Ndugu zangu,
Zamani sana kule kijijini kwetu Nyeregete wenyeji walibuni ushirikiano katika kilimo. Waliita ' mgowe'.
Msimu wa kilimo ukiwadia hutokea
ndugu, jamaa na marafiki wa mwenye shamba wakakusanyika. Kwa pamoja
walishiriki kulima shamba la mwenzao. Kazi hiyo ilienda haraka na kwa
ufanisi. Siku nyingine walihamia kwa mwingine. Ni utaratibu tu
waliojiwekea wa kuchangiana nguvu kwenye jambo la maendeleo.
Na leo nchi yetu iko kwenye mgogoro wa
elimu. Hatua mbali mbali zinachukuliwa kujaribu kuutatua mgogoro huu.
Tumeona juzi hapa , kuwa mabadiliko makubwa yamefanyika kuhusiana na
mitihani, na Daraja la Sifuri limefutwa.(P.T)
Lakini, tufike mahali tukubaliane kama
taifa, kuwa bado hatujawekeza vya kutosha kwenye elimu. Ni tofauti na
miaka ili ya baada ya Uhuru.
Pendekezo langu la moja kwa moja; kama
taifa, tuanzishe sasa kampeni ya kuchangia shilingi moja tu kwa elimu.
Kwamba kila mwenye kupiga simu, basi, akatwe shilingi moja tu , na kiasi
hicho kiingizwe moja kwa moja kwenye mfuko wa kuchangia elimu.
Kwa idadi kubwa ya watumiaji wa simu
waliopo na wanaoongezeka kila kukicha, kuna uwezekano mkubwa wa
kupatikana fedha nyingi kuwawezesha Watanzania kusoma bure na kwa elimu
bora kuanzia chekekechea hadi Chuo Kikuu. Na hapo tutakuwa tumejitahidi
sana kupunguza matabaka katika jamii. Hapa Makabwela watakuwa
wamejichangia katika jambo lao la maendeleo. Na hakika wengi wako
tayari, hata kesho.
Maana, inatokea siku hizi kuwaona
baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, na hasa watoto wa Makabwela,
wakidhalilika kwa kulazimishwa kufunga virago kurudi makwao. Ni kwa kuwa
hawana sifa za kupata mikopo. Kwamba hawakufaulu kwa kiwango cha daraja
la kwanza kama ni wavulana, na daraja la kwanza au la pili kama ni
wasichana.
Hapa haki ya kupata elimu tunaipa
madaraja. Ni kwanini mtoto wa Kabwela mwenye sifa ya kujiunga na elimu
ya juu asiwe na haki ya kupata mikopo ya elimu?!
Mwandishi Ngugi wa Thiong'o alipata kusema; Ukitaka kuelewa hali ya baadaye ya nchi itakavyokuwa, basi, angalia hali za vijana wa nchi
hiyo kwa wakati uliopo.
hiyo kwa wakati uliopo.
Nami nitaongezea hapo alipoishia
Ngugi, kwa kusema, na ukitaka kuelewa hali ya baadae ya nchi
itakavyokuwa, basi, angalia hali za akina mama wake vijijini. Angalia
pia hali za watoto wa akina mama hao.
Na tujiulize, je, vijana wetu leo wako katika hali gani? Je, akina mama wa leo wa vijijini na watoto wao wako katika hali gani?
Maana ni ukweli, kuwa karibu asilimia
84 ya Watanzania wanaishi vijijini. Na huko ndiko waliko akina mama
wengi na watoto. Na akina mama wanabaki kuwa ndio mihimili halisia ya
familia nyingi za vijijini. Hivyo basi, ni mihimili ya nchi. Na nimepata
kuandika, kuwa ukitaka kuujua moyo wa nchi, nenda vijijini.
Swali, je, akina mama wa vijijini tunawajengee misingi gani ya kujikwamua kutoka katika hali zao duni walizo nazo sasa?
Jibu; ni kwa kupitia elimu bora kwa watoto wao.
Hivyo, na tuwe Wazalendo na Waaminifu
kwa Nchi yetu tuliyozaliwa na tunayoipenda. Na tuamini pia, kuwa kama
mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe, basi, mtaji wa Nchi Masikini
ni Watu Wake Wenyewe.
Watanzania tuwe tayari sasa kuchangia
shilingi moja ya kupigia simu, kwa Maendeleo ya Elimu. Hivyo basi, kwa
Maendeleo ya Nchi Yetu. INAWEZEKANA.
Ni Neno la Leo.
Maggid Mjengwa.
Iringa.
Iringa.
No comments:
Post a Comment