahi. Mwenzetu Sengondo Mvungi alidamka
saa kumi na moja za asubuhi akavaa nguo za mchakamchaka (bukta na
fulana), mkoba mgongoni, akakimbia toka Mwenge hadi ofisi za Uhuru.
Mwaka 1976 hakukua na barabara ya mkato ya Sam Nujoma au Nelson
Mandela kutokea njia ya Nyerere. Ama kupitia Kawawa na Mpiji sijui.
Ilibidi akimbie hadi Magomeni, ashukie Kigogo hadi Ilala na hatimaye
Pugu.
Hiyo ni alfajiri ya hatari za vibaka na mbwakoko.
Lakini Mvungi kajaaliwa azma na ari. Akishafika ofisi za Uhuru atakoga
kisha abadili nguo, afungue msosi alioubeba na kujisetiri.
Sikumbuki kama alikoga kwa maji ya ndoo au kama
tulikua na mabafu; ila saa mbili na nusu ambazo wafanyakazi wenzake
tuliingia mgodini, yeye tayari mezani kwake akisubiri wanahabari
wenzake, tuingie. Kati yao – wote marehemu- Abdi Mushi (mtangazaji
mashuhuri wa redio), Omar Bawazir (michezo), Costa Kumalija (mhariri
mkuu), Yahya Buzaragi, John Rutayisingwa, Hannah Kasambala, John Mkamwa,
nk.
Wengine walio hai ni akina Salva Rweyemamu (Ikulu), Dk Harrisson Mwakyembe (Waziri), Ndimara Tegambwage, nk.
Hapo sasa utafuata mkutano wa wanahabari kupanga
kazi za siku. Utamsikia Mvungi (kama wenzake) akichangia mawazo.
Hachelei kusema, haachi kucheka panapostahili. Kifupi si mwongo; si
mnafiki. Jioni wanahabari tukielekea mabaa hakuwepo. Sikuwahi kumwona
Mvungi ulevini.
Ndiyo kati ya mambo aliyoendelea nayo miaka
iliyofuata. Nilijiuzulu 1978 nikazama ndani ya muziki na magazeti
mengine; Mvungi akaelekea masomo ya juu hadi alikofikia na huo udokta wa
sheria.
Alipenda kusoma ndiyo
Tulisoma wote, awali, Sekondari ya Mzumbe.
Kule alikua kiranja mkuu wa shule.
Alishangaza kwa kutokuchoka.
Kila mara anaongelea matatizo ya wanafunzi,
anakutana nao, anasikiliza, anatatua na kutanzua. Kuna wakati
nilimuuliza: “Hivi wewe unalala saa ngapi?”
Maana alijituma sana; hakua na uvivu na kero za
vijana wa mijini, ana hulka na tabia za shamba, za wana jembe vijijini.
Kama hachezi mchezo fulani (alihusudu riadha), atasoma kitabu au
kusikiliza redio. Kawaida vijana Mzumbe tulipenda sana kufanya masihara
na kutembelea shule za akina dada, hususan, Kilakala. Mazungumzo
yatakuwa utani utani wa kirijali na mavazi. Ukiwa naye Mvungi ataongea
hayo lakini utajua masikio na hisia zake zilikua kwingine. Tulimstahi na
kumheshimu, tukinong’onezana, iko siku atakuja kuwa mtu wa mfano.
Takriban miaka 40 imepita toka enzi hizo.
Sasa hivi Sengondo Mvungi yu mahututi.
Tungependa kusikia kapona; ari yake ya kuishi
kali. Swali muhimu la kujiuliza ni je, kiongozi wa hadhi yake alikosaje
ulinzi imara?
Mwaka juzi, Dk Mvungi alifurahisha sana alipotoa
kauli ya kupinga kuweka hoja ya ‘mapenzi na ndoa za jinsia moja’ katika
Katiba Mpya.
Akasema kuipachika kauli hiyo ndani ya utamaduni
wetu ni mchango wa udunishaji wa akili za watu. Msimamo thabiti
ukizingatia Wazungu wameisimanga Afrika kufuata ‘itikadi hii’ la sivyo
kunyimwa misaada. Kauli dhahiri ya ukoloni mambo leo!
Nchi yetu inasifika dunia nzima kwa uadilifu na
amani. Miaka 100 sasa hatujawa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mara ya
mwisho kupigana ilikua Maji -Maji dhidi ya Mjerumani 1905- 1907. Vita
nje vimekua kuchangia tu ukombozi barani (Uganda, 1979 nk).
Kilichotufanya tuwe vile, ni kujaaliwa viongozi
wasiochinjachinja na kuonea wananchi; ingawa hapa na pale machache
yametokea. Tofauti za umaskini na utajiri zinakua haraka na wezi na
majambazi wanatumia ukatili wa giza kufikia malengo. Tuombe Mungu
yasigeuke kinyaa cha Kongo, Mexico na Somalia.
-Bpepe: kilimanjaro1967@hotmail.com
-Tovuti: www.freddymacha.com
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment