WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, November 25, 2013

TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB)- NA UONGOZI NDANI YA CHADEMA

TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA
UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA
1. Utangulizi

i. Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 22
Novemba 2013,

Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua
nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama
iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22
Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk
Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana
kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu
ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha
Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha
Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia
zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba
mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa.
Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika
vikao mbalimbali vyama.

ii. Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa
hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa
chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha
hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na
atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na
chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana,
leo na kesho.

2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na
nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha
kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama
changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa
nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.

i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika
uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

● Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
● Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine
16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga,
Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo
mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
● Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
● Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma
Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.

ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni
wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo.
Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga
kura wa Kigoma walivyoamua.

iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya
majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM
wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na
Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama nilivyokwisha kueleza katika
vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa
tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa
uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si
afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila
uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.

iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli
ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya
nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012

baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012
kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi.
Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa
mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.

v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu
za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu
nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae.
Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na
nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na
chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa
kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:

● Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda
chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile
ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
● Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya
chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu
tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa
hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.

vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho
za Vikao

Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara
ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na
matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani
yetu ya mwaka 20102015.

Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema
amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu
ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti
wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

● Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu
mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge
ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
● Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na
kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama
wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana
na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa
chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na
kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa,
kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
● Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la
msingi katika chama chetu.
3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la
tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu
ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA. Jambo hili pia
lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni
kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika
mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:
i. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa
chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye
amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao
watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
ii. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu
za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile
wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
a) Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na
ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania.
Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya
5.siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'.
Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea
kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya
demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. Napenda
wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini
watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na
nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu
zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
b) Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia
ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za
uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania
wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
c) Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi
mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa
niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
d) Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni
mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa
uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa
majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi
shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia. Kama alivyopata
kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika
nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa
chama chetu.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam.
24 Novemba, 2013

No comments:

Post a Comment