WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, November 16, 2013

Wingu la majonzi latanda mapokezi ya mwili wa Dr Mvungi Dar



Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Dk Sengondo Mvungi, baada ya kuwasili jana jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam, ukitokea Afrika Kusini.

Dar es Salaam. Vilio na majonzi vilitawala katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere mara baada ya mwili wa Dk Sengondo Mvungi kutua jana na ndege ukitokea Afrika Kusini ambako mauti yalimkuta.

Mwili huo ambao uliwasili saa 1:05 jioni kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini(SAA), ulipokewa na wanafamilia akiwamo mke wake pamoja na watoto ambao walikuwa wamevalia suti nyeusi,

Viongozi mbalimbali wa kitaifa walifika uwanjani hapo kuupokea mwili wa Dk Mvungi, akiwamo Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kariuki.

Pia wajumbe wote wa Tume ya Katiba walikuwapo uwanjani hapo wakiongozwa na Mwenyekiti, Jaji Joseph Warioba pamoja na Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba.

Akizungumza na gazeti hili uwanjani hapo, mtoto wa kwanza wa marehemu Dk Mvungi, Dk Natujwa Mvungi alisema, pengo aliloliacha baba yao ni kubwa kwa familia nzima, kwani licha ya kuwa baba, Dk Mvungi alikuwa mwalimu, kiongozi na kocha wa maisha yao.
“Hatuwezi kumlaumu Mungu kuwa baba amefariki tunachoshukuru ni kuwa alituandaa kuyakabili maisha kimasomo na kibusara. Kwa hivyo tunamwombea apumzike salama,” alisema Dk Natujwa.

Dk Natujwa alisema jambo ambalo analifurahia kwa baba yake ni kuwa aliifanya kazi yake ambayo alikuwa akiitamani kwa muda mrefu ya kushiriki katika mchakato wa kuunda Katiba Mpya.

“Ingawa hakuimaliza safari yote ya kuunda Katiba Mpya, lakini ameshiriki na amefanya kazi ambayo kila siku katika maisha yake alikuwa akiitamani. Alitamani sana kuifanyia marekebisho Katiba ya Tanzania,” alisema.

Dk Natujwa alisema baba yake aliipenda nchi yake na aliweka mbele utaifa kwanza kabla ya mambo yote, kwani siku zote katika maisha yake alitamani Mtanzania amiliki rasilimali za taifa.

Mratibu wa Tume ya Katiba, Abdallah Witawi alisema tume hiyo imepoteza nguzo muhimu ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza kuiziba kutokana na umahiri, elimu na uhodari aliokuwa nao Dk Mvungi.

Witawi alisema Dk Mvungi alikuwa ni mwadilifu, mchapakazi na mzalendo ambaye alikuwa na uwezo wa kutumia chochote na wakati wowote ili kushiriki katika kuijenga Tanzania,

“Alikuwa ana ndoto ya kuibadilisha katiba ili tu Mtanzania anufaike na kile anachokifanyia kazi, lakini kikubwa zaidi kwake ni kuwa alikuwa na ushirikiano mzuri na wajumbe wote. Alikuwa anasikiliza ushauri wa mtu yeyote bila kujali elimu, umri au chama gani cha siasa,” alisema.

Mwili wa Dk Mvungi (61) uliwasili jana saa 12:45 jioni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Mwili huo uliletwa  na Ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA).

Leo Novemba 16, saa 3:30 asubuhi mwili huo utapelekwa Viwanja vya Karimjee  jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuagwa.

Saa 4:00 hadi saa 5:45 asubuhi itafanyika misa takatifu ya kumwombea marehemu katika viwanja hivyo na baadaye salamu za rambirambi pamoja na neno la shukurani litatolewa.

Taratibu za kuuaga mwili huo zitaanza saa 6:55 hadi saa 8:40 mchana na baada ya kumalizika, mwili utapelekwa nyumbani kwake Kibamba, Msakuzi.

Ratiba hiyo itaendelea kesho, saa 2:30 asubuhi ambapo misa ya kumwombea marehemu itafanyika nyumbani kwake na saa 5:00 asubuhi msafara wa kuelekea Chanjale, Kisangara Juu, Mwanga, mkoani Kilimanjaro nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya mazishi utaanza.

Novemba 3, mwaka huu, Mvungi alivamiwa nyumbani kwake Kibamba na watu wanaoaminika kuwa ni majambazi ambao walimpiga na kumjeruhi kwa mapanga.

 Alipelekwa Hospitali ya Lugalo kwa huduma ya kwanza na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kabla ya kupelekwa Hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini kwa matibabu ya kina.

Hata hivyo, mjumbe huyo wa katiba na mwanasheria aliyebobea, alifariki dunia Novemba 13, nchini Afrika Kusini.

Kufutia tukio hilo, Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam linawashikilia watu sita wanaotuhumiwa kumvamia na kumsababishia majeraha yaliyosababisha kifo chake.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment