Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi alizikwa jana kijijini kwake, Chanjale,
Kisangara Juu katika mazishi ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wajumbe wa tume
hiyo, vyama vya siasa na wananchi.
Akizungumza katika mazishi hayo,
Askofu Rogath Kimario wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Same alisema tukio
la kushambuliwa lililosababisha kifo chake halikuwa la ujambazi.(P.T)
Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi
iliyofanyika Kanisa la Moyo Mtakatifu Yesu la Parokia ya Kisangara Juu
iliyopo Chanjale, ambayo pia ilihudhuriwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la
Arusha, Josephat Lebulu; Askofu wa Jimbo la Mbulu, Beatus Kinyaiya na
Askofu Damiani Ngalu wa Geita wote wa Kanisa Katoliki, Askofu Kimario
alisema waliofanya mauaji hayo ni wauaji wa kimtandao na kuitaka
Serikali kutoa majibu sahihi kuhusiana na tukio hilo badala ya majibu
mepesi yasiyofanyiwa utafiti.
Kauli hiyo ilionekana kujibu ile ya
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa
mauaji ya Dk Mvungi ni tukio la ujambazi.
"Eti waliotenda hilo ni majambazi,
nani kasema ni majambazi?... Ni research (utafiti) ipi ama upelelezi
gani umefanyika?... Hawa ni wauaji wa kimtandao, kuna maswali mengi
yasiyo na majibu," alisema Askofu Kimario na kuongeza:
"Ni kifo cha fedheha hata kuku hauawi
hivyo. Watu wana uchungu, kila mtu ana maswali ambayo hayana majibu...
kwa nini auawe? Kwani alikuwa tajiri hata majambazi watake pesa?"
Askofu Kimario alisema Watanzania
wanamlilia Dk Mvungi na familia yake inamlilia kama ambavyo wasomi na
wanazuoni wanavyomlilia hivyo Serikali inawajibika kutoa majibu sahihi
juu ya kifo chake.
"Damu yake inadai Watanzania tujiulize
Dk Mvungi yuko wapi... wanausalama ndugu yetu yupo wapi? Wasomi mlikuja
hapa kwenye harusi yake mkafurahi naye leo mnatuletea marehemu,"
alisema.
Askofu huyo alisema kinachofanya taifa
kubwa kama Marekani liheshimike ni wepesi wake wa kuwaeleza wananchi
wake ukweli na kutaka Watanzania wasiridhike na majibu mepesi ya kifo
hicho.
"Tusiridhike na majibu rahisi.
Marekani wanafanya uchunguzi mpaka ukweli unajulikana kama ilivyokuwa
kwa Osama Bin Laden... ilichukua muda mrefu lakini ukweli ulijulikana,"
alisema.
Akitoa salamu za Serikali katika
mazishi hayo, Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali inafanya jitihada
kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.
"Ni kweli Serikali inafanya jitihada
za kuwakamata waliofanya tukio hili la ovyo lakini hata tukiwapeleka
mahakamani wakahukumiwa kunyongwa hiyo si mbadala wa Dk Mvungi,"
alisema.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema watamuenzi Dk Mvungi kwa kukamilisha
kazi ya kutunga Katiba Mpya yenye masilahi ya nchi.
"Tunawaomba wananchi wote tumuenzi Dk
Mvungi kwa kuangalia mapendekezo ya Katiba kwa masilahi ya Taifa ili
tupate Katiba ya maridhiano," alisema.
Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema kifo cha Dk Mvungi
kimewaumiza lakini akasisitiza kuwa tukio hilo halitarudisha nyuma
harakati za kupigania haki ya Watanzania.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria
mazishi hayo ni Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mwanga, Profesa
Jumanne Maghembe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),
Steven Wassira, Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe na Naibu Waziri
wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki.
Wengine waliohudhuria ibada hiyo ni
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Naibu Katibu Mkuu wa CCM
(Bara), Mwigulu Nchemba.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment