Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe
(katikati) akiwa na walinzi wake akiwasili katika Jengo la Ubungo Plaza,
Dar es Salaam, jana kushiriki kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho.
Picha na Michael Jamson
Hali ya wasiwasi iligubika eneo
kinapofanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kilichoanza Dar es Salaam jana.
Ulinzi mkali wa walinzi wa Chadema
(Blue Guard), uliimarishwa katika ukumbi wa Ubungo Plaza kinapofanyika
kikao hicho ambacho kinatarajiwa kumalizika leo, huku kukiwa na maagizo
yaliyoashiria kuwapo kwa mambo mazito.
Maazimio ya kikao hicho yanasubiriwa
kwa hamu na wafuatiliaji wa mambo ya siasa nchini kwani kinafanyika
katika kipindi ambacho chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapita
katika misukosuko na hasa ya malumbano baina ya makamanda wake wa juu.(P.T)
Maelekezo ya ulinzi
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
aliwasili ukumbini hapo saa 5.20 asubuhi na baada ya kuingia, wapiga
picha waliruhusiwa kuingia kuchukua kumbukumbu ya tukio hilo kwa dakika
moja tu.
Waandishi wa habari hawakutakiwa kuingia na badala yake walielezwa kuwa wangepewa taarifa baadaye.
Wakati wapiga picha wakiwa ndani,
mmoja wa wajumbe wa mkutano huo alitoka na kutoa maelekezo kwa walinzi
wa Chadema akiwataka kuwa makini kutekeleza kazi yao watakapopewa amri
ya kumwondoa mjumbe yeyote mkutanoni.
"Kama mkipewa amri ya kuondoa mtu
ingieni na mtekeleze amri hiyo mara moja," alisisitiza mjumbe huyo na
kuingia ndani haraka. Walinzi hao zaidi ya 10, walipokea maelekezo hayo
kwa kutikisa kichwa kuashiria kukubaliana na amri hiyo.
Kikao kufunguliwa
Kikao hicho ambacho kilifunguliwa dakika nane baada ya Mbowe kuwasili, kilipangwa kujadili mambo matatu jana.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo ambaye
hakutaka kutajwa jina lake alisema kingepitia taarifa za vikao viwili
vya Kamati Kuu vilivyopita.
Suala jingine ambalo lilipangwa
kujadiliwa jana ni ushiriki wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa Mjumbe
wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar na kupitia
taarifa ya fedha.
Leo moto
Ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa leo
ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa Kampeni ya 'Movement For Change'
(M4C) na hali ya siasa.
Ajenda hiyo inatazamiwa kugusa matukio
ya hivi karibuni ndani ya chama hicho. Hayo ni pamoja na malumbano kati
ya Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema kuhusiana na masuala ya posho, kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa
Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuvunjwa kwa uongozi wa Mkoa
wa Mara na pia kuondolewa kikaoni kwa Mbunge wa Maswa Magharibi, John
Shibuda.
Zitto na Lema waliingia katika vita ya maneno mwanzoni mwa Novemba kuhusiana na masuala ya posho ya vikao.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Lema alimtuhumu Mbunge huyo wa Kigoma
Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho
nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye
Mtandao wa Jamii Forum huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya
chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususan, mitandao ya
kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Akijibu hoja hizo, Zitto alisema tangu
siku nyingi alikwishapiga marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa
na kamati hiyo.
Alisema tangu alipokuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alipiga marufuku
posho na pia aliwahi kuwashtaki Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru) wabunge wanaochukua posho kutoka taasisi za Serikali.
Zitto pia alipata msukosuko mwingine
baada ya kusambazwa ripoti inayoitwa 'Taarifa ya Siri ya Chadema'
iliyomtuhumu kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na viongozi wa Idara ya
Usalama wa Taifa kuhujumu chama hicho.
Ripoti hiyo inayodaiwa kuwa
iliandaliwa na Idara ya Upelelezi ya Chadema, ilieleza kuwa Zitto
alikuwa akipokea fedha kutoka kwa maofisa wa usalama na kuzisambaza kwa
makada wengine wa chama hicho ili wafanye kazi ya kukihujumu. Hata
hivyo, Chadema kupitia kwa Mnyika ilitoa taarifa kupinga vikali suala
hilo.
CAG kukagua ruzuku
Pia, Zitto aliingia katika malumbano
na chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake
hazikaguliwi na CAG. Chadema ilipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa
imekuwa inatumia taasisi binafsi kufanya kazi hiyo.
Suala jingine linalotazamiwa
kujadiliwa katika kikao hicho ni kusimamishwa kwa Mwigamba na Baraza la
Uongozi Kanda ya Kaskazini ambako kulizuka vurugu kiasi cha
kunyang'anywa kompyuta mpakato (laptop) baada ya kudaiwa alikuwa
anasambaza taarifa za kuhujumu chama hicho.
Suala lake linasubiri uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kama lile la kuvunjwa kwa uongozi wa Chadema wa Mara.
Pia kitendo cha Baraza la Kanda ya
Ziwa Mashariki kumtimua Shibuda kwa madai kwamba halina imani naye nacho
kina uwezekano mkubwa wa kujadiliwa.
Zitto na Mnyika wakosekana
Zitto na Mkurugenzi wa Uenezi wa chama hicho, John Mnyika walikuwa miongoni mwa wajumbe walioshindwa kuhudhuria jana.
Zitto yuko na Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) huko Sudan Kusini na Mnyika pia yuko
katika ziara ya kibunge Uturuki.
Kikao cha jana kilihudhuriwa na wajumbe 23 kati ya 32.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment